Dunia hii hakuna asiyejua umuhimu wa muziki katika kufikisha ujumbe kwa jamii. Muziki unatumika kuelezea hisia za furaha, huzuni na majonzi. Muziki hutumika kufariji, kufundisha, kuburudisha,na kuwaleta watu pamoja.
Watunzi na waimbaji husukumwa na matukio mbali mbali yaliyomo katika jamii au yanayotokea kwenye maisha yao. Mara nyingi mazingira yanayomzunguka mwimbaji yanaweza kumsukuma kutunga na kuimba kuhusu jambo fulani, mfano anaweza kuimba kuhusu mapenzi, fedha, utajiri, umasikini, siasa, utamaduni, mazingira nk.
Hata wakati Mbaraka Mwinshehe ana tunga na kuimba wimbo wake wa “MOROGORO YAPENDEZA” miaka 1960 na 1970 alisukumwa na vitu vizuri alivyoviona kipindi hicho ikiwemo Morogoro. Naamini kabisa Mbaraka Mwinshehe alipata msukumo wa kutunga na kuimba nyimbo ya kusifia mazuri ya mkoa wa mkoa wa Morogoro.
Mbaraka Mwinshehe, alizaliwa Juni 27 mwaka 1944 na kufariki Januari 12 mwaka 1979. Alikuwa ni nguli mwenye uwezo na kipaji kikubwa cha kutunga, kupiga gitaa na kuimba muziki wa dansi kwa uhodari mkubwa. Baadhi ya nyimbo zake nyinginge ni kama Barua, Enyi Vijana na Ester wangu, bado zinapigwa sehemu mbali mbali zikiwa na jumbe maridhawa kabisa.
Licha ya uwezo wake mkubwa katika Sanaa ya muziki, Mbaraka alitumia kipaji na uwezo wake huo kutunga wimbo ulioitwa “MOROGORO YAPENDEZA”. Mbaraka alitaja vitu vilivyoifanya Morogoro ya nyakati hizo za miaka ya 1970 ipendeze, alitaja milima, mito, mabonde na hali ya hewa nzuri.
Mbaraka Mwinshehe, hakuimba kuhusu mila na tamaduni za makabila ya mkoa wa Morogoro, wala ngoma za asiliza na vigodoro. Hakuimba kuhusu uwepo wa mashamba makubwa ya miwa na mabonde makubwa ya mpunga Kilombero. Mbaraka hakuimba kuhusu fahari ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi wala uwepo wa vipaji vingi vya mpira wa miguu na ngumi.
Mbaraka alivutiwa zaidi na Morogoro iliyozungukwa na milima inayotiririsha maji mwaka mzima, alivutiwa na uoto wa asili uliotanda katika mabonde na vilele vya milima ya Uluguru. Aliona fahari kuimba upekee huu ambao huenda hakuuona sehemu nyingine alizowahi kwenda.
Morogoro ya kipindi hicho ilikuwa inavutia sana kiasi cha kumfanya nguli huyu wa muziki kuimba akiisifia Morogoro, aliimba kwa hisia sana, akiwakaribisha watu wafike wajionee uzuri na mandhari inayovutia ya mkoa wa Morogoro.
Baadhi ya comments za wadau wakiwa wanasema habari za Morogoro ya Mbaraka Mwinshehe
Wakati nasikiliza wimbo huu wa Morogoro yapendeza, ilibidi niitafute hiyo Morogoro inayoimbwa kiasi hiki ilikuwaje. Nilipitia nakala kongwe, tafiti na ripoti za kiserikali ili nione kulikuwa na nini kwenye hiyo Morogoro ya Mbaraka Mwinshehe.
Baada ya kupitia maandiko kadhaa niligundua kuwa uwepo wa milima ya Uluguru ndio unaopendezesha Morogoro. Milima hii ya uluguru ni moja ya maeneo yaliyo katika safu za Milima ya Tao la Mashariki (Eastern Arc Mountains). Milima ya Tao la Mashariki ni safu za milima iliyoanzia katika miinuko ya Taita nchini Kenya na kuishia katika milima ya Mahenge na Malundwe nchini Tanzania.
Milima hii ya Tao la Mashariki ni pamoja na milima ya Taita, milima ya kaskazini na kusini mwa Pare, milima iliyopo Magharibi na Mashariki mwa Usambara, milima ya Nguru, Ukaguru, Uluguru, Rubeho, Udzungwa Mahenge na Malundwe. Milima hii ina sifa ya kuwa na bayoanuai ya kipekee sana kutokana na upekee wa mazingira yake na hali ya hewa.
Milima ya Uluguru ambayo huonekana vizuri ukiwa Morogoro Mjini, na katika wilaya ya Mvomero ni muunganiko wa vilima vingi; kilele kirefu kikiwa na urefu wa mita 2,630 kutoka usawa wa bahari. Ukaribu wa bahari ya Hindi (Kilomita180) na milima ya Uluguru imechangia upekee wa hali ya hewa katika eneo hili.
Upekee wa hali ya hewa katika eneo hili umefanya milima ya Uluguru kuwa na misitu minene na vyanzo vingi vya maji. Ndio maana Mbaraka Mwinshehe aliona maji yakitiririka kutoka milimani enzi hizo. Hata hivyo, moja ya faida ya uwepo wa Milima ya Uluguru ni chanzo kikuu cha maji kwa mkoa wa Morogoro na Dar es Salaam. Mito mingi inayotiririka kutoka milima hii inasaidia kwa umwagiliaji na matumizi ya maji ya nyumbani.
Kutokana na upekee wa eneo hili, tafiti zinaonyesha kuwa kuna zaidi ya spishi 1500 za mimea ambayo haipatikani sehemu nyingine duniani. Pia eneo hili linamiliki asilimia 70 ya miti yake ya asili. Na pia ni miongoni mwa maeneo 35 muhimu zaidi duniani kwa uhifadhi wa bayoanui, kama ilivyoripotiwa na Profesa Neil Burgess na wenzake mwaka 2002.
Maeneo mengi yenye mazingira kama haya ni makazi muhimu ya wanyama, ndege, wadudu, reptilia na amfibia. Uwepo wa reptilia, amfibia, ndege na wanyama wengine katika eneo ni kiashiria kizuri cha afya ya mazingira na uhifadhi.
Hivyo, namuelewa sana Mbaraka Mwinshehe alipoimba Morogoro yapendeza na kutaja mito na maji yanayotirika kutoka milimani. Nafikiri Morogoro ya Mbaraka Mwinshehe ilikuwa inavutia sana. Kuna siku nikawa najiuliza, hivi huyu Mbaraka anaisifia Morogoro ipi? Maana Morogoro ya sasa sio kama ile ya akina Mbaraka Mwinshehe.
Siku hizi milima ya Uluguru imegeuka kuwa mashamba ya mazao, vyanzo vingi vya maji vimekauka, watu wamevamia maeneo ya misitu ya asili na kuyafanya kilimo. Miti inakatwa kwa ajili ya mbao, ujenzi, mkaa na kuni. Zaidi ya asilimia 70 ya eneo la misitu ya milima ya tao la mashariki imepoteza ule uasilia wake kutokana na shughuli za ukataji miti na mmongonyoko wa udongo.
Siku hizi ukifika Morogoro ukaangalia vilele vya milima ya Uluguru utaona mlima umejaa matuta na mashama na nyumba za bati. Maeneo yaliyo wazi ni yale ambayo hayafai kwa kilimo kutokana na kuwa na miamba na mawe makubwa.
Siku hizi milima ya Uluguru inaungua moto, moto umekuwa ni janga kubwa sana kwenye milima hiI yenye utajiri mkubwa wa bayoanuai duniani. Maeneo mengi yamevamiwa na idadi ya watu inazidi kuiongezeka. Eneo hili la milima ya Uluguru inazungukwa na vijiji zaidi ya 50, na inakadiriwa kuwa na watu zaidi ya 150,000 wanaishi ndani ya milima ya Uluguru, idadi hiyo ikizidi kuongezeka kila siku.
Milima ya Uluguru inavyoonekana kwa sasa
Hali hii inaongeza mashaka na hatari kwa hifadhi za wanyama na misitu. Tafiti za jumla zinaonyesha zaidi ya mbili ya tatu ya watanzania wanaishi vijijini, na ni asilimia 17 tu ya watanzania ndio hutumia nishati ya umeme. Hii inamaanisha watanzania wengi tunategemea nishati ya kuni na mkaa kila siku. Mfano, taarifa za mwaka 2019 zinaonyesha mkoa wa Dar esaalamu unatumia tani za 1900 za mkaa kila siku.
Haya ni matumizi makubwa ya nishati ya mkaa katika maeneo ya mijini. Mahitaji haya makubwa ya mkaa, kuni na mazao mengine ya misitu ndio yanaongeza kasi ya uharibifu wa maeneo ya hifadhi ya misitu. Mfano, Tanzania inapoteza karibia hekari zaidi ya 469,000 za misitu kila mwaka kutokana na mahitaji ya watu. Shughuli za kilimo zinakadiriwa kuchangia kupotea kwa asilimia 10 ya maeneo muhimu ya hifadhi ya misitu kila mwaka hapa Tanzania.
Licha cha maeneo haya kukabiliwa na changamoto nyingi za kimazingira, bado ni maeneo yenye mvuto na yenye fursa nyingi za uwekezaji. Makala hii isingetosha kuelezea kila kitu kilichopo katika eneo hili la hifadhi ya milima ya Uluguru. Labda kwenye makala nyingine tutaongelea kuhusu vivutio vilivyomo katika maeneo haya.
Pamoja na hayo, serikali na wadau wengine wa mazingira na uhfadhi kama vile WWF wanafanya juhudi kubwa kunusuru uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji katika maeneo haya. Mfano, serikali kupitia gazeti la serikali namba 296, iliamua kutangaza eneo hili kuwa eneo la Hifadhi ya Msitu Julai, mwaka 2008, hii imepunguza sana uvamizi na kuongeza uhifadhi kwa kushirikiana na jamii za eneo hilo.
Hata hivyo, wadau wengine wanafanya kazi kubwa kuhakikisha usimamizi mzuri wa rasilimali, sio tu katika milima ya Uluguru, bali katika maeneo mengine ya hifadhi ya Milima ya Tao la Mashariki. Mfano, kazi nzuri inafanywa na Mfuko wa uhifadhi wa milima ya tao la mashariki yaaani, the Eastern Arc Mountains Conservation Endowment Fund (EAMCEF).
Sijui Mbaraka Mwinshehe akifufuka ataimba wimbo gani tena, huenda akaufuta wimbo wa Morogoro yapendeza usiwepo tena kwenye albamu yake. Lakini bado hatujachelewa sana, tunaweza kushirikiana na serikali na wadau wengine wa uhifadhi kwa kushiriki katika program mbali mbali za uhifadhi kama vile kupanda miti, kuzuia mioto kwenye maeneo ya hifadhi, kutunza vyanzo vya maji na kuelimisha wengine kufanya hivyo ili tuirudishe ile Morogoro ya Mbaraka Mwisnshehe.
Imeandikwa na Hillary Mrosso, +255 683 862 481, hmconserve@gmail.com