Mwani ni aina ya viumbe hai wanaopatikana katika maeneo ya bahari wajulikanao kwa lugha ya kiingereza kama “Sea moss”. Katika uasili wake, viumbe hawa huota na kukua kwenye fukwe zenye asili ya mawe au mchanga mzito, nyasi za baharini na kwenye matumbawe. Kuna aina mbalimbali za mwani ambazo hutofautiana kutoka ukanda mmoja wa bahari na ukanda mwingine, Mfano Tanzania kuna aina mbili za mwani zinazopatikana ambazo ni “Eucheuma denticulatum” au kwa jina lingine hujulikana kama “Eucheuma spinosum” na aina ya pili inaitwa “Kappaphycus alvarezii”.
Aina hizo za Mwani hustawi vizuri Sana katika ukanda huu, hususani ukanda wa kaskazini na kusini mashariki mwa bahari ya Hindi. Hii inatokana na hali nzuri ya mazingira ya bahari yanayosaidia ustawi wake na kufanya wakulima wa Mwani kupata Mwani wa kutosha katika kipindi cha mavuno. Vikundi vingi vya wanawake hujishughulisha na kilimo cha zao hili huku wakisaidiwa na wataalamu wa Mwani ili kujikwamua kiuchumi pamoja na kupata chakula kwaajili ya familia zao.
Pichani: wakulima wa Mwani, Chanzo cha picha: Google
Sambamba na hayo, Mwani hustawi vizuri pia kwenye maji baridi ikijumuisha maeneo ya mito, maziwa na mabwawa japokuwa makala hii itajikita zaidi kuzungumzia Mwani unaostawi katika maeneo ya bahari. Ukiwa katika fukwe za bahari Mwani huwa na rangi mbalimbali zinazoipamba bahari na kuifanya iwe ya kuvutia na kubwa kuliko yote ni kwamba Mwani ni viumbe hai wa bahari ambao hawatumii tu mizizi katika kufyonza virutubisho ila hutumia sehemu zote katika kufyonza virutubisho na kufanya ustawi wake kuwa mzuri bila kutegemea mizizi kwa kiasi kikubwa kama ilivyo mimea mingine ya baharini na nchi kavu. Mwani huwa na rangi ya kijani, kahawia na nyekundu. Rangi hizo zimekuwa zinasababishwa na kuongezeka au kupungua kwa kina cha maji ya bahari.
Pichani: Mwani wa kijani, Chanzo cha picha; Google
Mwani wa kijani kama inavoonekana pichani huwa na rangi ya kijani katika uasili wake. Mwani huu wenye rangi ya kuvutia ni muhimu sana kiafya hususani kwa chakula licha ya kuwa Mwani huu unaweza kutumika katika kutengeneza mapambo na vipodozi.
Pichani: Mwani wa kahawia ukiwa umeanikwa; Chanzo cha picha: Google
Aina nyingine ya Mwani ni ule wenye rangi ya kahawia ambao hupendwa sana na watu kwa matumizi ya chakula. Baadhi ya mataifa kama Asia na Korea hutumia aina hii ya Mwani katika kuandaa vyakula vyao kutokana na virutubisho vinavyopatikana katika aina hii ya Mwani. Aina hii inaweza kuliwa ukiwa mbichi au ukiwa umeiva, vile vile Supu iliyotengenezwa kutokana na Mwani wa kahawia huwa na ladha nzuri ambayo huvutia walaji wengi na katika mataifa haya makubwa Supu inayotengenezwa kutokana na Mwani wa kahawia huwa na gharama kubwa. Lakini pia Mwani wa kahawia hukaushwa vizuri baada ya kuvunwa shambani na kuanikwa Kama inavyoonekana katika picha. Huu pia hutumika katika matumizi ya aina mbalimbali ikiwemo chakula na mapambo.
Pichani: Mwani mwekundu
Mwani mwekundu una rangi nzuri na ya kuvutia hasa ukiutazama ukiwa katika fukwe za bahari. Ukiangalia mwani huu baharini huonekana kama maua mazuri yanayoipamba bahari. Licha umuhimu wake kiafya katika kubeba virutubisho muhimu vya mwili wa binadamu pia Mwani huu hutumika katika kutengeneza vipodozi mbalimbali vinavyotumika katika maisha ya kila siku na Wanasayansi wengi na watafiti hupendelea kutumia aina hii ya mwani katika kufanya tafiti mbalimbali za bioteknolojia ambazo husaidia katika kutatua changamoto mbalimbali.
Nchini Tanzania zao la Mwani ni zao ambalo halifahamiki sana ukilinganisha na mazao mengine katika ukanda wa bahari japokuwa ni zao Muhimu sana katika Nyanja za chakula na biashara. Kuna machapisho mbalimbali ambayo yamejaribu kuelezea uotaji, ukuaji na ustawi wa Mwani katika ikolojia ya bahari mfano (Chapisho la Oliveira 2003). Muktadha wa chapisho hili unaeleza jinsi ambavyo Mwani unaweza kustawi kuendana na mazingira kwa kujishikiza katika matabaka laini mfano maeneo yenye tope. Licha ya hayo ukuaji wa mwani katika maeneo ya bahari umekuwa ukikumbwa na changamoto mbalimbali zikihusisha magonjwa, mabadiliko ya tabia ya nchi na mawimbi makali ya bahari.Changamoto hizi zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa uzalishaji wa Mwani.Changamoto hizo zimepelekea wadau mbalimbali kama serikali, mashirika ya uhifadhi wa bahari kama Global Seaweed na wananchi kuhamasika kuanzisha mashamba ya Mwani ili kukabiliana na changamoto hizo katika kutengeneza mazingira rafiki ya ustawi wa Mwani.
Kutokana na umuhimu wa Mwani kama chanzo cha kujipatia kipato kwa maana ya biashara na chakula, nchini Tanzania kumekuwa na harakati mbalimbali za kuhamasisha kilimo cha Mwani kutokana na uhitaji wake kuwa mkubwa kuliko uzalishaji kwa upande wa Tanzania bara na Visiwani Zanzibar. Harakati hizo zimetokana na ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuvutiwa na kilimo cha mwani tangu miaka ya 1980. Baadhi ya maeneo ambayo serikali ilitilia mkazo katika kilimo hicho ni pamoja na Visiwa vya Zanzibar, Tanga, Mafia na lindi katika wilaya ya kilwa. Wakulima wa zao la mwani wamekuwa wakinufaika sana na uwepo wa zao hili muhimu katika kujikwamua kiuchumi na ulimaji wa Mwani umekuwa ukifanyika mara nyingi katika maji yenye kina kifupi. Mfano madhubuti unaoonesha umuhimu wa zao hili ni huko nchini Zanzibar ambapo Mwani ni sekta ya tatu kwa ukubwa unayoiingizia Zanzibar pesa nyingi za kigeni na kukuza pato la Taifa.
ATHARI ZA KILIMO CHA MWANI KATIKA UHIFADHI WA BAHARI.
Ulimaji wa Mwani katika ukanda wa bahari umekuwa ukihusishwa sana na uchafuzi wa mazingira na ikolojia ya bahari kutokana na njia zinazotumika katika ulimaji wa Mwani pamoja na njia za uandaaji wa shamba la Mwani. Athari hizo ni pamoja na,
- Husababisha mlipuko wa Magonjwa kwa viumbe wa baharini. Mara nyingi viumbe wa baharini wamezoea kuishi katika mazingira yao ya asili ambapo ulimaji wa Mwani unasababisha uchafuzi wa maji ya bahari na kupelekea mlipuko wa magonjwa kwa viumbe wengine kama Samaki, matumbawe na viumbe wengine. Mlipuko wa magonjwa haya umepelekea vifo vya spishi mbalimbali za viumbe wa baharini.
- Hupelekea kupungua kwa oksijeni baharini. Viumbe wanaopatikana baharini huishi kwa kutegemea Oksijeni inayopatikana katika maji ya bahari tofauti na viumbe wengine wanaopatikana nchi kavu, Hivyo basi kilimo cha Mwani kinasababisha kupungua kwa kiasi cha oksijeni baharini kutokana na kuwa Mwani hustawi juu ya maji ya bahari kwa kuelea huku ukishikiliwa na vigingi vilivyo tia nanga baharini na hali hii sababisha eneo la bahari kufunikwa na Mwani jambo linalopelekea kupungua kwa oksijeni ya kutosha baharini na kuhatarisha maisha ya viumbe wa baharini.
- Huathiri kiasi cha joto na chumvi ya Bahari. Kilimo cha mwani kinaathari kubwa katika uwiano bora wa joto na chumvi inayopatikana katika maji ya bahari kwa ustawi wa viumbe waliomo. Dawa zinazotumika katika kudhibiti magonjwa yanayoathiri Mwani Pamoja na michanganyiko mingine ya kustawisha Mwani hupelekea kuathiri joto, PH na chumvi ya bahari. Kubadilika kwa joto na chumvi ya bahari kutokana na kilimo cha Mwani hupelekea kupotea kwa baadhi ya viumbe Muhimu wa baharini kutokana na kuwa hawawezi kuishi na kuendana na mazingira hayo ambayo yako tofauti na baiolojia ya miili yao.
- Husababisha kupotea kwa misitu pembezoni mwa bahari. Wakati wa kuandaa mashamba ya Mwani kwaajili ya msimu wa kilimo cha Mwani baharini Misitu inayopatikana kando kando ya bahari imekuwa ikipotea kwa kiasi kikubwa. Miti ya mikoko na Mianzi imekuwa ikitumiwa kwa kiasi kikubwa katika kuandaa vigingi, Nanga na Chelezo ili kufanya Mwani uelee juu ya Maji na hii inatokana na uimara wa miti hiyo na uwezo kukaa majini kwa muda mrefu bila kuharibika. Mkoani Lindi hususani katika wilaya ya Kilwa Viongozi mbalimbali wa Serikali wamekuwa wakitoa elimu kwa wananchi juu ya utunzaji wa bahari na misitu asilia katika kudumisha matumizi endelevu ya bahari.
- Uchafuzi wa fukwe za Bahari. Moja Kati ya changamoto zinazosababisha maendeleo hafifu ya fukwe zetu hasa utalii wa fukwe ni Uchafu ambao unasababishwa na shughuli mbalimbali za kibinadamu zinazofanyika katika maeneo ya bahari. Kilimo Cha Mwani kimekuwa kikihusishwa na uchafuzi wa mazingira ya bahari hasa fukwe na Jambo hilo limepelekea watu wengi kutovutiwa kutembelea fukwe ambazo zinamashamba ya mwanai. Harufu mbaya, Uchafu wa mabaki ya Mwani katika fukwe na bahari, kutoweka kwa viumbe wanaopatikana ufukweni kutokana na kilimo hicho ni baadhi ya vitu vinavyopelekea kupoteza mvuto wa fukwe. Hivyo basi jamii inatakiwa kujua namna Bora ya kutunza mazingira ya bahari ili kuepukana na Uchafu unaosababishwa na kilimo cha Mwani.
Kwa kuhitimisha, nipende kutoa maoni yangu kwa Serikali, Wadau mbalimbali na wataalamu kuwa licha ya faida mbalimbali ambazo tunazipata kutokana na kilimo cha Mwani nchini Tanzania, wananchi wanatakiwa kupewa elimu ya kitaalamu ambayo itapunguza athari za kilimo hiki katika Mazingira ya Bahari kwa kutambua kuwa uwepo wa bahari ndio ustawi wa Mwani hivyo tuitunze bahari ili kunufaika na kilimo hiki. Kampeni mbalimbali za usafi wa bahari zinatakiwa kuundwa katika vikundi mbalimbali vya wakulima ili kuongeza tija,ujuzi na uelewa juu ya umuhimu wa kutunza na kuhifadhi bahari. Aidha nipende kutoa rai yangu kwenye wizara ya Mifugo na uvuvi hususani idara ya viumbe hai wa baharini kutoa mwongozo mahususi utakaosaidia wakulima kufaidika na kilimo cha Mwani huku wakitunza na kuhifadhi mazingira ya bahari.
Makala hii imeandaliwa na kuandikwa na Muhitimu wa Shahada ya Usimamizi wa Wanyamapori ambaye pia ni mbobezi katika Uhifadhi wa Bahari (Marine conservationist), Kwa maoni au fursa usisite kuwasiliana na Mimi kwa namba zifuatazo,
Vile vile Makala hii imehaririwa na Alphonce Msigwa, afisa Uhifadhi kutoka shirika la hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).
Victor Obadia Wilson
Simu: +255620861002/+255743880175
Barua pepe: wilsonvictor712@gmail.com
Idara ya Usimamizi wa wanyamapori
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, SUA