Habari msomaji wa wildlife Tanzania, karibu kwenye makala ya leo tujifunze mambo ambayo yatatupa ufahamu kuhusu maeneo na vipindi vizuri vya kutalii hifadhini. Njia ya uhakika ya kufanya mambo kwa usahihi ni kujua majira, majira ni muhimu kwa sababu yatakusaidia kufanya mambo sahihi kwenye wakati sahihi. Kitu kinapofanyika kwenye majira sahihi huwa na matokeo mazuri ambayo yamekusudiwa. Kutokujua majira mazuri ya kufanya mambo ni hatari kwani itapelekea kufanya mambo sahihi kwenye wakati ambao sio sahihi, jambo la nmna hii litakupotezea nguvu, hamasa na rasilimali nyingine muhimu, na pia hutaona matokeo mazuri ya jambo hilo. Hivyo ndivyo ilivyo kwenye utalii na sehemu nyingine. Kuna kipindi kwenye utalii wanaita “High season”, hiki ni kipindi ambacho wageni wengi sana hutembelea hifadhi, na pia kuna kipindi kinaitwa” low season”, ambacho huwa na wageni wachache sana.

Kuna mambo mengi yanayosababisa kuwe na high season na low season, kitu kikubwa ni mazingira na hali ya hewa. Kwa jinsi mzunguko wa dunia ulivyo, unakuta kuna majira tofauti kwenye nchi mbali mbali, mfano kwa nchi za Ulaya  Marekani na Asia kipindi kama hiki ni baridi sana, hivyo wageni wengi hupenda kusafiri kipindi kama hiki na kuja kwenye nchi ambazo zina joto. Pia kwa kipindi kama hiki kwa nchi nyingi za Afrika ni kipindi ambacho kinaenda kiangazi, ambapo ndio kipindi kizuri sana kwa wageni au watalii kuja kutembelea hifadhi zetu.

Vile vile kipindi kama hiki kwa nchi yetu ndio kizuri sana kwa wageni kuja kutembelea kwa sababu ya hali ya barabara zetu kuwa nzuri na kupitika. Endapo ni kipindi cha mvua inakuwa ni changamoto sana kwa miundombinu ya barabara zetu kupitika kwa urahisi, hivyo hupelekea hifadhi zetu kuwa na idadi ndogo za watalii. Miezi mizuri ya kutembelea hifadhi zetu huwa ni mwishoni mwa mwezi wa tano (Mei) hadi mwanzoni mwa mwezi wa kwanza (Januari) mwaka uanofuata.

Hivyo kama unapanga ratiba zako za kutembelea hifadhi ni muhimu ukajua mambo hayo ili ujipange vizuri na safari yako. Tambua majira na vipindi vizuri vya kutembelea hifadhi ni kipindi cha kiangazi. Tena kwenye kipindi hiki ndio wanyama huonekana vizuri zaidi kuliko kipindi cha mvua, ambapo majani huwa makubwa sana na kusababisha kutoona wanyama wengi.

Kwa wale watakopata nafasi ya kutembelea hifadhi basi, huu ndio wakati bora kabisa wa kutembelea hifadhi za wanyama. Ingawa Tanzania kuna vivutio vingi sana ambavyo unaweza kwenda wakati wowote ule na kufurahia utalii wa ndani. Kuna watu wanapenda kusafiri kipindi cha low season ambacho kina wageni wachache sana, kwa ajili ya kuona mazingira na vivutio vingine. Kwa hifadhi nyingi za Tanzania endapo kutakuwa na miundombinu mizuri hasa ya barabara, ina uwezekano mkubwa wa kuwa na wageni wengi kipindi cha low seanon. Hivyo serikali inaweza kuwekeza kuinua utalii wetu kwa kuweka miundombinu bora.

Pamoja na hayo yote, kuna maeneo yenye vivutio yanafikika kwa wakati wote wa mwaka, hivyo unaweza kuamua kipindi cha low season kutembelea maeneo ya kihistoria, makumbusho nk, na kipindi cha high season ukatembelea hifadhi za wanyama.

Mpaka kufikia hapa naamini umepata kitu cha kukusaidia kujiandaa na kupanga safari zako za kitalii vizuri. Ahsante sana kwa kusoma makala hii, mshirikishe na mwingine.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

0742092569/0683248681

hillarymrosso@rocketmail.com