Habari Rafiki, karibu kwenye makala ya leo ambayo tutaona na kujifunza mambo ambayo tunayafanya au yanafanywa jamii zetu wanaoishi karibu na maeneo au makazi ya wanyamapori ilivyo hatari kwenye uhai wa wanyamapori na mazingira yao. Kwa kiasi kikubwa tumelea jambo hili kwa miaka mingi, jamii nyingi zilizo sahaulika huwa zinajihusisha na ujangili kwenye maeneo ya karibu na hifadhi za wanyamapori, inahitajika hekima, udadisi na umakini wa hali ya juu kujua kiini na mahali tatizo hili lilipoanzia.

Unaweza kujiuliza maswali kwanini pamoja na juhudi zote za serikali na watu binafsi kuelimisha na kutumia rasilimali nyingi kwenye kutoa elimu kuhusu uhifadhi wa wanyamapori kwenye meneo ya vijiji vilivyo kando kando ya hifadhi za wanyamapori, bado kuna watu wanafanya ujangili, bado watu wanaingia hadi hifadhini kuwinda wanyamapori, kurina asali na kuvua samaki bila kibali chochote. Kinacho nishangaza hata kwenye maeneo yenye ulinzi na usimamizi mkubwa kama maeneo ya hifadhi za Taifa bado nako sio salama kwa asilimia mia moja, bado kuna shughuli nyingi sana za ujangili zinaendelea kwenye maeneo hayo.

Kuna kitu kikubwa sana nimekiona kwenye jamii hizi za watu wanaofanya ujangili. Inaonekana ujangili unaofanywa na wanajamii huwa unaridhishwa kutoka kizazi hadi kizazi. Fuatilia mwenyewe utaona mambo yalivyo, ukimuuliza yule ambaye anafanya ujangili atakwambia mimi nafanya ujangili kwa kuwa baba na babu yangu walikuwa wanafanya ujangili na ujangili ndio ulkuwa ni njia yao ya kuingizia kipato. Nilibahatika kukutana na kufanya kazi na moja wa majangili waliostaafu alinieleza kama yeye angekuwa anaendelea na ujangili, basi angekuwa tayari ameshamrithisha mtoto wake wa kiume mikoba hiyo, anasema yeye mwenyewe alianza ujangili akiwa na umri mdogo kwa hiyo mpaka kufikia umri wa mtu mzima anafahamu mambo mengi sana kuhusu ujangili na pia anafahumu mbinu zote za kufanya ujangili hata maeneo yaliyo na usimamizi mkali.

Kitu kingine kilicho nishsngaza ni kwamba wanajuana kabisa, kama Kijiji fulani kinajihusisha na ujangili basi wanafahamiana vizuri wale wote wanao husika na ujangili. Pia vijiji vilivyopo kando ya hifadhi za wanyamapori vinatofautiana kwa viwango vya kiuwindaji na kiujangili, hapa namaanisha kwamba kuna vijiji ambavyo vina idadi kubwa sana ya majangili, na vingine vina idadi ndogo ya majangili. Ukianza kufuatilia vile ambavyo vina idadi kubwa ya majangili utashangaa, utafikiri kila mtu kwenye Kijiji hicho ni jangili, na watu hawa wameanza siku nyingi sana shughuli zao za ujangili, na kama nilivyokudokeza hapo juu kwamba ujangili huridhishwa kutoka kwa babu au baba kwenda kwa watoto, na hivyo kuwa na jamii au watu ambao wanaijua kazi hii haramu vizuri sana.

Aidha, kutokana na hali hiyo kuwepo kwa muda mrefu kwenye vijiji hivyo, ndio imekuwa kama ni lango la majangili wakubwa kutumia watu walio na uzoefu wa kufanya shughuli hii haramu kuwasaidia kufanya ujangili hasa wa tembo, ndio maana ujangili wa aina yoyote ile ni mtandao ambao umesukwa vizuri sana na watu wanaofanya kazi hizo. Ukifuatilia na kuuliza waliokumbwa na sakata la operesheni tokomeza watakusimulia mpaka utashangaa jinsi walivyokuwa wanatumika kuua wanyama kwa maagizo ya watu walio juu yao.

Nilichojifunza kuhusu ujangili ni kwamba hakuna mtu anayeweza kwa mara ya kwanza kuanza kufanya ujangili yeye mwenyewe bila kushirikiana na wanyeji au wazoefu wa kazi hizi. Hivyo kwa kuwa wanapata wanavijiji ambao wanafanya kazi hizi kwa muda mrefu ambao wanajua milango yote ya kuingilia na wanajua maeneo yote yenye wanyamapori basi wamekuwa wanatumi watu kutoka vijiji vya jirani na maeneo ya hifadhi ya wanyamapori. Hii ndio sababu ya kukua na kuendelea kwa ujangili kwenye maeneo ya vijiji vinavyozunguka hifadhi au maeneo yaliyohifadhiwa.

Kwa hiyo utaona mwenyewe kwamba wanavijiji ambao walikuwa wanawinda wanyamapori wadogo kwa ajili ya kitoweo sasa wanajihusisha na ujangili mkubwa wa tembo na wanyamapori wengine. Wale wanaofanya biashara haramu ya meno ya tembo huwachukua watu wa namna hii na kufanya nao kazi ya kuua wanyamapori, kwa kuwapa mafunzo namna ya kutumia bunduki na vifaa vingine vya kufanyia ujangili, na kuwapa fedha kidogo kwa shughuli hiyo haramu na hatari sana. Hivyo wanavijiji ambao walikuwa wanatumia mitengo ya nyaya, mishale, marungu na kwa kutumia mbwa kufanya ujangili sasa wanawezeshwa kutumia silaha za moto kufanya ujangili.

Kwa kweli bila ya ile opereheni tokomeza kuwepo na kufanyika kwenye maeneo ya hifadhi ya wanyamapori, tungekuwa tumepoteza idadi kubwa sana ya rasilimali zetu muhimu kama vile wanyamapori. Naishukuru Serikali kwa jambo hili kubwa na zuri ambalo limepelekea kwa kiasi kikubwa kutokomeza ujangili wa wanyamapori wetu hasa tembo.  Sasa wanyamapori kwa kipindi cha miaka miwili hii wanaishi kwa raha na kwa amani kwenye maeneo yao.

Kazi bado inatakiwa kufanyika kwenye jamii na familia zile ambazo bado zina chembe chembe za ujangili, tunatakiwa tufanye kazi kuhakikisha hawa ambao bado wanaendelea na biashara hii wajue na watambue kwa kuendelea kufanya biashara ya ujangili wanahatarisha maisha ya wanyamapori na maisha  yao kwa ujumla. Wanatakiwa wafanyiwe kitu ambacho hawatakisahau, kitu ambacho kitawafanya wachukie kabisa ujangili na wala wasirithishe kabisa ujangili kwenye familia na Kijiji chao.

Kuna mambo mengi ambayo yanaweza kufanyika kwenye maeneo haya ili kupunguza na kuondoa kabisa ujangili na biashara za njara. Naamini tuna uwezo mkubwa wa kushirikiana na jamii hizi kwa karibu ili kutokomeza kabisa biashara hii haramu, serikali inaweza, wadau wengine wa uhifadhi na miradi ya uhifadhi wa wanyamapori na watu binasfsi tunaweza jambo hili kulikomesha, tena kwa kuwa tunajua lilikoanzia basi tuende kukata mizizi yote ya jambo hili kwenye maeneo hayo. Pia kushirikiana na  juhudi za kimataifa kuharibu na kupinga biashara ya nyara kama vile meno ya tembo na meno ya faru na nyara nyingine.

Ahsante sana kwa kusoma makala hii naamini umepata kitu kikubwa ambacho kinaweza kukupa picha nzuri ya kudhibiti na kukomesha ujangili kwenye hifadhi zetu. Jambo hili linahitaji ushirikiano wa karibu na wa mbali ili lifanyike vizuri. Tupambane kila siku tuweke mazingira salama kwa wanyamapori wetu na rasilimali nyingine.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 248 681/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania