Biashara haramu ya nyara za wanyamapori imeshamiri sana katika miongo ya hivi karibuni. Biashara hii imetajwa kuwa ndio biashara inayoshika nafasi ya tatu kwa kuingiza mapato mengi kwa njia haramu baada ya biashara ya madawa ya kulevya na silaha. Inakadiriwa kuwa, biashara haramu ya wanyamapori na nyara zake inaweza kufikia dola za kimarekani bilioni 5 hadi bilioni 20 kwa mwaka. Kutonana na faida kubwa inayopatikana kwenye biashara ya nyara za wanyamapori, watu wengi na vikundi vya kihalifu vimeingia kwenye biashara hii na kuchochea ongezeko la kupungua kwa idadi kubwa ya wanyamapori kwenye maeneo mengi duniani.
Picha hii imepigwa na Mwangi Kimenyi, ikionyesha meno ya tembo, ambayo ndio yanahusika kwenye biashara haramu
Kwa mujibu wa sheria ya uhifadhi wa wanyamapori Tanzania namba 5 ya mwaka 2009, nyara maana yake ni kila sehemu ya mwili mnyamapori aliye hai au aliyekufa, inaweza kuwa ni pembe, meno, kucha, ngozi, magamba, nyama, mifupa, kwato, mafuta, damu, manyoya, mayai, na pia inaweza kuwa ni nyara zilizotengenezwa au kuchakatwa viwandani (manufactured trophy). Hivyo endapo mtu atapatikana na moja wapo ya nyara hizo zilizotajwa hapo juu bila kibali atakuwa amefanya kosa, pia anaweza kwenda jela au kulipa faini au vyote kwa pamoja. Soma zaidi hapa Zifahamu Nyara Za Serikali Kwa Kina (Government Trophies)
Pamoja na hayo, sheria hii pia inatoa ruhusa na vibali kwa watu kumiliki baadhi ya nyara. Hivyo, kama unapenda kumiliki nyara za wanyamapori unaweza kuwasiliana na mamlaka husika na kupeleka maombi yako ili upewe kibali cha kumiliki nyara unazotaka. Ikumbukwe kuwa, nyara zote za wanyamapori ni mali ya serikali kwa mujibu wa sheria ya uhifadhi wa wanyamapori Tanzania. Endapo utafanya kinyume na utaratibu huo, utakuwa umefanya kosa kwa mujibu wa sheria hii. Soma zaidi makala hii Tishio Kubwa Kwa Wanyamapori Na Mazingira Tanzania
Mara zote ujangili kwa ajili ya nyara za wanyamapori umekuwa ukilenga wanyamapori wenye thamani kubwa kama vile tembo, faru, simba, chui milia (tiger), kakakuona nk. Wanyama hawa wamekuwa na matumizi makubwa sana sehemu nyingi duniani hasa katika nchi za Asia kama vile China. Hivyo, kutokana na mahitaji kuwa makubwa katika sehemu hizo, imepelekea kushamiri kwa ujangili na biashara haramu ya meno ya tembo na wanyama wengine ili kukidhi mahitaji ya nchi za magharibi na mashariki ya mbali. Soma zaidi kwenye makala hii Nyamapori Bado ni Sehemu Muhimu ya Mlo wa Jamii Nyingi za Watu Zinazoishi Karibu na Maeneo ya Hifadhi za Wanyamapori
Biashara hii ya nyara za wanyamapori imepelekea kupungua kwa idadi kubwa sana ya wanyamapori muhimu kama tembo. Mfano, utafiti uliofanyika hivi karibuni (2023) na Timothy Kuiper na wenzake unaonyesha tembo wamepungua kwa asilimia 30 tangu mwaka 2006. Katika utafiti huo uliofanyika katika vituo 64 kwenye nchi 30 za Afrika umeainisha sababu za kupungua kwa tembo maeneo mengi, na sababu kubwa ikiwa ni kushamiri kwa biashara ya meno ya tembo, umasikini, rushwa, kukosekana kwa usimamizi imara kwenye maeneo ya wanyamapori.
Kupungua kwa tembo katika maeneo yao kuna madhara makubwa sana kiuchumi, kiikolojia na kisiasa. Mfano, kupungua kwa tembo kunasababisha kuyumba na kuharibika kwa mifumo mingi ya kiikolojia ambayo inapelekea madhara kwa vimube hai wengine kama vile wanyama na mimea. Pia kupungua kwa tembo kunasababisha upungufu wa shughuli za utalii hivyo kupelekea kushuka kwa pato la taifa. Tembo Kupungua au kutoweka kwenye maeneo yao itasababisha maeneo hayo kuvamiwa na kuwa mashamba au makazi ya watu, hivyo kusababisha kukosekana kwa maeneo muhimu ya hifadhi ya wanyama na mimea.
Licha ya uwepo wa sheria za ndani na mashairika yanayosimamia biashara halali za wanyamapori na nyara zake kama vile Shirika la Kimataifa linalosimamia Biashara za Spishi Mwitu za Wanyama na Mimea ambayo ipo hatarini kutoweka, kama inavyojulikana kwa kingereza “Convention on International Trade in Endangered Species of Wild Fauna and Flora” (CITES), bado biashara haramu ya nyara za wanyamapori ni tishio kubwa kwenye uhifadhi wa wanyamapori. Wadau wengi wa uhifadhi wamekuwa wakitoa maoni na malalamiko yao kuhusu uwezo wa CITES katika kutimiza majukumu yake kikamilifu, wengi wanapendekeza kuwa na maboresho ya vipengele ili kupunguza kushamiri kwa biashara haramu za wanyamapori. Unaweza kusoma makala hii zaidi Ifahamu Biashara Ya Nyara Inavyoendeshwa Kisheria
Kutokana na kasi ya ujangili kwenye maeneo mengi duniani, ni vizuri kukafanyika tafiti za mara kwa mara kwa wanyamapori na mimea. Hii ni kutokana na wanyama wengi wanawindwa na kuuwawa kila siku, lakini wanyama hao hawatambuliwi na CITES kama wapo katika hatari ya kutoweka kutokana na shughuli za ujangili ambazo zinafanyika kwa usiri mkubwa. Hata hivyo, taarifa za ujangili ni ngumu kupatikana hali inayopelekea wasiwasi kuwa wanyama wanaowindwa kwa ujangili ni kubwa kuliko inavyotazamiwa na wengi.
Katika mapendekezo aliyoyatoa Timothy na timu yake, wamependekeza kuwepo kwa miradi na namna nyingine ya kutatua tatizo la umasikini kwa jamii ambazo zinategemea rasilimali za wanyamapori kuendesha maisha yao. Rushwa ni tatizo jingine ambalo linatakiwa kutatuliwa haraka maana imechangia usimamizi wa wanyamapori kuwa dhaifu na kutoa nafasi kwa ujangili na biashara haramu kushamiri.
Asante sana kwa kusoma makala hii, usiache kuwashirikisha wengine makala hii ili nao wajifunze na kwa pamoja tushiriki katika kupiga vita ujangili na biashara haramu ya wanyamapori na nyara, ili wanyamapori wetu waendelee kuwepo na kutunufaisha kizazi cha sasa na cha baadaye. Chukua hatua!
Imeandikwa na;
Hillary Mrosso, hmconserve@gmail.com +255 0683 862 481