Hifadhi yetu ya Taifa ya Serengeti imekuwa ikituwakilisha vyema kiukanda, barani Afrika na duniani kwa ujumla kupitia tuzo hii ya hifadhi bora barani Afrika inayoandaliwa na shirika binafsi, World Travel Awards.

Serengeti imekuwa ikishinda tuzo hii adhimu kwa miaka saba sasa mfululizo, 2019 – 2025.

Shirika hili la World Travel Awards lenye makao makuu mjini London – Uingereza, limekuwa likijihusisha katika uandaaji na ugawaji wa tuzo mbalimbali katika sekta ya utalii, usafiri, hotelia na huduma kwa wageni.

Tuzo hizi zimekuwa kama sehemu ya kutambua na kupongeza ubora na juhudi kubwa za uhifadhi wa hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Wawakilishi wa Tanzania waliopokea tuzo ya hifadhi bora barani Afrika, hifadhi ya taifa ya Serengeti 2024; picha na World Travel Awards

Tuzo hii ilianzishwa mwaka 2013 ikiwa na wawaniaji sita, ambao ni;

  • Hifadhi ya taifa ya Serengeti – Tanzania,
  • Maasai Mara – Kenya,
  • Etosha – Namibia,
  • Kidepo – Uganda,
  • Kruger – Afrika kusini na
  • Central Kalahari nchini Botswana.

Wawaniaji hawa idadi yao imekuwa hivyo kwa miaka yote isipokuwa mwaka huu 2025, Maasai Mara – Kenya imejitoa katika orodha.

Hifadhi hizi zimekuwa zinafuata taratibu za usajili na uandikishaji, kisha kufuatiwa na upigaji kura wa wazi wenye kuruhusu watu wote kupiga kura. Baada ya hapo, shirika hufanya mchujo na mwishowe kutangaza mshindi.

Mshindi wa kwanza wa tuzo hii kwa miaka sita mfululizo ni hifadhi ya Maasai Mara nchini Kenya, (2013 – 2018) kisha kupokelewa na hifadhi yetu ya taifa ya Serengeti kwa miaka saba mfululizo, 2019 – 2025.

Tuzo ya mwaka 2025 iliyotolewa jijini Dar es salaam – Tanzania, tarehe 28 Juni.

Tuzo hii ya hifadhi bora barani Afrika, ni miongoni mwa tuzo kubwa sana za kikanda barani Afrika, ikifuatiwa tuzo ya Kivutio bora cha utalii barani Afrika na Eneo Bora la Safari Duniani.

Ukubwa wa tuzo hizi umesababishwa na chachu yake katika kutangaza vivutio vyetu vya utalii na kuvutia uwekezaji wenye tija.

Hifadhi zinazowania tuzo hii, ni hifadhi bora barani Afrika na duniani kwa ujumla zenye vigezo vifwatavyo; –

Uzoefu wa mgeni; hapa kuna mambo mengi sana ambayo yanategemea juhudu jumuishi za hifadhi, wawekezaji na wamiliki wa kampuni za utalii, hoteli na kambi.

Mandhari nzuri ya miundombinu ya nyumba za wageni, zikiwa zimejengwa kuzingatia mazingira asilia kabisa; Picha kutoka Serengeti National Park, https://www.serengetiparktanzania.

Juhudi hizi kwa pamoja zina nafasi kubwa ya kumfanya mgeni afurahie safari yake hivyo kuitangaza hifadhi kwa ukubwa na hata kupiga kura kwa urahisi.

Juhudu hizi huanzia kwenye ubora wa miundombinu ya hifadhi husika kama vile barabara, mitandao, viwango vya ubora wa hoteli na kambi, huduma zinazotolewa pamoja na watoaji huduma, upatikanaji wa habari sahihi, ulinzi na usalama wa hifadhi husika na nchi kwa ujumla pia aina mbalimbali za shughuli anazoweza kuzifanya.

Vile mgeni anavyojisikia kuanzia kupokelewa, atakavyohudumiwa hotelini/ kambini ile miingiliano na wafanyakazi, pia upatikanaji wa taarifa wa wazi na sahihi husaidia kumridhisha mgeni na hivyo kuongeza nafasi kubwa sana ya kuwania tuzo hii.

Athari za uhifadhi; kigezo hiki huangaza katika athari chanya za uhifadhi. Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, kupitia shirika la hifadhi za Taifa TANAPA, imewekeza juhudi nyingi katika uhifadhi endelevu wenye matokeo chanya kama vile ongezeko la idadi ya wanyama ndani ya mifumo ya ikolojia.

Juhudi hizo ni pamoja na ufanyaji doria usiku na,mchana, angani na nchi kavu kuhakikisha usalama na utulivu wa binadamu na wanyama.

Pia sheria zenye kuonya na kuzuia uendeshaji mbaya wa magari hifadhini zimewezesha hifadhi ya Serengeti kushuhudia ongezeko kubwa la wanyama kama nyati na tembo.

Kupungua kwa changamoto za ujangili umechangia wanyama kuongezeka na kuifanya hifadhi ya Serengeti kuwa na mvuto na mandhari nzuri .

Uhifadhi chanya pia unahusisha kusaidia jamii za pembezoni mwa hifadhi katika kubuni na kuanzisha miradi ya kiuchumi kwa mfano utengenezaji na uuzaji wa shanga, picha za wanyama, vikoi na shuka za kimasai. Juhudi zote hizi huchangia kuwezesha shughuli za utalii ndani ya hifadhi.

Bayoanuai ya viumbe na mifumo ya ikolojia ndani ya hifadhi; Viumbe hai kama vile ndege, wanyama, wadudu na mimea ndani ya mifumo ya kiikolojia huwezesha mlinganyo wenye kuleta usawazishi baina yao.

Ndani ya hifadhi tunaona viumbe mbalimbali wakubwa kwa wadogo wenye kupeperusha vyema bendera ya Serengeti kwa mfano nyumbu, pundamilia, jamii mbalimbali za swala.

Pia Seregeti ni miongoni mwa hifadhi zinazotunza spishi zilizoko hatarini kutoweka katika uso wa nchi kwa mfano faru weusi, mbwa mwitu na jamii nyingi za tumbusi.

Bayoanuai hizi zote huchangia sana katika kumfanya mgeni kuifurahia safari yake hivyo huzingatiwa zaidi katika mchuano wa tuzo hii.

Utalii endelevu; aina hii ya utalii huhimiza zaidi kupunguza uzalishaji wa uchafu pia unagusa maisha ya jamii jirani kupititia ajira na uchangiaji wa mifuko ya maendeleo ya jamii.

Mandhari nzuri na yenye mvuto ya Hifadhi ya Taifa; Picha na Kjekol

Aina hii ya utalii hulenga wamiliki na wawekezaji wa utalii katika matumizi bora ya vifaa, mifumo na sheria wezeshi za utunzaji taka pia huhimiza utumiaji wa nishati bora kama ya jua.

Kambi na hoteli nyingi ndani ya hifadhi ya Serengeti hutumia nishati ya umeme wa jua kuendesha shughuli zao mfano kuchaji ‘golf car’ kwa matumizi madogo ndani ya kambi.

Baadhi ya kampuni gari zao zimekuwa zikitumia nishati hii ya umeme wa jua kuendeshea gari za watalii kama vile Miracle experience, hivyo kupunguza uchafuzi wa hali ya hewa.

Utalii huu endelevu pia umekuwa msaada katika kutunza na kuheshimu tamaduni za wazawa kama vile Wamaasai kuishi kwenye boma zao na Wahadzabe kuishi msituni. Zaidi soma makala hii Fahamu Vichochezi Tisa (9) vya Kusaidia Kutangaza na Kukuza Utalii Duniani

Mashirika mbalimbali duniani yamekuwa yakijitokeza kusisitiza aina hii ya utalii ili kutunza na kusimamia usalama kwa binadamu na wanyama.

Uzuri wa asili wa hifadhi; uzuri huu huzingatiwa kwenye uasilia wa eneo husika pamoja na viumbe wake, mimea mbalimbali, aina za uoto na jiographia nzima kama vile milima, miinuko na tambarare za nyasi.

Makundi ya Nyumbu yakiwa yanavuka mto Mara katika hifadhi ya taifa ya Serengeti. Picha na Janie Nikola

Hifadhi ya Serengeti ina uzuri wa asili mkubwa kuanza na aina za wanyama wengi wenye kuvutia ndani ya tambarare kubwa ya nyasi fupi.

Pia hifadhi yetu imepabwa kwa mawe makubwa na miamba inayochangia uzuri wake, ikijaziwa na uoto wa aina tofauti tofauti wenye kusaidia ukuaji na muingiliano mzuri wa wanyama ndani ya hifadhi.

Tuzo hizi zina mchango mkubwa sana katika sekta ya utalii hasa kwenye kutangaza na kukuza jina la nchi na hifadhi husika.

Tuzo hizi zimekuwa chachu katika kuhamasisha juhudu za nchi kwenye kuendeleza na kutunza vivutio vyetu.

Na hivyo kufananishwa na tuzo za Oscar ambazo ndizo tuzo kubwa sana duniani katika uwanja wa filamu.

Kwa nafasi hii mpendwa msomaji naamini utakuwa balozi mzuri wa kuhamasisha upigaji kura, utunzaji mazingira na kudumisha utalii endelevu.

Kwa maoni na ushauri usisite kuwasiliana na mwandishi wa makala hii kwa mawasiliano hapo chini

 Leena Lulandala – +255 755 369 684|| leenalulandala0@gmail.com

 

Tunaandika makala hizi ili tuongeze uelewa wetu kuhusu wanyamapori, tunaamini tukipata uelewa tutachukua hatua kushiriki katika uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yake asilia.Kazi hii tunafanya kwa kujitolea na hakuna malipo yoyote, endapo umefurahia kazi zetu unaweza kutuunga mkono kwa kiasi chochote ili tupate mtandao, vifaa vyua kufanyia kazi kama kamera na komputa. Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana kwa mawasiliano haya; hmconserve@gmail.com  |+255-683-862-481