Mikoko ni aina ya miti inayoota pembezoni mwa Bahari (katika fuko za Bahari), na hustawi vizuri katika udongo au maji yenye chumvi hususani katika kanda za kitropiki. Ukuaji na ustawi wa miti ya mikoko huweza kuathiriwa na sababu mbalimbali kama vile hali ya hewa (hususani kiasi cha mvua), kupwa na kujaa kwa maji baharini (tidal regime), kiasi cha chumvi na historia ya jiolojia ya eneo ( geological history of the area).

Miti ya mikoko hushangaza watu wengi hasa wanaopenda kutembelea maeneo ya fuko za bahari katika namna ambavyo hustawi tofauti na aina nyingine ya miti. Miti mingi katika hatua za awali za ukuaji wake mpaka kustawi vizuri hutengeneza mizizi inayokuwa kuelekea chini kwenye udongo na mizizi hii hufunikwa na udongo kwa ajili ya kujipatia mahitaji muhimu. Lakini aina nyingi za miti ya mikoko huwa tofauti na miti ya kawaida na utofauti huu umeifanya kujizolea umaarufu mkubwa kwa kuwa na mizizi (pneumatophores) inayopumua (breathing Roots) na mizizi hii huota nje ya udongo (haifunikwi na udongo moja kwa moja) na mizizi mingine huonekana ikining’inia juu ya maji. Mizizi ya mikoko inauwezo wa kushika matope na hivyo husaidia kukinga pwani na kujenga visiwa ndani ya bahari. Hivyo Basi katika muktadha huu kiikolojia msitu wa mikoko huitwa “kapa” au “ wangwa”.

Aina ya mikoko inayopatikana Tanzania

Kuna aina nane (8) za spishi za mikoko ambazo tayari zimeshagundulika mpaka Sasa nchini Tanzania japo wanasayansi na watafiti bado wanazidi kuongeza juhudi katika kubaini aina mbalimbali za miti ya mikoko ambayo bado haijagunduliwa .

Zifuatazo ni aina za miti ya mikoko iliyopo Tanzania.

  •   Mkoko wimbi (Bruguiera gymnorhiza). Aina hii ya mkoko huwa na majina mengi Kama vile ;mchofi, mshinzi, msindi, msinzi au mui. Huwa na majani yenye rangi nyeusi-kijani hivyo kwa kingereza huitwa (Black mangrove). Lakini pia majani haya huwa na upana unaokadiriwa kuanzia sentimeta 4-8 na urefu wa sentimeta 5-15. Hii ni aina ya mkoko Inayopatikana katika familia iitwayo Rhizophoraceae. Mti huu wa mkoko huweza kukuwa mpaka urefu mita 18 au zaidi kutegemeana na mazingira.
Pichani ni mwonekano wa aina ya mikoko inayoitwa Bruguiera gymnorrhiza, picha imetolewa https://commons.wikimedia.org/wiki/File:Bruguiera_gymnorrhiza_habit2.jpg
  • Mkoko mkandala au mkandaa (Ceriops tagal) ambao pia kwa kingereza huitwa Indian mangrove. Aina hii ya  mkoko hupatikana magharibi mwa Bahari ya hindi mpaka Bahari ya pasifiki. Lakini pia aina hii hupatikana katika familia ya Rhizophoraceae na hutengeneza aina ya tunda ambalo linauwezo wa kuota baada ya kuanguka kutoka mti mama. Tunda hutoa  mbegu na kuanza kuweka mizizi na kustawi na kuwa mti mkubwa urefu wa cha mita 7 au zaidi. Mkandaa au mkandala huwa na majani yenye rangi ya njano-kijani yenye upana wa sentimeta 2 mpaka 5 na urefu wa sentimeta 3 mpaka 10.
Aina ya mikoko ya Ceriops tagal picha hii imechukuliwa na Ria Tan
  • Mkoko magondi au mkoko mwekundu mashariki (Rhizophora mucronata). Kwa kingereza huitwa, Asiatic mangrove na huwa na  na urefu wa mita 20 kwenda juu au Zaidi na majani yenye rangi nyeusi-kijani.  Ila tofauti ya majani haya na majani ya mkoko wimbi ni kwamba huwa na urefu mkubwa zaidi upatao sentimeta 9 mpaka 18 japo huwa na upana unaolingana wa sentimeta 4 mpaka 8. Hupatikana magharibi mwa Bahari ya hindi mpaka magharibi mwa Bahari ya pasifiki.
Pichani ni aina ya mikoko ya Rhizophora, Photo source: https://www.google.com/url
  • Mchu (Avicennia marina) hupatikana katika familia Avicenniaceae na hukuwa hadi kufikia urefu wa mita 30 na maua madogo yenye kipenyo cha milimita 5 ambayo mara nyingi huchanua mwezi oktoba mpaka mwezi januari. Mkoko aina ya Mchu ni aina pekee ya mkoko ambayo huweza kustahimiri kiasi kikubwa cha chumvi na vipindi mbalimbali vya mafuriko. Hivyo miti hii huifanya kupatikana kwa wingi sehemu kubwa ya ukanda wa kitropiki.
Pichani ni aina ya mikoko ya Avecenia Marina Source: https://www.researchgate.net/profile/Ruben-Amparado
  • Mpira (sonneratia alba)  hujulikana pia  kwa jina la kiswahili Kama “mlilana” katika familia Sonneratiaceae. Aina hii ya mkoko inauwezo wa kukua mpaka urefu wa mita 12 ikiwa na mizizi yake stahimirivu (pneumatophores) na majani yenye urefu wa sentimeta 3 mpaka 12 na upana wa sentimeta 2 mpaka 9. Hii ni aina pekee ya mizizi ambayo mara nyingi inapendwa kutumiwa  na wavuvi katika shughuli zao za uvuvi.
Mikoko aina ya Sonneratia alba chanzo cha picha ni : https://www.flickr.com/photos/jbfriday/42418452561/
  • Mka daa dume (Lumnitzera racemosa) hupatikana katika familia Combretaceae na  mara nyingi hutokea kama vichaka vifupi (shrubs) vikiwa na urefu wa mita 2 mpaka 3 na majani yake huwa na urefu wa sentimeta 2 mpaka 8 na upana wa sentimeta 1 mpaka 3. Hutoa maua mwaka mzima na watu wengi hupenda kutumia aina hii ya mkoko Kama kuni (Good fuel wood).
  • Mkungu au Msikundazi (Heritiera littoralis) hupatikana katika familia sterculiaceae na huweza kukua mpaka urefu wa mita 35,na kimo cha urefu mkubwa zaidi ukilinganisha na aina nyingine ya mikoko. Huwa na majani makubwa yenye urefu wa sentimeta 20 na upana wa sentimeta 12 .
  • Mkomafi ( Xylocarpus granatum). Katika ukanda wa magharibi mwa Bahari ya hindi mikoko hii hupatikana kwa wingi na hukuwa mpaka kimo cha urefu wa mita 10, pia haìna mizizi inayopumua (no breathing Roots).Huwa na maua madogo na hutengeneza tunda linaloitwa “Granatum”.  Aina hii ya mkoko haina uwezo mkubwa wa kustahimiri hali ya chumvi kama ilivo kwa mikoko mingine.
Source: https://www.dreamstime.com/photos-images/xylocarpus-granatum.html

Athari za uvunaji haramu wa mikoko.

Zifuatzo ni athari ambazo zinaweza kutokea kwasababu ya uvunaji haramu wa mikoko;

  • Huongeza kasi ya mawimbi baharini.
  • Mizizi ya miti ya mikoko inasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza kasi ya mawimbi baharini kwasababu mizizi hii inauimara wa kipekee katika kustahimiri mawimbi yenye kasi kubwa hivyo hufanya mazingira yaliyo kando kando ya bahari kuwa salama.
  • Hupunguza kiasi cha samaki kuzaliana.

Miti ya mikoko imekuwa na mchango mkubwa hasa katika kutengeneza mazingira mazuri ya samaki kuzaliana na kupelekea kuwa na mchango mkubwa katika pato la Taifa. Hivyo kuvunamiti hii kunachangia kupunguza kiwango cha Samaki kuzaliana katika sehemu tulivu ambayo haina mawimbi makali hivyo hukimbilia kwenye mikoko hasa kwenye mizizi yake..

  • Inapunguza uwezo wa kuhifadhi hewa ya ukaa (carbon dioxide) kutoka angani.

Miti ya mikoko inauwezo mkubwa wa kuhifadhi kiasi kikubwa cha hewa ya ukaa kupitia mchakato unaoitwa “photosynthesis”.  Licha ya hivyo uvunaji haramu na uharibifu wa mikoko umeathiri kwa kiasi kikubwa uhifadhi wa hewa hii na kupelekea hewa hii kujikusanya kwa wingi angani jambo linasababisha mabadiliko ya tabia ya nchi.

  • Huharibu muonekano mzuri wa mandhari ya Bahari.

Uwepo wa miti ya mikoko huipamba Bahari na kuifanya kuwa na mwonekano mzuri kutokana na uwezo wa Mikoko kutengeneza muonekano wa visiwa vidogo vidogo ndani ya Baharina huleta mvuto.

  • Huharibu makazi ya viumbe hai.

Miti ya Mikoko ni makazi ya bayoanuai nyingi ikiwemo wadudu, ndege, na reptilia, amphibia, wanyamana. Viumbe Hawa hukuwa na kuzaliana Katika miti ya mikoko kama sehemu yao ya makazi.

Kwa kuhitimisha makala hii napenda kutoa rai kwa watanzania wote hususani wale wanaoishi kando kando ya bahari kutunza mazingira ya miti ya mikoko. Ili kujiepusha na majanga yatokanayo na uharibifu wa mikoko. Juhudi za serikali zimesaidia kwa kiasi kikubwa hasa kupitia mradi wa mazingira ya Baharini na ukanda wa pwani (MACEMP) na mradi wa mikoko Development Foundation pamoja na wadau wengine ambao kwa mwaka 2021/2022 wamelenga kupanda Miche ya miti ya mikoko ipatayo milioni moja (1,000,000) ambayo itaweza kuchukua ukubwa wa zaid ya ekari 506. Hivyo sisi Kama watanzania tuunge mkono hizi juhudi ili kufikia lengo kuinusuru miti hii.

Imeandaliwa na Victor Obadia Wilson, kuhaririwa na Alphonce Msigwa-Mwikolojia Hifadhi za Taifa Tanzania, pamoja na Hillary Mrosso.

Victor Obadia Wilson

Mwanafunzi Shahada ya kwanza ya usimamizi wanyamapori.

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo

Mobile: +255743880175/+255620861002

Email: obadiavitor1998@gmail.com