Baada ya ugunduzi wa moto, maisha ya binadamu yalibadilika kwa kiasi kikubwa, uzalishaji uliongezeka, ulinzi dhidi ya maadui zake uliimarika, afya iliimarika zaidi na ubunifu uliongezeka sana. Licha ya faida nyingi za moto kwenye maisha ya binadamu, kumekuwa na majanga mengi yaliyosababishwa na moto. Majanga hayo ni kama moto kuunguza na kuchoma vitu muhimu kama nyumba, mali, mazao mifugo na hata kuua watu.
Hata hivyo moto umekuwa na faida nyingi katika viumbe wa mwituni kama vile mimea na wanyama. Moto husaidia sana mifumo mingi ya ikolojia kukaa sawa. Moto husaidia kuchoma na kuondoa mrundikano wa majani katika hifadhi za misitu na wanyamapori, hivyo kufanya miti na mimea mingine mipya na yenye afya kuota. Miti na mimea mipya huwa ndio chakula kikuu cha wanyama walao majani kama vile swala, nyati, pundamilia, nyumbu, tembo, nk.
Umuhimu wa moto katika uhifadhi wa wanyamapori ni mkubwa sana. Kwa kutambua hilo mamlaka za uhifadhi wa wanyamapori na misitu hupangilia namna bora ya kuchoma baadhi ya maeneo ya hifadhi au mbuga za wanyama ili kuiweka hifadhi katika hali ya usalama, na wanyamapori waweze kuwa na chakula cha kutosha katika maeneo waliyochoma.
Licha ya kuwa na faida za kiikolojia, moto umekuwa na hasara kubwa sana kiikolojia endapo moto huo umewaka bila kupangiliwa. Mioto mingi yenye madhara kwa viumbe hai kama vile mimea na wanyamapori huwa imewashwa kiholela, au na watu wanaoishi kando ya hifadhi, au na majangili wanaotumia moto kama nyenzo za uwindaji wa wanyamapori.
Mioto inayowashwa kiholela ndio huleta hasara sana kwa wanyamapori na hifadhi ya misitu. Mfano mzuri ni moto uliotokea hivi karibuni katika hifadhi ya mlima Kilimanjaro, moto huu umewashwa kiholela na kusababiha uharibifu mkubwa wa mandhari ya hifadhi ya mlima Kilimanjaro na wanyamapori wake.
Shughuli za kibinadamu kama vile maandalizi ya mashamba kwa ajili ya kilimo, kurina asali , ujangili au uwindaji haramu wa wanyamapori vimetajwa sana kuwa ni chanzo cha mioto haribifu. Moto haribifu ina madhara makubwa na husababisha gharama kubwa za kuudhibiti mioto hii. Hivyo ni jukumu letu kama jamii kuwa makini wakati tunafanya shughuli zetu zinazohusisha moto kwenye maeneo yaliyo karibu na hifadhi za misitu na wanyamapori.
Halikadhalika, katika kipindi hiki ambacho kuna mabadiliko makubwa ya tabia nchi, ukame umeongezeka, mvua hazinyeshi kwa wakati, jua limekuwa kali sana, joto limeongezeka hivyo kupelekea maeneo mengi kuwa na vipindi virefu vya ukame. Hali hii inapelekea kukauka kwa majani na mimea mingi hivyo endapo moto utawashwa kiholela kwenye misitu au hifadhi za wanyamapori unakuwa na nguvu na kuenea kwa kasi na kusababisha hasara na majanga makubwa kwa viumbe hai.
Katika vipindi vingi vya ukame ndio majanga ya moto hushamiri sana, mfano maeneo mengi ya nchi kama vile kwenye misitu ya asili na ile ya kupandwa kama ile ya SAOHILI imeripotiwa sana kuathirika na mioto holela.
Jamii inatakiwa kuwajibika na utunzaji wa mazingira, kwa kuhakikisha mioto holela inadhibitiwa, elimu inatolewa na wanaojihusisha na uchomaji moto hovyo kuchukuliwa hatua kali za kisheria. Kwa mujibu wa sheria ya uhifadhi wa wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009, kifungu cha 18, kipengele cha 1. Ambacho kimetoa katazo la mtu yeyeyote kuchoma majani, kuangusha miti, kujeruhi, au kuondoa mti wowote uliosimama, au majani, mbegu, mimea au sehemu yoyote ya mti au mnyama katika hifadhi ya wanyamapori bila kuwa na kibali cha maandishi kutoka kwa Mkurugenzi wa wanyamapori. Endapo mtu atakiuka kifungu hiki na kuhusika na makosa yaliyotajwa katika kifungu cha kwanza atalazimika kulipa fainiii isiyopungua shilingi laki mbili (200,000) lakini isiyozidi shilingi laki tano (500,000), au kwenda jela kwa kifungo kisichopungua miaka miwili lakini kisichozidi miaka mitano au vyote kwa pamoja, kama ilivyoainishwa katika kufungu cha 18, kipengele cha 2 cha sheria ya uhifadhi wa wanyamapori Tanzania.
Ndugu msomaji wa makala hii, tunatakiwa kujua kuchoma au kusababisha moto kwenye maeneo ya hifadhi za misitu au wanyamapori ni kosa kisheria. Pia tujue kuwa majanga ya moto yanaleta hasara na uharibifu mkubwa kuliko faini na adhabu zinazotolewa kisheria. Pamoja na hayo,tunatakiwa kuwa walinzi wa mazingira yetu na maliasili zetu kwa kuzuia aina zote za mioto haribifu. Pia tunatakiwa kuongeza umakini kwenye shughuli zetu zote zinazohusisha matumizi ya moto; kuwa balozi mzuri wa kuzuia majanga ya moto kwenye mazingira yetu na hifadhi zetu.
Nakupongeza kwa kusoma makala hii hadi mwisho, usiache kuwatumia wengine makala hii ili wajifunze na kuchukua hatua muhimu kudhibiti mioto holela.
Imeandikwa na Hillary Mrosso
Simu: 0683862481
Email: hillarymrosso@rocketmail.com.