Habari za leo msomaji wa wildlife Tanzania, karibu tena leo tujifunze na tuzijue sekta muhimu sana zinazohitaji kushirikiana na sekta ya maliasili na utalii ili kuhakikisaha na usawa unapatikana kwa watu na wanyamapori. Tunaamini siku zote katika umoja, na kama vile wahenga walivyosema umoja ni nguvu na utengano ni dhaifu. Kitu chochote kikubwa na chenye manufaa na kinachogusa watu wengi kamwe huwezi kukifanya mwenyewe, unahitaji ushirikiano kutoka kwa kila mmoja wetu. Kwa kuwa na mawazo mengi na ya watu mbali mbali wanaofanya kazi katika sekta mbali mbali ni muhimu sana ili kuboresha kila hatua na maamuzi yetu kwenye uhifadhi wa wanyamapori. Hivyo hizi ni baadhi ya sekta muhimu sana ambazo zinapswa kutoa ushirikiano kwenye masuala ya uhifadhi wa wanyamapori.

Sekta ya Ardhi

Kati ya sekta zenye mambo mengi ni sekta ya ardhi, hii ni kwasababu hakuna kinachoendelea kwenye maisha ya binadamu bila ushiriki au utumia ardhi. Kwenye mambo yoyote ya maendeleo masuala ya ardhi yanapaswa kuwa yameshughulikiwa na kila mtu anajua wapi anapaswa kwenda na wapi hapaswi kwenda, kila mtu anapaswa kuelewa mipaka ya maeneo muhimu kwenye maenoe mbali mbali. Hali hii lazima iwe wazi kwa hifadhi za Taifa na kwenye maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya wanyamapori na shughuli nyingine. Mara kwa mara kunakuwa na migogoro isiyoisha kwa watu waishio kando ya hifadhi, hasa wafugaji kutojua mipaka halisi ya hifadhi au maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili ya wanyamapori, au hata watu wengine kama vile wakulima.  Kila mtu analinda mipaka yake na endapo mipaka ikavunjwa na watu wakaingia kwenye maeneo ambayo hawakupangiwa kwa shughuli zao hapo ndipo mwazo wa miogoro. Hivyo basi sekta ya ardhi ni kiungo muhimu sana kwa kila sekta, hivyo kwa sekta ya wanyamapori wanatakiwa kuwa karibu zaidi na sekta hii kwa ajili ya kujiboresha.

Sekta ya Maji

Hii ni sekta nyeti sana kwa maisha ya watu na viumbe hai wengine, kila kiumbe hai kinahitaji maji kwa ajili ya kuendelea na maisha juu ya uso wa nchi. Ingawa viumbe hai vinatofautiana kwenye matumizi ya maji lakini vyote vinahitaji maji ili maisha yaendelee kuwepo. Setka hii inashughulika na maji na vyanzo vyote vya maji nchi nzima, hivyo ni muhimu sana kwa sekta ya wanyamapori kushirikiana kwa karibu na sekta hii kwani maji ni muhimu sana kwa viumbe hai waliopo kwenye maeneo yaliyotengwa na kuhifadhiwa, kuna mito ambayo inaazia sehemu mbali mbali, kuna mabwawa makubwa kuna maziwa hivi vyote vinatakiwa kuangaliwa kwa ukaribu zaidi na sekta ya maji. Hivyo endapo sekta hii itajisahau tu, mambo mengi yanaweza kuharibika na kusababisha maisha kuwa magumu kwa iumbe hai na kwa sekta nyingine.

Sekta ya Mazingira

Mazingira ni kila kitu, ili kuwepo na afya nzuri kwenye jamii yetu lazima sekta hii ifaanye kazi kwa weledi na kwa juhudi kubwa; hii ni sekta ambayo inahakikisha watu, na viumbe hai wengine wankuwa na makazi salama ya kuishi mahali popote kwa kutoa miongozo na viashiria vya mapema sana ili hatua stahiki zichukuliwe. Mazingira ya hifadhi za wanyamapori na viumbe hai wengine yanatakiwa kuchukuliwa kwa umakini na kwa weledi mubwa ili yaendelee kuwa katika hali ya asili kama mwanzo, ili makazi ya viumbe hai yaendelee kuwepo, tena sekta hii inatakiwa kuto elimu bila kukoma kwa jamii kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira na faida na hasara za kuharibu mazingira.

Sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi

Hii ni sekta inayowagusa asilimia 80 ya Watanzania wote, hivyo juhudi za makusudi ziznatakiwa kuchukuliwa ili kuwepo na hali nzuri kwa wakulima na wafugaji. Kikubwa hapa ni kupanga na kuielea sehemu ambayo sekta husika inatakiwa kufanyia kazi, kama ni mfugaji aelewe mipaka yake ya kulishia mifugo yake pamoja na sharia muhimu zitakazo mlinda hivyo hivyo kwa wakulima na wavuvi. Pia sekta hii inatakiwa kushirikiana na sekta ya wanyamapori ili kuweka usawa na maelewano kwenye mipaka, sharia na masula yote muhimu ya kimaendeleo kwenye sekta hii.

Hivyo kwa haraka  hizi ni baadhi ya sekta muhimu sana zinazopaswa kushirikiana kwa karibu na sekta ya wanyamapori, kila sekta inahitaji mchango wa sekta nyingine ili kufanya maamuzi mazuri. Hivyo uelewa  na ushirkiano baina ya sekta hizi kutaleta hali ya amani, kwenye maeneo yetu. Hivyo sekta hizo inatakiwa kukaa chini mara kwa mara kwa ajili ya kupitia sharia, kanuni na mambo mengine yanayohitaji mawazo mapana na ya kina kwenye sekta husika.

Ahasante sana kwa kusoma makala hii, usiache kumshirikisha na mwezako makala hii kwa kusambaza link ya makala hii. Karibu tufanye kazi kwa pamoja na kuifanya Tanzania kuwa sehumu salama kabisa ya kuishi.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

0742092569/0683248681

hillarymrosso@rocketmail.com