More

    Safari ya Hillary Thomas Mrosso Katika Uhifadhi wa Wanyamapori Tanzania

    Wakati nasoma elimu ya msingi na sekondari, nilikuwa na ndoto za kuwa daktari wa binadamu, hivyo nilipenda sana masomo ya sayansi, na pia nilikuwa naweza kufanya vizuri ili nijie kutimiza ndoto yangu ya kuwa daktari hapo baadaye.
    Lakini siku moja wakati wa likizo nikiwa nyumbani, nilikutana na mzee mmoja amestaafu, aliyewahi kufanya kazi katika hifadhi za taifa Tanzania, maarufu kama TANAPA. Huyu mzee nilikutana naye hapo nyumbani kwake akiwa kibarazani anasoma magazeti maarufu yaliyoitwa KAKAKUONA.
    Magazeti haya yalikuwa yanaelezea uzuri wa hifadhi za taifa, wanyamapori, na Maliasili zinazopatikana Tanzania, magazeti haya yalipambwa na picha nzuri zenye mvuto kuhusu wanyama na tabia zao, mambo ya kipekee ya wanyamapori na uoto asilia. Siku hizi haya magazeti hayapo tena.
    Niliongea na yule mzee mambo mengi kuhusu wanyamapori, hifadhi za taifa na utalii. Baadaye nilimuomba baadhi ya magazeti hayo ili nikajisomee nyumbani, yule mzee alinipa magazeti kama 5 hivi. Nilipofika nyumbani nilianza kuyasoma yote. Kwa kweli nilivutiwa sana na hadithi nzuri za wanyama na maisha yao, hifadhi za wanyamapori na mandhari nzuri za wanyama nchini Tanzania.
    Tangu siku ile niliamua kubadili kabisa ndoto yangu ya kuwa daktari wa binadamu na kutaka kusomea mambo ya uhifadhi wa wanyamapori. Baada ya kumaliza kidato cha sita, nilichagua kusomea Shahada ya Usimamizi wa Wanyamapori katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine.
    Nilifurahia sana masomo na mafunzo kwa vitendo, hasa tulipokuwa tunaenda hifadhini kwa ajili ya elimu ya mafunzo kwa vitendo, kama vile kujua tabia za wanyama, njia zinazotumika kuhesabu wanyamapori wakubwa kwa wadogo, njia zinazotumika kuhesabu ndege na kuwatambua na namna ya kupima uoto wa asili.
    Nilikuwa nafurahia sana maana huku tunaona wanyama wengi wakiwa katika mazingira yao, tuliwaona tembo, nyati, fisi, simba, twiga, nyani, ngiri, nyumbu, pundamilia, swala na ndege wa aina nyingi. Tulifundishwa mbinu nyingi za uhifadhi wa wanyamapori na changamoto zake kama vile ujangili, uchomaji moto, mimea vamizi, na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi.
    Baada ya kumaliza shahada ya kwanza katika uhifadhi wa wanyamapori, niliendelea kujifunza kupitia makala mbali mbali za wanyamapori na uhifadhi, nilikuwa nasoma majarida ya kisayansi kuhusu wanyamapori na uhifadhi na kufuatilia habari za wanyamapori.
    Hata hivyo, nilibahatika kupata nafasi ya kujitolea katika mradi wa Kanivora ambao unafanya kazi zake katika eneo la Ruaha, Iringa Tanzania. Nilifurahi sana kupata nafasi hii ya kujitolea ili kujifunza kwa undani na kwa vitendo namna jamii zinavyoishi na wanyamapori, hasa kanivora. (kanivora ni wanyama wanaokula nyama, kama simba, chui, mbwa mwitu, fisi, duma nk). Baadaye niliajiriwa na mradi huu kama mtafiti msaidizi.
    Nikiwa katika mradi huu wa kanivora ndio niliona mambo yalivyo halisi, changamoto, na faida za kuishi na wanyamapori. Niliona jinsi kanivora wakubwa kama simba, chui na fisi walivyokuwa wanasababisha migogoro kwa wafugaji, walikuwa wanakula mifugo na kuleta migogoro isiyoisha. Pamoja na hayo, eneo hili la Ruaha lina changamoto nyingi za wanyamapori kama tembo, nyani na ndege, wanakula mazao na kuharibu mali za watu.
    Hata hivyo nikiwa katika mradi wa kanivora, tulitumia njia mbali mbali kupunguza migogoro hiyo kama vile kuwajengea mazizi imara ya waya, ambapo simba na fisi hawawezi kuingia na kula mifugo. Mimi nilikuwa nasimamia programu za vijiini, kuelimisha watu na jamii kuhusu kanivora, lakini pia nilisimamia programu ya utoaji wa faida zinazotokana na uwepo wa wanyamapori kwenye maeneo ya vijiji katika eneo la Ruaha. Mradi wa kanivora unatoa hela nyingi sana kwa jamii zinazoishi kando ya hifadhi ya Ruaha ili kusaidia jamii kuvumilia kuishi na kuhifadhi kanivora.
    Mwaka 2017, ndio nilipata wazo la kuanzisha blogu hii ya WILDLIFE TANZANIA kwa ajili ya kushirikisha jamii kubwa zaidi mambo ya uhifadhi wa wanyamapori, faida zake na changamoto zilizopo katika uhifadhi kwa ujumla. Hii ilinisaidia kuandika baadhi ya makala na hadithi kuhusu uhifadhi, faida zake na changamoto zake, hadi sasa bado naenelea na kuandika makala hizi.
    Tumeandika zaidi ya makala 400, kwenye maeneo mbali mbali kama uhifadhi, ujangili, biashara haramu za wanyamapori na utalii. Hata hivyo, nimewasaidia wengine pia zaidi ya 15 kuandika makala nzuri zenye kutoa elimu kwa jamii kuhusu uhifadhi.
    Mwaka 2019, niliacha kazi katika mradi wa kanivora kwa lengo la kujiendeleza zaidi kwa elimu ya uzamili, (masters), ambapo nilimaliza mwaka 2021. Elimu hii imekuwa chachu ya kukuza sana uelewa wangu kuhusu uhifadhi na kuona mambo kwa undani zaidi.
    Disemba 2021, mimi na wenzangu tulianzisha taasisi ya utafiti na uhifadhi Tanzania. Lengo likiwa kuwa sehemu ya suluhisho kwa changamoto zilizopo katika uhifadhi. Katika taasisi hii tunafanya tafiti nyingi za kakakuona, tembo na twiga. Tulitumia uzoefu tuliopata kwenye miradi na taasisi nyingine tukanzisha taasisi hii.
    Pamoja na mambo mengine tumekijita kutafiti zaidi kakakuona, wanyama ambao wapo hatarini kutoweka, lakini hakuna taarifa za kutosha kuhusu wanyama hawa hapa Tanzania, hata uelewa wa jamii kuhusu wanyama hawa ni mdogo sana. Lakini kakauona ni wanyama walio hatarini kutoweka kutokana na biashara haramu, kupungua na kuharibika kwa makazi yao, ukosefu wa tafiti, imani potofu kuhusu kakakuona na ukosefu wa uelewa kuhusu wanyama hawa.
    Hadi sasa machapisho mawili ya kisayansi kuhusu kakakuona yameshatoka. Mengine 5 yapo katika hatua za mwishoni kutoka. Hii imesaidia kutoa taarifa za kina kuhusu wanyama hawa na mitazamo ya watu kuhusu wanyama hawa wa kipekee.
    Juhudi hizi na nyingine katika uhifadhi, zimefanya nichaguliwe na Wizara ya Maliasili na Utalii kuwania tuzo za Mshawishi Bora katika masuala ya Uhifadhi (Best Conservation Influencer). Nawashukuru sana wale walionipigia kura ili nishinde tuzo hii, pia wale waliojitoa kuwashirikisha wengine ili nipate kura kwa ajili ya tuzo hii muhimu.
    Tuzo hii itakuwa chachu kubwa sana katika safari yangu ya uhifadhi, pia inaonyesha mchango wetu katika uhifadhi unaonekana na kudhaminiwa. Hii inatia moyo na kufariji na kufariji sana.
    Mwisho wa kupiga kura ni tarehe 27/01/2026. Kama bado hujapiga kura, tafadhali naomba unipigie kura kuwa Best Conservation Influencer. Nitaweka hapa link na utaratibu wa kupiga kura.
    Bonyeza link hiyo HAPA SERENGETI AWARD
    • Utaona sehemu imeandikwa, Search for Applicant,
    • Hapo utaandika jina langu, Hillary Thomas Mrosso,
    • Utaendelea chini, itakuletea kipengele cha besti conservation influencer na picha yangu utaona hapo
    • Utabonyeza hapo, halafu chini utaona sehemu ya kuweka email au namba ya simu.
    • Utaweka namba ya simu kuanzia na +255, utaweka namba yako ya simu au email yako
    • Ukifanya hivyo utapokea ujumbe wa uthibitisho kuwa umepiga kura tayari, ya verification code.
    • Hapo utakuwa umepiga kura tayari.

    Ukipata changamoto yoyote tafadhali wasiliana na mimi kwa namba hizi
    NICHAGUE TUENDELEE KUFANYA MAKUBWA KWENYE UHIFADHI.
    +255 683862481
    Hillary Mrosso.

    Latest articles

    Related articles

    Leave a reply

    Please enter your comment!
    Please enter your name here