Habari za siku nyingi ndugu msomaji wa makala hizi za wanyamapori. Ni muda mrefu kidogo sasa umepita tangu nitume Makala kwa mara ya mwisho katika kuwajuza mambo machache kuhusu wanyamapori na maendeleo ya wanyamapori hapa nchini na kwingineko duniani kwa ujumla.

Basi kama ilivyo kawaida yetu leo tena tutaingia darasani kujifunza mambo machache kuhusu wanyamapori huku tukiendelea kujuzana pia mambo kuhusu uhifadhi wa wanyama hawa na changamotio zinazo wakumba wanyama hawa bila kusahau changamoto pia zinazo zikumba mamlaka mbali mbali hapa nchini zinazo shughulika na uhifadhi wa wanyamapori.

Katika mfululizo wa Makala zilizopita nilijikita sana kuelezea wanyama katika kundi la wanyama wajulikanao kama mamalia (yaani wanyama wanaozaa na kunyonyesha watoto wao). Leo nitakwenda nje kidogo ya kundi hili na kupepesa macho kidogo katika kundi lingine la wanyama lijulikanalo kama tambaaji (reptilian)

Kundi hili la reptilia lina jamii nyingi sana za wanyama na waliyo gawanyika katika spishi nyingi sana. Mfano wa wanyama wanaopatikana katika kundi hili la reptilia ni jamii zote za nyoka na jamii zote za mijusi bila kuwasahau kobe na kasa. Katika historia ya mabadiliko ya viumbe hai (Organic evolution) wanyama hawa jamii ya reptilia ni wa miaka mingi sana kabla hata ya binaadamu.

Moja kati ya sifa kubwa katika baadhi ya spishi za wanyama hawa ambayo ina watofautisha na wanyama wengine duniani ni uwezo wa kutumia ulimi wao katumika kutambua kemikali kwenye angahewa ambazo huwasaidia kujua uelekeo wa vitoweo lakini pia hata kutambua harufu ya vitu mbali mbali kupitia ulimi.

Katika Makala ya leo nitagusia mnyama mmoja katika kundi hili la reptilia ambae wengi wetu tunamfahamu kwa juu juu tu lakini kuna mengi na ya kustaajabiisha kuhusu mnyama huyo. Mnyama huyo si mwingine bali ni MAMBA na hususani ajulikanae kama Mamba Nile.

Picha ya mamba nile, picha imepigwa na https://www.yourafricansafari.com/wildlife/nile-crocodile

UTANGULIZI

Kama nilivo kwisha kudokeza hapo juu, mamba ni miongoni mwa wanyama wapatikanaio katika kundi la reptilia. Kuna aina nyingi sana za mamba duniani kwa ujumla na wapo ambao wanapatikana kwa baadhi ya mabara tu na si kila bara utawakuta mamba hao. Mamba hutofautiana kutokana na mazingira wanayoishi lakinui pia kwa mtu aliye bobea kwenye taaluma za wanyamapori huweza kuwatofautisha mamba hata kwa kuwatazama tu maumbile ya hasa kwa kuangalia ukubwa wa miili yao na namna umbile la midomo ya mamba kwani hutofautiana sana kati ya jamii moja na nyingine.

Mfano mzuri ni ni namna ya kuwatofautisha mamba wa Nile na American alligator kwa kutazama miomo yao basi niwazi kuwa utawweza kuwatofautisha kwa urahisi zaidi.

Hivyo nikusihi ndugu msomaji wa akala hii kuisoma makala hii mwanzo mpaka mwisho kwa umakini zaidi kwani utajifunza mambo mengi sana kuhusu mamba wa Nile lakini pia utajifunza mambo ambayo kwa hakika ulikuwa huyajui kuhusu mamba kwa ujumla. Makala hii pia itakupa uwezo wa kuelezea sifa mbali mbali za mamba hasa kwa upande wa tabia zao, namna wanavyoishi hali kadhalika namna wanavyo zaliana wanyama hawa katika mazingira yao asilia.

SIFA NA TABIA ZA MAMBA NILE.

Ni wanyama wakubwa wenye umbo kama la mjusi huku mikia yao ikiwa mirefu na yenye nguvu sana kutokana na misuli iliyopo kwenye mikia yao. Mamba hawa ndio mamba wakubwa kuliko jamii za mamba zote zipatikanazo barani Afrika.

Mamba hawa wana rangi tofauti tofauti katika miili yao ukianzia na kijani, kahawia na kijivu. Sehemu ya juu hasa mgongoni wana mikanda yenye rangi nyeusi iliyo pandiana.

Sehemu ya chini yaani tumboni mpaka kifuani wana rangi ya njano.

Miili yao imezungukwa na magamba yaliyo pangika kijiometri ambayo kwa chini magamba hayo yana mifupa iliyoundwa kwa madini ya kalisi fosfate na kalisi kaboneti. Magamba haya sehemu ya kichwa yameungana na kutengeneza fuvu.

Wana vichwa vyembamba huku macho, masikio na matundu ya pua yakiwa yanaonekana sehemu ya juu ya kichwa. Mamba hawa wana macho yenye rangi ya kijani.

Taya za juu na chini kwa mamba hawa zinalingana upana. Hii ni moja kati ya sifa inayo watofautisha mamba hawa na mamba wa Marekani (American Alligator). Wanakadiriwa kuwa na meno kati ya 64-68 huku meno 4 ya mwanzo huonekana hata wawapo wamefunga midomo yao.

Wana miguu mifupi, miguu ya mbele ina vidole 5 ambavyo havina kimia huku miguu ya nyuma ikiwa na vidole 4 vinavyo onekana vizuri zaidi na cha 5 kikiwa ni kidogo sana hali ambayo inafanya kisionekane kwa nje. Kati ya vidole 4 vya nyuma, 3 vina kucha na vimeunganishwa na kimia (utando wa ngozi kati ya vidole).

Mamba wana uwezo wa kusikia nje na ndani ya maji pia. Uwezo wa kuskia ndani ya maji hutokana na kuwa na utando pembeni mwa fuvu ambao husaidia kupeleka mitetemo ya sauti ndani ya maji kwenye sikio la kati.

Wanyama hawa wana uwezo pia wa kuona ndani na nje ya maji na tafiti zinaonesha wana uwezo wa kuona kwa nyuzi 270.  Macho yana vigubiko vya macho ambavyo hulinda macho hususani wawapo kwenye maji.

Mamba wana namna tofauti ya kupumua tofauti sana na viumbe wengine. Wana uwezo wa kusukuma ini dhidi ya mapafu ili kuruhusu kutoa hewa nje na pale wanapo tenganisha ini na mapafu basi huwasaidia kuingiza kiwango kikubwa sana cha hewa ya oksijeni mwilini.

Wana uwezo wa kufanya shughuli zao majira yote yaani mchana na usiku japo kwa mara nyingi huwa wanafanya usiku. Majira ya mchana huonekana sana wakiwa wamejipumzisha kwenye kivuli hasa chini ya miti au hata kuota jua. Kipindi cha majira ya joto kali wanyama hawa huacha midomo wazi ili kusaidia kupunguza joto la miili yao.

Madume wakubwa ambao hasa ndio huwa watawala huwa wana linda himaya ambapo kwa nchi kavu himaya huweza kuchukuwa urefu wa mita 60 na kwenye maji huwa inakadiriwa kuwa na mita 50. Wakati madume wanapambana kutawala himaya, majike pia hupambana ili kuongoza kundi la majike wingine ndani ya himaya. Anaeshindwa katika mapigano haya basi huinua kichwa juu na kuashiria kuwa kashindwa na hana uwezo wa kutawala himaya au kuongoza majike.

KIMO NA UZITO

Kimo= Mamba wakubwa hufikia urefu wa mita 5-6 sawa na futi 16-20

Uzito= Hufikia uzito wa kilogramu 225-900.

Je, Wajua!!!!!

1.Mamba wakubwa hutoa sauti ambapo kila sauti huwa na maana yake?

Mamba hawa hutoa sauti aina 5 tofauti na kila sauti huwa na maana yake. Huwa kuna sauti inayo tolewa na madume yenye kuashiria utawala na kuzuia madume wengine wasiingie kwenye himaya yake. Sauti nyingine hutolewa na dume ili kuvutia majike waje ndani ya himaya yake kwaajili ya kuzaliana. Sauti nyingine hutolewa na wanyama hawa pale wanapohisi kuna hatari. Sauti ya 4 hutolewa dume pale anapoona kuna dume kashaingia kwenye himaya yake na sauti ya tano hutolewa na majike kuwalinda watoto pale wanapohisi kuna hatari.

2.Mamba wana uwezo wa kuishi muda mrefu sana bila?

Mamba wana uwezo mkubwa sana wa kuishi kwa miezi mingi bila kula. Tafiti zinaonesha kuwa mamba hawa wana uwezo wa kuishi miezi 6 au zaidi bila kula.

3.Jinsia ya watoto wa mamba watakao toka kwenye mayai hutegemea jotoridi la kiota?

Jinsia ya watoto wa mamba hutegemea jotoridi la sehemu ambapo jike kataga mayai. Kama sehemu hiyo ina jotoridi la nyuzi za sentigredi 30 ºC watoto wengi hutoka majike, kama jotoridi ni nyuzi za sentigredi 31 ºC basi kutakuwa na angalau uwiano sawa kati ya majike na madume na kama jotoridi la kiota ni nyuzi za sentigredi 32 ºC basi asilimia kubwa watakuwa ni madume.

4.Mamba ndio wanyama wenye uwezo mkubwa sana na taya zenye nguzu kung’ata kuliko wanyama wote duniani. Inakadiriwa kuwa uwezo wa mamba kung’ata ni mara 8 zaidi ya samaki ajulikanae kama papa mkubwa mweupe.

5.Mamba wakubwa huwa wanameza mawe na kuwasaidia kuwa sawa chini ya maji lakini pia huwasaidia katika usawa walalapo kwenye maji. Tafiti zinaonesha kuwa mawe haya huchangia asilimia moja (1%) ya uzito wa miili yao.

MAENEO WANAYOPATIKANA MAMBA NILE

Mamba hawa wanapatikana bara la Africa na sisi hapa nchini Tanzani tukiwa ni miongoni mwa nchi chache tunao jivunia kuwa na idadi kubwa tu ya mamba hawa nchini. Kuna baadhi ya nchini inasadikika mamba hawa walikuwepo lakini mpaka sasa wamesha toweka katika nchi hizo. Mfano ni nchi za mashariki ya kati inasadikika kuwa mamba hawa walikuwa wanapatikana baadhi ya maeneo lakini kwasasa wametoweka.

MAZINGIRA

Mamba ni wanyama wenye uwezo wa kuishi kwenye maji na nchi kavu. Mazingira wanayo pendelea mamba nile kuishi ni kwenye mito, mabwawa ya maji baridi na sehemu yenye mikoko.

CHAKULA

Kama tulivyoona hapo juu mamba wana uwezo wa kukaa muda mrefu sana bila kula.

Tafiti zinaonyesha kuwa mfumo wa mmeng’enyo wa chakula wa mamba ni tata sana na hii inampa uwezo wa kumeng’enya vitu vigumu kama mifupa ambayo huimeza bila hata kuisaga.

Asilimia 70 ya chaula cha mamba ni samaki. Japo baadhi ya wanyama ambao mamba hawa huwawinda sana na hasa wanapoingia kwenye maji ni swala, kakakuona, nyumbu, pundamilia na kuro.

Mfumo wa chakula wa mamba unafanana kwa asilimia kidogo na ule wa ndege na zaidi kabisa hufanana na wa mijusi. Kitu kinacho mtofautisha mamba na wanyama wengine jamii ya reptilia kwenye mfumo wa mmeng’enyo wa chakula ni uwepo wa firigisi kwa mamba wakati reptilia wengine hawana firigisi.

Pichani mamba akiwa katika mawindo yake, akimkamata nyumbu na ;http://www.tripadvisor.com

KUZALIANA

Dume anapokuwa mtawala wa himaya basi huwa na mamlaka ya kupanda majike waliyopo ndani ya himaya yake na hii ni baada ya kutoa aina ya sauti ili kuwavutia majike kama nilivyo eleza hapo juu. Hatua ya upandaji majike hufanyika ndani ya maji kasha muda wa kutaga unapo karibia jike hutafuta eneo zuri nje ya maji na kutaga mayai.

Mara nyingi jike hutaga mayai kando kando ya mto ambapo huchimba shimo na kutaga kasha huyafukia. Hii humsaidia kuyalinda kwa urahisi zaidi. Kwa msimu mmoja wa uzaji jike hutaga mayai kati ya 25 hadi 100. Majike huonekana wakitaga mayai mara nyingi kuanzia mwezi Novemba na Disemba na huchukua miezi 3 kutotolewa. Jike hulazimika kuyalinda mayai dhidi ya mamba wengine ili wasiyafukue.

Watoto wa mamba wanapo karibia kutoka kwenye mayai huanza kutoa sauti na hii humfanya jike awe karibu zaidi na kiota chake kwaajili ya usalama wa watoto wake. Tafiti zinaonesha kuwa watoto huanza kulia nusu saa kabla ya kutoka kwenye mayai kasha jike hulazimika kuanza kufukua kiota ili kuwasaidia watoto kutoka aridhini na kuwabeba kuwapeleka kwenye maji. Jike hutumia mdomo wake kuwabeba watoto kasha kuwapeleka kwenye maji na huwa na uwezo wa kubeba watoto zaidi ya 10 kwa wakati mmoja.

Ndani ya maji mama hukaa na watoto karibu na kuwalinda kwa hali na mali dhidi ya maadui. Mama anapo hisi hatari hutoa sauti ambayo huwafanya watoto wazame ndani ya maji na kujificha ili kukwepa hatari hiyo. Watoto wengi wa mamba huwa wanakufa kabla ya kufikia umri wa kujitegemea kutokana na maadui mbali mbali wakiwemo maadui asilia na wengine ni nje ya mazingira yao. Zaidi ya asilimia 40 ya watoto wa mamba hufa kabla ya kuanza kujitegemea.

Watoto wa mamba huanza kuzaliana hususani majike wafikishapo umri wa miaka 10 na kuendelea. Mamba hawa wana uwezo wa kuishi miaka 45 na kuendelea katika mazingira yao asilia. Japo tafiti zinaonesha kuwa kama wanafugwa basi huweza kuishi miaka hadi 80.

UHIFADHI.

Ni jambo la kujipongeza kuwa wanyama hawa bado hawajawa hatarini kutoweka duniani na kwamba idadi yao bado ni yenye kuridhisha. Hii ni kutokana na tafiti zinazofanywa na mashirika mbali mbali hapa duniani lakini pia taarifa zinazo tolewa na shilika la umoja wa mataifa linali husika na uhifadhi wa maumbile asili duniani (International Union for Conservation of Nature-IUCN).

Japo idadi ya wanyama hawa ni ya kuridhisha, hii haimaanishi kuwa wanyama hawa hawana changamoto katika maisha yao ya kila siku. Zipo changamoto nyingi sana zinazo wakumba mamba hawa na tutazielezea ka ufupi katika vipoengele vinavyo fuata.

HATARI

Ni vigumu sana kwa mamba kumshambulia mtu akiwa nje ya maji. Hivyo taarifa nyingi za mashambulio ya mamba dhidi ya binaadamu hutokea ndani ya maji. Hivyo kuepukana na tatizo hili hatuna budi kuwa makini na matumizi ya maji katika mazingira ambayo yana mamba au kusadikika kuwa na mamba.

UMUHIMU WA MAMBA

Mamba ni muhimu sana kwenye ikolojia kwani husaidia kupunguza idadi ya wanyama wengine na kufanya mazingira kutosheleza kwa idadi ya wanyama wanaobaki. Lakini pia kwenye suala la usawa wa ikolojia mamba hawa husaidia kula samaki jamii ya kambale ambao kama mamba wasinge kuwepo basi kambale hawa wangekuwa wengi sana na kula baadhi ya samaki ambao ni chakula cha ndege waishio pembezoni mwa vyanzo vya maji.

Kwa wale wenye vibali vya ufugaji wa mamba wanafaidika kwa namna mbili tofauti. Kwanza hufaidika kwa biashara ya nyama ya mamba ambapo bei ya kilo moja ya nyama ya mamba ipo juu sana ukilinganisha na wanyama wengine wengi.

Si nyama tu bali hata ngozi ya mamba ni biashara nzuri sana kwani ngozi yake hutumika kutengenezea bidhaa mbali mbali kama mikanda, mabegi na hata baadhi ya mikoba mbali mbali ya kina mama au kina baba kwaajili ya kubebea tanakilishi.

Utalii hasa kwa wenye maeneo ya bustani za wanyamapori kwani watu hutembelea maeneo hayo ili tu kuwaona mamba na kuacha kiasi kikubwa tu cha pesa.

Serikali pia inanufaika sana kupitia utalii na nchi inaingiza fedha nyingi za kigeni kutikana na idadi ya watalii kuwa kubwa kutoka nchi mbali mbali. Mfano mzuri ni msimu wa uhamaji wa wanyama kama nyumbu, pundamilia na jamii nyingine za swala, katika msimu huu watalii wengi hupenda kushuhudia mamba wanavyo winda wanyama wahamao katika mto Masai mara. Tukio hili la uhamaji wa nyumbu ni moja kati ya maajabu ya dunia.

CHANGAMOTO ZINAZO WAKUMBA MAMBA

Migogoro kati ya binaadamu na mamba; hii ni moja kati ya changamoto kubwa sana ambayo inawakumba mamba kwani maeneo wanayo ishi ni kwenye maji ambapo maji hayo ni rasilimali muhimu sana kwa binaadamu. Hali hii inapelekea vifo kwani watu hushambuliwa na mamba wakati wakienda kwenye vyanzo vya maji pia hata mifugo imekua ikikumbwa na hali hii. Hii husababisha watu kuwauwa mamba kama kulipa kisasi na kusababusha wanyama hawa kupungua baadhi ya maeneo.

Ujangili; mamba wamekuwa wakiwindwa sana kinyume na sheria na majangili. Hii ni kutokana na thamani ya mazao ya mamba kama nyama, ngozi na hata kucha zao. Hali hii inachangia wanyama hawa kuadimika sana na kuwa hatarini kutoweka baadhi ya maeneo. Mfano mnamo miaka ya 1960 wanyama hawa waliwindwa sana mpaka kufukia hatua ya kukaribia kutoweka nchini Misri. Katika chapisho la mwaka 2009 la IUCN, mamba nile ndio mamba wanaoongoza kwa kuuzwa katika masoko kuliko jamii nyingine zote za mamba duniani.

Neti za wavuvi; Maeneo mengi ya mito au vyanzo vya maji huwa na shughuli za uvuvi zikiendelea kwa kiasi kikubwa sana. Kuna wakati wavuvi hulazimika kutega nyavu zao na kuziacha kwenye maji hata kwa kutwa nzima ili kupata samaki wa kutosha. Nyavu hizi kuna wakati huwakamata mpaka mamba hasa mamba wadogo na kushindwa kutoka hatimae hupoteza maisha kwa kushikiliwa na nyavu. Lakini pia huliwa na baadhi ya samaki au mamba wengine wakubwa pale wanapokuwa wamenasa na kushindwa kujinasua kwenye nyavu.

Uchafuzi wa mazingira; Baadhi ya maeneo yamekuwa yakikumbwa sana na athari za uchafuzi wa mazingira hasa kwenye vyanzo vya maji. Uchafuzi huu umepelekea mpaka maeneo ambayo wanaishi mamba hawa kuchafuka sana na kupelekea mamba kuhama baadhi ya maeneo ili tu kukwepa madhara yatokanayo na uchafuzi wa mazingira. Baadhi ya viwanda vimekuwa vikisababisha uchafuzi wa maji kutokana na kemikali zitikazo viwandani humo kuingia kwenye vyanzo vya maji na kusababisha upungufu wa hewa ya oksijeni kwenye maji na kupelekea mamba hawa kupata shida kwenye upumuaji wawapo ndani ya maji.

Mimea vamizi; Hii ni mimea ambayo sio asilia katika maeneo husika na huota kutokana na sababu mbali mbali. Mimea hii kwa kiasi kikubwa huathiri mazalia ya mamba. Mfano mimea ambayo inaota maeneo ya viota vya mamba husababisha jotoridi la viota kupungua kutokana na kutanda juu ya ardhi. Hivyo kama jotoridi litapungua basi niwazi kwamba watoto watakaotoka kwenye mayai wanaweza kuwa wakike wote kama nilivyo kwisha eleza hapo juu. Athari ya kuzaliwa jinsia moja tu kwa wingi basi huathiri mfumo mzima wa kuzaliana kwa mamba hawa.

NINI KIFANYIKE ILI KUEPUKANA NA CHANGAMOTO HIZI HUSUSANI HAPA KWETU TANZANIA

Serikali ijitahidi kusambaza maji katika vijiji hasa kwenye vile vijiji ambavyo vinazunguka vyanzo vya maji kwani kumekuwa na matukio mengi ya watu kushambuliwa na mamba pale wanapokwenda kutafuta maji. Endapo upatikanaji wa maji utakuwa wa haraka na wepesi zaidi maeneo yao basi hakutakuwa na sababu ya watu kwenda maeneo hayo na hii itapunguza kwa kiasi kikubwa matukio ya mamba kushambulia watu.

Wizara ya maliasili kwa kushirikiana na mamlaka mbali mbali zinazo simamia uhifadhi wa wanyamapori hapa nchini ishughulikie changamoto ya ujangili na kupambana na biashara haramu ya nyama na mazao mengine ya mamba. Wapo mamba ambao wanapatikana kwenye maeneo ya hifadhi na wengine wapo nje ya maeneo ya hifadhi. Kwa mamba waliyopo nje ya maeneo ya hifadhi ndiyo wanakumbwa na tatizo la ujangili kwa kiasi kikubwa sana.

Mamlaka za hifadhi za wanyamapori hasa kwenye hifadhi zenye mamba kama kisiwa cha Rubondo, Saanane, Hifadhi ya taifa ya Gombe na maeneo ya Masai Mara katika hifadhi ya taifa ya Serengeti zijitahidi sana kutokomeza matumizi ya neti hasa neti ndogo ambazo zimekuwa na athari kubwa sana kwa mamba. Niwazi kwamba maeneo yote yaliyopo chini ya hifadhi za taifa hairuhusuwi kufanya shughuli yoyote tofauti na utalii wa kutembea na picha tu, hivyo kama kuna kiashiria chochote cha uvuvi katika maeneo hayo basi mamlaka haina budi kushughulikia tatizo hilo haraka sana ili kuzuia athari ambazo zinaweza kujitokeza hapo baadae.

Wana ikolojia katika hifadhi za wanyamapori ambazo zina mamba wajitahidi sana kufanya ufuatiliaji wa kila siku, wiki au mwezi kuhakikisha maeneo ya mazalia ya mamba yanabaki katika uasilia wake ili kuzuia mimea vamizi kutawala eneo hilo. Hii itasaidia kupunguza athari za kutotolewa watoto wa jinsia moja kwenye vviota vya mamba kutokana na mabadiliko ya jotoridi.

Kuna umuhimu mkubwa sana wa kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi ili waweze kujua umuhimu wa wanyamapori kwa ujumla. Serikali inaingiza fedha nyingi za kigeni kupitia utalii ambao kwa namna moja au nyingine huchangiwa na uwepo wa wanyamapori hapa nchini. Jamii nyingi zimekuwa zikunufaika kupitia uhifadhi wa wanyamapori kama kujengewa vyumba vya madarasa, zahanati, madaraja na shughuli nyingine nyingi tu za kijamii kama ujengaji wa maboma na miradi mingine ya kijamii.

HITIMISHO

Mamba ni wanyama ambao hawazungumzwi sana katika midomo ya watu kwani watu wengi hawajui thamani ya wanyama hawa. Ukweli ni kwamba mamba wana thamani kubwa sana na wanao fuga mamba ndio wanajua thamani ya wanyama hawa. Vile vile mamlaka za uhifadhi na usimamizi wa wanyamapori zinajua kwa undani ni kwanamna gani baadhi ya wageni wanakuja hapa nchini kuwashuhudia mamba tu.

Mbali nakuwa wanyama hawa kwa asilimia kubwa maisha yao ni kwenye maji, lakini wamekuwa wakikumbwa na changamoto mbali mbali; asilimia 90 changamoto zao zinatokana na binaadamu. Hivyo tunaweza kusema kwamba adui mkubwa wa mamba ni binaadamu na pia huyu huyu binaadamu anainekana kuwa adui mkubwa kwa wanyamapori wengi sana.

Uhifadhi wa wanyamapori sio jukumu la serikali pekee tu kupitia mamlaka husika za uhifadhi bali ni jukumu la kila mtanzania kuhakikisha ustawi wa wanyama hawa. Ni vigumu sana kwa mtu aliyopo mjini kutambua thamani ya wanyama hawa kwani haoni faida ya moja kwa moja itokanayo na wanyama hawa.

Serikali kupitia mapato yatokanayo na utalii hujenga majengo ya hospitali na zahanati, barabara, shule na madaraja. Vitu vyote hivi kwa ujumla vinapelekea ukuaji wa uchumi hapa nchini kwa kiasi kikubwa sana.

……..MWISHO…………..

Kwa kupata mengi zaidi kuhusu wanyamapori wasiliana nami kupitia

Sadick Omary Hamisi

Simu=0714116963/0765057969

Email=swideeq.so@gmail.com

Instagram=wildlife_articles_tanzania

Facebook= Envirocare and wildlife conservation au Sadicq Omary Kashushu

Au tembelea tovuti yetu= www.wildlifetanzania.home.blog

……….”I’M THE METALLIC LEGEND”………..