Utangulizi

Katika misitu, mashamba na karibu na makazi ya watu, nyakati za usiku husikika sauti zisizo za kawaida.

Jua linapozama huamka ndege wawindaji ambao mara nyingi huonekana kama ishara ya jambo baya, na ndege hao ni bundi.

Lakini je, kweli bundi ni ishara ya kifo au ni viumbe muhimu wanaostahili heshima na ulinzi?

Makala hii inalenga kubainisha uhalisia wa maisha ya bundi, upekee wao wa kisayansi, changamoto wanazopitia kutokana na imani za kishirikina, na hitaji la haraka la kuwaelimisha watu juu ya umuhimu wa kuwalinda.

Upekee wa Bundi

Bundi ni ndege wa kipekee wanaofanya shughuli zao usiku, japo zipo jamii chache za bundi hufanya shughuli zao mchana.

Wana uwezo mkubwa wa kuona gizani, kusikia sauti kwa usahihi mkubwa, na kuruka kimya kimya bila kusikika kabisa.

Hii huwafanya kuwa wawindaji hodari wa panya, nyoka, ndege, popo, wadudu na viumbe wengine wadogo, hivyo kusaidia kulinda afya ya mazingira na mashamba ya watu.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye aina za bundi ambao hawapatikani sehemu nyingine duniani kama bundi mtiti wa Sokoke (Otus ireneae) na bundi-tai wa Usambara (Bubo vosseleri). Soma hapa kufahau zaidi aina za bundi waliopo Tanzania

Hawa bundi ni wa pekee sana na wako hatarini kutoweka kutokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Licha ya umuhimu wao wa kisayansi, bundi wanakabiliwa na changamoto kubwa zinazotokana na uharibifu wa mazingira, imani potofu, mila zinazochochea matambiko, na biashara haramu.

Pichani kushoto ni Bundi-tai wa Usambara, na kulia ni Bundi mtiti wa Sokoke; Picha na Ezra Mremi

Mila na Imani Zinazohusishwa na Bundi Nchini Tanzania na Afrika Mashariki

Katika jamii nyingi za Kiafrika, bundi huonekana kama viumbe wa ajabu au alama za bahati mbaya. Baadhi ya watu huamini kuwa kuonekana kwa bundi juu ya paa ni ishara ya kifo au mkosi.

Wengine huamini kwamba sauti ya bundi ni wito wa roho, ambapo huamini washirikina wamekuja kwa njia ya ndege hao kuchukua uhai wa mtu. Soma hapa kufahamu zaidi kuhusu mila na imani potofu kuhusu bundi

Lakini hatari kubwa zaidi ni imani kuwa mayai ya bundi yana nguvu za kishirikina.

Biashara ya Mayai ya Bundi na Bundi Hai

Katika maeneo mbalimbali ya Tanzania, tumeweza kufanya mahojiano na watu waliowahi kushiriki au kushuhudia biashara ya mayai ya bundi.

Kwa mujibu wa maelezo yao, baadhi ya watu huamini kuwa mayai ya bundi yakitazamwa kupitia darubini yanaonesha michoro au alama maalum zinazofanana na umbo au mpangilio wa nyota, misikiti, au makanisa.

Umbo hilo huaminika kuwa na nguvu za kichawi au tambiko, na linaweza kutumika kuleta mafanikio ya biashara au utajiri.

Katika hali hii:

  • Mtu akikutwa na yai la bundi, huambiwa asiliguse kwa mkono wala mwili wake wote usigusane nalo.
  • Badala yake, yai hubebwa kwa kipande cha jani au nguo hadi kufikishwa kwa “mtaalamu” anayelichunguza.
  • Mayai haya huuzwa kwa bei kubwa sana, hadi kufikia maelfu ya shilingi kwa kila yai.

Wapo pia watu wanaonunua bundi akiwa hai kwa lengo la kufanya tambiko maalum, kwa imani kuwa bundi anaweza ‘kuamsha biashara’ au kuimarisha miradi yao ili “iishi usiku na mchana.”

Kwa mujibu wa makala ya “The criminal hunt for owl eggs in Kenya and Tanzania – A new sad poaching, between profits and beliefs” iliyoandikwa na Leni Frau mwaka 2024, biashara hii imehusishwa na mitandao ya uhalifu wa kimataifa, na inahusiana pia na imani za uponyaji wa magonjwa kama saratani na matatizo ya utotoni.

Bei ya mayai hayo imepanda hadi kufikia shilingi 100,000 kwa jozi (mayai mawili), na thamani yake kwa kilo inaweza kuzidi ile ya pembe ya kifaru au meno ya tembo.

Wanunuzi wakubwa wametajwa kuwa ni waganga wa kienyeji pamoja na wafanyabiashara toka mataifa ya Mashariki ya Kati.

Hali hii inaonyesha uhitaji wa haraka wa elimu ya jamii, uimarishaji wa sheria za uhifadhi, na kampeni za kubadili mitazamo kuhusu bundi kama viumbe wa mikosi.

Ukweli kuhusu michoro inayoonekana ndani ya mayai ya bundi kwa kutumia darubini

Michoro inayoonekana kwenye mayai ya bundi chini ya darubini ni matokeo ya muundo wa kibaolojia unaojulikana kama micropyle, ambayo ni sehemu ndogo inayoruhusu mbegu ya kiume kuingia na kurutubisha yai.

Aidha, mayai ya ndege huwa na matundu madogo sana (pores) yanazowezesha kubadilishana hewa, na yanaweza kuunda miale au mizunguko ya muundo wa mviringo unaoonekana kuwa wa kuvutia chini ya darubini.

Ingawa baadhi ya watu huona miundo hii kama inayofanana na nyota au nyumba za kuabudia, tafiti za kisayansi zinaonyesha kuwa hizi ni sifa za kawaida za kimaumbile katika mayai ya ndege, na hazina uhusiano wa moja kwa moja na alama za kidini au kiroho. Tafsiri hizo ni za kiimani na hazina msingi wa kisayansi.

Ukweli kuhusu Bundi kuhusishwa na Kifo

Katika jamii nyingi za Kiafrika, kumekuwa na imani potofu kwamba mlio wa bundi usiku ni ishara ya kifo kinachokaribia katika familia au nyumba fulani.

Wakati mwingine, hali ya mtu kufariki baada ya bundi kusikika akilia karibu na eneo hilo huchukuliwa kama uthibitisho wa imani hiyo.

Kuna nadharia isiyo na msingi wa kisayansi inayodai kuwa bundi ana uwezo wa kunusa seli za mwili zinazokufa, hivyo huanza kusogea karibu na eneo husika kwa matarajio ya kupata kitoweo endapo kiumbe hicho kitafariki.

Hata hivyo, utafiti wa kisayansi unaonyesha kuwa bundi hana uwezo mkubwa wa kunusa vitu vilivyo mbali.

Badala yake, ana uwezo wa kipekee wa kuona gizani na kusikia kwa usahihi mkubwa, ambao humsaidia kuwinda mawindo hai. Bundi si ndege anayekula mizoga, na ndiyo maana hawaonekani kwenye hospitali, mochwari, au maeneo yenye miili ya wafu.

Ukweli ni kwamba, baadhi ya wagonjwa walioko katika hali mbaya huweza kukata tamaa ya maisha wanaposikia mlio wa bundi, hasa pale ambapo imani za kijamii zinawafanya waamini kuwa mwisho wao umefika.

Hofu hiyo inaweza kuchangia kuzorota kwa hali ya mgonjwa, na wakati mwingine hata kifo. Lakini mara nyingi, tukio la kifo kufuata mlio wa bundi ni bahati isiyotarajiwa (coincidence) na si uhusiano wa moja kwa moja.

Imani hizi zimejengeka kwa karne nyingi, na zimechochewa zaidi na matumizi ya bundi na viumbe wengine kama njiwa, popo, na paka katika imani za jadi au kishirikina.

Hata hivyo, hofu kubwa imeelekezwa kwa bundi kutokana na sauti, sura yake ya kipekee na tabia yake ya usiku, hali inayohitaji kubadilishwa kupitia elimu na uhamasishaji wa jamii.

Athari za Imani hizi kwa Uhifadhi

  • Bundi wanawindwa, kukamatwa na kuuawa kinyume cha sheria.
  • Mayai yao huibwa kwenye viota kwa ajili ya biashara haramu, na kuathiri uzalianaji wao.
  • Makazi yao yanaathiriwa kwa kukata miti hovyo.
  • Hifadhi ya asili inapotea, na mnyororo wa chakula (food chain) unavurugika.

Kwa kuwa na imani potofu, jamii inaweka hatarini viumbe wanaosaidia kupunguza magonjwa (kwa kula panya, wadudu, nyoka n.k.), na kulinda kilimo chao.

Suluhisho Kupitia Uimarishaji wa Sheria, Elimu na Ushirikiano

Ingawa sheria za uhifadhi wa wanyamapori zipo nchini, utekelezaji wake kwa spishi zisizo maarufu kama bundi bado ni hautoshelezi hususani kwenye biashara haramu.

Sheria nyingi hulenga wanyama wakubwa kama tembo na vifaru, huku ukiukwaji wa haki za ndege wa porini ukiwa bado haujatiliwa maanani.

Ukosefu wa adhabu kali, pamoja na changamoto za ukosefu wa rasilimali kwa taasisi zinazohusika na uhifadhi, unachangia kuendelea kwa uhalifu huu.

Kuna haja ya kutunga sera mahsusi na kuimarisha utekelezaji wa sheria zinazolinda ndege wa porini, hasa wale walioko hatarini kama bundi, ili kuhifadhi urithi wa asili wa Afrika kwa vizazi vijavyo.

Mwandishi wa Makala hii pamoja na timu yake wanaendesha mradi wa utafiti na uhifadhi wa bundi na mazingira yao katika Milima ya Usambara Mashariki, na wamebaini kuwa taswira hasi katika jamii zinaweza kubadilika. Kupitia warsha, elimu za mazingira mashuleni, na video za elimu kwa lugha ya Kiswahili, wamefanikisha:

  • Kuongeza uelewa juu ya umuhimu wa bundi.
  • Kupunguza imani potofu na uoga wa usiokuwa na sababu.
  • Kuanza safari ya kurejesha mazingira na kuwa na jamii zinazoshiriki kikamilifu katika uhifadhi.

Kwa kushirikiana na makundi ya kijamii, serikali za vijiji, na mashirika ya ufadhili kama Rufford Small Grants, Conservation Leadership Programme, Raptors Aid, na Mohamed bin Zayed Species Conservation Fund, tumeanza safari ya kulinda viumbe hawa wa kipekee na kuhifadhi mazingira yao.

Hitimisho

Kupitia Makala hii fupi, tunapenda kubadili fikra na mitazamo ya kila msomaji wetu aliyekuwa na imani potofu juu ya bundi, na badala yake aanze kuwafurahia na kutamani kujifunza zaidi kuhusu maisha yao.

Bundi si ishara ya kifo ni viumbe wa kipekee wenye mchango mkubwa kwa mazingira yetu. Kupitia elimu na ushirikiano, tunaweza kubadili fikra potofu na kuhakikisha kwamba hata vizazi vijavyo vitawashuhudia viumbe hawa. Bonyeza hapa kusoma zaidi

Ni wajibu wetu sote kuwa walinzi wa viumbe hai na mali ya taifa letu.

Makala hii imeandikwa na Ezra Peter Mremi na kuhaririwa na Hillary Mrosso

Kwa maoni, ushauri au maswali unaweza kuwasiliana na mwandishi wa makala hii kwa mawasiliano yake hapo chini.

Ezra Peter Mremi
Mtaalamu wa Uhifadhi wa Wanyamapori | Mwanaharakati wa Mazingira | Mtafiti wa Bundi

Email: mremiezra@gmail.com

Phone: +255 756 438692

Tanzania