Uwepo wa wanyamapori katika maeneo mbalimbali yaliyohifadhiwa nchini Tanzania umekuwa kichocheo kikubwa cha kukua kwa sekta ya utalii. Shughuli mbalimbali za utalii ambazo huhusisha kukutana na wanyamapori kwenye mazingira yao zimeendelea kuwa na mvuto mkubwa.
Shughuli hizi ndani ya hifadhi za taifa zinaweza kuwa kwenye makundi makubwa manne; shughuli za vyombo vya moto nchikavu kwa kutumia magari, majini kwa kutumia boti zenye injini na angani kwa kutumia puto inayorushwa kwa gesi na ya mwisho ni matembezi ya miguu na upandaji wa farasi.
Sio kila hifadhi huruhusu kufanyika kwa shughuli hizi lahasha zinategemea na mazingira wezeshi ya hifadhi husika.
Hii imepelekea baadhi ya shughuli kufanyika kwa hifadhi chache na hivyo hifadhi husika kujitwalia upekee mkubwa na kuwekwa kwenye mkakati wa kutangaza na kuvutia watalii wengi zaidi.
Shughuli zinazofanyika katika hifadhi za taifa nyingi na kufahamika zaidi ni pamoja na utalii wa kuangalia wanyamapori ukiwa ndani ya gari, kupanda milima na kupiga kambi kwenye hema.
Leo tutajifunza zaidi kwa zile zenye upekee mkubwa japokuwa shughuli zote za kitalii zinakulazimu kuzingatia na kufuata kanuni na taratibu kabla na wakati wa kuzifanya kama zilivyoainishwa na shirika la hifadhi za taifa Tanzania.
Kwa shughuli tajwa hapo chini lazima uwe na askari mwenye silaha, mavazi/ vifaa wezeshi vya shughuli husika, lazima uzingatie muda, idadi ya watalii na umri.
Safari ya puto/ baluni inayorushwa kwa kuungua kwa gesi hewani
Shughuli hii imekuwa ikifanyika ndani ya hifadhi za taifa Ruaha, Serengeti na Tarangire. Inasaidia watalii wengi kuona eneo kubwa na vivutio vingi kwa mara moja na muda mchache.
Safari hii inawawezesha watalii kuwaona wanyamapori na mito mikubwa kwa juu, misitu na kupata picha nzuri ya mandhari ya hifadhi husika. Pia aina hii ya utalii husaidia zaidi kuufurahia upepo na hewa ya angani.

Baloon likiwa angani na watalii huku gesi inayotumika kulirusha ikionekana

Puto lenye watalii juu ya tembo ndani ya hifadhi ya TaifaSerengeti; picha na Hemedi Rasuli
Safari za usiku za kuangalia wanyamapori
Shughuli hii ya utalii hufanyika katika hifadhi za taifa nyingi kwa lengo la kutafuta / kuona wanyamapori wa usiku ambao wengi ni jamii ya paka kama vile simba na chui.
Pia shughuli hii hufanyika kwa lengo la kutazama/ kusoma anga hususani mwezi na nyota lakini pia kuufurahia utulivu wa wanyamapori wakati wa usiku kwa kuwa huwa wametulia na kulala.

Mama simba akiwa na watoto wake barabarani usiku, hifadhi ya taifa Ruaha; picha na Leena Lulandala.
Matembezi ya miguu ndani ya hifadhi
Aina hii ya utalii hufanyika zaidi hifadhi ya taifa ya Ruaha, Serengeti, Udzungwa, Nyerere pia Tarangire ambapo wageni huvutiwa zaidi kwani hupata fursa ya kukutanishwa na mazingira asili ya wanyamapori,
Husaidia kuwafahamu kwa ukubwa viumbe wadogo ambao sio rahisi kuwaona ukiwa kwenye gari mfano wadudu pia ni namna nzuri ya kusoma nyayo/ kwato za wanyamapori.
Matembezi haya yamegawanyika katika makundi mawili, matembezi mafupi (hufanyika ndani ya masaa manne tu) na matembezi marefu ambayo ni zaidi ya masaa manne.

Watalii wakiwa katika matembezi ya miguu, hifadhini Ruaha; picha na Leena Lulandala
Safari ya uendeshaji wa mitumbwi na boti
Utalii huu hufanyika zaidi hifadhi za taifa za Arusha – ziwa Momella, Ziwa Manyara pia Nyerere – mto Rufiji na katika ziwa Nzelekela pia Siwandu. Unaweza kusoma hapa zaidi
Aina hii ya utalii hufanyika kwenye baadhi ya maeneo ya mito na maziwa yaliyokubalika na uongozi wa hifadhi ya taifa husika.
Utalii huu hulenga zaidi kufurahia viumbe vya majini kama mamba, kiboko, samaki na ndege, mimea, maua pia kusoma mito na kuona jinsi ilivyojengeka. Inakufanya kuwaona wanyamapori wengine kwa ukaribu wanavyokunywa maji.

Watalii wakishuka kwenye boti ndani ya mto Ruaha mkuu, hifadhini Ruaha; picha na Anderson Mgesi.
Utalii wa kula chakula hifadhini
Hii ni aina nyingine ya utalii inayofanywa kwa lengo la kuongeza ukaribu na mazingira asili kwa jinsi ya utulivu wakati wa kula.
Chakula hiki na vinywaji kinaweza kuwa kile ambacho kimefungwa kwenye box/ mifuko au kile cha kupika moja kwa moja porini wakati wa asubuhi au wakati wa usiku.
Hii husaidia kuongeza uwezo wa kuvumbua vitu vipya kwenye eneo husika na hupendelewa wakati wa jua kuzama; ukipata nyama kavu, karanga, kurosho, biskut na vinywaji baridi. Aina hii ya utalii hufanywa ndani ya hifadhi zote za taifa na mara nyingi huwa kwenye vibanda maalum vilivyojengwa au maeneo ya wazi.

Chakula kilichoandaliwa kwa ajili ya watalii, hifadhini Ruaha; picha na Leena Lulandala
Safari ya uendeshaji wa farasi ndani ya hifadhi
Hii ni aina ya utalii ambao hufanywa kama sehemu ya kuwa jirani zaidi na mazingira asili kwa kuendesha farasi. Utalii huu pia hufanywa kwa lengo la kuimarisha mifumo ya mwili na ubongo (hufanywa kama sehemu ya zoezi), kupunguza msongo wa mawazo na inasaidia kuongeza umakini na ujasiri kwa anayefanya kwa sababu unahitaji ujasiri mkubwa na umakini wa kuongoza farasi.

Watalii wakiwa wanaendeshai farasi; picha na Daudi Mollel
Safari ya kutembea kwenye madaraja ya juu ya msitu na mito hifadhini
Aina hii ya utalii husaidia kuona sehemu ya juu ya wanyamapori na kufurahia viumbe wa juu wa msitu kama vile vipepeo, jamii mbali ya nyani na ndege hasa kwa daraja la juu la ziwa Manyara.
Daraja hili la ziwa Manyara ndilo daraja la juu refu zaidi barani Afrika, likiwa na umbali wa mita 370. Aina hii ya utalii hufanyika pia katika daraja la juu ya mto Mdonya hifadhini Ruaha pia hifadhi ya taifa ya Udzungwa.

Daraja la juu ya mto ndani ya hifadhi ya taifa Ruaha; picha na Wolfgang Sagari
Mchezo wa kuvua Samaki hifadhini
Ambao hufanyika katika hifadhi za Taifa Ruaha, Nyerere, Rubondo, Kisiwa cha Saanane na Burigi-Chato.Shuguli hii ya utalii humsogeza zaidi mtalii jirani na mazingira asili haswa ya majini hivyo kujifunza zaidi.
Utalii huu hufanyika katika mito mikubwa au maziwa yenye samaki ambayo hulenga zaidi samaki aina ya kambale na jamii nyingine ya tilapia. Katika ufanyaji wa shughuli hii husaidia utulivu wa akili, kuongezeka umakini na furaha.

Watalii katika mchezo wa kuvua samaki na kurudisha mtoni, hifadhini Ruaha; picha na Leena Lulandala
Naamini mpendwa msomaji wetu wa makala umejifunza vitu vingi na umeelewa kwa upana shughuli hizi za utalii, hivyo siku utakapofanya safari yako ya utalii hifadhini utafanya chaguo sahihi la shughuli za kitalii. (Sehemu kubwa ya makala hii imetafsiriwa kutoka chapisho la mamlaka ya hifadhi ya taifa TANAPA, unaweza kuisoma kwa kubonyeza hapa
Imeandaliwa na Leena Lulandala na kuhaririwa na Alphonce Msigwa
Leena Lulandala – +255 755 369 684|| leenalulandala0@gmail.com
Tunaandika makala hizi ili tuongeze uelewa wetu kuhusu wanyamapori, tunaamini tukipata uelewa tutachukua hatua kushiriki katika uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yake asilia.Kazi hii tunafanya kwa kujitolea na hakuna malipo yoyote, endapo umefurahia kazi zetu unaweza kutuunga mkono kwa kiasi chochote ili tupate mtandao, vifaa vyua kufanyia kazi kama kamera na komputa. Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana kwa mawasiliano haya; hmconserve@gmail.com |+255-683-862-481