“Only when the last of the animals’ horns, tusks, skin and bones have been sold, will mankind realize that money can never buy back our wildlife”

_______ Paul Oxton

Habari Rafiki na msomaji wa mtandao wa Wildlife Tanzania, karibu kwenye tafakari ya leo ambayo tutaichambua na kujifunza kutoka kwenye msingi huu wa nukuu hii iliyosemwa na Paul Oxton. Maisha tuliyopewa kuyaishi hapa duniani yanaendeshwa na kanuni za asili ambazo zikifuatwa kila kitu kitafanyika vizuri kabisa bila kuathiri kitu kingine chochote. Mfumo wa maisha wa viumbe hai umeundwa kwa namna hii ya kufuata kanuni za asili ambazo zipo wazi, na zikifuatwa kila kitu kitakaa sehemu yake inayosthili.

Katika tafakari ya leo tunaangalia matumizi ya maliasili kama vile wanyamapori na bidhaa zinazotokana na wanyamapori. Kumekuwa na vita vikali sana juu ya uuzaji na upatikanaji, na bidhaa za wanyamapori. Mataifa Tajiri yamekuwa ndio kichocheo cha kuendelea kuwepo kwa ujangili wa tembo, faru, simba, chui na wanyama wengine ambao sehemu za miili yao imekuwa na matumizi ya kianasa kwenye nchi hizo. Kwa miaka mingi nchi za bara la Asia hasa China imetajwa sana kwenye uagizaji na hata matumizi ya rasilimali hizi. Ingawa kumekuwa na sheria na usimamizi mkali bado tumeshuhudia kupotea na kuuwawa kwa wanyamapori na mazingira yake.

Ingawa sheria za kimataifa zimezuia na kuweka sheria zinazozuia uuzaji wa wanyamapori na hata sehemu za miili yao kama vile Ngozi, meno, pembe, na mifupa kwa wanyama ambao wapo hatarini kutoweka, bado kumekuwa na kustawi kwa biashara hii haramu ya uuzaji na usambazaji wa meno ya tembo na faru. Baada ya kujifunza na kusoma tafiti mbali mbali nikagundua kuwa sisi wenyewe ndio wenye kuleta matatizo haya, jamii na watu waliopewa dhamana ya usimamizi wamechangia kwa kiasi kikubwa kupotea kwa wanyama wetu kwa maslahi yao binafsi. Ujangili hasa wa meno ya tembo na pembe za faru ni mtandao mkuwa sana unaoanzia ngazi ya chini hadi kufikia wakuu huko waliko kwenye nchi zao, watu tunaoishi nao ndio wanaofanya mambo haya maovu na yasiyokubaliwa na jamii yoyote ile duniani.

Mambo haya maovu ya kuua wanyamapori kwa sababu ya tamaa ya mali na utajiri imetishia sana uhai wa wanyamahawa pamoja na wanyama wengine, endapo wanyamapori hawa wataendelea kuuliwa na kupungua ndio kutapelekea kuupungua hata kwa wanyama wengine muhimu na pia itasababisha uwiano wa kiikolojia kuharibika na hivyo kupelekea makazi na mazalia ya wanyama wengine kupotea kabisa.

Hakuna sababu nzuri ya kufanya ujangili, huwezi kufa kwa kukosa meno ya tembo, faru, au Ngozi ya chui au simba. Hayo sio mahitaji ya msingi ya binadamu, kwamba akiyakosa atakufa. Matumizi ya aina hii ni anasa na ubinafsi. Tuwaachie tembe meno yao na faru pembe zao, maana wana haki ya kuishi na kuendelea kuwepo kwenye makazi yao. Pia ikumbukwe kwamba tunaporuhusu wanyama wetu kuuwawa na majangili kisa kupata fedha, nakwambia hivi hakuna fedha itakayomrudishia tembo uhai wake au wanyama wengine. Tuwaache wanyama waishi watakavyo na sisi tutapata faida nzuri ambayo itawasaidia na wao pia waendelee kuishi.

Meno ya tembo, pembe za faru, Ngozi, na sehemu ningine za wanyama sio mahitaji ya msingi ya binadamu, ni mahitaji ya msingi ya wanyama hao. Ndio maana akiyakosa anakufa, sisi tukiyakosa tutaendelea kuishi. Hivyo tuwaachie mahitaji yao, na tuwalinde dhidi ya wenye tamaa na nia mbaya ya kuwaharibu na kuwaua wanyama hawa wasioweza kuongea; tuwe sauti yao!

Ahsante sana!

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania