Habari rafiki yangu, karibu kwenye makala nyingine ya leo ambayo itatuwezesha kuwa na maarifa ambayo ni muhimu sana kwenye uhifadhi wa wanyamapori. Wanyamapori kama ilivyo sekta nyingine yoyote inahitaji ukuaji na maendeleo kwenye mambo yote muhimu. Makala hii itatusaidia kuchukua hatua mbali mbali ili kuboresha kazi zetu na majukumu yetu mengine ya kila siku. Naamini kwenye kujifunza na kushirikishana maarifa na uzoefu mbali mbali tunao upata kwenye sekta hii utaboresha zaidi kazi zetu.
Kutokana na changamoto iliyopo kwenye maeneo haya ya uhifadhi wa wanyamapori, hasa kwa watu wanaoishi karibu na hifadhi au maeneo yaliyohifadhiwa yanaumiza sana vichwa vya watu wengi kwenye sekta hii. Tunataka wanyama waendelee kuwepo lakini pia tunataka jamii ipate faida kutoka kwenye maeneo waliyopo, tunapenda wanyamapori wasiuwawe lakini pia wanyamapori hao hao wanasababisha hasara kubwa sana kwa wafugaji na wakulima walio kando kando ya maeneo haya yaliyohifadhiwa, ambao wanaharibiwa mifugo na mazao yao kuliwa na wanyamapori.
Kwa sababu changamoto hii sio ya nchi moja, kwa Afrika hii ndio changamoto kubwa kwa wanaofanya kazi kwenye sekta hii. Pamoja na njia mbali mbali kutumika kupunguza hali hii, bado kuna sehemu nyingi hasa hapa Tanzania zina migogoro hii ya wanyamapori na watu wanaoishi karibu na maeneo yaliyohifadhiwa. Bado kuna maeneo mengi watu wanalalamika kuhusu hali hii ya wanyamapori kuua mifugo yao, na kuharibu mazao yao. Kwa watu waishio karibu na hifadhi ya Taifa ya Ruaha wanajua jinsi wanavyo anathiriwa na changamoto hii kwenye maeneo yao.
Kutokea kwa mambo haya ni kwa sababu ambazo hatukuzichukulia kwa makini miaka ya nyuma, na kuna mambo ambayo tunayafumbia macho ambayo sasa yanatugharimu sana. Kuna mambo ya ardhi, mipaka, mito ya maji, kuna maeneo ya malisho yanatakiwa kuangaliwa kwa upya, pia hata idadi ya wafugaji kwenye eneo hili lenye migogoro ya mara kwa mara linatakiwa kuangaliwa upya. Kwa mfano huku Ruaha kumekuwa na ujio wa wafugaji wapya wanaotoka maeneo mbali mbali wanakuja wakiwa na mifugo mingi, huja na kuomba kuishi maeneo ambayo yapo karibu na hifadhi, na wengi wamekubaliwa kuja kuishi kwenye maeneo haya.
Kutokana na hali hii ya wafugaji kuhama hama wakiwa na mifugo yao ili kuja kuishi karibu na maeneo yaliyohifadhiwa ni jambo ambalo siku za baadaye litatusumbua sana, na kama unavyojua wafugaji huwa wanatabia ya kuitana, kwa hiyo kwa muda mfupi utakuta kijiji au eneo hili limejaa wafugaji wengi na pia mifugo yao itazaliana na kuongezeka, wao wenyewe wataongezeka na kusababisha idadi kubwa ya watu kuishikwenye maeneo haya, pia wataamua kujishughulisha na shughuli nyingine kama vile kilimo ambacho nacho kitakuwa na athari kwenye mazingira. Na kutokana na uelewa mdogo walio nao jamii hizi hasa kwenye utunzaji wa mazingira, basi wataharibu mazingira kweli kweli. Hapo ndipo tunaanza tena kutafuta mchawi.
Tunatakiwa kujifunza kwa yanayotokea na yaliyotokea, pia tunatakiwa kujifunza kwa wenzetu wanaofanya shughuli kama zetu, hapa namaanisha tujifunze kutoka kwenye hifadhi nyingine ambazo zina kabiliana na changamoto kama hii ya watu na wanaoishi kando ya hifadhi, tujifunze mbinu zao na pia tuwe wabunifu ili kuboresha mazingira ya wanyamapori.
Napongeza serikali na wadau wengine kwenye sekta hii kwa mikakati ambayo mnaendelea kuiweka ili kuboresha hifadhi zetu na watu wanaoishi kando ya hifadhi wawe na maisha mazuri. Kuna mashirika mengi sana yanafanya vizuri, kuna miradi mingi sana inafanya vizuri ili kupunguza changamoto hii, tuwaunge mkono na tushirikiane nao, pia tuwe na utaratibu wa kwenda kutembelea hata hifadhi na miradi mingine kwa lengo la kujifunza na kupeana uzoefu. Hili ni jambo ambalo linatakiwa kufanyika mara kwa mara kwa weledi na umakini mkubwa ili kuboresha hifadhi zetu, hatuwezi kufanya uhifadhi peke yetu, tunahitaji ujuzi, juhudi na maarifa ya kila mmoja wetu kwenye sekta hii hata kama ni kwenda nchi za mbali kujifunza na kupeana uzoefu bado hili litakuwa ni jambo jema ili kunusuru maisha ya watu na wanyamapori wetu.
Ahsante sana kwa kusoma makala hii;
Hillary Mrosso
07420925689/0683248681