Utangulizi

Habari Mpendwa msomaji makala za wanyamapori, ni siku nyingine tena  nakukaribisha katika makala hii nzuri na itakayokuelimisha mengi kuhusiana na hali ya uhifadhi wa aina mbalimbali za bioanuai (spishi). Makala iliyopita ilijikita katika uhifadhi shirikishi jamii, hivyo basi leo nimeona nikuletee  makala hii ili jamii inapokuwa inashiriki katika shughuli mbalimbali za uhifadhi iwe inatambua kuhusu hali za uhifadhi wa spishi mbalimbali ambazo zinapatikana katika hifadhi zilizopo maeneo mbalimbali. Pia Makala hii  itajikita katika kuangalia Shirika la kimataifa la Uhifadhi wa Asili au kama linavyojulikana kwa kingereza “International Union for Conservation of Nature” (IUCN) lenye jukumu la kutathimini hali ya uhifadhi wa spishi mbalimbali dunia.

Nini Maana ya Hali ya Uhifadhi (Conservation Status)

Hali ya uhifadhi wa spishi inaonyesha iwapo kikundi /spishi za wanyama au mimea inakabiliwa na hatari ya kutoweka katika eneo lao la asili, au inaonyesha iwapo aina fulani ya spishi ipo au inakabiliwa na hatari ya kutoweka siku za usoni. Hali ya uhifadhi wa spishi mbalimbali hufanyiwa tathimini na shirika la kimataifa la Hali Ya Uhifadhi wa asili, maarufu kama IUCN.

Shirika la Kimataifa la Uhifadhi Wa Asili (IUCN) Ni shirika la Kimataifa linalopima hali ya uhifadhi wa spishi na mifumo ya ikolojia duniani. Shirika hili ndilo lenye mamlaka kuu duniani ya kuchunguza hali ya uhifadhi wa spishi mbalimbali. Hivyo basi hauwezi kuongelea hali ya uhifadhi wa spishi duniani bila kuongelea shirika hili la IUCN.

Shirika hili linaundwa na serikali na mashirika mbalimbali ya kiraia. Kuna  takribani mashirika wanachama zaidi ya 1400 na mchango wa wataalamu zaidi ya 15000. Kwa ujumla shirika hili la IUCN ni mamlaka ya ulimwengu kuhusu hali ya ulimwengu wa asili na hatua zinazohitajika kulinda.

Malengo ya shirika la kimataifa la uhifadhi wa asili (IUCN) ni Kutoa data za kisayansi kuhusu hali ya uhifadhi wa spishi mbalimbali  ulimwenguni. Lakini pia shirika hili lina jukumu la Kushughulikia mambo yanayoathiri spishi na kusambaza elimu kuhusiana na spishi hizo na pia  hali ya  kutoweka kwa viumbehai duniani.  Vile vile shirika lina jukumu la kupanga mipango ya kuhifadhi spishi mbalimbali duniani.

Vigezo Vinavyotumika  Kutathimini Hali ya Uhifadhi Wa Spishi.

Ili kuweza kutathimini hali ya uhifadhi wa spishi mbalimbali duniani shirika la IUCN lilianzisha vigezo ya kutathimini hali ya uhifadhi wa spishi. Vigezo hivi mara nyingi hurejewa kama “Vigezo vya orodha nyekundu ya IUCN”(IUCN Red List). Vigezo hivi vinasaidia kuweza kutambua hali ya uhifadhi wa spishi fulani kwani tathimini haiangalii idadi ya spishi zilizo hai pekee inaangalia vigezo vitano vifuatavyo.

Kigezo A (Criterion A):Kupungua kwa Idadi

Katika kigezo hichi cha kupungua kwa idadi tathimini  hufanywa kwa kuangalia kama  namba ya spishi wakubwa katika kundi lao  wanapungua. Tathimini hufanywa kwa kipindi cha miaka 10 hadi miaka 30 ili kuweza kubaini hali ya uhifadhi wa spishi anayefanyiwa tathimini.

Matokeo ya tathimini

Kiwango cha kupungua kwa idadi Hali ya uhifadhi
Ikiwa idadi itapungua kwa asilimia  sawa au zaidi ya 80% – 90%. hatari kubwa sana ya kutoweka (Critically endangered). 
Ikiwa idadi itapungua kwa asilimia sawa au Zaidi ya 50% – 70%. hatari ya kutoweka (Endangered). 
Ikiwa spishi itapungua kwa asilimia sawa au Zaidi ya 30% -50%. Hatarini kutoweka (Vulnerable). 

Kigezo B: (Criterion B): Eneo la Jiografia

Kigezo hiki kinatathimini kuangalia eneo la mtawanyiko wa spishi mbalimbali na eneo la makazi ya spishi hao. Kigezo hiki kinajikita zaidi katika eneo la asili ambalo spishi Fulani wanatakiwa wakae au watawanyike kwa kuangalia mazingira ya asili ya spishi na athari zinazoweza  kupatikana katika eneo hilo na kuikumba spishi husika

Ili kuweza kujua hali ya uhifadhi ya spishi Fulani katika kigezo hiki vitu vifuatavyo huzingatiwa

  1. Eneo la utawanyiko
Ikiwa eneo la mtawanyiko ni chini ya kilomita 100. hatari kubwa sana ya kutoweka (Critically endangered) 
Ikiwa eneo la mtawanyiko ni chini ya kilomita 5000. hatari ya kutoweka (Endangered). 
Ikiwa eneo mtawanyiko ni chini ya kilomita 2000. Hatarini kutoweka (Vulnerable). 
  • Eneo la makazi
Ikiwa eneo la makazi ni chini ya kilomita 10. hatari kubwa sana ya kutoweka (Critically endangered) 
Ikiwa eneo la makazi ni chini ya kilomita 500. hatari ya kutoweka (Endangered). 
Ikiwa eneo la makazi ni chini ya kilomita 2000. hatarini kutoweka (Vulnerable). 

Kigezo C (Criterion C) : Idadi Ndogo ya  Spishi Wakubwa  na Inapungua.

Katika kigezo hiki tathimini inafanyika kwa kuangalia spishi ambazo zina idadi ndogo ya viumbe na pia zinakabiliwa na kupungua kwa idadi yao hiyo ndogo hivyo spishi  huwa katika hatari kubwa ya kuweza kutoweka.

Idadi ya Spishi wakubwa Hali ya Uhifadhi
Ikiwa idadi ya spishi wakubwa ni chini ya 250 hatari kubwa sana ya kutoweka (Critically endangered) 
Ikiwa idadi ya spishi wakubwa ni chini ya 2500 hatari ya kutoweka (Endangered). 
Ikiwa idadi ya spishi wakubwa ni chini ya 10000 Hatarini kutoweka (Vulnerable). 

Kigezo D: (Criterion D ): Idadi Ndogo Sana au Iliyozuiliwa

Kigezo hiki hutumika kwa spishi ambazo zina idadi ndogo sana na pia zinapatikana katika eneo dogo  la kijiografia. Kigezo hichi hutathimini hatari ya kutoweka kwa spishi hizo kutokana na idadi yao kuwa ndogo na kupatikana katika eneo dogo lenye kikomo.

Idadi yaspishiwakubwa hatari kubwa sana ya kutoweka (Critically endangered)  hatari ya kutoweka (Endangered).  Hatarini kutoweka (Vulnerable). 
Chini ya 50 Chini ya 250 D1. Chini ya 1000
    D2.kwa kawaida eneo la makazi ya spishi ni chini ya kilomita 20 au idadi ya maeneo ya makazi ni chini ya matano.

Kigezo E: (Criterion E) : Uchambuzi wa Kiasi/Wingi.

Kigezo E hutumika kufanya tathimini kwa spishi ambazo zinaonyesha uwezekano wa kutoweka katika mazingira ya  porini. Kigezo hiki hakizingatii moja wa moja  idadi ya spishi au eneo la makazi ya spishi ,  badala yake kinazingatia matokeo ya uchambuzi wa takwimu  za kisayansi. Kigezo hiki kinatumika pale ambapo kuna Ushahidi wa kuaminika unaopendekeza kwamba spishi inaweza kuwa katika hatari ya kutoweka , hata kama idadi yao ni kubwa au eneo lao la makazi linaweza kuonekana kuwa kubwa.

Hii inamaanisha kwamba spishi ambazo zinaonyesha kuwa na uwezekano wa kutoweka kutokana na uchumbuzi wa   takwimu mbalimbali za kisayansi zinaweza kufikiliwa kuwa katika hali ya hatari bila kuzingatia vigezo vya idadi na usambaaji wa kijiografia .Baadhi ya mambo yanayozingatia ni Pamoja na;

Ikiwa uchambuzi wa takwimu  a utaonesha  uwezekano wa spishi kupotea porini ni mkubwa au sawa na asilimia 50% kwa muda wa miaka kumi mpaka miaka 30 . hatari kubwa sana ya kutoweka (Critically endangered) 
Ikiwa takwimu au uchambuzi wa taarifa  utaonesha  uwezekano wa spishi kupotea porini ni mkubwa au sawa na asilimia 20% kwa muda wa miaka ishirini mpaka miongo mitano. hatari ya kutoweka (Endangered). 
Ikiwa takwimu au uchambuzi wa taarifa utaonesha  uwezekano wa spishi kupotea porini ni mkubwa au sawa na asilimia 10% kwa muda wa miaka mia moja. Hatarini kutoweka (Vulnerable). 

Makundi Mbalimbali ya    Uhifadhi ya IUCN

Orodha nyekundu ya IUNC (IUCN Red List) imewatenga spishi mbalimbali katika makundi mbalimbali kutokana na hali yao ya uhifadhi kwa kuzingatia vigezo vilivyoelezewa hapo juu.

1.Kutoweka kabisa (Extinction)

Kundi hili linahusisha spishi ambazo zimetoweka kabisa ulimwengunu yaani hazipatikani porini wala katika mashamba ya ufugaji wa spishi. Kundi hili linajumuisha spishi zote ambazo zilikuwepo ulimwenguni lakini kutokana na sababu mbalimbali zikatoweka kabisa nao hakuna spishi hata moja iliyobaki hai.

2.Kutoweka kabisa porini (Extinct in the wild)

Kundi hili linahusisha spishi ambazo hazipatikani tena porini bali zinapatikana katika mashamba ya ufugaji (zoo). Kukosekana kwake porini kunaweza sababishwa na kupungua sana idadi yao na hivyo mamlaka husika ikachukua  spishi walio baki na kuwafuga  k ili kuhakikisha hawapotei na wanaendelea kuzaliana.

3.Hatarini sana (Critically endangered)

Kundi hili linahusisha spishi ambao wako kwenye hatari kubwa sana ya kutoweka hivi karibuni. Viumbe walio katika kundi hili wanahitaji usimamizi mkubwa  wa kuhakikisha hawapotei na waendelee kuzaliana.

4. Hatarini (Endangered)

Hili ni kundi la spishi zinazokabiliwa na hatari kubwa  ya kutoweka porini hivi karibuni.

5.Kupatikana kwa hatari (Vulnerable)

Kundi hili linalohusisha spishi ambazo zinakabiriwa na hatari kubwa ya kutoweka porini.

6.Karibu kuwa hatarini (Near threatened)

Kundi hili linalohusisha spishi ambazo ziko karibu kufikia kiwango cha kuwa hatarini lakini bado hazijakizi vigezo hivyo kwa sasa.

7.Hatarini kidogo (Least concerned)

Hili ni kundi linalohusisha spishi wote ambao hawako kwenye hatari ya kutoweka kwa sasa

8. Upungufu wa takwimu  (Data deficient)

Kundi hili linahusisha spishi ambazo taarifa  zake kuhusu hatari ya kutoweka ni duni/zina upungufuau hazitoshi.

9.Haijathaminishwa (Not evaluated)

Kundi hili linahusisha spishi ambazo bado hazijathaminishwa kulingana na vigezo vya IUCN

Hitimisho.

Katika Makala hii nimeangalia zaidi vigezo na makundi ya  uhifadhi ya bioanuai mbalimbali  ili mpendwa msomaji unapokutana na maneno haya uelewe yanamaanisha nini katika uhifadhi. Katika Makala ijayo nitaangalia baadhi ya wanyama na Mimea inayopatikana nchini Tanzania na hali ya uhifadhi wao. Hili litatupa mwamko wa ksuhiriki katika shughuli mbalimbali za uhifadhi na kuungana na wadau wengine kama  serikali na mashirika binafsi

Makala hili imeandaliwa na; Monica C. Mahilane  na kuhaririwa na Alphonce Msigwa

Kama una maoni, ushauri au maswali, unaweza kuwasiliana na mwandishi wa makala hii kupitia mawasiliano  hapo chini;

Monica C. Mahilane

Mahilanemonica49@gmail.com