Kwa hakika ni matumaini yangu ulikuwa na mapumziko mazuri ya sikukuu ya Eidi na kufurahi vyema na familia kwa pamoja. Basi kama ilivyo kawaida yetu leo tuingie darasani huku tukiendeleza darasa letu huru la wanyamapori na kujuzana mengi kuhusu wanyama hawa.

Leo kwa mara nyingine tena tutamuelezea NDEGE fulani hivi kwa hakika ni mzuri na anavutia pia kama alivyo kuwa ndege wa makala iliyopita. Ndege ambae ni mkubwa kuliko ndege wote duniani ila kanyimwa sifa moja kubwa kama walivyo ndege wengine. Hatimae waswahili husemahata kwa ukarimu ndege huyu aliamua kuwapa manyoa na mbawa zake ndege wengine ili wapate kuruka. Na moja kwa moja leo tutamzungumzia “MBUNI”

Mbuni ni miongoni mwa ndege wanao vutia sana hasa wanapokuwa katika maeneo asili na kwenye kundi kubwa kutokana na tabia na michezo yao kwa ujumla. Kwa walio bahatika kutembelea baadhi ya Hifadhi za Taifa mfano Serengeti au Tarangire basi ni dhahiri kwamba watakuwa walijionea mengi yanayo vutia toka kwa ndege hawa. Mbali na michezo yao pia rangi ya mbuni hususni mbuni dume inavutia sana kumwangalia.

SIFA ZA MBUNI

1. Mbuni ndiyo ndege mkubwa kuloko ndege wote duniani na asiye na uwezo wa kuruka.

2. Wana miguu mirefu na shingo iliyo chomoza juu ya miili yao huku umbo la miili yao likiwa la duara.

3. Dume huwa na manyoa yenye rangi nyeusi na nyeupe huku jike akiwa na manyoa yenye rangi  tu ifananayo na kijivu iliyo pauka.

4. Mbuni ana uwezo wa kukimbia kilometa sabini kwa saa (70km/saa) huku akiweza kukimbia kwa kasi ya kilometa 64.3km bila kupunguza mwendo.

5. Huwa wanakuwa wakali hasa pale wapokuwa na mayai au watoto.

6. Huishi kwenye kundi kubwa linaloweza kufikia hadi mbuni 100 japo makundi mengi huwa na idadi ya mbuni 10.

7. Kila kundi la mbuni huwa na jike na dume ambao ni watawala wa kundi hilo.

UREFU NA UZITO

Urefu-Mbuni huweza kurefuka mpaka kufikia urefu wa futi 9 (sawa na mita 2.7)

Uzito-Mbuni huweza kufikia mpaka uzito wa kilogramu 145kg.

USIYO YAJUA KUHUSU MBUNI

1. Mbuni ndiyo ndege pekee mwenye vidole viwili kwenye kila mguu. Ndege wengine wote wana vidole vinne.

2. Mbuni hupigana kwa kutumia miguu na inaaminika kuwa teke la mbuni lililopigwa kwa nguvu lina uwezo wa kumuuwa simba.

3. Si kweli kwamba mbuni huzamisha kichwa chake kwenye mchanga, bali hukunja shingo na kuficha kichwa ili adui aone kichwa kimezama ndani ya mchanga. Na hii hupenda kufanya hasa pale anapohisi kutishiwa na adui yake.

4. Jicho la mbuni lina ukubwa wa kipenyo cha sentimita 5 (sawa na inchi 2). Hii inamfanya mbuni kuwa mwenye jicho kubwa kuliko viumbe wote waishio nchi kavu.

5. Jicho la mbuni ni kubwa kuliko ubongo wake.

MAZINGIRA WAISHIO MBUNI

Mbuni huishi maeneo ya savana kavu na joto, pia maeneo miti miti. Hapo zamani mbuni walikuwa wanapatikana karibu maeneo yote ya bara la Asia. Afrika na Ghuba ya Arabuni. Lakini kutokana na kuwindwa sana baadhi ya maeneo, kwa sasa mbuni wanapatikana maeneo ya Sahara tu barani Afrika.

Japo mbuni unaweza kuwakuta nchi yoyote ile duniani, ila wanakuwa wanafugwa au chini ya uangalizi madhubuti na si katika mazingira asili kama wanapokuwa kwenye Hifadhi za Taifa au mapori ya akiba.

CHAKULA

Mbuni ni ndege ambao wanakula aina mbali mbali za vyakula. Hivyo wana uwezo wakula majani na nyama pia. Ila chakula wanacho pendelea sana ni mimea hususani mizizi, mbegu na majani. Wakati mwingine wamekuwa wakila mijusi, nyoka na panya. Huwa wanakula udongo na mchanga ambao huwasaidia katika usagaji wa chakula kwenye firigisi.

Mbuni hawana ulazima sana wamaji ya kunywa. Hii ni kwasababu wanapata maji yakutosha kutoka kwenye mimea wanayo kula. Hivyo huwa hawa hangaiki kutafuta maji, japo kwenye matembezi wakikutana na maji njiani huwa wanakunywa.

KUZALIANA

Kabla ya kupandana ili kumvutia jike, dume huwa anacheza huku akipiga mbawa zake kwa juu kuoesha manyoa yake ndani. Wanapo kuwa tayari kwa kupandana mdomo wa dume hubadilika rangi na kuwa rangi nyekundu inayo ng’aa. Wakati mwingine hata shingo nayo hubadilika rangi ili kuendana na rangi ya mdomo.

Jike nae huanza makeke yake ili kumuhamasisha dume zaidi na pia hubadili rangi ya manyoa yake na kuwa na rangi ya fedha.

Jike hutaga mayai 40-60. Yai la mbuni huwa na ukubwa wa sentimita 15 na uzito hadi kufikia kilogramu 1.3kg. Jukumu la kutamia mayai ni la wote jike na dume na mayai hutamiwa kwa takribani siku 42-46.

Watoto wa mbuni wanapo zaliwa huwa ni wakubwa kuliko watoto wa ndege wengine wote na huweza hata kulingana na kuku jike kwa ukubwa. Dume na jike hulea watoto pamoja.

Mpaka kufikia miezi sita watoto huwa wameshakuwa wakubwa na kuwa na urefu sawa karibu na mbuni wakubwa. Mbuni hufikia umri wa kutaga au kupanda afikishapo umri wa miaka 3 au 4.

Maisha ya mbuni ni myaka 50 mpaka miaka 70.

UHIFADHI

Idadi ya mbuni kwa sasa bado haijafanyiwa utafiti, na hii ni kutokana na malezo ya shirika la umoja wa mataifa liashughulika na uhifadhi wa maumbileasili (International Union for Conservation of Nature-IUCN). Japo shirika hili linakiri kuwa idadi ya mbuni inazidi kupungua kutokanana kuwindwa kwao.

MAADUI WA MBUNI

Maadui wakubwa wa mbuni ni Binaadamu, Simba, Duma, Chui, Mbwa mwitu na Fisi. Kwa ufupi tu maadui wa mbuni ni wanyama jamii ya walanyama.

HITIMISHO

Nimatumaini yangu kwa darasa hili fupi na huru umejifunza machache kuhusu ndege, mbuni ambayo kwa namna moja au nyingine ulikuwa huyafahamu kuhusu ngege huyu.

Nikusihi tu kama ilivyo kawaida tega sikio kusubiri makala ijayo kwani kila makala inakuja na mnyama tofauti ili kufikisha elimu na machache kwa jamii kadiri itakavyo wezekana.

Ahsante na shukrani sana kwa kuwa nami pamoja mwanzo mpaka mwisho wa makala hii.

 

Unaweza kuwasiliana na mwandishi wa makala hii kwa namba zifuatazo;

Sadick Omary,

  Simu- 0714-116963 / 0765057969 / 0785813286

 

Email – swideeq.so@gmail.com