Chanzo cha picha: https://towardsdatascience.com/wildfire-destruction-a-random-forest-classification-of-forest-fires-e08070230276

Maana ya Moto Kichaa

Moto kichaa ni moto ambao hutokea kwa bahati mbaya au kusudi, ambao mara nyingi ni ngumu sana kuudhibiti. Katika maeneo yaliyohifadhiwa, moto huu unaweza kusababishwa na shughuli za binadamu, ukame, au asili kama radi. Moto kichaa ni tatizo kubwa linaloathiri mazingira, maisha ya viumbe hai, na uchumi nchini. Katika maeneo yaliyohifadhiwa kama hifadhi za taifa, mapori ya akiba, na misitu ya asili, moto kichaa una madhara makubwa zaidi, ukiharibu rasilimali ambazo ni muhimu kwa taifa.

 Historia ya moto kichaa

Moto umekuwa ukitumika Tanzania kwa miaka mingi katika kuandaa ardhi kwa ajili ya kilimo na malisho ya wanyama pamoja na shughuli za uwindaji, udhibiti wa wadudu waharibifu na kwa sababu nyinginezo za usimamizi wa ardhi.

Mioto inayoanzishwa na watu wa eneo husika huchangia kutengeneza mfumo wa ikolojia na viumbe hai katika nyika za misitu mbalimbali ya miombo. Katika shughuli za uhifadhi, moto ni nyenzo mojawapo ya ya kufikia malengo ya usimamizi na uhifadhi wa wanyamapori katika maeneo mbalimbali yalihofadhiwa nchini Tanzania. Unaweza kusoma makala hii kufahamu zaidi Tushiriki Kupiga Vita Uchomaji Holela Wa Moto Kwenye Maeneo Ya Hifadhi Za Wanyamapori Na Misitu.

Hata hivyo, uwiano unaofaa kati ya watu, moto na mazingira ya asili umekuwa mgumu kufikiwa kutokana na mabadiliko ya idadi ya watu, vitendo vya usimamizi wa ardhi na vikwazo katika njia za usambazaji wa maarifa yanayotumika katika usimamizi wa maliasili.

Kuna ongezeko la hofu juu ya hatma ya ongezeko la matukio ya moto na athari zake hasi katika misitu na maeneo ya mapori, pamoja na maisha ya binadamu katika hali iliyo na mabadiliko ya tabianchi. Tafiti za hivi karibuni kutoka kwenye picha za satelaiti zimeonyesha kuwa wastani wa hekta milioni 11 huungua kila mwaka nchini Tanzania.

 Uchomaji mwingi hutokea katika mikoa ya magharibi ya nchi na nyanda za juu kusini hasa Rukwa, Tabora, Kigoma na Mbeya, wakati katika maeneo ya Kusini Mashariki, mkoa wa Lindi huathiriwa zaidi na moto. Maeneo  yanayoathiriwa zaidi ni mapori na vichaka ambavyo hufikia takribani asilimia 70 ya ardhi inayoungua kila mwaka yenye wastani wa hekta milioni 6.8 kwa mwaka.

 Uunguaji mwingi hutokea kwenye maeneo yaliyohifadhiwa, kwa wastani wa hekta milioni 3.7 kwa mwaka katika hifadhi za misitu, hekta milioni 3.3 katika hifadhi za wanyamapori na hekta milioni 1.46 katika hifadhi za taifa, zikifikia jumla ya karibia hekta milioni 8.5 au asilimia 77 ya ardhi inayoungua kila mwaka nchini Tanzania. Mengi kuhusu moto kichaa na madhara yake unaweza kusoma hapa

Madhara ya Moto Kichaa Katika Maeneo Yaliyohifadhiwa.

  1. Uharibifu wa Mazingira
  • Makazi ya wanyamapori: Moto kichaa huharibu malisho na makazi ya wanyamapori kama simba, tembo, nyati, na ndege adimu.
  • Kupotea kwa mimea: Mimea muhimu kwa ajili ya mzunguko wa maji na hewa hupotea, na baadhi yake huwa haipatikani tena.
  • Mmomonyoko wa udongo: Moto unapoondoa mimea, udongo huwa wazi na rahisi kusombwa na maji au upepo, hivyo kusababisha mmomonyoko.
  1. Athari za Kiuchumi
  • Kupungua kwa utalii: Moto huharibu mandhari za asili zinazovutia watalii, hivyo kupunguza mapato yanayotokana na sekta ya utalii.
  • Gharama za kudhibiti moto: Serikali na wadau wa uhifadhi hutumia fedha nyingi kuuzima moto na kurejesha mazingira yaliyoharibiwa.    

Wanafunzi wa shahada ya kwanza ya uhifadhi kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya baada ya shughuli ya kudhibiti moto kichaa katika hifadhi ya taifa Ruaha. Picha na Yusto Godfrey

  1. Kupotea kwa viumbe hai
  • Moto huangamiza wanyama wadogo na viumbe vidogo kama wadudu na ndege ambao hawawezi kutoroka haraka.
  • Huharibu mnyororo wa chakula, kwani wanyama wanaotegemea mimea iliyoungua wanakosa chakula na hivyo kufa na wakati mwingine kuhama kutoka eneo moja kwenda jingine.
  1.  Uchafuzi wa Mazingira
  • Moshi kutokana na moto kichaa huchafua hewa, na masalia ya moto huongeza uchafuzi wa udongo na maji. Uchafuzi huu huathiri afya ya wanyama na hata binadamu wanaoishi karibu na maeneo ya hifadhi

Sababu za moto kichaa katika maeneo yaliyohifadhiwa

Shughuli za kibinadamu:

  • Uandaaji wa mashamba husababisha moto kichaa kutoka katika maeneo ya mashamba na hivyo kuvamia maeneo yalihifadhiwa na hivyo kushinwa kudhibitika.
  • uwindaji haramu ili kurahisha wawindaji kuona Wanyama kwa urahisi. Lakini pia wawindaji haramu hutumia moto ili kuweza kusababisha nyasi kuchipua na hivyo kuvutia wanyama wanaokula nyasi na kuwawinda kwa urahisi.
  • Uchomaji mkaa ambao hupelekea ukataji wa miti hovyo na kuacha moto ukiwaka katika matanula waliyotumia kuchoma mkaa na baadae kusambaa katika maeneo mbalimbali.
  • Ukame: Hali ya hewa kame husababisha moto kuenea haraka.
  • Radi: Moto wa asili unaweza kutokea kutokana na radi, hususan wakati wa mvua za msimu.

Mifano ya moto kichaa katika maeneo yaliyohifadhiwa Tanzania

  1. Hifadhi ya Taifa Mlima Kilimanjaro

Mwaka 2020, moto mkubwa uliteketeza hekari nyingi za misitu, ukiathiri mandhari ya mlima na kuharibu makazi ya wanyama na ndege wa eneo hilo. Kutokana na hilo, sekta ya utalii ilipata hasara kubwa kutokana na uharibifu wa mandhari na kuongezeka kwa uchafuzi wa hewa.

Chanzo cha picha: https://amp.dw.com/sw/mtafiti-wa-ujerumani-angazia-athari-ya-moto-uliotokea-mlima-kilimanjaro/a-55664876

  1. Hifadhi ya taifa ya Serengeti.

Moto kichaa mara kwa mara huharibu maeneo ya savanna, ambayo ni makazi muhimu kwa nyumbu, pundamilia, na simba.

Namna ya kukabiliana na moto kichaa

  1. Elimu kwa Jamii; Kuwahamasisha watu wanaoishi karibu na maeneo yaliyohifadhiwa kuhusu athari za moto kichaa na kufundisha mbinu salama za kilimo na uchomaji wa mashamba. Lakini pia kutoa taarifa za ujangiri kwenye mamlaka zinazohusika ili zizibitiwe haraka kwani tafiti zinaonyesha shughuli za ujangiri ndio chanzo kikuu cha moto kichaa katika maeneo yalio hifadhiwa.
  2. Udhibiti wa Shughuli za Binadamu; Kuwashirikisha wananchi katika mipango ya uhifadhi kama walinzi wa mazingira. Kuweka sheria kali na faini kwa wanaosababisha moto katika maeneo yaliyohifadhiwa.
  3. Kuimarisha Miundombinu ya Kudhibiti Moto, Kuongeza vifaa na rasilimali kwa vikosi vya zimamoto vinavyoshughulikia moto kwenye hifadhi.
  4. Kutumia teknolojia kama droni na satelaiti kwa ufuatiliaji wa moto mapema.

Hitimisho

Moto kichaa katika maeneo yaliyohifadhiwa nchini Tanzania una madhara makubwa yanayoathiri mazingira, uchumi, na maisha ya viumbe hai. Elimu kwa jamii, udhibiti wa shughuli za binadamu, na matumizi ya teknolojia vinaweza kusaidia kupunguza visa vya moto na kulinda maliasili za taifa. Ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha kwamba tunatunza mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.

Asante kwa kusoma makala hii hadi mwisho, makala hii imeandikwa na Daudi Jacob Kanyamaha, mwanafunzi anayesomea Shahada ya kwanza ya Sayansi ya Maliasili na Uhifadhi katika Chuo Kikuu cha Mbeya cha Sayanis na Teknologi, pia shukrani za pekee ziende kwa wahariri wa makala hii, Alphonce Msigwa, mwikolojia hifadhi za taifa Tanzania

 Kwa maswali, maoni, ushauri, mapendekezo, usisite kuwasiliana na mwandishi wa makala hii kwa mawasiliano hapo chini;

Daud Jacob Kanyamaha

0746423034

Kanyamaha.dj@gmail.com