Habari rfiki yangu katika uhifadhi wa wanyampori, karibu tena leo tuweke jicho letu kwenye wanyamapori hawa wanaoelekea kupotea kwenye uso wa dunia. Naamini umewahi kusikia kuhusu Mbwa mwitu, au kama hujasikia basi fuatana nami kwenye makala hii fupi ili nikujuze historia na mwenendo wa wanyama hawa walioadimika kwa miaka ya hapa karibuni. Historia inaonyesha wanyama hawa walipoanzia walipo, na wanakoelekea. Kwa taarifa ya tafiti mbali mbali kuhusu wanyama hawa inaonyesha kuendelea kupungua kwa kasi sana idadi ya wanyama hawa. Ni ukweli usiopingika kwa watu wengi wanaofanya kazi kwenye sekta hii ya wanyamapori kwamba inaweza kupita hata miezi na masiku yake hawajawaona wanyama hawa kwenye hifadhi. Hii ndio sababu iliyonisukuma kukaa chini na kuandaa makala hii ili tujue kwa uchache kinachoendelea kuhusu wanyama hawa.
Historia inaonyesha kuwa mbwa mwitu walienea na kuwapo kwa wingi sana Kusini mwa Jangwa la Sahara kuliko sehemu nyingine yoyote ile duniani, maandiko mengi na tafiti nyingi zinasema sehemu za Kusini mwa Jangwa la Sahara ndio ilikuwa maeneo mazuri ya wanyama hawa adimu, lakini pamoja na kwamba maeneo hayo ndio yalikuwa mazuri na yanayowafaa sana mbwa mwitu, bado kumekuwa na changamoto sana kwa upatikanaji wake sehemu hizo. Hii ni kutokana na mitazamo ya watu wengi kuhusu wanyama hawa wazuri.
Mbwa mwitu ni wanyama wanaokula nyama, na pia ni wanyama ambao hupenda kuishi kwa makundi, makundi yao hufika hadi 20, 40 na hata unaweza kuwakuta 60. Mitazamo mibaya juu ya wanyama hawa ilisababisha kuuliwa kabisa huko Afrika Magharibi, na kupungua kwa kasi sana maeneo ya Kaskazini Mashariki mwa Afrika. Kwa hali hii sehemu iliyobaki kuwa na idadi kubwa ni Kusini mwa Afrika kwa nchi za Botswana, Magharibi mwa Zimbabwe na Mashariki mwa nchi ya Namibia na pia kwa nchi za Kusini mwa nchi za Afrika Mashariki ambazo ni Tanzania na Kaskazini mwa nchi ya Msumbiji.
Mbwa mwitu ni wanyama waliowekwa kwenye mstari mwekundu na shirika la kimataifa linaloshughlikia viumbe hai walio hatarini kutoweka kabisa, shirika hili maarufu linalojulikana kama ICUN (International Union for Conservation of Nature). Hawa ni wanyama waliohatarini zaidi kutoweka katika uso wa dunia.
Pamoja na kwamaba mbwa mwitu wnapatikana sana sehemu hizo za Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa nchi nilizotaja hapo juu, bado kumekuwa na changamoto nyingi sana zinazowakabili wanyama hawa wanao vutia sana. Kutokana na mfumo wa maisha wa wanyamapori hawa kupenda kuishi sehemu zenye eneo kubwa sana na hupenda kutembea na kuhama hama, hupelekea matatizo na kutishia uhai wao kwenye maeneo ya watu. Ndio maana kwa hapa Tanzania sehemu zenye mbwa mwitu ni lazima ziwe na maeneo makubwa, kama ni hifadhi lazima iwe kubwa sana, mfano hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Pori la Akiba la Selous na hifadhi ya Taifa ya Serengeti ndio maeneo yanayoripotiwa kuwa na idadi inayoonekana ya wanyama hawa.
Kwa mwenendo ulivyo kwa nchi zetu, inatakiwa kuwepo kwa elimu ya kutosha pamoja na kila juhudi inayopelekea kuwepo kwa wanyamapori hawa. Wanyama hawa wanafaida kubwa sana, na uwepo wao kwenye hifadhi yoyote ni dalili nzuri ya utunzaji wa hifadhi na mazingira yote yanayowafaa wanyama hawa. Tafiti za kiikologia zinaonyesha kwamba kuharibika kwa makazi au mazingira ya wanyama hawa ndio tishio la mbwa hawa kuhama na kutafuta eneo jingine lenye utulivu ambalo halijaguswa kabisa na shughuli za kibinadamu, yani wanyama hawa wanapenda maeneo yaendelee kubakia katika uasili wake. Endapo mabadiliko hata kidogo yatatokea kwenye makazi ya wanyama hawa basi huhama na kwenda sehemu nyingine nzuri.
Jitihada za makusudi zinahitajika sana kwenye hili suala la uhifadhi wa wanyamapori kama mbwa mwitu ambao wamekuwa kivutio kwa watu wengi sana, endapo itajulikana eneo lina mbwa mwitu, basi utaona watafiti kutoka nchi mbali mbali wakija na kufanya tafiti zao za kisayansi kuhusu wanyama hawa, pia kwa wageni ambao ni watalii wanatoa fedha nyingi sana kwa ajili ya kuja kuwaona wanyama hawa adimu sana. Sehemu zote ambazo wanyamapori hawa wameondoka au wametoweka ni kutokana na uharibifu wa mazingira na kukosekana kwa uelewa wa kutosha kuhusu faida za wanyamapori hawa.
Leo nimeamua kuandika kwa ujumla kuhusu mbwa mwitu, ila kadri siku zinzvyokuja nitaelezea kwa undani tujue mfumo mzima wa wanyamapori hawa. Hivyo usiache kufuatana nami kwa makala zijazo. Mshirikishe na mwenzako makala hii kwa kumtumia link ya makala hii, ili kila mmoja wetu apate uelewa na ufahamu kuhusu mbwa mwitu. Kwa pamoja tunaweza kuwahakikishia mbwa mwitu kuwa Tanzania ni sehemu yao salama ya kuendelea kuishi na kuwepo.
Ahsante sana kwa kusoma makala hii
Hillary Mrosso
0742092569/0683248681