
Picha ya Twiga katika hifadhi ya Taifa ya Nyerere; Picha na Hillary Mrosso
Twiga ni miongoni wa wanyamapori wa kipekee sana, upekee wao unawafanya wawe ni wanyama wanaovutia na wanaopendwa sana duninani. Hii inachangiwa na umbo lake kubwa na shingo ndefu kuliko wanyamapori wote.
Ni wanyama wanaopatikana barani Afrika pekee, ukienda Ulaya au mambara mengine wanafugwa kwenye bustani za wanyama. Twiga ni wanyama wanaotembea kwa madaha na maringo, hali ambayo inaongeza mvuto kwa watu wengi wanaomtazama.
Hata asili ya jina lake linahusishwa na namna anavyotembea kwa upekee, mfano, Waarabu walimuita “zaraf”, wakimaanisha ni mnyama anayetembea haraka na kwa madaha au maringo.
Twiga kwa kingereza anaitwa “Giraffe” na jina lake la kisayansi ni Giraffa camelopardalis. Ukiangalia hili neno camelopardalis. utaona kuna maneno mawili ambayo ni camel na pardalis, camel ni ngamia, na pardalis ni jina la kisayansi la chui, linaandikwa “pardus’ kwa kilatini.
Hii ni kwasababu walimuona twiga ana umbo lenye mchanganyiko wa wanyama wawili, ambao ni ngamia na chui. Ukiangali vizuri utaona mwili wa twiga unakaribia kufanana na ngamia, lakini ngozi yake inafanana na chui.
Mpangilio wa madoa yaliyopo katika ngozi ya twiga haifanani na twiga mwingine. Unaweza kuwaona twiga wengi sehemu moja, lakini wanatofautiana katika mpangilio wa madoa yao ya ngozi. Hawafanani kabisa.
Miguu ya mbele ni mirefu kuliko miguu ya nyuma, hivyo humsaidia kukimbia kwa haraka. Hata hivyo twiga dume ni mrefu na mkubwa zaidi kuliko twiga jike. Dume ana urefu wa mita 5.3, jike mita 4.2.
Twiga jike anabeba mimba kwa siku 453-464, sawa na miezi 15. Mara nyingi huzaa mtoto mmoja, na mtoto jike akifikia miaka 3-4 anaweza kuchukua mimba, dume akifikisha miaka 4 -7 anaweza kuzalisha jike.

Twiga katika hifadhi ya taifa ya Saadani: Picha na Leon Hermenegild
Kuna aina au spishi 4 za twiga duniani. Tafiti za mwanzoni kabisa zilionyesha kuna spishi 9 za twiga. Lakini baada ya tafiti za kina za mazingira yao na kuchunguza kwa makini vinasaba vya kila spishi za twiga waligundua kuwa kuna spishi 4 tu za twiga na sio 9 kama ilivyokuwa mwanzoni.
Watafiti wa twiga, kama vile Shirika la Uhifadhi wa Twiga walifanya tafiti hizo na kubaini kuna aina 4 za twiga. Lakini pia shirika hili ambalo limejikita kufanya tafiti za kina kuhusu twiga, imesaidia sana sehemu nyingi Africa ambako kuna twiga.
Spishi 4 za twiga ni kama ifuatavyo;
- Twiga wa Kimasai, Masai (G. tippelskirchi), –Tanzania and Kenya -45,400
- Twiga wa Kaskazini-Kusini mwa Chadi, Northern (G. Camelopardalis), CAR, DRC, W. Sudani-5900
- Twiga wa Madoa ya Wavu, Reticulated (G. reticulata), Ethiopia, Somalia and Kenya- 15,950
- Twiga wa Kusini, Southern (G. giraffa)- Botswana, Namibia, Zimbabwe, Zambia, SA-49,850
Tanzania tuna Twiga wa Kimasai au masai giraffe. Hii ni aina moja tu ya twiga iliyopo Tanzania. Lakini pia Tanzania ndio nchi yenye twiga wengi zaidi barani Afrika. Twakwimu kutoka TAWIRI zinaonyesha tuna zaidi ya twiga 28,850.
Twiga ni mnyama wa taifa la Tanzania, ni mnyama anayeheshimika na kupendwa, ndio maana serikali imezuia mnyama huyu kuwindwa.
Kutokana na upekee wa mnayama huyu, serikali ya Tanzania iliamua kumfanya awe ni mnyama wa taifa. Utaona picha ya mnyama huyu ikitumika kama nembo kwenye maeneo mbali mbali. Mfano, kwenye fedha kuna nembo ya twiga, kwenye baadhi ya nyaraka za serikali kuna nembo ya twiga.
Hata Banki ya Taifa ya Biashara NBC, wanatumia nembo yenye picha ya twiga. Shirika la umeme Tanzania TANESCO nao wanatumia nembo yenye picha ya twiga. Bidhaa mbali mbali pia zina nembo zenye picha ya twiga, mfano kiwanda cha simenti cha twiga, shule nk wanatumia twiga kama nembo yao.

Nembo au logo ya benki ya taifa ya biashara ikiwa na picha ya twiga
Wengi wanavutiwa na mnyama twiga na kuweka kama alama ya ufahari na mvuto. Ukienda kwa wale watu wanaochonga vinyago utaona nao wamechonga vinyago vingi vya wanyama mbali mbali, lakini huwezi kukosa kinyago cha twiga.
Kuna wengine wamefikia hatua ya kununua vinyago vya twiga na kuviweka nyumbani kwao kama urembo fahari na upekee. Hii inaonyesha ni kwa jinsi gani binadamu tunapenda wanayama na pia tuna mahusiano na viumbe wengine wanaotupa furaha.
Hata mashirika makubwa dunani mfano Shirika la Kimataifa la Ufalidhili kwa Watoto UNCEF wanatumia nembo ya twiga, ikimaanisha maono na ukuaji.
Matumizi ya twiga ni makubwa sana, picha za twiga, alama za twiga, nembo za twiga, vinyago vya twiga kwa watu binafsi, mashirika, makampuni na serikali zimekuwa zikitumia mnyama huyu wa kipekee.
Hata hivyo, lincha ya kuwa ni mnyama anayependwa sana, na kutumika sehemu mbali mbali kama nembo, picha au vinyago, twiga ni wanyama wanaokabiliwa na changamoto kubwa ya ujangili.
Twiga wengi wanawindwa kwa njia haramu kwasababu ya nyama, kitoweo, ngozi, dawa na Imani. Idadi ya twiga ilishuka kwa kasi sana, kwa kipindi cha miongo mitatu iliyopita, twiga wamepungua kwa silimia 30.
Hii ndio imesababisha hata Shirikika la Kimataifa la Hifadhi ya viumbe Mwitu na Mazingira (IUCN). limewaweka twiga kwenye kundi la wanyama walioko hatarini kutoweka yani Vulnerable, hii ni kwa mujibu wa taarifa yam waka 2016. Idadi ya twiga duniani kwa sasa inakadiriwa kufikia 177,000.
Hii ni idadi ndogo sana, tunatakiwa kuchukua hatua za haraka kuzuia ujangili wa twiga, biashara haramu za twiga, kugongwa na magari, magonjwa ya ngozi na kulinda makazi ya twiga. Shirikiana na serikali, wadau, na mamlaka za uhifadhi wa wanyamapori katika uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yake.
Asante kwa kusoma makala hii! Karibu tuendelee kujifunza zaidi na kufahamu mengi kuhusu twiga na wanyama wengine, washirikishe wengine makala hii.
Hillary Mrosso: hmconserve@gmail.com |+255-683-862-481
Tunaandika makala hizi ili tuongeze uelewa wetu kuhusu wanyamapori, tunaamini tukipata uelewa tutachukua hatua kushiriki katika uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yake asilia.Kazi hii tunafanya kwa kujitolea na hakuna malipo yoyote, endapo umefurahia kazi zetu unaweza kutuunga mkono kwa kiasi chochote ili tupate mtandao, vifaa vyua kufanyia kazi kama kamera na komputa. Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana kwa mawasiliano haya; hmconserve@gmail.com |+255-683-862-481