Nyegere jina lake la kingereza anaitwa “Honey badger” na jina lake la kisayansi anajulikana kama “Mellivora capensis”
Nyegere ni mnyama anayepatikana kusini mwa Asia, Iran na Afrika .Mnyama Huyu anakimo cha 23-28cm ,ufupi wa kimo unamlazimu Nyegere kuwadhuru Adui zake katika maeneo ya tumboni na aghalabu machoni. Pia anaurefu wa 55 -77cm. Wanaume huwa ni wazito 9-16kg wakati wanawake wakiwa na uzito wa 5-10kg.
Nyegere anauwezo wa kuishi miaka 10 akiwa porini na 25 akiwa anatunzwa na binadamu.
Nyegere huanza kujitegemea baada ya miezi 24 ambapo Huenda kumtafuta jike nakuishi nae mara nyingi jike huzaa watoto mapacha.
Nyegere ni omnivora hii inamaanisha kuwa anauwezo wa kula aina flani ya majani ,matunda,ndege, nyamafu nk. Mnyama huyu kama walivyo wengine kuna chakula maalumu ambacho anakipenda.
Asali ni chakula ambacho kimemfanya Nyegere kuingia kwenye uadui na nyuki kwani bila ya woga wala ruhusa Nyegere huvamia asali na mafunza nta yaliyoko kwenye mzinga.
Ikumbukwe nyuki si wanyonge ila Nyegere ana ngozi ngumu isiyopenyeza miiba na vilevile huwalevya Nyuki kwa harufu mbaya anayoitoa.
Nyegere pia huingia kwenye uadui na binadamu ambao wanategemea kurina asali.
Nyegere anatukumbusha kwenye ubaya wema haukosi , mnyama huyu amekuwa msaada mkubwa kwa ndege wanaokula asali kama Kiongozi Kuya lakini wanawaogopa nyuki hivyo Nyegere amekuwa mtetezi na wao hula makombo yake.
Nyegere hapendi kushirikiana eneo lake ni wanyama wengine haswa kipindi anapokuwa na jike,desturi hii inamfanya aonekane mnyama mwenye wivu wa kupindukia kwani atamdhuru yeyote atakaekiuka desturii hiyo ,eneo lake huwa na ukubwa wa kilomita za mraba 5 na huliweka alama kwa harufu yake kali na mikojo.
Nyegere ni mnyama asiye na woga haswa pale wanyama kama simba ,fisi na chui wanapotaka kumfanya chakula, yeye hupigana nao kwa kutumia makucha yake marefu na ushuzi wenye harufu kali ya kupalia vilevile ngozi yake ni nene mno hivyo meno makali hayawezi kumtoboa na kama simba ,chui au fisi amefanikiwa kumng’ata yeye hujigeuza nyuzi 180 na kuchoropoka.
Ujasiri wa bwana Nyegere unaenda mbali zaidi kiasi cha kupambana na sumu za nyoka wakali kama Koboko, Fira na Kifutu.
Wakati nyoka hawa hatari wanapokuwa tishio kwa simba ,Faru,Tembo,Nyati hata binadamu hawafui dafu kwa Nyegere ambaye sumu yao humfanya azimie kwa dakika chache na kurudi katika mpambano na mwisho kumuua adui huyo.
Nyegere pia ni mnyama mvivu ,yeye akichoka huweza kujilaza popote au kwenye mashimo ya wanyama wengine kama Nungunungu,mbweha .
Jambo hili linamfanya kuonekana jeuri na asiye na woga.
Hitimisho
Nyegere ni wanyama wenye upendo haswa kwa watoto wao ambao huzaliwa vipofu pasipo na magojwa tofauti na wanyama wengine wao hawawafukuzi watoto wanapokuwa wakubwa pia bila kuchokozwa ni wanyama wapole na wenye aibu.
Nyegere wamekua wakikumbwa na changamoto mbalimbali kama Uhasama na binadamu haswa warina asali hivyo huwekewa mitego ili kuwaua, kuwindwa kwa ajili ya kujipatia nyama , na imani potofu kuwa Nyegere ni dawa ya mapenzi na ujasiri.
Juhudi zinahitajika kuhuhakikisha Nyegere wanatunzwa ili wasije kupotea Siku za usoni kwani ni muhimu katika tafiti na utalii.
Makala hii imeandikwa na
Maureen FN Daffa
+255 626 331 871