Habari rafiki, karibu tena leo kweye makala hii inayohusu ujenzi wa miundo mbinu ndani ya maeneo yaliyo hifadhiwa. Kuna makala moja nilieleza jinsi maisha na taratibu ndani ya hifadhi zilivyo, nikasema kila kitu ndani ya hifadhi kinaendeshwa na sharia za asili. Kwa hiyo tunapojifunza mambo ya uhifadhi wa wanyamapori tunajifunza jinsi mambo yanavyoendeshwa ndani ya hifadhi kwa sharia za asili ambazo wanyama na viumbe hai wengine wanazifuata. Hivyo basi tunapotaka kuingia na kujenga nyumba, barabara au miundombinu mingine katika maeneo haya hatuna budi kuwa na uelewa wa namna ya kujenga majengo hayo yasije yakawabugudhi wanyamapori au kuharibu tabia zao.

Kuna watu wanaangalia majengo na miundombinu ilivyojengeka ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa na kuona kama ndio fasheni fulani hivi, au ni watu tu wameamua kujenga kwa namna hiyo. Hayo majengo na yote yanayojengwa ndani ya hifadhi huwa yanajengwa kwa kufuata sharia za asili za wanyama. Huwezi kujenga hifadhini kama unavyojenga nyumbani au kwenye maeneo mengine ambayo siyo ya hifadhi. Ndio maana utakuta hata uwe na fedha kiasi gani huruhusiwi kujenga maghorofa ndani ya hifadhi, hairuhusiwi kabisa, kila kitu kinafanyika ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa kwa lengo moja tu, kuhakikisha usalama na kuendelea kuwepo kwa wanyamapori hao kwenye eneo hilo bila kuwasumbua.

Majengo mengi ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa huonekana nadhifu na yenye mvuto kwa watu wengi, na wageni hupenda sana majengo ya namna hii ambayo ni rafki kwa wanyama na viumbe ahai wengine. Majengo hayo hujengwa kwa kutumia vitu vya asili ambavyo ni rafiki kwa wanymapori. Ndio maana utakuta mabanda yaliyojengwa vizuri kwa miti mizuri na juu huezeka nyasi ili kutobadilisha mazingira hayo kwa wanyama.

Wanyamapori kama tembo na wengine wengi huwa wanaadhiriwa na vitu vinavyo ng’aa hii ni tabia ya asili kwa wanyama wengi, hivyo ndio maana huwezi kukuta watu wanajenga nyumba za bati, au mabati yanayong’aa ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa. Hii ndio sababu ukitaka kujenga ndani ya hifadhi kama mwekezaji lazima uwasiliane na uongozi mzima wa mamlaka ya hifadhi, kuna sharia na masharti ambayo lazima yafuatwe na wanaotaka kujenga ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa.

Vile vile katika maswala yote ya ujenzi ndani ya hifadhi wanazingatia sana maeneo maalumu ambayo sio makazi ya kudumu ya viumbe hai, mfano labda unataka kujenga sehemu ambazo ndio makao makuu ya wanyamapori kama simba, fisi au mbwa mwitu, huwezi kuruhusiwa kujenga kwenye maeno kama hayo hata kama ni mazuri kiasi gani. Pia huwa kuna watalamu wa mambo ya mazingira lazima waje wafanye ukaguzi na mambo mengien mengi ili kuhakikisha majengo na miundombinu mingine haiwaathiri wanyama.

Vile vile hata suala la miundombinu ya barabara ni la kuzingatia sana kwani, huwezi kukuta barabara za ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa zimejengwa kwa lami, hii ni kwasababu ya kufuata sharia za asili za mazingira na wanyama au viumbe hai wote. Hakuna kitu kinafanyika ndani ya maeno yaliyohifadhiwa bila kuwepo kwa makubaliano na uelewano wa kutosha kwa mamlaka zote muhimu katika maeneo yote yaliyohifadhiwa. Vile vile kwa kuzingatia sana sharia mbali mbali za wanyamapori mambo yote yanatakiwa kufanyika bila kukiukwa kwa sharia hizi za wanyamapori.

Pamoja na hayo yote, bado sharia ni kali sana kwa uanzishwaji wa viwanda ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa, kuna maeneo yaliyohifadhiwa au yaliyopo ndani ya hifadhi na yana utajiri mkubwa wa madini au gesi asilia ambayo ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi. Hivyo endapo mtu anataka kueweka kiwanda au mitambo ya uchimbaji wa madini hayo au rasilimali hizo ambazo zipo chini ya ardhi lazima mambo mengi ya msingi yafuatwe, na pia sio rahisi wala haiwezi kuwa rahisi hata kidogo. Kwa sababu kunatakiwa kuwe na uchunguzi na tafiti nyingi za kutosha kuhusu madhara ya ujenzi wa viwanda ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa. Ndio maana hata serikali yenyewe ikiridhia uchimbaji wa madini au rasilimali nyingine ndani ya hifadhi bado kutakuwa na maoni na kutokukubaliana kwa wadau wa utunzaji wa mazingira na wanyamapori. Ndio maana hata kama itaruhusiwa kuendesha shughuli hizi ndani ya hifadhi inatakiwa ifanyike kwa makini na uangalizi mkubwa sana. Kwani unaharibu kabisa makao ya wanyamapori, unaharibu pia hata tabia za wanyapori, na pia hata kutishia uhai wa viumbe hai. Ni jambo zito sana, na kama halina maslahi mapana na ya muda mrefu kwa nchi ni bora likaachwa kabisa jambo hili.

Tunaweza kuona majadala unavyoendelea kwa Pori la Akiba la Selous, jinsi serikali inavyotaka kuweka mitambo ya kuzalisha umeme ndani ya eneo hili ambalo limetajwa na shirika la UNESCO kuwa ni moja ya eneo la uridhi wa dunia. Eneo hili la Selous ndilo lenye idadi kubwa sana ya tembo na wanyama wengine kama vile simba wanapatikana sana hapa, ni kati ya maeneo makubwa sana yaliyohifadhiwa na yenye wanyama wengi, ambao wapo hatarini kutoweka.

Ahsante sana kwa kusoma makala hii, karibu tena Kesho tujifunze zaidi hapa hapa, usisahau kumshirkisha mwenzio maarifa haya.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

0742092569/0683248681

hillarymrosso@rocketmail.com