Wildlife Ranching, Farming, Breeding and Sanctuaries
Inawezakana kufuga wanyamapori? Inawezekana kuwa na mashamba ya wanyamapori? Nani anatakiwa kujihusisha na ufugaji wa wanyamapori ni mgeni au ni raia ya wa Tanzania? Nianzie wapi nikitaka kujihusisha na ufugaji wa wanyamapori? Natakiwa kuzingatia nini? Rafiki yangu leo tunaendelea na uchambuzi wa sheria ya uhifadhi wa wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009, hayo ni baadhi ya maswali yanayoulizwa sana na watu wanaotaka kujihusisha kujua kuhusiana na ufugaji wa wanyamapori kwa manufaa mbali mbali.
Kuanzia kifungu cha 89 cha sheria hii kinaelezea vigezo, na masharti muhimu yanayohusiana ufugaji na kutoa nafasi kwa raia wa Tanzania kujihusisha kwenye ufugaji wa wanyamapori. Kama ni mfuatiliaji mzuri wa makala hizi basi leo tunachambua Sehemu ya Kumi na Mbili (Part XII). Sasa ngoja tuingie kwenye sheria tuone maelekezo yaliyopo kuhusiana na ufugaji wa wanyamapori. Karibu sana!
89._(1) Kila mtu mwenye haki milliki aliyopewa na Mkurugenzi kwa kusudi la kifungu hiki, ambaye angependa kujihusisha na uzalishaji, kutunza wanyama, bustani za wanyama (zoos), ranchi, vituo vya kulelea wanyama wasio na msaada au yatima au mashamba ya wanyamapori kwenye ardhi aliyonayo anaweza kuomba au kutuma maombi kwa Mkurugenzi kwenye fomu itakayo elezezewa kwenye kanuni. Ufafanuzi kidogo hapa ni kwamba, baada ya kupata eneo au ardhi ambayo imekidhi vigezo vyote kwa ajili ya ufugaji na utunzaji wa wanyamapori, mkurugenzi anaweza kukupa mamlaka au kibali cha kufuga au kutunza wanyamapori
(2) Mkurugenzi anaweza, kwa kushauriana na Waziri-
(a)kwa kuendana au kulingana na mpango wa matumizi bora ya ardhi;
(b)kwa kufuatana au kullingana na sheria zozote zilizoandikwa;
(c)kutengemea na malipo ya ada kama itakavyo kuwa imependekezwa; na
(d)kwa vigezo na masharti kama atakavyoona ni muhimu au inafaa au inapendeza, kutoa mamlaka au kibali kwa maombi yaliyofanywa chini ya kifungu kidogo cha (1), hakuna mtu tofauti na raia wa Tanzania, au kwa kesi ya kampuni, hisa au kiwango kikubwa cha umiliki wa kampuni unatakiwa umilikiwe na raia wa Tanzania. Ufafanuzi kwenye sehemu hii ni kwamba, mtu ambaye siyo raia wa Tanzania harusiwi kumiliki kampuni ya kutunza au kuzalisha wanyamapori, sheria inaelekeza endapo mtu anataka kufuga au kutunza wanyamapori anatakiwa kushirikiana na raia wa Tanzania na hapo kwenye kampuni hiyo inatakiwa umiliki wa kampuni hiyo uwe chini ya raia wa Tanzania au huyo raia wa Tanzania awe na hisa nyingi za kampuni hiyo.
(3) Bila kuathiri masharti ya kifungu hiki, hakuna mtu mwingine tofauti na raia wa Jamhuri ya Muungano atakayejihusisha na ranchi za wanyamapori kama kampuni, na hisa nyingi za kampuni iliyoanzishwa kwa ubia kati ya mgeni na raia wa Tanzania zitamilikiwa na raia wa Jamhuri ya Muungano. Hapa ni kwamba sheria imekataa kabisa kwa wageni na watu ambao sio raia wa Tanzania kumiliki kampuni au ranchi ya wanyamapori. Endapo mgeni anataka kufnya hivyo anatakiwa kufanya kwa ubia na raia wa Tanzania na akubali kuwa hatakua na umiki kwenye kampuni hiyo ya ufugaji wa wanyamapori.
(4) Mkurugenzi baada ya kutoa tangazo kwenye Gazeti la serikali, atatoa kibali chini ya kifungu kidogo cha (1) kuchapishwa kwa tangazo, na tangazo hilo linatakiwa kubandikwa kwenye maingilio ya shamba, eneo la mazalio, sehemu ya kupumzishia au kuhifadhi wanyama ambao hawana uwezo wa kujitegemea, bustani za wanyama, vituo vya kulelea wanyama yatima na wasio na uwezo au ranchi. Ufafanuzi kidogo hapa ni kwamba kwa wale ambao wataanzisha ufugaji wa wanyamapori, sheria inataka kuwepo na tanzazo kutoka kwenye mamlaka ya wanyamapori au kwa Waziri mwenyewe kuonyesha sehemu hiyo kuna shughuli za ufugaji wa wanyamapori zinaendelea. Na chapisho hilo au tangazo hilo linatakiwa kubandikwa sehemu ya kuingilia kwenye shamba au eneo la ufugaji, na liwe linaonekana na kusomeka na kila mtu.
(5)Mamlaka yoyote itakayotolewa na Mkurugenzi chini ya kifungu hiki inaweza kutenguliwa au kutolewa pale ambapo mtu aliyepewa mamlaka hayo ataonekana kuwa na hatia ya kosa chini ya Sheria hii, au pale ambapo mtu huyo amevunja au kukiuka vigezo au masharti ya mamalaka au kibali alichopewa. Ufafanuzi kwenye kifungu hiki ni kwamba ingawa mtu anaweza kupewa mamlaka na kibali au lesseni ya uzalishaji na ufugaji wa wanyamapori, ikagundulika anavunja sheria au anakwenda kinyume na utaratibu wa masharti aliyopewa chini ya sheria hii, kibali chake kinaweza kutenguliwa na kusitisha shughuli hizo za ufugaji wa wanyamapori.
90.Shughuli zozote zinazohusisha na ranchi za wanyamapori, mashamba ya wanyamapori, bustani za wanyamapori (zoos), maeneo ya mapumziko ya wanyama wenye matatizo na ukamataji wa wanyamapori kwa ajili ya kuwazalisha unatakiwa kufanyika kwa mujibu wa kanuni zilitugwa na Waziri. Ufafanuzi kidogo, hapa ni kwamba mambo yote na shughuli zote zinazohusisha ufugaji na utunzaji wa wanyamapori hazitakiwi kufanyika kiholela, na wala hazitakiwi kufanyika kwa njia ya mkato. Utaratibu ambao umewekwa na wataalamu wa eneo hili ni wa muhimu na unatakiwa kuzingatiwa mara zote shughuli za ufugaji wa wanyamapori zinapofanyika, pia ikumbukwe kuwa hakuna kitakachofanyika nje ya sheria hii na sheria nyingine zinazosimamia shughuli hii.
Mwisho, lakini sio mwisho wa ujio wa makala nyingine, nakushukuru sana kwa kuendelea kufuatilia na kujifunza mambo haya, naamini yanakusaidia na yanawesaidia wengine ambao unawashirikisha. Pia kama ungependa kuniandikia kupitia mawasiliano yangu hapo chini jinsi ambavyo makala hizi zinakusaidia nitashukuru sana, au unaweza kuacha komenti yako hapo chini pia ni jambo zuri. Hata kama huoni kilichokusaidia hapa, unaweza pia kutoa ushauri nini kifanyike, au unaweza kuuliza maswali, kutoa maoni yako nk. Nawashukuru sana wale wanaoniandikia na kuniambia jinsi makala hizi zinavyowasaidia nawashukuru sana, hata unayesoma na kufuatilia nakushukuru sana. Tupo pamoja!
Ahsante sana!
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 248 681/+255 742 092 569