Habari msomaji wa wildlife Tanzania, karibu kwenye makala ya leo ambapo tunakumbushana mambo kadhaa wa kadha ambayo yataanza kujenga fikra za kizalendo kwa Watanzania wote ambao walikuwa hawana utaratibu wa kutembelea maeneo ya vivutio mbali mbali ndani ya nchi yetu. Ikiwa imebakia miezi minne kufikia mwezi wa kumi na mbili ambapo watu wengi huwa kwenye mapumziko makubwa ya kumalizia mwaka na kusherekea sikukuuu ya Krismasi na Mwaka Mpya. Kwa miezi na siku zilizobaki kama unataka kutembelea hifadhi na maeneo yaliyohifadhiwa au maeneo mengine yenye vivutio mbali mbali unaweza kufanya hivyo kwa kujiandaa mapema kabisa .
Makala hii itasaidia Watanzania wote wanaoisoma kuwa na utamaduni wa kutembelea hifadhi za taifa, pia nitaandika kuhusu mambo yote ya uhifadhi wa wanyamapori ili kuwepo kwa umoja kwenye ulinzi wa maliasili zetu. Nimeandika makala hii mapema kabisa kwako Mtanzania ili ujipange ndani yam waka huu angalau utembelee hata hifadhi moja, ni jambo ambalo linawezekana kabisa kulifanya. Endapo kweli una nia ya dhati ya kufanya hivyo utaanza kujitunzia na kuweka bajeti kidogo kidogo kwa ajili ya kufanikisha safari yako ya kwenda hifadhini, au hata maeneo mengine yenye vivutio mbali mbali.
Njia ya haraka ya kuonyesha uzalendo kwa nchi yetu ni kudhamini kile tulicho nacho, na njia ya kudhamini kile tulicho nacho ni kwa kulipa gharama kidogo ili kwenda kutembelea maeneo hayo. Huwezi kusema unaipenda Tanzania halafu hujawahi hata kutembelea hifadhi yoyote. Njia ya moja kwa moja ya kuchangia kuinua uchumi kwa mapato ya ndani ni kupitia utalii na maliasili, utalii wa ndani ambao unafanywa na wazawa. Yani sisi Watanzania ndio tunao weza kuupeleka mbali utalii wetu kwa kuwa na utamaduni wa kutembelea hifadhi na maeneo mengine.
Siku zote kwenye maisha yako jaribu kufanya mambo mapya ambayo yana mchango chanya kwa maisha yako na  ya watu wengine, kama hujawahi kufikiria kuhusu kutembelea maeneo yenye vivutio na mbuga za wanyama, basi fanya maamuzi hayo, usikubali kukaa sehemu moja tu maisha yako yote, nenda sehemu nyingine ukutane na watu au hata vitu ambavyo hujawahi kuviona, nenda hifadhini, nenda kafanye utalii wewe na mwezi wako, nenda hata mwenyewe, nenda na watoto wako nenda na familia yako, nenda na marafiki zako, nendeni nje ya mji mliouzoea kwa miaka mingi, nendeni porini mkaone maisha yanavyoongozwa na sharia za asili, nenda ukajifunze vipande vingine vya maisha ambavyo havipo kwenye sehemu ulipo, fanya jambo hili Mtanzania maana lipo kwenye uwezo wako kabisa.
Elewa hili siku zote wanaokwenda hifadhini na kutembelea maeneo yenye vivutio sio watu wenye pesa nyingi zilizokosa kazi, hapana, ni watu wenye utaratibu mzuri wa maisha ya kujiwekea bajeti ya kutembelea sehemu ambazo hawajawahi kwenda, ni jambo ambalo kila Mtanzania analiweza, kutenga fedha kidogo kwa kufanya safari za kitalii na kimafunzo, jinsi upendavyo wewe. Jiunze jambo hili, sio mpaka uwe na utajiri na fedha zilizokosa kazi ndio uwaze kwenda hifadhini. Kwa taarifa yako hakuna fedha iliyowahi kukosa matumizi, hata ukiwa na fedha nyingi kiasi gani, kama hujajenga utamaduni wa kutembelea hifadhi kamwe hiyo hela haitakwambia sasa bwana unapesa nyinyi twende hifadhini. Amua wewe mwenyewe matumizi yako ya fedha hata kama ni kidogo, pangilia tu, weka hata elfu moja akiba kwa ajili ya kutembelea maeneo ambayo hujatembelea.
Mwisho, una miezi minne imebakia kufikia Krismasi na Mwaka Mpya, unaweza kabisa kuweka akiba ya kukuwezesha utembelee kivutio chochote ndani ya  mwaka huu. Vipo vivutio vingi sana ndani ya nchi yetu, amua mwenyewe uanze na kipi kulingana na uwezo wako na bajeti yako, uzuri wa nchi yetu karibu kila mkoa una vivutio na maeno yenye vivutio mbali mbali, kuna maeneo ya kihistoria, kuna maeneo ya kiasili, kuna maeneo ya wanyamapori, kuna mapori kuna millima yenye mvuto kuna mabonde , kuna mito, kuna maziwa na tambarare nyingi sana zenye mvuto. Uamuzi ni wako, naamini utafanya uamuzi mzuri uanzie wapi. Niambie hapa chini kwenye sehemu iliyoandikwa add comments, unampango wa kutembelea kivutio gani? Nitafurahi sana kupokea maoni na shuhuda za sehemu uliyokwenda kutembelea na unayotaka kutembelea. Kumbuka ushuhuda wako utasaidia kuwapa hamasa wengine ili wafanye maamuzi kama yako ya kutembelea hifadhi na maeneo yenye vivutio. Karibu tushirikiane kwenye hili, tuna weza na ina wezekana sana.
Ahsante sana, kila la kheri kwenye maandalizi yako ya kutembelea vivitio.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
0742092569/0683248681
