Habari wasomaji wa makala za wanyamapori, karibuni tuendelee na mwendelezo wa makala yetu ya orodha ya ndege wanaopatikana Tanzania pekee. Makala iliyopita tulijifunza aina 20 za ndege wanaopatikana Tanzania tu, kwasababu ya ukubwa na urefu wa makala ile tuliamua kuivunja ziwe makala mbili, zenye sehemu ya kwanza na sehemu ya pili. Makala ya leo ni sehemu ya pili ya muendelezo wa makala iliyopita kuhusu ENDEMISM, au UENDEMIKI, au UKOMO, zote zikiwa na maana ya kuonyesha spishi za ndege wanaopatikana Tanzania pekee na sio nchi nyingine. Kama hukusoma makala ya sehemu ya kwanza hapaSEHEMU 1: Orodha ya Spishi za Ndege Wanaopatikana Tanzania Pekee. Karibuni tuendelee na makala hii tujifunze pamoja.

21.Kokoko wa Usambara (Usambara Eagle Owl)

Hawa ni jamii ya kokoko wakubwa ambao wana rangi ya kahawia sehemu ya chini ambayo imefunikwa na rangi ya kahawia iliyo kolea na maziwa sehemu ya chini pia. Wana madoa ya rangi ya kahawia sehemu ya kifuani na ufito usio wa kawaida wenye rangi nyeusi sehemu ya tumboni. Paji la uso lina rangi ya mchanga ulio pauka yenye ukingo mpana na mweusi pembeni. Midomo yao ina rangi ya bluu na weupe, Macho yao yana rangi ya njano mchanganyiko na ya machungwa na kope zenye rangi ya bluu na nyeupe, miguuni na kwenye vidole wana rangi ya nyeupe.

Ndege hawa wanapatikana sana kaskazini-mashariki mwa milima ya Usambara. Baadhi ya tafiti zilizo fanyika hivi karibuni zimeonesha kuwa ndege hawa wanapatikana pia katika milima ya Uluguru na kuna uwezekano wakawa wanapatikana katika milima ya Nguru. Kokoko hawa wanapatikana maeneo yenye muinuko kati ya mita 900-1,500 kutoka usawa wa bahari. Idadi halisi au makadirio ya idadi ya ndege hawa bado haijajulikana kwa kina.

Shirika la IUCN limewaweka ndege hawa kwenye kundi la viumbe ambao wapo kwenye tishio kutokana na kupungua kwa ndege hawa. Moja ya sababu ambayo inapelekea ndege hawa kupungua ni uharibifu wa mazingira hasa ukataji wa miti ambao unasababisha kupotea kwa makazi ya kokoko hawa.

Kokoko wa Usambara (Picha na eBird)

22.Hondohondo wa Ruaha (Tanzania Red-billed Hornbill)

Hawa ni miongoni mwa hondohondo ambao ni wadogo na wembamba. Wana midomo iliyo jikunja yenye rangi nyekundu inayo ng’aa huku nchani ikiwa na alama ndogo yenye rangi ya machungwa iliyofifia na weusi kwenye taya ya chini. Macho meusi ambayo yana duara la ngozi nyeusi na mgongo wenye madoa madoa mengi. Shingo na maeneo ya tumboni wana manyoya yenye rangi ya kijivu na nyeupe kama walivyo hondohondo wengine. Manyoya ya mkiani ni marefu yenye rangi nyeusi upande wa juu na nyeupe upande wa chini.

Hondohondo hawa wanapatikana sana maeneo ya kati nchini Tanzania na mara nyingi maeneo haya huwa ni ya savana au misitu ambayo chakula cha ndege hawa kinapatikana kwa urahisi. Moja ya sehemu ambazo utaweza kuwaona ndege hawa kwa urahisi ni ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Taarifa za kina kuhusu ndege hawa bado pia zinaendelea kutafutwa kwani bado pia hawajaingizwa kwenye shirika la IUCN kwa maelezo zaidi.

Hondohondo wa Ruaha (Picha na NatureRules1)

23. Kibwirosagi wa Rubeho (Rubeho Warbler)

Madume wana ukosi wenye rangi ya kahawia, rangi ya kijivu sehemu ya chini huku sehemu ya mabawa na kwenye mkia wana rangi nyeusi. Kicwani, usoni, taji, mashavu, shingoni na sehemu ya kifuani kwa juu wana rangi ya uchafu iliyo kolea.Wana midomo myembamba ambayo imechongoka na yenye rangi nyeusi. Wana macho ya kahawia huku miguu na vidole vina rangi ya kijivu ambayo inataka kufanana na rangi nyeusi.

Ndege hawa wanapatikana maeneo machache sana na hasa maeneo ya katikati mwa nchi hapa Tanzania. Maeneo hayo ni sehemu ya juu kabisa ya milima ya Ukaguru na katika msitu wa Ukwiva katika milima ya Rubeho. Maeneo haya yana misitu yenye unyevu wakutosha na yenye mimea iliyo stawi kwa kufunfana sana. Kibwirosagi hawa wanaonekana sana maeneo yenye muinuko kati ya mita 1,300-1,900 kutoka usawa wa bahari.

Kibwirosagi wa Rubeho ni ndege ambao hawazungumziwi sana kwasababu bado hawajafanyiwa sana tafiti na shirika la kimataifa la maisha ya ndege. Ndege hawa wana athiriwa sana na kuharibiwa kwa mazingira yao ambao unatokana na ongezeko la watu, ukataji wa misitu lakini pia uchomaji wa misitu kwa ajili ya kutanua maeneo ya kilimo.

Kutokana na kupungua kwa ndege hawa, wataalamu wa masuala ya ndege wanapendekeza ndege hawa waingizwe kwenye kundi la viumbe waliyo hatarini kutoweka duniani au kundi la viumbe ambao wanakaribia kuwa tishio kutoweka duniani.

Kibwirosagi wa Rubeho (Picha na eBird)

24.Chozi wa Hofmann (Hofmann’s Sunbird)

Kama zilivyo spishi nyingi za chozi, chozi hawa pia madume na majike wanatofautiana sana hasa mpangilio wa rangi kwenye miili yao. Madume wana rangi ya kijani ya zumaridi kichwani, kifuani na sehemu ya juu ya mgongoni. Mkiani, tumboni na kwenye mabawa wana rangi ya kahawia iliyo fifia na mstari mwekundu sehemu ya kifuani. Majike wana rangi ya kijivu iliyo changanyikana na kijani sehemu ya juu huku sehemu ya chini wakiwa na rangi ya njano iliyo changanyikana na kijivu na mstari mweusi hasa sehemu ya kifuani. Mikia na mabawa ya majike huwa na rangi ya kahawia iliyo fifia.

Ndege hawa wanapatikana sana maeneo ya mashariki mwa Tanzania. Maeneo hayo huwa na sifa yakuwa na miti mingi, mapori na bustani ambayo yanapatikana katika muinuko kati ya mita 500-1,200 kutoka usawa wa bahari.

Ndege hawa hawafahamiki sana na watu wengi, pia hata shirika la IUCN halija waingiza ndege hawa kwenye mfumo wao wa kanzidata hivyo inakuwa vigumu kujua idadi yao na kundi la kuwaweka kwa kuzingatia hali zao.

Chozi wa Hofmann (Picha na Holmen Birding Safaris)

25.Kwera wa Ruvu (Ruvu Weaver)

Jamii hii ya kwera, madume huwa na rangi ya njano inayong’aa, uso huwa na rangi ya machungwa iliyo changanyikana na nyekundu na macho yao huwa na rangi ya kahawia iliyo fifia. Majike huwa na rangi ya kufifia zaidi, mstari wa kahawia sehemu ya mgongoni na uliyo pauka chini, macho meusi na mdomo ambao una rangi nyeusi nusu, na rangi ya pinki nusu.

Ndege hawa wanapatikana maeneo ya mashariki mwa Tanzania ambayo ni mto Ruvu, mto Wami na bonde la mto Rufiji. Japo tafiti zinaonesha kuwa kuna baadhi ya makundi ya ndege hawa huwa kwa mara chache wanaonekana pia mkoani Morogoro.

Idadi kamili ya ndege hawa pia haijajulikana japo inasemekana wanendelea kupungua siku baada ya siku kutokana na uharibibu wa mazingira yao na makazi. Hali hii inasababisha kupungua kwa kasi ya kuzaliana kwa kwera hawa kitu ambacho kama hali ikizidi huenda ndege hawa wakawa hawapatikani kwenye baadhi ya maeneo ambayo kwasasa wanapatikana wa kutosha.

Kwera wa Ruvu (Picha na eBird)

26.Kwale wa Udzungwa (Udzungwa Forest Partridge)

Wana migongo yenye rangi ya kahawia na sehemu ya chini wana rangi ya kijivu yenye makokwa. Midomo yao  ina rangi nyekundu, mboni za kahawia na miguu yao ina rangi ya njano. Kwale hawa majike na madume wana fanana sana hivyo ni vigumu kuwatofautisha kwa mbali au hata kwa kuwasogelea karibu kama mtu sio mtaalamu wa ndege.

Ndege hawa wanapatikana nyanda za juu za Udzungwa na misitu inayopatikana katika muinuko wa Chugu kaskazini mwa milima ya Rubeho. Ni miongoni mwa jamii za ndege ambao wanaishi sehemu moja tofauti na ndege wengine ambao wanaishi kwa kuhama hama. Maeneo ambayo wanapatikana ndege hawa huwa na muinuko kati ya mita 1,300-2,400 kutoka usawa wa bahari.

Tafiti zilizo fanyika mwaka 2021 na IUCN zinaonesha idadi ya ndege hawa ni kati ya 2,000-2,700 na idadi hii inaonekana kupungua kwa kasi sana kutokana na sababu mbali mbali. Kutokana na takwimu hizi ndege hawa wameingizwa kwenye kundi la viumbe ambao wanakaribia kutoweka duniani.

Miongoni mwa sababu zinazo pelekea kupungua kwa kasi kwa ndege hawa ni uwindaji haramu kwani wamekuwa wakiwindwa sana kwa matumizi ya chakula na biashara. Sababu nyingine ni uvamizi wa watu kwenye maeneo ambao ni mazalia ya ndege hawa kusababisha ndege hawa kukosa maeneo tulivu kwaajili ya kuzaliana na uchomaji wa misitu.

Kwale wa Udzungwa (Picha na Pinterest)

27.Kereng’ende kidari kijivu (Grey breasted Francolin)

Hawa ni ndege wenye rangi ya kijivu na kahawia wenye ngozi ya rangi nyekundu shingoni na sehemu ya kuzunguka jicho. Wana midomo myekundu, miguu ya kijivu, ngozi nene na alama za madoa sehemu ya tumboni. Wana mabaka yaliyo pauka sehemu ya nje ya mabawa ambayo huonekana vizuri pale wanaporuka.

Ndege hawa wanapatikana maeneo mengi sana hapa nchini hasa maeneo yanayo patikana katikati mwa Tanzania. Idadi halisi ya ndege hawa pia haijulikani kwasababu ni ndege ambao wanapatikana maeneo mengi na wametawanyika sana. Mbali na kuwa wametawanyika maeneo mengi, lakini idadi ya ndege hawa inaonekana kupungua kutokana na changamoto mbali mbali ambazo zinawakumba ndege hawa kwenye makazi yao.

Moja kati ya changamoto kubwa kwa kereng’ende hawa ni uharibifu wa mazingira unao sababishwa na shughuli za kibinaadamu lakini pia watu wamekuwa wamevamia maeneo ambayo ndege hawa wanaishi.

Kereng’ende kidari kijivu (Picha na Wikipedia)

28.Ninga wa Pemba (Pemba Green Pigeon)

Hawa ni ndege jamii ya njiwa wenye maumbo ya kati wenye migongo yenye rangi ya zaituni na kijani, kichwa cha kijivu na sehemu ya tumboni pia wana rangi ya kijivu.

Jamii hii ya njiwa wanapatikana visiwani Pemba tu na hasa maeneo karibu na pwani za bahari kwenye matumbawe na maeneo ya umbali wa kilometa 55 kutoka pwani za kaskazini. Maeneo haya ambayo ni rahisi kuwapata au kuwaona ndege hawa huwa na muinuko wa mita kati ya 0-80 kutoka usawa wa bahari. Maeneo haya ni ambayo yana misitu, mashamba ya karafuu na bustani. Japo mazingira yao halisi ni sehemu zenye misitu asilia.

Kwa mara ya mwisho tafiti kuhusu ndege hawa zilifanyika mwaka 2021 na kuonesha idadi ya ndege hawa ni kati ya 2,500-9,999 lakini idadi hii inapungua sana. Kama ilivyo kwa jamii nyingine za viumbe wengi ambao ni wa ukomo, njiwa hawa wanaishi sehemu moja na sio kwa kuhama hama kama ndege wengine.

Kuna sababu nyingi ambazo zinachangia kupungua kwa kasi sana kwa ndege hawa. Miongoni mwa sababu hizo ni kuwindwa kama chakula kwa ngazi ya jamii hadi taifa kwa ujumla, uwindaji wa kitalii na pia uharibifu wa mazingira hasa maeneo ya misitu na kwenye mashamba ya karafuu.

Ninga wa Pemba (Picha na eBird)

29.Mtiti wa Pemba (Pemba Scops Owl)

Hawa ni mtiti wakubwa wenye muonekano wa kufifia na wenye Manyoya mafupi kwenye masikio. Sehemu ya chini wana rangi ya kahawia iliyo changanyikana na rangi ya uchafu. Wana mstari unaong’aa kichwani lakini pia sehemu ya chini unaweza kuuona mstari huo kuanzia maeneo ya kifuani. Wana midomo myeusi lakini macho na miguu ina rangi ya njano.

Mtiti hawa wanapatikana katika visiwa vya Pemba tu na ni umbali wa kilomita 55 kutoka fukwe za bahari. Japo wanapatikana katika maeneo mengi kisiwani humo, idadi yao kubwa wanapatikana sehemu mbili ambazo ni Msitu wa Ngezi wenye ukubwa wa kilomita za mraba 14 na Msitu Mkuu ambao una kilomita za mraba 3. Maeneo haya ambayo wanapatikana mtiti hawa yana muinuko wa mita kati ya 0-79 kutoka usawa wa bahari.

Utafiti wa mwaka 2016 katika visiwa vya Pemba kuhusu ndege hawa unaonesha kuwa idadi ya ndege hawa ambao wanaishi kwa jizi ni 1,500 na kwa wale ambao ni wakubwa lakini hawajaanza kuzaliana wapo 3,000 ambapo kwa ujumla wanakuwa mtiti 4,500. Idadi hii inapungua kwa kasi sana kutokana na kupungua kwa makazi ya ndege hawa ambao unasababishwa na maendeleo ya biashara ambayo watu wanajenga nyumba kwa kuharibu misitu, kilimo na ufugaji wa Samaki, uvunaji wa miti na ukusanyaji wa kuni, uvamizi wa spishi nyingine za kigeni katika mazingira wapatikanao mtiti haw ana mabadiliko ya tabia ya nchi.

Hii imepelekea shirika la IUCN kuwaingiza ndege hawa kwenye kundi la viumbe ambao wapo au wanaishi kwenye mazingira magumu.

Mtiti wa Pemba (Picha na eBird)

30. Zuwakuku wa Emin (Emin’s Barbet)

Ni ndege wenye vichwa vya njano vyenye madoa myeusi huku mbawa zao zikiwa nyeusi na madoa myeupe.Sehemu ya kifuani wana rangi ya njano na alama ya mstari mweusi uliyo katiza sehemu ya kifuani. Sehemu ya tumboni wana rangi ya njano iliyo pauka na kitako cha mkia kikiwa na mchano wenye rangi nyekundu.

Zuwakuku hawa wanapatikana maeneo mengi sana hapa nchini na hii ni kutokana na uwezo wa ndege hawa kutawanyika katika maeneo mbali mbali. Japo ndege hawa wametawanyika maeneo mengi lakini sio miongoni mwa jamii za ndege ambao wanaishi kwa kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Wanapendelea maeneo ya savana, maeneo yenye majani na vichaka ambayo yanakuwa kwenye muinuko wa mita 200-1,900 kutoka usawa wa bahari.

Idadi kamili au makadirio ya ndege hawa bado haijajulikana. Baadhi ya tafiti zinaonesha kuwa ndege hawa bado wanaonekana kwa wingi katika maeneo mbali mbali hasa maeneo ambayo ndege hawa wanapatikana kwa wingi. Kutikana na matikeo ya utafiti huu ndege hawa bado hawajawa kwenye kundi la viumbe waliyopo kwenye mazingira magumu na hivyo idadi yao na utawanyikaji wao ni wakuridhisha.

Zuwakuku wa Emin (Picha na iNaturalist)

31Zuwakuku mstari-mwepe (White-lined Barbet)

Zuwakuku hawa wana kichwa chenye rangi nyeusi sehemu ya juu, shingo nyeusi, macho meusi na mdomo mweusi. Sehemu ya masikioni wana alama nyeupe ambayo imeanzia nyuma ya jicho kuelekea upande wa nyuma mpaka karibu na mgongo. Migongo yao ina rangi ya kahawia, wana rangi nyeusi kwenye mikia na miguu huku sehemu ya tumboni wakiwa na rangi nyeupe. Kwenye kifua kuna mchanganyiko wa rangi nyeupe na kahawia ambayo inashabihiana na nyeusi.

Zuwakuku hawa pia wanapatikana maeneo mengi sana kama walivyo zuwakuku wa Emin. Ni ndege ambao wanapendelea maeneo ya misitu nae neo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 20,000. Maeneo ambayo ndege hawa wanapendelea huwa na muinuko wa mita 2,600 kutoka usawa wa bahari.

Mara ya mwisho utafiti kuhusu ndege hawa ulifanyika mwaka 2016 na shirika la IUCN na idadi kamili ya ndege hawa haikuweza kufahamika. Japo idadi yao inaonekana ni ya kuridhisha lakini inaonekana kupungua sana kutokana na sababu mbali mbali. Hivyo ndege hawa bado sio viumbe waliyopo kwenye mazingira magumu.

Moja kati ya sababu kubwa ambayo inapelekea idadi ya ndege hawa kupungua ni uondoaji wa miti iliyo dondoka na kuoza ambayo ni mahitaji muhimu sana kwa ndege hawa kwenye malazi na kutengeneza viota lakini pia hutumia miti hiyo kama sehemu ya mazingira ya kupumzikia.

Zuwakuku mstari-mwepe (Picha na Birds of the World)

32.Cherero Machungwa (Fischer’s Lovebird)

Cherero hawa wana rangi nyingi ambazo zimejipanga kwa kuvutia. Wana rangi ya kijani mgongoni, kifuani wana rangi ya nyano, usoni wana rangi ya machungwa na midomo yao ina rangi nyekundu.  Shingoni wana rangi ya dhahabu iliyo changanyikana na rangi ya njano na kadiri unavyosogea mbele rangi hii hubadilika na kuwa rangi ya machungwa iliyo fifia. Sehemu ya juu ya mkia huwa na rangi ya zambarau au bluu. Wana duara lenye rangi nyeupe ambalo limezunguka jicho.

Ndege hawa wanapatikana kaskazini na maeneo ya kati kati ya Tanzania ambapo historia yao inaonesha wanapatikana maeneo 14 ambayo kati yao maeneo matatu ni Hifadhi za Taifa. Ndege hawa hawaishi kwa kuhama hama na maeneo ambayo wanapatikana huwa na muinuko wa mita 1,100-2,200 kutoka usawa wa bahari.

Chapisho la mwisho kuhusu ndege hawa lilitoka mwaka 2021 na kuonesha kuwa idadi ya cherero hawa ni kati ya 290,000-1,002,000 huku idadi yao ikidhaniwa kupungua sana. Idadi ya ndege hawa inaonekana kupungua kuanzia myaka ya 1970 kutokana na sababu nyingi tu. Hali hii ilipelekea ndege hawa kuwa miongoni mwa viumbe ambao wanakaribia kuingia katika kundi la viumbe walio hatarini.

Miongoni mwa sababu zinazo pelekea kupungua kwa ndege hawa ni biashara ya ndege ambayo imekithiri. Mwaka 1987 hawa walikuwa ndege maarufu zaidi kwenye soko la biashara ya ndege duniani. Ndege hawa wamekuwa wakiuzwa sana na kutumika kama mapambo ndani ya majumba ya watu. Sababu nyingine ni kuzaliana kati ya ndege hawa na cherero shingo-njano ambapo wanazalisha spishi nyingine kabisa tofauti ya spishi yao.

Cherero Machungwa (Picha na eBird)

33.Cherero shingo-njano (Yellow-collared Lovebird)

Hawa pia ni jamii ya cherero ambao wana rangi za kuvutia. Wana migongo ya rangi ya kijani iliyo fifia sehemu ya juu ukilinganisha na sehemu ya chini mgongoni na vifua vyenye rangi ya njano. Kichwani na soni wana rangi nyeusi na midomo yao ina rangi nyekundu huku sehemu ya juu ya mdomo ikiwa n rangi nyeupe. Hawa pia wana duara lenye rangi nyeupe lililo zunguka jicho.

Jamii hii ya cherero wanapatikana maeneo mengi sana hapa nchini. Miongoni mwa maeneo ambayo ndege hawa wanapatikana kwa idadi kubwa kwa wanaonekana kwa urahisi ni maeneo ya mikoa ya kati kati mwa Tanzania mfano mkoa wa Singida. Ndege hawa wana uwezo wa kuishi katika mazingira tofauti na hii imewasaidia ndege hawa kuweza kutawanyika katika maeneo mbali mbali ya nchi. Maeneo ambayo wanapatikana sana ndege hawa huwa na muinuko kati ya mita 1,100-1,800 kutoka usawa wa bahari.

 Tafiti kuhusu ndege hawa zilifanyika na kuchapishwa mwaka 2018 na idadi yao haikiuweza kufahamika. Idadi ya ndege hawa inaonekana kuimarika kwa sababu mpaka sasa hakuna Ushahidi unaoonesha kuwa ndege hawa wanapungua ama kwa kuwindwa sana au kutokana na sababu mbali mbali.

Cherero shingo-njano (Picha na Tanzania Bird Atlas)

34. Tatata wa Reichenow (Reichenow’s Batis)

Hawa ni ndege wadogo na wenye mikia mifupi. Madume wana rangi ya kijivu sehemu ya mbele kichwani, taji, ukosi na joho. Wana mbawa zenye rangi nyeusi, zenye rangi ya kijivu nchani na mistari ya mbawa nyeupe iliyo jificha. Mpangilio huu unatengeneza herufi “V” ukimtazama ndege kwa upande wa nyuma. Mikia yao ina rangi nyeusi na alama nyeupe nchani. Sehemu ya chini wana rangi nyeupe ambayo kama ina mistari myeusi hasa eneo la kifuani. Wana barakoa nyeusi ambayo imezunguka jichoni mpaka kwenye masikio. Wana midomo myeusi, miguu na vidole vyeusi huku macho yao yakiwa na rangi nyekundu iliyo kolea sana. Majike wana rangi ya kijivu iliyo fifia kifuani na sehemu ya pembeni, maranyingi rangi ya uchafu shingoni na rangi ya kutu sehemu ya ubavuni. Wana barakoa nyeusi nyembamba, midomo myeusi, macho myeusi na rangi ya kijivu kwenye miguu na vidole.

Ndege hawa wana uwezo wa kutawanyika katika maeneo madogo sana. Ndege hawa wanapatikana kusini-mashariki mwa Tanzania katika hasa maeneo ya Mikindani na Lindi. Maeneo haya ni pwani zenye misitu ya nyanda za chini ambayo yanapatikana kwenye muinuko wa mita zisizo zidi 2,300 kutoka usawa wa bahari.

Utafiti wa mara ya mwisho kuhusu tatata hawa ulifanyika mwaka 2021 japo idadi yao haijafahamika. Mbali na idadi kuto fahamika, idadi ya ndege hawa inaonekana kupungua kutokana na shughuli za kilimo na ufugaji samaki ambao unapelekea kuharibiwa kwa mazingira ya mazalia na mapumziko ya ndege hawa. Hii imepelekea tatata hawa kuingizwa katika kundi la viumbe ambao wanakaribia kuwa tishio.

Tatata wa Reichenow (Picha na eBird)

35.Mbweta wa Uluguru (Uluguru Bush-shrike)

Huyu ni miongoni mwa mbweta wa ajabu mwenye mdomo mikubwa ambayo imejikunja kama ndoano nchani, kichwa cheusi, mgongo wa kijani na rangi ya njano sehemu ya chini.

Mbwata hawa wanapatikana katika milima ya Uluguru nchini Tanzania pekee. Maeneo halisia kabisa ya ndege hawa ni ndani ya kwenye eneo la Hifadhi Asilia ya Uluguru na maeneo machache kando kando ya eneo hili lililo hifadhiwa. Hawa ni ndege ambao pia wanaishi sehemu moja na sio kuhama hama. Ni jamii ya mbweta ambao maisha yao hutegemea uwepo wa misitu na hasa misitu yenye unyevu kipindi kirefu. Maeneo wapatikanayo ndege hawa huko milima ya Uluguru huwa na muinuko wa mita kati ya 1,100-1,950 kutoka usawa wa bahari.

Upembuzi yakinifu ulio fanyika mwaka 1999-2000 ulikadiria idadi ya ndege hawa kuwa 3,600. Baada ya hapo mnamo mwaka 2006-2007 na hatimae mwaka 2015, tafiti nyingine zilifanyika na kuchapisha kuwa idadi ya ndege hawa haijabadilika sana. Japo idadi inaonekana kuwa imara lakini ndege hawa ni miongoni mwa viumbe ambao wanakaribia kutoweka duniani kutokana na takwimu zilizo chapishwa na shirika la IUCN.

Miongoni mwa sababu ambazo zimekuwa tishio kwa mbweta hawa ni kilimo ambacho watu hulazimika kuharibu misitu na ukusanyaji kuni, uvamizi wa spishi nyingine za ndege kwenye mazingira halisi ya ndege hawa, vinasaba lakini pia magonjwa ya ndege.

Mbweta wa Uluguru (Picha na eBird)

36.Kucha wa Usambara (Usambara Hyliota)

Hawa ni spishi ya kucha ambao wana migongo yenye rangi ya bluu iliyo changanyikana na nyeusi, mbawa zenye alama nyeupe vifua vyenye rangi ya sufu iliyo pauka vyenye dalili ya rangi ya njano au machungwa. Wana mwako nuru mweupe ulio jitokeza kwenye mbawa zao.

Ndege hawa hawafahamiki sana. Kucha hawa wanapatikana katika milima ya Usambara tu. Na katika milima hiyo wanapatikana maeneo ya Magharibi na Mashariki mwa milima ya Usambara. Ndege hawa wanategemea sana misitu kama makazi yao na sehemu za kuzaliana na huishi sehemu moja bila kuhama hama. Maeneo ambayo wanapatikana ndege hawa katika milima ya Usambara yana muinuko wa kati ya mita 300-1,200 kutoka usawa bahari. Kwa Pamoja Mashariki na Magharibi mwa milima ya Usambara ndege hawa wanapatikana katika maeneo kati ya 2-5.

Idadi ya ndege hawa inakadiriwa kuwa kati ya 600-1700 kutokana na chapisho la shirika la IUCN la mwaka 2016 na idadi hii inaonekana kupungua sana katika maeneo hayo. Kutokana na takwimu hizi ndege hawa wameingizwa kwenye kundi la viumbe hai ambao wapo hatarini kutoweka duniani.

Changamoto kubwa ambazo zinapelekea idadi ya ndege hawa kupungua tena kwa kasi ni uchanaji wa mbao hasa kwa wale wanaochana mbao kupitia mashimo kando kando mwa hifadhi ya msitu, kilimo, lakini pia ukataji wa miti kwa matumizi ya nguzo hasa kwa ujenzi.

Kucha wa Usambara (Picha na eBird)

37.Kibwirosagi mdomo-mrefu (Long Billed Forest Warbler)

Hawa ni miongoni mwa ndege wadogo wenye mikia mirefu, midomo myembamba iliyo nyooka na Ngozi nene yenye rangi ya kahawia sehemu ya mbele kichwani. Wana rangi ya kijivu iliyo kolea sehemu ya juu huku sehemu ya chini wana rangi ya kijivu iliyo pauka.

Kibwirosagi hawa wanapatikana eneo dogo tu Mashariki mwa uwanda wa Usambara ambalo linakadiriwa kuwa na kilomita za mraba zipatazo 110 tu. Huko Mashariki mwa uwanda wa Usambara ndege hawa wanapatikana maeneo mawili tu ambayo ni Hifadhi ya Asili ya Amani na Hifadhi ya Asili ya Nilo. Maeneo haya yana muinuko wa mita kati ya 800-1,250 kutoka usawa wa bahari. Maeneo haya ya uwanda wa Usambara yanaonekana kuwa na ukomo mwingi sana wa viumbe hai.

Katika chapisho la mwaka 2018 la shirika la IUCN, idadi ya ndege hawa inakadiriwa kuwa 50-249 na idadi yao inazidi kupoungua tena kwa kasi kubwa sana. Kutokana na takwimu hizi ndege hawa wapo katika hatari kubwa zaidi ya kutoweka duniani. Zipo sabaabu mbali mbali ambazo zinapelekea halii hii kutokea kwa spishi hii ya kibwirosagi.

Miongoni mwa sababu kubwa zinazo pelekea kupungua kwa kasi kwa idadi ya ndege hawa ni kilimo hasa kwenye maeneo tegemezi kwa ndege hawa, ukataji wa miti na uvunaji wa mbao, ndege wavamizi, vinasaba na magonjwa mbali mbali yanayo washambulia ndege hawa. Changamoto nyingine ni mabadiliko ya tabia ya nchi na hali ya hewa hatari zaidi ambayo ndege hawa wanashindwa kustahimili.

Kibwirosagi mdomo-mrefu (Picha na eBird)

38. Shoro wa Uluguru (Winifred’s Warbler)

Ndehe hawa jamii ya shoro wana rangi ya kijivu iliyo kolea sehemu ya juu huku sehemu ya mbele kichwani na kwenye taji wakiwa na rangi ya kahawia. Rangi hii ya kahawia imeenda hadi sehemu ya pembeni mwa kichwa na kifuani. Kwenye kidevu ndege hawa wana rangi nyeupe. Wana macho myeusi, mikia mifupi huku na rangi nyeusi kwenye miguu na vidole.

Ndege hawa wanapatikana katika misitu mitatu tu ya milimani Mashariki mwa Tanzania. Safu hizi ni safu za milima ya Uluguru, Ukaguru na Rubeho na katika safu yam ilima ya Rubeho wanapatikana sana katika Hifadhi ya Misitu ya Ukwiva ambayo inapatikana kati kati ya Udzungwa na Ukaguru. Maeneo haya yanakadiriwa kuwa na muinuko wa mita kati ya 1,300-2,430 kutoka usawa wa bahari.

Idadi ya ndege hawa inakadiriwa kuwa 330-1000 huku ikionekana kupungua kwa kasi sana. Hii ni kutokana na chapisho la shirika la IUCN la mwaka 2020. Ndege hawa wapo kwenye kundi la viumbe ambao wanakaribia kuwa tishio kutokana na kupungua kwao hasa kwa sababu mbali mbali.

Upungufu wa idadi ya ndege hawa unasababishwa na kilimo na ufugaji pia wa samaki kwenye maeneo ambayo ni tegemezi kwa ndege hawa. Mabadiliko ya tabia ya nchi na mabadiliko ya hali ya hewa pia vinaonekana kuwa ni tishio kwa ndege hawa.

Shoro wa Uluguru (Picha na Holmen Birding Safaris)

39.Nyembelele koo-njano (Yellow-throated Mountain Greenbul)

Hawa ni ndege jamii ya nyembelele wenye maumbo ya kati wenye vichwa vyeusi au kijivu na shingo zenye rangi ya njano. Migongo yao ina rangi ya zaituni iliyo changanyikana na na rangi ya kijani huku sehemu ya chini wakiwa na rangi ya kijivu. Wana midomo iliyo chongoka na macho meusi yenye alama nyeupe sehemu ya chini na juu.

Ndege hawa wanapatikana sana mikoa ya kati kati na kusini mwa Tanzania. Katika maeneo wapatikanayo ndege hawa wanaonekana kuwa na uwezo wa kutawanyika katika eneo kubwa sana. Maeneo ambayo ndege hawa wanapatikana huwa na muinuko wa mita 1,350-3,300 kutoka usawa wa bahari.

Idadi halisi ya ndege hawa bado haijulikani na takwimu zinaonesha idadi yao bado imeendelea kuimarika hasa kutokana na kutokuwepo kwa viashiria au Ushahidi wowote ambao unaonesha ndege hawa wanapungua.

Nyembelele koo-njano (Picha na Tanzania Bird Atlas)

40. Nyembelele wa Uluguru (Uluguru Mountain Greenbul)

Nyembelele hawa pia wana maumbo ya kawaida. Wana vichwa vyenye rangi ya kijivu lakini pia sehemu ya chini wana rangi ya kijivu. Sehemu ya mgongoni ndege hawa wana rangi ya zaituni iliyo changanyikana na kijani. Sehemu ya mashavuni wana mstari mdogo unao onekana kwa mbali.

Ndege hawa wanapatikana katika milima ya Uluguru tu na wanaonekana kuwa na utawanyikaji mdogo sana katika maeneo hayo. Misitu hii ya Uluguru inaonekana kuwa pia na ukomo mkubwa sana wa ndege na viumbe hai wengine. Ndege hawa wanapatikana katika maeneo yenye muinuko wa mita 1,350-3,300 kutoka usawa wa bahari huko milima ya Uluguru.

Idadi ya ndege hawa pia bado haija fahamika lakini inaonekana ipo imara na ni ya kuridhisha. Hii ni kutokana na chapisho la IUCN la mwaka 2016 ambalo linaonesha kuwa hakuna viashiria wala sababu zozote ambazo zinaonesha kupungua kwa idadi ya nyembelele hawa wa milima ya Uluguru.

Nyembelele wa Uluguru (Picha na Birds of the World)

41. Korogoto Mdogo (Montane Tiny Greenbul)

Hawa ni korogoto wadogo wenye rangi ya zaituni na kijani mgongoni na rangi ya kupauka sehemu ya chini. Wana chepeo na ukosi wenye rangi ya zaituni iliyo changanyikana na kijivu. Machi ya ndege hawa yana rangi ya njano au machungwa.

Ndege hawa wanapatikana maeneo matatu tu na maeneo yote haya ni kwenye milima. Maeno hayo ni milima ya Usambara, milima ya Nguru na milima ya Nguu. Maeneo asilia ya ndege hawa huwa ni yale yanayo patikana sana kwenye ukanda wa kitropiki na nusu-tropiki zenye majani. Muinuko ambao wanapatikana ndege hawa huwa ni mita 600-2,150 kutoka usawa wa bahari.

Idadi kamili ya ndege waha bado haijulikanu na takwimu zinaonesha ndege hawa idadi yao inapungua kutokana na sababu mbali mbali. Hii ni kutokana na chapisho la shirika la IUCN la mwaka 2016. Miongoni mwa sababu ambazo zinapelekea kupungua kwa idadi ya ndege hawa ni kilimo na ufugaji lakini pia ukataji wa miti na uvunaji wa magogo kwaajili ya matumizi mbali mbali. Hali hii imepelekea ndege hawa kuingizwa kwenye kundi la viumbe ambao wanakaribia kuingia kwenye tishio hapa duniani.

Korogoto Mdogo (Picha na eBird)

HITIMISHO

Tanzania tumebarikiwa kuwa na ukomo mkubwa sana wa viumbe mbali mbali na hao ni ndege takribani 41 ambao huwezi kuwapata sehemu nyingine yoyote ile hapa duniani isipokuwa Tanzania tu. Tuna kila sababu ya kujivunia juu ya uwepo wa ndege hawa hapa nchini na ni dhahiri kwamba taifa linaingiza fedha nyingi za kigeni kupitia utalii wa ndege ambao kwa sasa unakuwa kwa kasi kubwa sana.

Ndege hawa wanakumbwa na changamoto nyingi sana na kupelekea wengi wao kuishi katika mazingira magumu, kuwa tishio na hata wengine kuwa katika hatari ya kutoweka hapa duniani. Katika changamoto hizo nyingi au zaidi ya 80% zinatokana na shughuli za kibinadamu ambazo zimekuwa mwiba mchungu kwa ndege hawa.

Kuna haja na kila sababu ya kupambana na changamoto zote ambazo zinawakumba ndege hawa na kwa kushirikiana na taasisi mbali mbali ili hata vizazi vijavyo viweze kuwashuhudia ndege hawa.

Napenda kuipongeza serikali kupitia mashirika ya uhifadhi hapa nchini kama TANAPA, TAWA, NCCA, na TFS kwa kazi kubwa sana ya ulinzi wa maeneo ya hifadhi za taifa, misitu na mapori ya akiba kwani kuna baadhi ya ndege wanapatikana katika sehemu hizo. Ndege hao wanakimbia katika makazi nje ya hifadhi kutokana na kuwindwa sana au mazingira yao kuharibiwa hivyo wanapokuwa kwenye maeneo a hifadhi wanakuwa salama zaidi. Pongezi pia kwa mashirika mengine yasiyo ya kiserikali kama IUCN, WCS, Birdlife International na wadau wote ambao wanafuatilia maisha ya ndege ili kuweza kuwanusuru kutokana na changamoto mbali mbali.

……………..MWISHO…………….

Makala hii imehaririwa na Ezra Peter Mremi, ambaye ni mwanafunzi wa shahada ya uzamili (masters) ya Usimamizi na Uhifadhi wa Wanyamapori, katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine. Kama una maswali na ushauri kuhusu makala hizi za wanyamapori usisite kuwasiliana na mwandishi wa makala hii kupitia;

Sadick Omary Hamisi

Simu: 0714116963/0765057969

Facebook: Sadicq Omary Kashushu

Instagram: sadicqlegendary

Au tembelea blog yetu: wildlifetanzania.home.blog

……………. I’M THE METALLIC LEGEND ……………