1. Utangulizi wa mwandishi;

Mwandishi wa Makala hii ni mtafiti mzoefu kwenye masuala yanayohusiana na mazingira, wanyamapori na binadamu kwa zaidi ya miaka kumi na saba.  Amefanya kazi na mashirika ya kitaifa na kimataifa ikiwemo taasisi za serikali kama vile Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokione katika miradi ambayo inajihusisha na uchunguzi wa kina juu ya magonjwa yanayoweza kuambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu. Kwa sasa ni mwikolojia wa hifadhi za Taifa Tanzania, Mratibu wa mradi wa Katavi-Mahale & Corirdor (KAMACO) na afisa usalama wa mazingira wa mradi wa kuimarisha usimamizi wa maliasili na kukuza utalii kusini mwa Tanzania (REGROW). Unaweza kuwasiliana nae kwa barua pepe alphonce84@yahoo.com/0755534513

  • Ugonjwa maana yake nini?

Ugonjwa ni ile hali ya mwili kushindwa kufanya kazi yake ipasavyo kutokana na sababu mbalimbali. Kuna aina kuu nne za magonjwa ambayo ni magonjwa ya kuambukiza, magonjwa ya upungufu, magonjwa ya kurithi na magonjwa ya kisaikolojia. Katika makala hii tutajikita zaidi katika magonjwa ya kuambukiza ambayo yanaweza kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadam yaani Zoonotic diseases.

Magonjwa haya ni yale ambayo yanaweza kuambukizwa kutoka kwa mnyama ambae tayari ana vimelea vya ugonjwa huo kwenda kwa binadamu kupitia matumizi ya nyama, majimaji kama vile mate, mkojo na damu. Lakini pia binadamu anaweza kupata magonjwa hayo kwa kutumia viungo kama vile maini, figo, moyo, ngozi, mifupa n.k.

Tafiti mbali mbali zimethibisha juu ya wanyamapori kuwa na vimelea ambavyo vina madhara kwa afya ya binadamu. Baadhi ya wanyama ambao wanapatikana Tanzania na tafiti zimethibitisha uwepo wa vimelea vyenye madhara ni pamoja na Nyati, digi digi, swala, twiga, kiboko, tembo, mbwa mwitu, fisi, na wengine wengi.

Baadhi ya magonjwa ambayo yamekuwa ni tishio kubwa kwa afya ya binadamu kutokana na matumizi ya nyama ni pamoja na;

  1. Kimeta (Anthrax)
  2. Kifua kikuu (Tuberculosis)
  3. Homa ya bonde la ufa (Rift valley fever)
  4. Ugonjwa wa kutupa mimba (Brucellosis

Namna magonjwa haya yanavyoweza kuenea kutoka kwa wanyamapori Kwenda kwa binadamu.

Katika sehemu hii ya kwanza ya Makala yetu tutajikita zaidi namna ambavyo binadamu anaweza kupata magonjwa haya kupitia kula nyamapori. Magonjwa tajwa hapo juuu yanaweza kuambukizwa kwa binadamu kwa kula nyama mbichi kutoka kwa mnyama ambaye tayari ana vimelea vya ugonjwa husika. Lakini pia, wakati wa kuandaa nyama hiyo muandaaji anaweza kupata maambuziki hususani kama ana vidonda mikononi, kushika sehemu zake za wazi kama vile macho, mdomoni na puani. Pia binadamu anaweza kupata ugonjwa kama kimeta kwa njia ya kuvuta hewa baada ya kumkaribia mnyama ambae ameathirka. Njia hizi zinaweza kuwa sehemu nzuri ya vimelea husika kupenya na kuingia kwenye mwili wa binadamu.

  • Namna ya kujikinga na magonjwa haya

Mara zote tunashauriwa kuhakikisha kwamba nyama inaandaliwa vizuri katika mazingira ambayo usafi umezingatiwa. Hakikisha nyama hiyo inapikwa au kuchomwa vizuri ili vimelea vya ugonjwa husika visilete madhara katika mwili wa binadamu. Kwa wale watu ambao mila zao huruhusu matumizi ya damu mbichi, pia ni hatari kwa afya zao endapo damu hiyo itatoka kwa mnyama aliye athirika.

Mwandishi wa makala hii akichukua damu kwenye kondoo kwa ajili ya uchunguzi wa magonjwa yanaweza kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.(Picha na Mwokozi Mwanzalila)

Pia njia nyingine ya kujikinga na magonjwa haya ni kuhakikisha kwamba baada ya kumaliza kuandaa nyama yako, basi unanawa mikono yako vizuri na ikiwezekana tumia viua wadudu yaani disinfectants. Pia muandaaji anaweza kuvaa mipira ya plastic ya mikononi (gloves) ambayo ni mahususi kwa ajili ya kuandaa nyama. Mwisho kabisa wakati wa uandaaji wa nyama hiyo hakikisha unaepuka kabisa suala la kujishika pua, macho, mdomo na sehem zingine za mwili ambazo zinaweza kuwa njia nzuri ya vimelea kuingia katika mwili wa binadamu na kuleta madhara.

  • Utaratibu wa kupata nyamapori

Sheria ya wanyamapori nchini Tanzania imeruhusu uwindaji wa nyamapori kwa kibali maalumu ambacho kinatolewa na mamlaka husika. Yapo maeneo na wanyamapori ambao mamlaka husika zinatoa vibali kwa ajili ya uwindani wa nyamapori kama vile jumuiya za hifadhi za wanyamapori, Mapori ya akiba, maeneo ya usimamizi wa wanyamapori na maeneo ya vijiji ambayo yanakuwa na wanyamapori. Kutokana na hilo, kila mwaka kuanzia mwezi July 1 hadi Disemba 31 msimu wa uwindaji huanza. Hivyo ni muhimu kwa mtu yeyote ambaye amekizi vigezo kufuata taratibu zilizowekwa na mamlaka husika ili kuweza kujipatia kitoweo cha nyamapori huku akichukua tahadhari za wakati wa uandaaji wa nyama ili kuhakikisha kwamba anajikinga na magonjwa.

Kwa kuhitimisha, sehem hii ya kwanza ya Makala yetu juu ya magonjwa yanayoweza kuambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu imegusa elimu ya jumla. Sehemu ya pili tutaanza uchambuzi wa kina wa ugonjwa mmoja baada ya mwingine. Tunategema kuanza kufanya uchanmbuzi wa ugonwa wa kutupa mimba ambao kwa sasa umekuwa changamoto kubwa. Hivyo usikose kupitia ukurasa wetu kwa ajili ya kujifunza Zaidi juu ya magonjwa haya.

Mkala hii imehaririwa na Hillary Mrosso, kama una maswali, maoni na mapendekezo usisite kuwasiliana na mwandishi wa makala hii.

Tumerithishwa……Tuwarithishe…Ni mimi Mwandishi wako Alphonce Msigwa