Habari za siku kidogo ndugu msomaji wa makala za wanyamapori. Ni matumaini yangu umzima na bukheri wa afya kabisa na kama dhana yangu ni sahihi basi hunabudi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kukujaalia afya hiyo. Leo tena nakukaribisha katika darasa letu huru la wanyamapori ili kuendeleza mfululizo wa makala za wanyamapori pamoja na kujua sifa mbalimbali za wanyama hawa hali kadhalika uelekeo wa wanyama hawa ndani na nje ya maeneo tengefu ya uhifadhi wa wanyamapori.
Leo tunarudi upande wa mamalia kidogo na tutamzungumzia mnyama ajulikanae kama “NGIRI” ambae wengi wamekuwa wakimwita nguruwe pori kumbe sio hivyo. Ngiri na nguruwe pori ni wanyama wawili tofauti kabisa. Sasa bila kupoteza muda twende moja kwa moja kumjua mnyama ngiri kwa undani huku tukiangalia sifa kama utambuzi lakini pia na tabia za wanyama hawa hasa wanapokuwa katika mazingira asilia na hapa nazungumzia mwituni.
Lakini kabla sijaendelea napenda ndugu msomaji ujue kuwa kuna spishi mbili za ngiri ambao ni
1.Ngiri wa kawaida na
2.Ngiri jangwa.
Sasa hapa tutamuona ngiri wa kawaida.
SIFA NA TABIA ZA NGIRI
1.Wana sura bapa na pua zilizo chongoka zaidi ambao hufanana na za nguruwe.
2.Macho ya ngiri yapo sehemu ya juu zaidi kichwani na huwa hawana uwezo wa kuona mbali zaidi. Macho kuwa sehemu ya juu ya kichwa humsaidia ngiri kumuona adui hata kama kainamisha kichwa wakati wa kula.
3.Wana jozi mbili za viungo ambazo huonekana chini ya macho na katikati ya macho na meno yaliyo chomoza, lakini dume huwa na ongezeko lla jozi moja ambayo huonekana kwa chini ya taya.
4.Wana meno yalio tokeza nje ambayo yapo manne, mawili yapo kwa pembeni mwa pua na yenye umbo la nusu duara, na mawili mengine yapo kwa upande wa chini ambayo hutumika sana kwa kukatia vitu.
5.Wana manyoa mafupi sana mwilini, japo sehemu ya juu kichwani kuelekea mgongoni wana manyoa mengi kidogo ukilinganisha na sehemu nyingine za mwili.
6.Ngozi zao zina rangi ya kijivu au nyeusi lakini anapokuwa ameingia kwenye tope basi huonekana akiwa na rangi ya manjano inayoshabihiana na wekundu.
7.Wana mikia myembamba na mirefu kidogo. Pindi wanapo kimbia mikia husimama juu mithili ya bendera na hasa kwa watoto hali ya kusimamisha mikia ni kama ishara ya wao kukimbia pamoja na uelekeo mmoja.
8.Mara nyingi hukimbia mwendo wa kawaida na unaweza kuwadharau lakini ukwelini kwamba wana uwezo wa kukimbia kwa kasi tena kubwa tu ambayo hufika kilometa 48km kwa saa.
9.Wanapenda sana kuogelea kwenye maji lakini hata mchanga pia kwani inawasaidia kuondoa wadudu katika miili yao.
10.Madume huishi peke yao na hukutana na majike wakati wanapo taka kuzaliana tu. Hali kadhalika majike huishi pamoja na kundi moja linaweza kuwa na kina mama hadi 40.
11.Hupumzika na kulala maeneo yenye mashimo na hasa maeneo yenye majani ili kupata joto. Japo wana uwezo wa kuchimba mashimo, ngiri huwa hawapendi kuchimba na maranyingi hutumia mashimo yaliyo chimbwa na wanyama wengine kama mhanga.
12.Wakati mwingine anapokuwa na hasira huamua kushambulia na yeye badala ya kujificha dhidi ya maadui zake.
13.Kama walivyo nguruwe, ngiri pia hawana matezi ya jasho mwilini na hupunguza joto mwilini kwa kuoga kwenye matope au maji safi.
14.Ngiri wa kawaida wana meno ya mbele mawili juu na manne hadi sita kwenye taya ya chini nah ii ni moja kati ya tofauti kati ya ngiri wa kawaida na ngiri wa jangwani kwani hawana meno haya.
15.Wana uwezo mkubwa sana wa kunusa na kusikia.
KIMO, UREFU NA UZITO
Kimo= ngiri hufikia kimo cha futi 2.1-2.8
Urefu= hufikia urefu wa futi 3-4
Uzito=ngiri hufikia uzito wa kilogramu 54kg hadi 113kg
MAZINGIRA
Ngiri hawa wanapendelea maeneo yenye majani ya savanna yenye miti miti. Kama tulivoona hapo juu wanapenda pia kukaa kwenye mashimo ambayo huwa yanachimbwa na wanyama wengine japo huwa hawagombanii au kumfukuza mnyama mwenye shimo lake. Wao huenda kwenye mashomo ambayo tayari yamesha achwa na wanyama wengine.
CHAKULA
Ngiri ni jamii ya wanyama walao majani na wanapo kula huwa wanapiga magoti. Wakati mwingine hutumia pua na meno kuchimba mizizi pamoja na baadhi ya mimea ambayo huifadhi chakula ndani ya ardhi.
Wakati wa ukame hasa panapokuwa hakuna majani ya kutosha ngiri hulazimika kula nyama japo huwa hawawindi. Hivyo hulazimika kula mizoga ambayo imeachwa na wanyama wawindao.
Hupendelea kunywa maji mara kwa mara kama walivyo wanyama wengine walao majani.
KUZALIANA
Kama tulivoona hapo juu, madume na majike hukutana wakati wa kuzaliana tu na baada ya hapo kila kundi huenda njia yake. Mara baada ya kupandana jike hukaa na mimba kwa muda wa miezi sita na huweza kuzaa watoto hadi wa nane japo maranyingi huzaa watoto wane.
Watoto wa ngiri huzaliwa wakiwa na uzito mdogo sana ambapo hukadiriwa kuwa na uzito wa gramu 450g hadi 900g. Kila mtoto huwa na chuchu yake ya kunyonya kwa mama na hata kama imetokea mtoto mmoja kafa basi chuchu yake haitanyonywa na wenzie na itabaki hinyo mpaka mama atakapo zaa tena. Japo watoto hunyonya kwa takribani miezi minne, ila mara tu baada ya miezi miwili tangu kuzaliwa watoto hupata lishe nyingi kupitia majani wanayo kula.
Ngiri huanza kuzaliana mara afikishapo miezi ishirini tangu kuzaliwa. Na wakati huu majike hubaki na kundi la kina mama wakati watoto wakiume hufukuzwa kisha kwenda kuungana na wenzao na hutengeneza kundi lao.
Maisha ya ngiri hasa katika mazingira asilia huwa ni myaka 12 hadi 18.
UHIFADHI
Shirika linalohusika na uhifadhi wa maumbile asili duniani (International Union for Conservation of Nature- IUCN) bado halija waweka wanyama hawa kwenye kundi lawanyama walio hatarini kutoweka na hii ni kwa sababu wanyama hawa bado wameendelea kutawanyika na kupatikana maeneo mengi sana katika mazingira yao.
Hivyo ni faraja kubwa sana kuona bado wanyama hawa wanaendelea kuwepo tena kwa idadi nzuri na yenye kuridhisha kwakweli.
MAADUI NA TISHIO KWA NGIRI
Maadui wakubwa wa ngiri ni simba na chui. Mara ngiri anapohisi kuna hatari au kumuona simba ama chui huamua kukimbia na endapo kuna shimo karibu basi huingia ndani ya shimo huku akitanguliza sehemu ya nyuma.
Tishio kubwa kwa wanyama hawa ni ujangili katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori. Hii inatokana na kuongezeka kwa mahitaji na biashara ya nyamapori miongoni mwa jamii mbali mbali kitu kinacho pelekea wanyama hawa kuwindwa sana.
Bila kusahau uharibifu wa mazingira na uvamizi wa watu katika maeneo ya wanyamapori. Watu wamekuwa wakiharibu sana mazingira na kuvamia maeneo ya hofadhi za wanyamapori kisha kuanzisha makazi maeneo hayo. Hali hii inasababisha mabadiliko ya kiikolojia na mabadiliko ya kitabia kwa wanyama hawa.
HITIMISHO
Tunaposema tuwatunze wanyapori wetu basi kweli tuwe na nia ya kutekeleza hilo kwa kuanzia ngazi ya jamii hadi mamlaka husika. Hawa ngiri ambao leo tunawaona ni wengi tusipokuwa makini nao watapungua kama walivyo tembo na faru kwa sasa na hata simba pia.
Uvamizi wa maeneo ya hifadhi za wanyamapori ni tatizo kubwa sana hasa kwa ngiri hawa. Ukiangalia pale Hifadhi ya Taifa ya Saadani, ngiri na mifugo ya kawaida wanaishi pamoja kabisa bila matatizo. Hili ni tatizo kubwa sana kwani hapa tayari kuna mabadiliko ya kitabia ya wanyama hawa na kuwa kama jamii ya wanyama wanao fugwa.
Inafika hatu ngiri hata wanapo fikia hatua ya kuzaa basi hulazimika kuingia kuzaa ndani ya nyumba za watu au kwenye mabanda ya mbuzi na ng’ombe kitu ambacho hakitakiwi kabisa kwa upande wa wanyamapori kuwa na mahusiano na binaadamu au wanyama wafugwa kwa kiasi hiki.
Kwaiyo inahitajika busara kubwa sana ili kuwaelimisha watu juu ya uvamizi wa maeneo ya hifadhi za wanyamapori na athari zake kwao lakini pia kwa wanyamapori pia.
AHSANTENI…..
Kwa mengi zaidi kuhusu wanyamapori na ushauri juu ya makala hizi wasiliana na mwandishi wa Makala hii kupitia
Sadick Omary
Simu- 0714 116963/ 0765 057969 / 0785 813286
Email= swideeq.so@gmail.com
Au tembelea= www.mtaalamu.net/wildlifetanzania
’I’M THE METALLIC LEGEND”….