Habari msomaji wa Wildlife Tanzania, karibu kwenye makala ya leo ambayo tutajifunza hatua kwa hatua namna ya kufanya uwekezaji kwenye sekta ya wanyamapori. Makala hii niliyokuandalia leo ni matokeo ya kazi kubwa iliyofanywa na Mamlaka Ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania- TAWA. Kwenye moja ya majarida yao nimekuta utaratibu huu umeandikwa vizuri, kwa mtu yeyote anayetaka kufanya ufugaji wa wanyamapori hapa Tanzania. Kwa maelezo zaidi unaweza kuangalia hapa: http://www.tawa.go.tz. Hivyo karibu tupate misingi na taratibu za biashara hii.
1.Utangulizi
Sere ya wanyamapori ya mwaka 2007 na sharia ya wanyamapori sura ya 283 zinahimiza ushiriki wa wananchi katika matumizi endelevu ya rasilimali ya wanyamapori. Matumizi ya wanyamapori yamegawanyika katika sehemu mbili ambazo ni;
- Maumizi yasiyo ya uvunaji
Aina hii ya matumizi hufanyika bila kuwaondoa wanyamapori katika maeneo yao ya asili, mfano kuwaangalia wanyamapori na mandhari.
- Matumizi ya uvunaji
Aina hii ya matumizi hufanyika kwa kuwaondoa wanyamapori katika maeneo yao ya asili, mfano uwindaji wa kitalii, uwindaji wa kitoweo, ukamtaji wa wanyamapori kwa ajili ya ufugaji wa biashara na wanyamapori hai.
- Ufugaji wa Wanyamapori nchini
Ufugaji wa wanyamapori nchini ni kitendo cha kuhifadhi au kuwatunza wanyamapori nje ya mazingira yao ya asili huku wakihudumiwa na kupewa mahitaji yao muhimu.
Sheria, kanuni, Mikataba ya Kiamataifa inayosimamia shughuli hii,
Sera ya wanyamapori ya mwaka 2007 na sharia ya ya kuhifadhi wanyamapori sura 283 zimetoa fursa ya ufugaji kwa yeyote anayehitaji. Utaratibu wa kufuga wanyamapori na matumizi yao umeainishwa katika kanuni zifuatazo:
- Kanuni ya Biashara ya Nyara Na. 230 za mwaka 2010
- Kanuni za Ufugaji Wanyamapori Na.379 za mwaka 2013
- Kanuni za Ukamataji Wanyamapori za mwaka 2010
- Kanuni zinazosimamia Utekelezaji wa Mkataba wa Biashara ya Kimataifa ya Wanyamapori na Mimea iliyo Hatarini kutoweka ya mwaka 2005.
2.Wanufaika wa Shughuli hii
Ufugaji wa wanyamapori nchini ni fursa kwa watanzania na wageni kujipatia kipato kwa njia ya utalii, kitoweo, kuzalisha kwa ajili ya biashara. Ufugaji wa wanyamapori hupunguza utegemezi na shinikizo na uvunaji wa wanyamapori katika maeneo ya asili. Ufugaji hufanyika nje ya maeneo yaliyohifadhiwa kisheria (protected areas).
3.Utaratibu wa kuanzisha Mashamba, Bustani na Ranchi za Wanyamapori
Kabla ya kuanzisha mradi wa ufugaji wa wanyamapori katika mashamba, bustani na ranchi za wanyamapori mwombaji anapaswa kufanya yafuatayo;
- Kuwa na eneo la mradi,
- Kuandaa andiko la mradi
- Kupata ushauri wa watalaamu kuhusu mradi unaopendekezwa
- Kusajili mradi kwa mamlaka ya Usajili (BRELA) – Jina la biashara au Kampuni
- Kuhakikisha eneo la mradi linaendana na Mpango wa Matumiza ya Ardhi,
- Kufanya tathmini ya athari katika mazingira kwa mradi pendekezwa
4.Masharti ya kupata Lesseni
Baada ya kukamilisha utaratibu wa kuanzisha shamba/bustani/ ranchi. Mwombaji anatakiwa kuwasilisha maombi ya lesseni kwa Mkurugenzi Mkuu wa Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA kwa kujaza fomu ya maombi. Mwombaji aambatanishe nyaraka zifutazo kwenye fomu ya maombi;
- Uthibitisho wa malipo ya ada ya maombi ya lesseni yaani Stakabadhi ya Serikali (ERV)
- Nakala ya hati ya usajili wa aina ya biashara/kampuni pamoja na nakala ya katiba na mwongozo wa kampuni (Memorandum and Articles of Association),
- Andiko la mradi likijumuisha Mpango wa Biashara (Project Propasal and Busness Plan),
- Uthibitisho wa umiliki wa eneo la mradi,
- Cheti cha Tathmini ya Athari katika Mazingira (EIA Certificate)
- Nakala ya utambulisho wa mlipa kodi (Taxpayer Identification Number -TIN). Muda wa kuwasilisha maombi ya lesseni ni kuanzia tarehe 1 Oktoba hadi tarehe 15 Novemba katika mwaka husika.
5.Lesseni zinazotolewa,
Ufugaji wa wanyamapori upo katika daraja tatu zifuatazo
- Daraja 17: Bustani ya Wanyamapori
- Daraja18: Mashamba ya Ufugaji wa wanyamapori
- Daraja 20: Ranchi za wanyamapori
6.Usajili wa mashamba, Bustani na Ranchi za wanyamapori
Baada ya kupewa lesseni, mradi wa ufugaji wa wanayamapori utatakiwa kusajiliwa. Uhai wa usajili ni miaka 15.
7.Ada zinazotozwa
Ada kwa maombi ya lesseni ya ufugaji ni kama ifuatavyo;
- Bustani ya wanyamapori; Dola za kimarekani 150 kwa mradi unaomilikiwa na mzawa peke yake. Na Dola 250 kwa mradi unaomilikiwa kwa ubia kati ya mzawa na mgeni.
- Mashamba ya ufugaji wanyamapori: Dola za kimarekani 200 kwa mradi unaomilikiwa na mzawa peke yake. Na dola 500 kwa mradi unaomilikiwa kwa ubia kati ya mzawa na mgeni.
- Ranchi za wanayamapori: Dola za kimarekani 500 kwa mradi unaomilikiwa na mzawa peke yake. Na dola za kimarekani 1000 kwa mradi unaomilikiwa kwa ubia kati ya mzawa na mgeni
8.Usimamizi wa Wanyamapori katika Mashamba/Bustani/Ranchi
8.1 Namna ya kupata wanyamapori wa mbegu
Baada ya kusajili mradi wa ufugaji, mwombaji atatakiwa kuomba wanyamapori wa mbegu (parent stock) kwa ajili ya uendelezaji wa mradi. Wanyamapori hao wanaweza kukamatwa kutoka maeneo ya wazi au kutoka katika mashamba, bustani na Ranchi za wanyamapori. Sharia imetoa fursa kuingiza wanyamapori nchini kwa kuomba kibali cha kuingiza wanyamapori (Import Permit).
8.2 Matumizi ya wanyamapori wanaofugwa
Matumizi ya wanyamapori wanaofugwa pia yako katika makundi mawili;
- Matumizi ya uvunaji
- Matumizi yasiyo ya uvunaji
Matumizi hayo hufanyika kwa ajili ya utalii wa ndani na nje, kuzalisha na kusafirisha nje ya nchi, kitoweo na kujipatia kipato.
Mpaka kufikia hapa naamini umepata maarifa na picha kubwa kama unataka kuwekeza kwenye ufugaji wa wanyamapori hapa Tanzania. Pia kutaka kujua na kupata maelekezo zaidi namna ya kuendesha biashara hii, usisite kuwasiliana na Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA, kwa email dg@tawa.go.tz
Ahasante sana!
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 248 681/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania