Picha imepigwa na Sheridan Wright, katika hifadhi ya taifa ya Serengeti, Tanzania
Leo twendeni mbugani, utalii mbuga zetu
Huko leo kuna nini, nataka ninene kitu
Leo huko duniani, siku ya bingwa wa mwitu
Agosti kumi ya Simba, ni jukumu tuwatunze
Simba ni bingwa wa mwitu, hakuna asiyejua
Anaogopwa na watu, na mbio wakatimua
Mnyama ni mthubutu, mwendo wake wa hatua
Agosti kumi ya Simba, ni jukumu tuwalinde
Simba huyu maarufu, kivutio duniani
Ila twaingia hofu, wachache wasothamini
Ni watu waharibifu, wawawindao porini
Agosti kumi ya Simba, ni jukumu tuwatunze
Tudhibiti majangili, waletao maumivu
Tuwe na moja kauli, na pamoja zetu nguvu
Mbinu zote mbalimbali, dhidi ya wa nia ovu
Agosti kumi ya Simba, ni jukumu tuwalinde
Tusifunge yetu macho, kila mara tuwalinde
Hadi kizazi kijacho, watusifu watupende
Kuwa tulikuwa jicho, wasituponde ponde
Agosti kumi ya Simba, ni jukumu tuwatunze
Siku hii ya Simba, tulinde hii zawadi
Hata simba mwenye mimba, alindwe tena zaidi
Kutolinda ni kuchimba, shimo letu makusudi
Agosti kumi ya Simba, ni jukumu tuwatunze
Kuwatunza ni muhimu, kivutio cha wageni
Tuwalinde zamu zamu, pato lisishuke chini
Wakiwa hawa adimu, tutapotea sokoni
Agosti kumi ya Simba, ni jukumu tuwalinde
Malenga wa Ubena
+255 676 559 211
Uhifadhi
Wildlife Tanzania