Habari rafiki, karibu kwenye makala yetu ya leo ambapo tunaangalia mambo kadha wa kadha ambayo yanatokea katika maeneo yetu na maeneo ya wanyamapori yanavyoweza kuwa na madhara makubwa kwa uhifadhi wetu. Katika makala hii tutaangalia zaidi watu au wanajamii ambao wanaishi kando au karibu na hifadhi au karibu na maeneo ya wanyamapori. Kwa asilimia kubwa wanajamii wanaoishi kwenye maeneo hayo ni wafugaji, wakulima wanaweza kuwa wachache lakini wengi wa jamii hizi zinazoishi karibu na maeneo yaliyohifadhiwa wengi wao ni wafugaji, na wapo wafugaji wengi katika nchi yetu na wengi huwa na mfumo wa maisha unaofanana.
Wanajamii ambao wanaishi kando kando ya hifadhi wanakabiliwa na changamoto nyingi sana kutokana na wanyamapori kuvamia na kuua mifugo yao na uharibifu wa mazao yao, na hivyo kunakuwa na uhasama na chuki dhidi ya wanyamapori. Kimsingi wanayamapori wanaosababisha usumbufu kwa wanajamii ni simba, fisi, chui, hawa huwa wanavamia sana mifugo ya wafugaji ambao wanachunga au wanaishi karibu na maeneo ya wanyama hawa, wanayama wengine ni tembo, nyani, tandala nk hawa ni wanyama wanaokula majani uharibifu wa wanyama hawa ni kwenye mazao ya wakulima waliolima karibu na maeneo ya wanayama hawa. Hivyo moja kwa moja vitu vinavyosababisha migogoro mingi na kutokuwa na mahusiano mazuri baina ya hifadhi na wanajamii ni uwepo wa wanyama hawa kwenye maeneo yao, pia kwa wakati mwingine uwepo wa wanyampori hawa umekuwa hauleti faida wanayoiona kwa macho badala yake ni hasara wanayoiona.
Sasa matokeo ya migogoro hiyo huwa na madhara makubwa sana, kwa mfano ulio hai kabisa wafugaji wengi ambao mifugo yao huliwa au kuvamiwa na simba au fisi, hukasirika sana na kuamua kujichukulia hatua mkononi bila hata kutoa taarifa sehemu husika kama vile kwa uongozi wa kijiji husika, TANAPA, na kwa mamlaka nyingine zinahusika na wanyamapori. Badala yake wafugaji hao huitana wenyewe kwa wenyewe na kutafuta nyia ya kumfuatilia huyo simba au fisi aliyesababisha mauaji kwa mifogo yao. Hivyo wanaingia msituni na kuanza kuwatafuta simba, na mnyama yeyote anayekula nyama atakayeonekana mbele yao wanaua, na hawishii tu kuua wanaweka na sumu kwenye mzoga ambao wameuua, jambo ambalo ni baya kuliko yote kwani kwa kuweka sumu kwenye mzoga huo utasababisha vifo vingi sana vya wanyama wanaokula nyama na wanyama wanao kula mizoga.
Na endapo watagundua simba ameacha mzoga wake alio uua wanachokifanya wanatia sumu kwenye mzoga huo wa ng’ombe au mbuzi amabao simba ameuacha baada ya kufukuzwa. Na mara zote simba akacha mzoga wake aliyeuua huwa lazima aurudie kuula, hivyo wanachofanya watu hawa ni kuweka sumu kali kisha kuondoka, na simba akirudi kuula ule mzoga tu, anafia hapo hapo hafiki mbali, hata wanyama wengine wanao kula nyama watakapokuja na kula ule mzoga watakufa bila huruma. Wanyama wanaokula nyama ni wengi sana porini, kuna simba, fisi, bweha, mbwa mwitu, duma, tumbusi, na hata nguchiro. Kwa kuweka sumu tu kwenye mzoga unaoliwa na wanyama wengine unaweza kusababisha vifo vya zaidi ya wanyamapori 1000, kwa wakati mmoja, hili ni jambo la hatari sana kwa uhifadhi wetu.
Licha ya kuwa watu hawa watamwekea sumu wanyamapori wetu na kuwaua lakini pia kuna athari kubwa sana kwa hii sumu kwenye maisha ya mwanadamu pia, fikiria wakaweka sumu hii kwenye vyanzo vya maji, au sehemu nyingine ambazo zina tumika na binadamu, itasababisha mauaji ya kutisha pia, hili ni jambo ambalo ni baya sana kwa watu wanaofanya au kupanga kufanya mambo ya namna hiyo.
Sisi kama wahifadhi tunatakiwa kuielewa jamii ambayo tunaishi nayo au jamii ambayo ipo karibu na maeneo yaliyohifadhiwa, hasa wafugaji, inatakiwa tutumie kila mbinu ya kuhakikisha elimu na faida zinazotokana na wanyamapori tunao wahifadhi zinaenda moja kwa moja kwa jamii hizi. Hivi ni vitu ambavyo tunatakiwa kuvichukulia kwa umakini wa hali ya juu sana endapo tunataka kuendeleza uhifadhi wetu.
Mambo haya ya kuwawekea wanymapori sumu inaweza kuwa nje ya hifadhi au hata ndani ya hifadhi endapo watapata nafasi ya kuingia kwa njia za panya, lakini mara nyingi hutokea nje ya hifadhi, hutokea sehemu ambazo kuna mwingiliano wa karibu kati ya watu na wanyamapori, kama vile mapori ya akiba, mapori tengefu au kwenye mapori ya vijiji.
Wanyamapori tunao wahifadhi hawajui huu ndio mpaka wetu kwamba hawatakiwi kuvuka mpaka na kwenda kwenye maeneo mengine yenye chakula, au sehemu ambayo chakula kinapatikana kwa urahisi, na mara nyingi endapo kuna wafugaji wana mifugo yao ipo maeneo ambayo ni jirani na hifadhi ndio huadhirika zaidi na wanyama hawa kwani simba huona njia rahisi ya kupata chakula ni kukamata ng’ombe au mifugo mingine iliyooneka na kuwa rahisi kwake kuikamata.
Kwa leo hayo yatufikirishe, cha msingi kabisa ni kuielewa ndani na nje jamii ambayo ipo kando kando ya maeneo yaliyohifadhiwa, uelewa huu utatufanya tuandae na kujiandaa jinsi ya kwenda nao sambamba, pia uelewa huu utaturahisishia kwenye namna ya kushirikiana na jamii hizi.
Ahsante sana rafiki kwa kusoma makala hii, najua tutaungana kwenye kuhifadhi wanyamapori wetu.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
0742092569/0683248681