Habari msomaji wa mtandao huu wa wildlife Tanzania, karibu sana kwenye makala ya leo ambayo tutazungumzia maeneo yote ambayo nchi ya Tanzania imeyatenga kwa uhifadhi wa maliasili kama vile wanyamapori na mimea. Leo tutaona idadi za maeneo hayo ambayo nchi yetu imeyatenga kwa ajili ya uhifadhi wa mazingira, uhifadhi wa maumbile asilia na wanyamapori. Uhifadhi mkubwa unaofanywa na Tanzania kwa kutenga maeneo mengi kwa ajili ya viumbe hai unaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi chache sana duniani zenye makazi na mazingira asilia kabisa ambayo yana idadi kubwa ya bionuai na ndege.
Tanzania yenye ukubwa wa kilomita za mraba zaidi ya 954,000, imetenga karibu robo tau ya eneo la ardhi yake kwa ajili ya maeneo ya hifadhi za wanyamapori. Hii ndio sababu ya mimi kuandika makala hii kuwajuza na kuwaelewesha jinsi mgawanyo wa maeneo hayo ulivyo katika nchi yetu. Maeneo yanayolindwa na kuhifadhiwa hapa Tanzania yamegawanyika katika makundi mawili makubwa kundi la kwanza ni maeneo ya Hifadhi za wanyamapori, na pili ni maeneo ya Kihistoria. Haya ni maeneo ambayo yanalindwa kisheria na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ili tuyaelewe na kuyafahamu maeneo haya hata kama hujawahi kwenda huko basi ujue kuwa ni maeneo yaliyotengwa na yana simamiwa kisheria.
Hifadhi za Taifa (Tanzania National Parks, TANAPA)
Tanzania imetenga maeneo maalumu kwa ajili ya hifadhi ya wanyamapori na mimea, maeneo haya yanafahamika sana na watu wengi, maeneo haya yanasimamiwa na serikali kupitia Shirika maarufu sana la Serikali linaloitwa TANAPA. Maeneo yote ambayo yanasimamiwa na TANAPA kwa sasa yapo 16, yanajulikana kama Hifadhi za Taifa, mfano ni Serengeti, Manyara, Mikumi, Kilimanjaro, Gombe, Katavi, Rubondo, Ruaha, Uduzunwa, Saadani nk. Usimamizi wa maeneo haya ni mkali sana na sharia zake haziruhusu shughuli zozote za kibinadamu kama vile kilimo, ufugaji, uwindaji na hata uchimbaji wa madini. Haya ndio maaeneo maarufu sana kwa utalii wa picha na utalii wa uwindaji hauruhusiwi kabisa kwenye maeneo haya.
Eneo la Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro ( Ngorongoro Conservation Area Authority, NCAA)
Hili ni eneo la kipekee sana na lipo kivyake vyake, ni eneo ambalo lipo kwenye maajabu nane ya Dunia. Ni eneo la hifadhi ambalo wanaruhusu shughuli za kibinadamu kama kilimo, ufugaji, na shughuli nyingine ambazo zinaruhusiwa na sharia ya hifadhi ya Ngorongoro. Kwa hiyo ni hifadhi pekee Tanzania ambayo shuguli za uhifadhi wanyamapori na shughuli nyingine za kibinadamu zinafanyika kwa wakati mmoja, lakini pia kwenye hifadhi hii uwindaji hauruhusiwi kabisa. Ngorongoro ni hifadhi yenye vivutio vingi sana vya wanyamapori na vya kihistoria.
Mapori ya Akiba (Game Reserves, GRs)
Mapori ya akiba nchini Tanzania yapo zaidi ya 28 ambayo yapo karibia kila mkoa Tanzania. Kwenye mapori haya ya akiba ambayo yanasimamiwa na Serikali kupitia Idara ya wanyamapori Tanzania. Kwenye maeneo haya wanaruhusu utalii wa picaha na pia utalii wa uwindaji, hivyo kwenye maeneo haya ndio uwindaji hufanyika kisheria. Mfano wa mapori ya akiba ni Selous, au Seluu, hii ni moja ya pori kubwa kuliko yote Tanzania na pili kwa Afrika ikiwa na idadi kubwa sana ya simba na tembo. Mapori mengine Biharamulo, Ikorongo, Kigosi, Moyowosi, Lukwati, Swagaswaga, Uwanda, Burigi. Nk zipo nyingi sana.
Mapori Tengefu (Game Controlled Areas, GCA)
Tanzania ina zaidi ya mapori Tengefu 43, haya ni maeneo ya hifadhi ya wanyamapori hivyo maeneo haya yanasimamiwa na serikali kupitia Idara ya wanyamapori ya wilaya na vijiji. Ni maeneo ambayo yalitengwa kwa ajili ya kuinua uchumi kwa wananchi waishio karibu na maeneo hayo. Ni maeneo yanayofaa kwa uwekezaji. Mfano wa maeneo haya ni Burunge, Loliondo, Longido, Mlele, Msima, Nyonga, Sanya Lelatema, Ugunda, Kilombero, Handeni, nk. Hayo ni baadhi tu ya Mapori Tengefu yalioyopo Tanzania.
Maeneo ya Hifadhi ya Jamii (Wildlife Management Areas, WMA)
Haya ni maeneo yaliyotengwa na serikali kwa madhumuni ya uhifadhi wa wanyamapori na kutoa faida kwa jamii kupitia utalii wa picha na utalii wa uwindaji. Maeneo haya yanayosimamiwa na jamii pamoja na Idara ya wanyamapori ya wilaya na Kijiji husika wanaruhusu uwindaji, na uwekezaji kwenye maeneo hayo lazima ufanyike kisheria. Kuna maeneo zaidi ya 38 ya hifadhi ya jamii Tanzania, ambayo kati ya hayo 17 tu ndio yameendelezwa vizuri. Lakini hayo mengine bado yanasua sua kwenye usimamizi na kuleta faida nzuri kwa jamii. Mfano wa maeneo haya ni; Pawaga- Idodi, Tunduru, Ipole, Ukutu, Makame, Enduimet, Makao , nk. Hizi ni baadhi tu ya WMA ambazo zipo Tanzania.
Maeneo Oevu ya Akiba (Wetland Reserves)
Pia Tanzania ina utajiri mkubwa wa maeneo Oevu ambayo yametengwa na kulindwa kisheria. Maeneo haya ni muhimu sana kwa hifadhi ya wanyamapori na ndege. Tafiti nyingi zinzonyesha makazi na mazalia ya viumbe hai wengi kwenye maeneo haya oevu. Sekta ya mazingira kwa kushirikia na sekta ya wanyamapori imeweka usimamizi na sharia za kuhifadhi na kuyalinda maeneo haya muhimu sana kwa uhifadhi wa wanyamapori na viumbe hai wngine. Mfano wa maeneo haya ni; Malagalasi- Moyowosi, Ziwa Balangida, Ugalla, Rukwa- Katavi, Ziwa Rukwa, Bonde la Kilombero, nk. Haya ni maeneo oevu yaliyotengwa na serikali ya Tanzania kwa ajili ya umuhimu wake wa kutunza Maisha ya viumbe hai na kuleta faida kwa jamii.
Mapori ya Wazi (Open Areas)
Pia Tanzania ina mapori mengi ya wazi ambayo yapo kwenye maeneo ya vijiji ili kulinda na kutunza uhifadhi wa wanyamapori na misutu. Maeneo haya yanasimamiwa na serikali za vijiji na wilaya. Uwindaji kwenye maeneo haya unaruhusiwa kwa sharia za eneo husika na sharia za wanyamapori Tanzania.
Maeneo haya yote yametengwa na serikali kisheria kwa ajili ya kutunza wanyamapori na rasilimali nyingine zilizopo kwenye maeneo haya. Hili ni jambo kubwa sana kufanywa na nchi yetu kwenye uhifadhi wa wanyamapori na kukuza uchumi kupitia utalii unaofanyika kwenye maeneo haya. Maeneo haya yote yakitumika vizuri yatainua sana uchumi wa nchi yetu. Naamini mpaka kufikia hapa utakuwa umepata picha kubwa ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wanyamapori na utajiri ambao taunaweza kuupata endapo tutayatumia maeneo haya vizuri.
Asante sana kwa kusoma makala hii, kwenye makala nyingine nitakuandalia maeneo ya kihistoria yaliyopo hapa Tanzania, na pia uhifadhi wa wanyamapori kwenye maeneo ya misitu ili tuyaue na tuyatumie kwa kuinua uchumi wetu na nchi yetu pia. Mshirikishe mwengine makala hii.
Hillary Mrosso
Wildlife conservationist
+255 683 258 681/ +255 742 092 569