Kila mwaka, mwezi Januari inafanyika sensa ya ndege wa maji yaani waterbird. Aina hii ya ndege ni wale ambao maisha yao yote wanategemea uwepo wa maji katika kujitafutia chakula, kuzaliana na pia kama makazi yao. Ni miongoni mwa kundi muhimu sana la ndege katika uhifadhi, utalii na Uchumi na huonekana sehemu zenye maji, kama vile maziwani, mitoni, baharini, kwenye mabwawa, au kwenye maeneo ya ardhi oevu yaani Wetlands.

Katika uhifadhi, ndege hawa hutumika kama kiashiria cha afya ya mifumo ya ikolojia ya mahali fulani, pia hutumika kusambaza mbegu, kula wadudu na kuweka sawia mifumo ya ikolojia ya majini na nchi kavu.

Hivyo basi kukosekana kwa ndege hawa sehemu zenye maji, ni ishara ya uharibifu wa mazingira kama vile uchafuzi wa maji, sumu au kupotea kwa chakula wanachokula ndegea hawa.

Tukiwa katika zoezi la kuangalia na kuhesabu ndege maji katika bwawa la maji lililopo ndani ya bustani ya miti ya SUA. Picha na Michael Kipilipili

Katika utalii, ndege hawa wamekuwa kivutio kikubwa  kwa wageni. Sehemu nyingi zenye mkusanyiko wa ndege hawa zimekuwa na mvuto wa kipekee kwa wageni na watu kwenda kutembelea na mfano mzuri ni ziwa Natroni lililopo mkoa wa Arusha nchini Tanzania ambapo ndege aina Heroe (flamingo) wamekuwa wakionekana katika makundi makubwa sana.

Kutokana na baadhi ya watalli wa ndani na nje kuvutiwa na utalii wa ndege, hivyo Taifa linapata fedha ambazo zinatumika katika uhifadhi na kujenga Uchumi imara wa nchi. Lakini pia hiki ni chanzo cha ajira kwa kuwa baadhi ya waongoza watalii ambao wameajiriwa kwa kuwa wabobezi kwenye kuongoza watalii kuona ndege hawa.

Picha ya pamoja WISASUA, HOWA na baadhi ya wahitimu walioshiriki zoezi la kuhesabu ndege maji katika eneo la Bustani ya miti SUA, Picha na HOWA

Nchini Tanzania, ambako kuna makazi na maeneo mengi yanayohifadhi ya ndege maji, serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori yaani Tanzania Wildlife Research Institute (TAWIRI), wanatoa wito kwa wadau mbali mbali wanaopenda kushiriki katika kuhesabu ndege hawa kwenye maeneo yao.

Lengo la kuhesabu ndege hawa ni kujua idadi yao, mwenendo wao na afya ya maeneo wanayopatikana. Kwasababu ndege hawa huchukuliwa kama kiashiria cha afya ya uhifadhi, husaidia kwa haraka kujua athari mbali mbali zinazoikabili sekta ya uhifadhi.

Kutokana na wito huo ambao umetolewa na TAWIRI, mwandishi wa makala hii pamoja na wadau wengine kama vile  Klabu ya ndege ya (HOWA), Chama cha Wanafunzi wa Sayansi ya Uhiifadhi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) Morogoro yaani WISASUA, na baadhi ya wahitimu wengine kutoka SUA, waliitikia wito huo na kushiriki katika zoezi la kuhesabau ndege maji katika eneo la Bustani ya Miti liliopo SUA kampasi kuu.

Wanafunzi wa Uhifadhi pamoja na wahitimu wengine kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kuhesabu ndege wa majini katika eneo la Bustani ya Miti. Picha na Hillary Mrosso

Baadhi ya ndege maji tuliofanikiwa kuwaona katika eneo hilo ni Pamoja na;

  1. African Open-billed Stork – Korongo Domonjia
  2. Long-tailed Cormorant – Mwani Mkia Mrefu
  3. African Jacana (Jesus Bird) – Kiundu or Kiswi
  4. Black Crake – Kifutu Cheusi
  5. Little Egret – Kware Mweupe Mdogo
  6. Malachite Kingfisher – Kidungi Kidogo
  7. Gray-headed Kingfisher – Kidungi Kichwa-Kijivu
  8. White-faced Whistling Duck – Bata Bukini Uso-Mweupe
  9. Hadada Ibis – Kwarara Hadada
  10. African Open-billed Stork – Korongo Domopengo
  11. Gray Heron – Korongo Kijivu
  12. African Jacana – Ndege-Maji (Kipondwa)
  13. Long-tailed Cormorant – Mbiha Mkia-Mrefu

Pamoja na mambo mengine, zoezi la kuhesabu ndege ni jumuishi na lina faida nyingi kwa wote wanaoshiriki, mfano utajifunza aina za ndege, makazi yao, chakula chao, na faida zake katika utalii. Kushiriki katika zoezi la kuhesabu ndege linakufanya ushiriki katika uhifadhi kwa ujumla, ni sehemu nzuri ya kuonyesha uzalendo na ulinzi wa rasilimali zetu.

Lakini pia kuhesabu ndege ni utalii tosha, utapata nafasi ya kutembea maeneo mapya na kuona viumbe wapya, uoto wa asili na pia utaburudika na kuufanya mwili wako kuwa na afya nzuri kwani ni sehemu ya mazoezi.

Hakuna gharama za kushiriki katika zoezi hili la kuhesabu ndege wa maji, hivyo sio kikwazo kwa mtu yeyote anayependa, inategemea na eneo linakofanyika zoezi hilo.

Huitaji ujuzi wa kuwajua ndege ndio ushiriki, zoezi hili ni kama utalii tu, utakutana na wanaojua ndege ambao  utajifunza kwao na kama utataka utajumuishwa kwenye klabu ya ndege ya mkoa au eneo hilo utajifuza kila siku.

Mwandishi wa makala hii akiwa katika zoezi la kuhesabu ndege maji katika eneo la bustani ya miti SUA; Picha na Michael Kipilipili

Pia ushiriki wako utakufanya kutaondoa msongo wa mawazo unaposhiriki zoezi la kuhesabu ndege, maana ni utalii tosha, utakuwa mbali na mitandao ya kijamii kwa muda, hivyo utauburudisha mwili wako na akili yako.

Vile vile ni Sehemu ya kufahamiana na watu wapya ambao unaweza kujifunza kwao vitu vingi kuhusu uhifadhi, wanyama, ndege na viumbe wengine, au fursa nyingine za Maisha. Hivyo, ni baadhi tu ya faida za kushiriki katika zoezi la kuhesabu ndege maji linalofanyika kila mwaka.

Mwisho kabisa, kuwaelewa ndege wanaotegemea maji kwenye maisha yao, itasaidia kueneza uhifadhi wake na kushirikii katika ulinzi wa makazi ya ndege hawa muhimu kwenye uhifadhi.

Kama utapenda kushiriki kwenye kuhesabu ndege maji, au hata zoezi lingine la kuwajua ndege unaweza kuwasiliana na mwandishi wa makala hii kwa barua pepe hapo chini au namba zake za simu.

Makala hii imehaririwa na Alphonce Msigwa; Mwikolojia kutoka hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA)

Hillary Mrosso: hmconserve@gmail.com  |+255-683-862-481

 

Tunaandika makala hizi ili watu waongezewe uelewa kuhusu kulinda na kutumia Maliasili muhimu bila kuathiri uwepo wao wa sasa na baadaye; kazi hii tunafanya kwa kujitolea na hakuna malipo yoyote, endapo umefurahia kazi zetu kutuunga mkono kwa kiasi chochote ili tupate nguvu, na ari ya kuandika makala nyingine nzuri, usisite kuwasiliana nasi kwa maelezo zaidi