Habari Rafiki! Karibu kwenye makala ya leo ambayo tutapata ufahamu kuhusu hifadhi hii ya Ruaha yenye historia ya kuvutia sana. Kutokana na kuwa na idadi kubwa sana ya viumbe hai wanyamapori na mimea, hifadhi hii iliongezwa ili kuwepo na sehemu kubwa zaidi ya kuwahifadhi wanyama na mimea mingine. Juhudi hizi ni kubwa sana kufanywa na serikali licha ya upnzani uliokuwepo lakini hadi sasa ndio hifadhi kubwa kuliko zote hapa Tanzania.
Kwa miaka mingi hifadhi hii imekuwa haijulikani kama hifadhi nyinginge za Kaskazini, kutokana na mambo mbali mbali likiwemo la miundombinu isiyo rafiki kwa watalii na wageni wengine wanaopenda kutembelea hifadhi. Licha ya kasoro zote hizo bado kumekuwa na wageni wanaopanga safari za kutembelea hifadhi hii kubwa. Hifadhi hii ambayo imejaa kila aina ya viumbe hai wakubwa kama vile tembo nyati, twiga, pundamilia, pofu, tandala, viboko,simba nk
Kuna wageni wengi sana wakija kutembelea hifadhi ya Ruaha, ukiwauliza katika hifadhi zoote ulizotembelea hapa Tanzania ni ipi inavutia na nzuri atakwambia ni hifadhi ya Ruaha. Hivyo endapo utatembelea hifadhi hii utafaidika na kujionea vivutio vifuatavyo;
Mto Ruaha Mkuu, huu ni mto maarufu sana, utakapoingia tu hifadhini utaona mto huu wenye kunywesha wanyama na mimea ya hifadhi hii. Ndani ya mto huu kuna idadi kubwa ya viboko, mamba na samaki, hivyo ni sehemu nzuri sana kwa ajili ya kujionea wanyama na mandhari nzuri sana ya mto huu, na kwa kuwa maji yamepugua sana kwenye mto huu utaona ndege wengi sana na mamba, na viboko wakiota jua, au wakionekana vizuri.Ni sehemu nzuri sana ya kupiga picha.
Idadi kubwa ya makundi ya tembo, twiga na nyati, tandala na swala huonekana sana ukiwa njiani. Pia katika hifadhi hii kuna wale wanyamapori wakubwa wanaokula nyama (carnivores) ambao ni simba, chui, fisi, mbwa mwitu na duma. Tafiti nyingi zinasema hifadhi hii ina idadi kubwa ya wanyama hawa kuliko hifadhi nyingine hapa Tanzania.
Daraja la Kamba, hii ni sehemu yenye mvuto sana, ambayo wageni wengi hupenda kwenda na kutembea juu ya daraja hili linalo nesa nesa, ambapo chini ya daraja hili kuna mto wenye mchanga mwingi sana, hivyo hata kama umechoka na safari ukifika kwenye daraja hili unajisikia vizuri sana, pia ni sehemu nzuri sana ya watu kupiga picha.
Serengeti ndogo, hapa ni sehemu inayofanana na Serengeti kwa sababu ya tambarare kubwa sana isiyo na mwisho, pia ni sehemu nzuri sana ya kuona swala tomi, ambao watu wegi husema hawapatikani katika hifadhi hii, lakini wanapatikana katika eneo hili la Serengeti ndogo.
Maji moto, ndio hifadhi ya ruaha ina chemi chemi za maji moto ambayo ni kivutio kikubwa kwa wageni wanaotembelea hifadhi hii. Pamoja na kwamba eneo hili lipo mbali kidogo, lakini ni sehemu inayovutia kufika na kuona chemi chemi hizi za maji moto.
Mara zote kila hifadhi huwa na kitu ambacho ni cha kipekee ambacho hakipatikani sehemu nyingine au kwenye hifadhi nyingine, kwa hifadhi ya Ruaha upekee uwepo wa Kudu, au tandala , na tandala hawa huonekana kwa wakati mmoja tandala wakubw na tandala wadogo, kitu ambacho sio cha kawaida kwenye hifadhi nyingi. Tandala ni wanyama wanaokula majani, ni wakubwa kuliko swala na wanapembe ndefu, hasa dume. Karibu ujionee mwenyewe.
Ahsante sana kwa kusoma makala hii, nakutakia kila la kheri kwenye safari yako ya kutembelea hifadhi ya Ruaha. USISAHAU KUBEBA KAMERA!
Hillary Mrosso
0742092569.0683248683