Kadri siku na miaka inavyokwenda ndivyo idadi ya watu inazidi kuongezeka hapa duniani, hali hii ya ongezeko la idadi ya watu inaenda sambamba na ongezeko la matumizi ya mahitaji muhimu ya maisha, kama vile chakula, maji, mavazi, na malazi. Hivyo bila kuwa na utaratibu mzuri wa kupata mahitaji hayo muhimu kwa jamii tutaishia kutumia njia ambazo sio sahihi katika utafutaji wa mahitaji hayo.
Maeneo mengi yenye rasilimali muhimu kwa ajili ya kilimo, ufugaji, madini au misitu na wanyamapori sasa yanakabiliwa na hatari kubwa sana kutokana na ongezeko la idadi ya watu, hasa kwenye maeneo hayo. Maeneo mengi duniani yamekuwa na matumizi ya rasilimali yaliyopitiliza ambayo yanasababisha kukosekana kwa usawa na matumizi endelevu ya rasilimali hizi muhimu.
Miaka ya 1980, nchi yetu Tanzania ililiona jambo hili na kuamua kuweka utaratibu mzuri wa kisheria ambao utasaidia kuepuka matumizi mabaya ya rasilimali hizi kwa kuweka sheria ya mipango ya matumizi bora ya ardhi namba 6 ya mwaka 2007, sheria ya ardhi ya vijiji namaba 5 ya mwaka 1999, na sheria ya taifa ya ardhi namba 4 ya mwaka 1999. Pia utaratibu wa serikali wa mpango ya matumizi bora ya ardhi ulitolewa mwaka 2006.
Uwepo wa sheria na taratibu zote hizi ni kuhakikisha rasilimali yoyote nchini Tanzania zinatumika vizuri, au zinakuwa kwenye matumizi endelevu. Hivyo mipango ardhi ni muhimu sana ikaeleweka kwa watumiaji wote wa ardhi, kwani hii itasaidia sana katika kuepusha migogoro mingi sana ambayo inaweza kutokea kwa sababu ya kutokuwepo kwa mipaka ya maeneo maalumu kwa ajili ya shughuli maalumu.
Migogoro mingi ya ardhi kwenye nchi yetu ipo kwa sababu nyingi, lakini sababu kuu ni hizi, huenda maeneo yenye migogoro hayajafanyiwa mipango ya matumizi bora ya ardhi, yani hakuna maeneo maalumu kwa ajili ya kufanya shughuli mbali mbali. Kwa mfano maeneo ya wafugaji na maeneo ya hifadhi ya misitu au maeneo ya hifadhi ya wanyamapori hayajaeleweka vizuri mipaka yake.
Sababu ya pili inayopelekea migogoro ya ardhi katika nchi zetu ni kutotekelezwa kwa sheria za ardhi na sheria za matumizi bora ya ardhi, kuna maeneo mengi yamefanyiwa mipango ya matumizi bora ya ardhi na maeneo maalumu kwa ajili ya shughuli mbali mbali za kijamii yametengwa lakini bado kuna migogoro isiyoisha ya ardhi, hapa ni utekelezaji wa mipango hiyo ndio umekosekana.
Katika hali ya namna hii tutaendelea kuwa na migogoro mingi sana isiyoisha kama tutakosa utekelezaji wa sheria na makubaliano ya matumizi bora ya ardhi. Migogoro sio mizuri kwenye matumizi na usimamizi wa maliasili, tunatakiwa kuelewa kuwa endapo migogoro itaachwa itasababisha hali mbaya sana kwenye uhifadhi wa maliasili zetu.
Jambo ambalo linatakiwa kufanywa sasa ni kurudia makubaliano tuliyokubaliana katika utekelezaji wa matumizi bora ya ardhi, tunatakiwa kutambua hilo na kuwa watekelezaji wa sheria za ardhi.
Ahsante sana!
Hillary Mrosso
+255 683 862 481
www.mtalaamu.net/wildlifetanzania