Ashukuriwe Maanani kwa kuitunuku nchi yetu Tanzania, Maliasili nyingi kama madini, vyanzo vya maji, misitu na wanyamapori wa aina tofauti tofauti. Upande wa wanyama pori wapo wakubwa kwa wadogo wa nyonyeshao(mammals),watambaao(reptiles),warukao(aves),na wamajini(amphibians and fish) pamoja na wadudu wa aina nyingi wenye faida kubwa katika mazingira yetu kiujumla.

Kwa wingi huu wa wanyamapori Tanzania imetengeneza maeneo mengi yenye sheria tofauti za kusimamia ili kuwahifadhi vyema wanyama hawa, maeneo yenyewe ni kama mbuga za wanyama chini ya TANAPA, mapori ya akiba chini ya TAWA, Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), mabaki ya sehemu asilia (Nature Reserves mfano Amani NR). Na jumla ya maeneo yote hayo yamechukua 38.8% ya eneo za mraba za nchi yetu. Takwimu kutoka “National report on the implementation of the convention on Biological diversity, Division of Environment-Vice president’s office, Dar es salaam, June 2001.”

Zijue sababu zenye usiri wake wa utajiri wa wanyama pori Tanzania

1.Mikakati mizuri na maeneo mengi yaliyotengwa kwa uhifadhi.

Katika nchi kumi bora duniani kwenye uhifadhi wa wanyamapori, Tanzania inashika nafasi ya tatu ikiongozwa na Botswana hii ni kwa sababu ina maeneo mengi ya kuhifadhia wanyama na kuwapa uhuru wao na kuweza kuzaliana mfano kwa sasa kuna mbuga za wanyama 21, mapori mengi ya akiba yasiyo chini ya 30, Ngorongoro (NCAA) na mapori  ya mabaki ya asilia. Hivi ni miongoni Mwa vichocheo kutokana na ulinzi mkubwa na sheria kali za usimamizi.

2.Vyanzo vingi vya maji.

Katika Afrika Mashariki Tanzania ni nchi inayoongoza kwa vyanzo vingi vya maji,  japokuwa vingi vikubwa viko pembezoni mwa nchi mfano maziwa makubwa Victoria, Tanganyika na Nyasa lakini pia kuna mito mikubwa inayotegemewa na wanyama kama sehemu ya kupata maji na wengine kama ndio makazi yao kwa wale wakaao majini mfano kiboko na mamba pia na samaki. Mfano wake ni ziwa Rukwa ndani ya mbuga ya wanyama Katavi ambapo limetawaliwa sana na kiboko, mto Rufiji ndani ya Pori la akiba Selous, ardhi owevu ya Usangu(wetlands) ambapo imekuwa ikutunza aina mbalimbali za ndege pia mto Ruaha ndani ya mbuga ya wanyama Ruaha.

3.Mgawanyiko mzuri wa kazi miongoni mwa wanyama wakubwa mbugani.

Wanyamapori wapo wakubwa kama tembo kwa wadogo kama tumbili, na kila ukubwa wa mnyama una mchango wake kiikolojia mfano wale walao nyama wanategemea wale walao majani na kutokana na mbuga nyingi kuwa na wanyama walao majani wengi kumesaidia idadi kubwa ya walao nyama.

Na kwa upande wa wanyama wakubwa kuanzia uzito wa 5000kg(5tons) mfano tembo, faru na nyati wamekuwa wakila majani ya miti mirefu (tembo kwenye Acacia spps) na kuivunja hivyo kuitunza savanna ya mbuga na kufanya wanyama wadogo na wengine kuishi kwa amani na kuzaliana kiurahisi.

  1. Joghrafia ya nchi yetu Tanzania iliyo na milima, mabonde ma miinuko na sehemu nyingine tambalale kabisa.

Joghrafia hii imetokana na miinuko ya Afrika Mashariki(East African plateau), Bonde kubwa la Ufa (Great Rift Valley) na Milima ya Tao la Mashariki (Eastern Arc Mountains).

Mfano miinuko ya Afrika Mashariki imetokea Ethiopia kwa upande wa Kaskazini na imeishia Msumbiji kusini na kwa upande wa mashariki ni bahari ya India na Magharibi ni “Congo basin” na kutokana na miinuko hii imepelekea nchi yetu kuwa na tabia ya nchi ambayo ipo katikati ya Ethiopia na Msumbiji, na ndio maana kuna wanyama wengi ambao hawezi wapata kati ya nchi hizo mbili mfano tandala wadogo.

Pia milima ya Mashariki inayotoka Kenya mpaka Tanzania mfano Ulugulu, Usambara na Kipengele pia Udzungwa imekuwa na hali ya kipekee katika kutunza mimea asilia na wanyama mfano kuna aina nne za ndege ambazo zipo huko na hazipatikani kungine kokote zaidi ya Asia.

  1. Hali ya hewa kuwa joto na ubaridi kwa pamoja.

Kaskazini mwa Tanzania ni umbali wa 100km kutoka kusini mwa Ikweta(equatorial regions) hivo kuifanya nchi yetu kuwa na hali ya ki- Ikweta na ki-tropika ambayo ndio imechukua eneo kubwa la nchi yetu. Na kutokana na miunganiko ya hali ya hewa hizi mbili kumekuwa na hali ya joto na baridi hivyo kusaidia wanyama wote waishio kwenye baridi na joto kuweza kuhifadhika kiurahisi. Mfano mbuga ya Saadani joto huwa 25-27°C na usiku kushuka mpaka 20°C.

6.Mazingira mengi kutawaliwa na joto wa savanna.

Maeneo mengi ya uhifadhi yametawaliwa na uoto wa savanna ambao ni nyasi nyingi na vichaka kuliko misitu ambayo inapatikana sana sehemu chache sana kama milima ya Usambara tu, kutokana na maeneo haya kutawaliwa na nyasi kunasaidia wanyama walao nyasi kupata chakula kwa urahisi na nyakati nyingi hujificha wasionekane kwa maadui na hivyo kuweza kuishi na kuzaliana sana.

7.Idadi kubwa ya aina tofauti za ndege.

Tanzania kwa Afrika Mashariki inaongoza kwa kuwa na maeneo mazuri na muhimu kwa ndege(Important Birds Areas) mfano “hornbills”, pia inashika nafasi ya 12 kwa kuwa na idadi kubwa ya ndege ikiongozwa na Colombia na sababu hio ndege wamesaidia sana kutawanya mbegu za miti mbugani ambazo ziliota hutumiwa na wanyama wakubwa kama chakula, pia huchavusha maua ambapo matunda yake huliwa na wanyama wengine vilevile wamesaidia kwa kiasi kikubwa kusafisha mazingira kwa kula mizoga mfano “vouchers” na hivyo kuacha mazingira kuwa pendwa kwa wengine kuzaliana zaidi.

  1. Pia idadi kubwa ya wadudu.

Wadudu hawa wamechangia kiasi kikubwa ongezeko la wanyama porini kutokana na kazi za kiikolojia wanazofanya mfano kumengenya uozo wa wanyama wengine au majani hivyo kurudisha virutubisho kwenye udongo na kusaidia nyasi kuota vizuri ambazo ni chakula kwa walao majani mfano “dung beetles” pia na wengi wao wanachavusha maua na kutengeneza asali mfano nyigu na nyuki na asali hiyo kuliwa na wanyama wengine vilevile mfano “honey badger”, pia wadudu wameongeza idadi kubwa ya ndege kwa sababu hutumiwa kama chakula na ndege hao na hata kwa sokwe na chura.

Kama jinsi maisha yetu yalivyo ya kutegemeana ndivyo yalivyo porini, ndege anategemea wadudu na wadudu kutegemea mimea ndivyo hivyo na hiyo ndio siri kubwa katika utajiri wa aina yeyote ile.Naamini mpaka hapo umepata baadhi ya siri juu ya utajiri wa nchi yetu.

Makala hii imeandikwa na Leena Lulandala, amabaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu Dar salaam; unaweza kuwasiliana naye kwa mawasiliano hapo chini.

Asanteee sana!!

     Leena Lulandala

       Lulandalaleena@gmail.com

        0755369684

     UDSM-Student.