Maeneo ovevu au wetlands, maeneo haya yanajumuisha mabwawa, maeneo yenye unyevu, mambonde yenye unyevu na maji, mito, maziwa na maeneo yote yenye matope kwasababu ya kuwa na maji muda mwingi.
Maeneo oevu yana faida nyingi sana kwa binadamu na kwa viumbe hai wengine. Taarifa yam waka 2022 kutoka shirika la chakula duniani FAO inayonyesha kuwa asilimia 40% ya uzalishaji wa samaki duniani unatoka katika maeneo oevu.
Hata hivyo, maeneo haya ni muhimu sana kama makazi ya aina nyingi za samaki. Samaki aina nyingi huzaliana na kupata hifadhi na chakula cha kutosha kutoka katika hifadhi ya maeneo oevu.
Hifadhi ya maeneo haya imesaidia sehemu kubwa ya maisha ya mamilioni ya watu katika kilimo, uvuvi na upatikanaji wa maji kwa ajili ya matumizi muhimu ya nyumbani na viwandani, kilimo cha umwagiliaji.
Ardhi oevu ni maeneo yenye rutuba nyingi, hivyo hufaa kwa kilimo cha aina mbali mbali kama vile mpunga, mahindi, miwa, migomba, viazi, mboga mboga nk. Mfano, maeneo ya bonde la Kilombero, bonde la Usangu, Mbarali, Rufiji, Mtera nk. Ni maeneo muhimu sana kwa uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.
Upatikanaji wa maji, maeneo haya yamekuwa sehemu salama kwasababu yanahifadhi maji mengi hasa katika kipindi cha ukame. Pia maeneo haya yanachuja maji na kuyafanya kuwa salama kwa matumizi, ni maeneo yanaweza kuhifadhi maji ya ziada ambayo yanaweza kusababisha mafuriko.
Mchango wa maeneo oevu kwenye uhifadhi wa wanyamapori ni mkubwa sana, spishi nyingi za wanyamapori kama vile kuro, viboko, mamba, na aina nyingi za wanyama wanategemea sana hifadhi ya ardhi oevu kwa ajili ya chakula, makazi na kuzaliana. Mfano, ziwa Natroni, bonde la Kilombero, Ruaha, Usangu, Rufiji ndani ya hifadhi ya Taifa ya Nyerere ni maeneo oevu ya uhifadhi wa wanyamapori.
Idadi kubwa ya ndege maji na ndege wanaohama hupatikana katika maeneo haya, ndege maji wanategemea sana maeneo haya kujipatia chakula, kuzaliana na kujilinda, mfano ndege maji aina ya heroe (flamingo) wa ziwa Natroni. Tafiti zinaonyesha maeneo oevu yanasaidia kuhifadhi asimilia 40 ya spishi wote wa ndege duniani.
Viumbe hai jamii ya amfibia, reptilian, wadudu mfano vyura, nyoka, mijusi na aina nyingine nyingi za wadudu wanapatikana katika maeneo oevu. Viumbe kama amfibia na reptilia ni viumbe wepesi sana kuathiriwa na ukame au uharibifu wa mazingira, hivyo maeneo ya ardhi oevu ndio kimbilio lao.
Licha ya umuhimu mkubwa wa maeneo haya katika uhifadhi, maeneo haya hasa yale yaliyopo katika fukwe za bahari kama vile maeneo ya misitu ya mikoko, husaidia sana kuzuia uharibifu unaoweza kusababishwa na mawimbi ya bahari au mafuriko.
Uwepo wa maeneo oevu unasaidia sana kukua na kusitawi kwa misitu ya mikoko ambayo husiadia kulinda majengo, mafuriko na majanga mengine yanayoweza kuletwa na maji ya bahari.
Maeneo oevu yana uwezo mkubwa wa kutunza na kuhifadhi kaboni kwa kiasi kikubwa sana kuliko misitu na maeneo mengine. Uwezo huu husaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi na ukame.

Picha ya eneo oevu, by Hillary Mrosso
Hata hivyo, kwasababu maeneo haya yana mkusanyiko mkubwa wa ndege na wanyama wengi, yamekuwa kivutio kukubwa kwa watalii. Watalii wanatembelea maeneo haya kwa ajili ya kuvua samaki, kuendesha boti, kuangalia ndege au kupumzika katika fukwe.
Maeneo haya yana mandhari nzuri na utulivu mkubwa, hivyo huwa na maji masafi na hewa nzuri. Hivyo ni maeneo yenye mvuto na yanachangia sana kukuza uchumi wa nchi kupitia utalii unaofanyika maeneo haya.
Licha ya faida zote hizo, maeneo haya yanakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinatishia kupungua, kutoweka na kuharibika kwa maeneo haya muhimu.
Mfano, ujenzi holela karibu na maeneo oevu umesababisha uchafuzi wa maeneo haya, ambao umechangia viumbe hai kufa kwasababu ya uchafuzi wa mazingira na maji.
Kilimo holela, maeneo haya yanakabiliwa na changamoto kubwa la ongezeko la shughuli za kilimo kwenye maeneo haya oevu. Mfano kilimo cha mpunga katika bonde la Usangu inachangia kupungua kwa maji katika mto Ruaha mkuu.
Maeneo haya ni rahisi sana kuharibiwa kutokana na kutopewa kipaumbele. Na jamii haifahamu sana umuhimu wa maeneo haya ya ardhi oevu. Tunatakiwa kuyalinda maeneo haya kwa nguvu zetu zot
Nimetaja tu faida chache za maeneo haya, lakini bila maeneo haya tunaweza kupata majanga mengi sana ya mafuriko, ukame, magonjwa, njaa, na kukosa mapato.
Ni muhimu tukashiriki katika ulinzi wa maeneo haya, kama vile kushiriki katika mikutano ya utoaji elimu ya mazingira, kushiriki zoezi la kupanda miti, kuepuka kulima au kuchafua maeneo ya ardhi oevu.
Kwa ufupi naamini umepata maarifa kidogo kuhusu umuhimu wa kuhifadhi maeneo ya ardhi oevu kwa manufaa ya uhifadhi, uchumi na utalii.
Asante, tukutane kwenye makala nyingine!
Hillary Mrosso|+255 683 862 481| hmconserve@gmail.com
Tunaandika makala hizi ili tuongeze uelewa wetu kuhusu wanyamapori, tunaamini tukipata uelewa tutachukua hatua kushiriki katika uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yake asilia.Kazi hii tunafanya kwa kujitolea na hakuna malipo yoyote, endapo umefurahia kazi zetu unaweza kutuunga mkono kwa kiasi chochote ili tupate mtandao, vifaa vyua kufanyia kazi kama kamera na komputa. Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana kwa mawasiliano haya; hmconserve@gmail.com |+255-683-862-481