Miongoni mwa mamalia, popo ni wanyama waliogawanyika katika spishi nyingi sana miongoni mwao, ikiwa ni idadi kubwa ya pili baada ya spishi za wanyama jamii ya panya. Kutokana na kuwa na spishi nyingi tofauti tofauti pamoja na kufanya shughuli nyingi za maisha yao wakati wa usiku, watu wengi wamekuwa na uelewa mdogo kuhusu popo. Popo wanapatikana duniani kote isipokuwa maeneo ya ncha ya dunia ambapo huwa na baridi sana kipindi chote cha mwaka.
Zipo sababu kadhaa za kisayansi zinazowatofautisha popo na ndege, ijapokuwa wote wanaweza kupaa. Tofauti na kuzaa, kunyonyesha, kuwa na damu moto, meno pamoja na nywele, popo anatofautiana na ndege kwenye vipengele vifuatavyo;
- Mabawa tofauti na viumbe wengine. Mabawa ya ndege huwa ni mfano wa miguu ya mbele iliyo mifupi ikifunikwa na nyama na manyoya ambayo huwasaidia ndege kupaa kwenda mbele au kuelea angani. Mabawa ya ndege pia hufanya kazi kwa mfanano, yani kwa uelekeo mmoja kwa wakati mmoja. Kwa upande wa popo, mabawa yao huwa ni mfano wa ngozi nyembamba kama karatasi, ambayo imeunganika tokea kwenye miguu ya mbele hadi mkiani. Mabawa ya popo pia huweza kufanya kazi kipekee, ikimaanisha siyo lazima yafanye kazi kwa mfanano kwa wakati mmoja, na kila bawa linaweza kuelekea upande tofauti (asymmetrical).
Hali hii huwafanya popo kuwa na uwezo wa kupaa kwa kasi ya hadi kilomita 80 kwa saa na kukata kona za haraka sana. Popo pia wana uwezo wa kuruka kwenye mstari usionyooka, na huweza kupita hata kwenye uwazi mdogo sana kwa kasi bila kujigonga, ambapo uwezo huo ndege wengi hawana.
Mabawa ya Popo katika maumbo mbalimbali
- Ubongo usioweza kuchunguzwa kwa urahisi. Bado ubongo wa popo umekuwa ni kitendawili kwa wanasayansi wengi, kwani popo huwaza tofauti sana na viumbe wengi. Katika uchunguzi, ndege huamka asubuhi na huwa na muda wa kutafuta chakula, kupumzika, kukutanana na ndege wengine na kutoana wadudu (grooming) n.k. Hali ni tofauti kwa popo kwani popo anaweza kufanya vitendo tofauti kwa mda mfupi sana. Ndani ya dakika chache popo anaweza kuwa ameamka na kuwinda wadudu kadhaa, amekutana na mwenza, kisha kurudi kulala, na kufanya vivyo tena mara kadhaa.
- Umri wa kuishi. Jamii nyingi za popo zinaweza kuishi kwa umri mrefu kuliko ndege wengi. Kwa wastani, popo huishi kati ya miaka 10-20 huku popo mwenye umri mkubwa zaidi akirekodiwa kuwa na miaka 41.
Faida za Popo kwa Binadamu na Mazingira
Kupunguza wadudu waharibifu kusikokuwa na madhara. Uchunguzi wa kitaalamu unaonyesha popo wanaokula wadudu huweza kuwinda kati ya wadudu 1000 hadi 4000 kwa usiku mmoja. Idadi ya wadudu anaoweza kuwawinda kwa usiku hutegemea ukubwa wa wadudu, ukubwa wa popo au kama popo ananyonyesha. Popo huwinda wadudu waharibifu wa mazao shambani, na kupunguza hasara kwa wakulima ambapo pia huondoa uhitaji wa kemikali za sumu ili kuua wadudu hao. Popo huweza kuwinda wadudu waletao magonjwa kama mbu, ambapo huweza kuwinda wadudu wa aina hiyo kwa wingi sana kutokana na wadudu hao kuwa wadogo. Takwimu zinaonyesha kila mwaka popo huokoa mabilioni ya dola katika sekta ya kilimo duniani ambapo hufanya kazi ya kusaidia wakulima kupata mavuno kwa njia salama.
Faida za kitabibu na kitafiti. Popo wameonekana ni viumbe ambao miili yao inaweza kubeba virusi vya magonjwa mbalimbali kama vile vya Uviko-19 (Covid-19) na Marburg, bila kuwaletea madhara wao wenyewe. Hii imepelekea watafiti kuwatumia popo mara nyingi wawapo maabara kujifunza namna miili yao inaweza kuishi na magonjwa hayo bila shida, ili waweze kutengeneza dawa za kinga kwa binadamu. Popo pia hutumika katika majaribio mbalimbali ya kitabibu kama kujaribu matumizi ya dawa mpya, ambapo ni ngumu kuanza kuijaribu moja kwa moja kwa binadamu bila kujua kama inaweza kuleta madhara.
Wanasayansi wakimtumia popo katika tafiti
Usambazaji wa mbegu za mimea na uchavushaji wa maua.
Baadhi ya jamii za hasa wale wala matunda na asali husaidia sana kwenye kuchavusha maua na kusambaza mbegu za mimea. Ushavushaji hutokea pale ambapo popo wanagusana na sehemu ya kiume ya ua iitwayo chavua (polen/anthers) ambayo inabaki mwilini mwao pale wanapokuwa wanatafuta asali (nectar) au chavua kwa ajili ya kula. Popo hutua kwenye ua lingine na kukutanisha ile chavua na sehemu ya kike ya ua (stigma), na kusaidia shughuli nzima ya uchavushaji. Mimea ambayo popo huchavusha ni pamoja na jamii ya ndizi za Asia, mimea ya agave (hutengeneza vilevi), kokoa, mipera, mikaratusi na miembe. Popo pia hula matunda na kumeza mbegu, huku mfumo wao wa umeng’enyaji ukishindwa kuchakata mbegu hizo, na kupelekea mbegu hizo kutoka zikiwa bado nzima kwenye kinyesi. Hii husaidia mbegu za mimea hiyo kuota tena, na popo wanaweza kusafirisha mbegu hizo kwa umbali wa kilomita 75 na kusaidia mimea ya asili kuendelea kuishi. Kufahamu zaidi soma makala hiiWanyamapori Katika Mtego wa Imani: Uharibifu Usioonekana na Jinsi ya Kupambana Nao
Popo akichavusha maua wakati wa kutafuta chakula
Mbegu za mimea zikisambazwa kupitia kinyesi cha popo
Upatikanaji wa mbolea. Sehemu ambapo popo hutumia kama makazi kwa mda mrefu huweza kusaidia upatikanaji wa mbolea kutokana na mkusanyiko wa kinyesi chao. Mbolea hiyo huweza kutumika kwenye shughuli za kilimo ili kuongeza rutuba ardhini.
Kitoweo. Zipo baadhi ya jamii huwatumia popo kama kitoweo chao binafsi au cha wanyama wanaowafuga. Jamii hizo huwinda popo kutumia mitego au silaha mahsusi kwa jamii hizo na kujipatia kitoweo. Jamii hizi zina fikra tofauti na jamii nyingi za watu ambao huogopa hata kukutana au kuwashika popo.
Popo akitumika kama kitoweo
Mitazamo ya Binadamu juu ya Popo
Kwa miaka mingi popo wamekuwa wakiishi karibu na mazingira ya binadamu, na kumekuwa na mitazamo mbalimbali juu ya popo. Miongoni mwa mitazamo hiyo ni pamoja na ifuatayo;
Kumuhusisha popo na magonjwa. Pengine hii ni miongoni mwa taswira iliyoenea zaidi duniani baada ya kutokea kwa mlipuko wa uviko-19 huko nchini China, huku popo wakitajwa kuwa ndiyo chanzo cha mlipuko huo. Magonjwa mengine ni kama kichaa cha mbwa (rabies) na ugonjwa wa Marburg. Kama Makala hii ilivyotangulia kueleza hapo awali, popo huweza kubeba magonjwa na virusi ambavyo vinaweza kuwa na hatari kwa binadamu, lakini bado hakuna uhakika kwa asilimia mia moja kuwa ndiyo walikuwa chanzo cha mlipuko wa uviko-19.
Viumbe wachafu na wasumbufu. Ni ukweli usiopingika kwamba ni rahisi kugundua sehemu wanapolala popo kutokana na kuwa na harufu kali ya vinyesi vyao pamoja na sauti zao kali. Hali hiyo imefanya watu wengi kuwaona popo kuwa kero hasa wanapokuwa kwenye makazi ya binadamu. Zipo jamiii pia barani Afrika zinaamini kuwa mtu anaweza kupata upofu endapo popo watamuangushia haja ndogo machoni, ilihali jambo hilo kutokuwa na uthibitisho wa kisayansi.
Imani za kishirikina. Jamii kadhaa duniani humuhusisha popo na mikosi au viumbe vyenye nguvu za giza. Hii ni kutokana na muonekano wa popo na shughuli za maisha yao kuwa za usiku zaidi, pamoja na popo kuwa na tabia au sifa ambazo ni tofauti na viumbe wengine wote. Nchini Tanzania, popo pia wamewahi kuhusishwa na mambo ya kishirikina hasa kwenye mikoa ya pwani ambapo roho iliyosemekana kuwa ya kichawi (jini) iliyoaminika kuwaingilia watu kimwili bila ridhaa yao wakati wa usiku ilipewa jina la “popo bawa”. Hili limepelekea kujenga chuki au hofu dhidi ya wanyama jamii ya popo pindi wanapowaona.
Viumbe wanyonya damu (Vampires). Hii ni taswira iliyojengwa miongoni mwa jamii nyingi duniani hasa upande wa nchi za magharibi na baadhi ya nchi za Afrika. Taswira hii imekolezwa zaidi na baadhi ya tamthilia hasa za magharibi (Hollywood) ambapo popo wamekuwa wakionyeshwa kuwa ni viumbe hatari wanaonyonya damu. Uhalisia wa taswira hii ni kwamba zipo jamii za popo zinazonyonya damu, ambazo hupatikana Amerika ya kati na Amerika kusini lakini ni nadra sana kuwa na madhara kwa binadamu kwani hunyonya damu ya wanyama zaidi.
Kitoweo. Kama ilivyoelezwa hapo awali, baadhi ya jamii duniani humuona popo kama kitoweo kizuri kwao.
Hali ya usalama wa Popo.
Licha ya kuwa na mitazamo tofauti juu ya popo, ukweli usiopingika ni kwamba wana faida kubwa katika mazingira na ikolojia ya dunia. Takwimu za kitafiti za hivi karibuni zinaonyesha kuwa popo wanapungua kwa kiwango kikubwa katika maeneo yote ambayo yamefanyiwa utafiti. Kupungua huku kwa kasi kunachagizwa na kupotea kwa mazingira rafiki kwao, hasa uoto wa asili ambamo baadhi ya jamii huishi humo. Binadamu pia katika maeneo mengi duniani huonekana kuwabugudhi popo au kuwaua kwa makusudi pale ambapo wanafanya makazi karibu na maeneo ya binadamu. Mfano, hivi karibuni watu wanaoishi Upanga Dar es salaam, Tanzania wamekuwa wakitoa malalamiko sana kuhusu popo kuwasumbua na kuwa kero kwenye maeneo yao. Hivyo wakiomba serikali na TAWIRI kuja kuwaondoa popo hao. Hata hivyo, wakazi hao wa Upanga wamekiri kukata miti mingi ili popo hao waondoke lakini bado wameendelea kusalia maeneo hayo.
Sababu kubwa za binadamu kuwabugudhi ni kama zilivyotajwa hapo awali, ikiwemo Imani za kishirikina, kuwaona ni wachafuzi, kuwafanya kitoweo au kuwaona wanaleta magonjwa na uharibifu mashambani. Mbali na binadamu, popo pia huwindwa na ndege wala nyama kama bundi na tai. Uhalisia ni kwamba maisha ya binadamu na baadhi ya viumbe wengine huenda yakawa na changamoto sana endapo popo watatoweka. Idadi ya wadudu waharibifu na waletao magonjwa itaongezeka kwa kasi mno, huku pia ueneaji wa miti ya asili ya matunda katika maeneo mbalimbali utaathirika. Kufahamu mengi kuhusu popo soma zaidi makala hii Zijue Jamii Mbalimbali za Popo, Tabia, Maisha Yao na Umuhimu Wake Katika Uhifadhi
Popo wakijihifadhi maeneo ya wazi baada ya mazingira yao kuharibiwa. Hii huhatarisha usalama wao kwani maadui huweza kuwapata kwa urahisi
Makala hii imeandaliwa na Ezra Mremi na kuhaririwa na Hillary Mrosso. Kwa maoni, ushauri, maswali na mapendekezo kuhusu makala hii unaweza kuwasiliana na mwandishi wa makala hii.
Ezra Peter Mremi- 0786078728/0756438692
Email: mremiezra@gmail.com