Habari msomaji wa wildlife Tanzania, karibu kwenye makala ya leo ambayo tunajifunza na kuangali jinsi ambavyo rasilimali muhimu ya MAJI kwenye maisha ya viumbe hai. Maji ni muhimu sana kwa matumizi mbali mbali, maji ni muhimu kwa mimea na wanyama, maji ni muhimu kwa binadamu. Hivyo makala ya leo nitazungumzia umuhimu wa kulinda na kuweka sharia kali sana kwenye vyanzo vya maji. Chanzo cha maji kikiharibika, kurudi katika hali yake ya mwanzo itachukua miaka mingi na gharama kubwa sana. Makala hii nimeandika kutokana na mambo niliyojionea mwenyewe, vile vile nimeona watu na viumbe hai kama vile wanyama na ndege wakisafiri umbali mrefu kwa ajili ya kutafuta maji, nimeona mimea ikifa kwa kukosa maji. Karibu.
Licha ya kuwa na vyanzo vingi vya maji katika nchi yetu, bado rasilimali hii inabakia kuwa ya muhimu na ni hitaji la msingi kwa kila kiumbe hai, nchi yetu ni nzuri sana imepambwa na mazwa makubwa yenye maji mengi, ambayo hutumika kwa shughuli mbali mbali za kibinadamu. Nchi yetu ina mito mingi sana ambayo vyanzo vya mito hii huanzia milimani. Yote hayo yamewekwa na Mungu kwa makusudi kabisa ili viumbe hai wasipate shida wnapohitaji maji. Ni jukumu letu kufanya kazi ya utunzaji wa rasilimali hii adimu.
Ukifuatilia mwenendo wa maji kwa nchi yetu, hasa mito utagundua kuwa kwa kadri tunavyosonga mbele, au miaka inavyokwenda idadi ya mito na vyanzo vya maji vinakauka na kupoteza maji yake. Utasikia watu wakisema mto huu ulikuwa unatiririsha maji mwaka mzima, au mto huu ulikuwa na maji mengi na ulikuwa haukauki mwaka mzima, lakini sasa ni tofauti mito mingi inapoteza maji, mito mingi inataka kukauka. Mito hii mingi ambayo husambaza maji kwa viumbe hai hupita kwenye maeneo mbali mbali mbali, hupita misituni, hupita kwenye mashamba ya watu hupita kwenye hifadhi za wanyama na kisha humwaga maji yake baharini. Sehemu zote hizo ambazo mito ya maji inapita kuna kuwa na matumizi mbali mbali, kama ni watu watachota kwa ajili ya matumizi ya nyumbani nk, ikipita kwenye mashamba watu watachota na kumwagilia mashamba yao, ikipita hifadhi za wanyama wanyama hunywa na kuendelea na maisha yao
Hofu niliyonayo ni mito kupita kwenye mashamba ya watu, huwa inaharibika sana, kuliko mito hiyo kupita kwenye meneo mengine. Ukifuatilia sababu ya maji kukauka na kupungua kila mara watu watakuja na sababu nyingi sana ambazo zinawafanya waonekane wamewajibika, watu wanasema ni kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, wengine ni kutokana na hali ya hewa nk. Sikatai kwamba mambo hayo yanaweza kubadili na kusababisha kupungua au kukauka kwa maji kwenye mito. Lakini kuna sehemu yetu kubwa sana ya kufanya ili kupunguza jambo hili.
Mambo yenye uumhimu mkubwa kwetu na kwa wanyamapori wetu hatupaswi kuyachukulia kawaida na kwa mazoe hata kidogo. Maji ni muhimu, maji ni muhimu sana, tuantakiwa kuwa na njia kali sana za kulinda rasilimali hii, tunatakiwa kuwa na sharia kali sana kulinda vyanzo vyote vya maji. Tunatakiwa tuangalie zaidi ya miaka 50 ijayo huo mto utakuwepo, hilo bwawa litakuwepo, tuangalie mbali zaidi ili tujipange kwa kulinda rasilimali hii muhimu.
Juzi nilikuwa napata historia ya Mto Ruaha Mkuu, mpaka nilishangaa jinsi mto huo ulivyokuwa unavutia na kuwa ndio sababu kuu ya jina la hifadhi ya Taifa ya Ruaha. Historia inasema mto huu ulikuwa haukauki kwa miaka mingi sana, kulikuwa na viumbe hai wengi sana ndani ya mto huu, lakini nenda leo kaangalie mwenyewe mpaka utaona huruma jinsi maji yalivyopungua. Na sehemu kubwa ya mto haina maji kabisa yamekauka. Ni mapema sana, nilienda kutembelea hifadhi hii mwanzoni kabisa wa mwezi Julai mwaka 2017 na kuona picha inayosikitisha, viboko na mamba walio kuwa wengi kwenye mto huu sasa wamebakia wachache sana, na wakati mwingine unaweza usiwaone kabisa.
Suala hili la kutunza maji, mito na vyanzo vyake sio la sekta ya maji pekee, ni la kila mtu anayetumia rasilimali hii, pamoja na hayo yote serikali inatakiwa kutoa tamko kali kwa wanaoendesha shughuli za kilimo kwenye vyanzo vya maji. Na watu wote wanaokata miti na kuharibu mazingira kwenye vyanzo vya maji wanatakiwa kushugulikiwa ipasavyo. Elimu ya kujitambua na kuyatambua mazingira ni muhimu sana kwa kipindi hiki. Ongezeko la watu lisiwe ndio chanzo cha kuharibu mazinira badala yake iwe ni chachu na kuongeza nguvu kwenye ulinzi, utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji.
Asante sana kwa kusoma makala hii.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
0742092569/0683248681