Habari za siku ndugu msomaji wa makala hizi za wanyamapori na mengi kuhusu wanyama hawa ikiwemo tabia na uelekeo wa wanyama hawa hasa hapa nchini kwetu. Ni kwa mara nyingine tena nakualika katika darasa hili huru la wanyamapori kwani kupitia makalahizi utajifunza mengi sana na kunufaika pia kuthamini uhifadhi wa wanyama hawa ambao ni rasilimali muhimu sana kwetu lakini pia wenye mchango mkubwa sana kwenye pato la taifa kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii.

Basi kama ilivo kawaida leo tena tuingie darasani kumjua mnyama ambae kwa hakika huwezi kumpata sehemu nyingine duniani zaidi ya hapa kwetu Tanzania na pia hupatikana maeneo ya ukanda mmoja tu hapa nchini.

Basi moja kwa moja ungana nami kwa utulivu kabisa kumjua “MBEGA MWEKUNDU WA UDZUNGWA”

UTANGULIZI

Kama nilivo tangulia kudokeza hapo juu kuwa wanyama hawa hupatikana hapa nchini tu basi ni dhahiri kwamba wanahitaji uangalizi mkubwa sana ili kunusuru maisha yao. Kabla hatujaanza kuwachambua mbega wekundu wa Udzungwa tukumbuke kuwa mbega wekundu wapo wa aina nyingi, lakini aina tatu tundo wana patikana hapa kwetu Tanzania na wote hawa wana tofautiana baadhi ya sifa lakini pia hata maeneo wanapo patikana.

Aina hizi za mbega wekundu ni kama ifuatavyo

1.Mbega Mwekundu wa Udzungwa

2.Mbega Mwekundu wa Zanzibar

3.Mbega Mwekundu wa Mashariki

Sasa leo tumjue huyu mbega mwekundu wa udzungwa tu kwanza.

SIFA NA TABIA ZA MBEGA WEKUNDU WA UDZUNGWA

1.Manyoa ya kichwani yametengeza umbo lifananalo na taji huku yakiwa na rangi nyekundu.

2.Sehemu ya juu ya mwili wao huwa wana manyoa ya rangi nyeusi huku upande wa chini wakiwa na rangi nyeupe.

3.Wana manyoa ya rangi nyeupe kwenye mashavu.

4.Mbega hawa hawana vidole gumba, ila wana vidole virefu na vyenye nguvu ili kuwasaidia kushikilia vizuri kwenye miti wakati wa kuruka. Na ukosefu huu wa vidole gumba ndio asili ya neno mbega kutokana na tafsiri za Kigiriki.

5.Mikono na sehemu za mapaja za mbega wekundu wa Udzungwa huwa na rangi nyeusi hasa upande wa nje, lakini kwa upande wa ndani na kwa juu kidogo manyoa huwa na rangi kama ya fedha inayoendana na weusi.

6.Wana mikia yenye rangi nyeupe kwa chini na rangi nyeusi au nyano ifananayo na nyeusi kwa upande wa juu.

7.Ni wanyama wenye uwezo wa kuona mchana zaidi kuliko usiku.

8.Huishi kwa makundi yenye mchanganyiko wa madume na majike ambapo kundi huweza kuwa na mbega 7 – 83 au na zaidi. Lakini mara nyingi wamekuwa wakionekana kwenye kundi lenye idadi ya mbega 24. Ndani ya kundi moja huwa kuna mgawanyiko wa makundi madogo madogo ambayo huwa yanaongozwa na dume mmoja au wakati mwingine madume wawili.

9.Wanapo muona adui basi hupeana taarifa kupitia sauti mbali mbali. Sauti hizi huwa zina utofauti, sauti inayotoka endapo adui yupo chini huwa ni tofauti na sauti inayo toka endapo adui yao nae yupo juu.

UREFU NA UZITO

Huwa kuna utofauti kidogo kati ya dume na jike hasa pale tunapo angalia mambo kama uzito na kimo cha mwili.

Dume

Uzito=kilogramu 9 – 13kg

Urefu=kichwa na kiwiliwili huwa na sentimita 46 – 70sm, mkia 55-80sm

Jike

Uzito=kilogramu 7 – 9kg

Urefu=kichwa na kiwiliwili huwa na sentimita 47- 62sm, mkia 42 80sm

MAZINGIRA NA MAENEO WANAYO PATIKANA

Mbega hawa hupendelea sana maeneo yenye misitu mitingi haya maeneo yenye misitu ya awali na upili na hasa maeneo ya nyanda za chini na juu.  Mara nyingi misitu wapatikanayo mbega hawa huwa ipo katika muinuko wa mita 250 – 2,200m kutoka usawa a bahari.

Maeneo wapatikanayo mbega wekundu wa udzungwa ni Hifadhi ya Misitu ya Magombero, Pori la Akiba la Seluu, Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa na Hifadhi ya Misitu ya Dabaga/ Ulangambi. Na baadhi ya maeneo mengine madogo yazungukayo maeneo hayo huku Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa ikiongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya mbega hawa.

Kumbuka kuwa maeneo yote yaliyo tajwa hapo juu kwa pamoja huitwa Safu za Milima ya Udzungwa.

CHAKULA

Mbega hawa chakula chao kikubwa ni majani ya miti. Lakini kuna wakati huwa wanakula maua na hata baadhi ya matunda yapatikanayo msituni. Pia utafiti unaonyesha kuwa mbega wekundu wa Udizungwa huwa wanakula hadi baadhi ya jamii ya fangasi.

KUZALIANA

Mbega huishi kwa makundi na kama tulivoona hapo juu kuwa kila kundi huwa na makundi madogo madogo ndani yake ambayo hutawaliwa na dume mmoja au wawili.

Mara tu baada ya kupata mimba, jike hukaa na mimba kwa muda wa miezi sita (6) na baada ya hapo huzaa mtoto mmoja tu. Mama humlinda mwanae na kuwa nae karibu kila anapo kwenda na mara nyingi humbebea mwanae sehemu ya tumboni.

Mama hukaana kumlinda mwanae kwa uangalizi mkubwa sana na hii huchukua takribani miezi mitatu (3) ndipo mtoto huanza kujifunza kutafuta chakula mwenyewe japo pia huwa bado yupo chini ya uangalizi wa mama.

Kwa pamoja mbega wekundu wa udzungwa hufikia hatua ya kuweza kuzaa pale wafikishapo umri wa myaka  4 wakati mwingine dume huenda mpaka myaka minne na nusu.

UHIFADHI

Mbega wekundu wa Udzungwa ni wanyama ambao wanakumbwa na matatizo mengi hasa kutokana na mazingira wanayoishi. Kama tulivoona hapo juu mbega hawa wanapatikana katika maeneo ya uhifadhi manne tu.

Kutokana na kupungua kwa idadi ya mbega hawa imepelekea Shirika la umoja wa mataifa linalo husika na uhifadhi wa maumbile asili ( International Union for Conservation of Nature – IUCN) kuwaweka mbega hawa katika kundi la wanyama walio hatarini kutoweka duniani.

Takwimu za mwaka 2001 zilionesha kuwa idadi ya wanyama hawa ni 15,000 lakini bado kulikuwa na utata kwani idadi hii ilionekana kuwa ni kubwa kwani kasi ya kuzaliana kwa wanyama hawa huwa ni ndogo sana. Utata huu ulikuja kwasababu takwimu za mwaka 1982 zilionesha kuwa idadi ya mbega hawa ni 10,000. Lakini kuzaliana kwa mbega hawa kwa wakati mmoja inaonekana huzaliwa mbega 2,000 na kuendelea japo wengine huwa wanakufa.

MAADUI NA TISHIO KWA MBEGA WEKUNDU WA UDZUNGWA

Maadui wakuu wa mbega hawa ni wanyama jamii ya sokwe kwani huwa wanawawinda mbega kwa kundi mpaka wana wakamata. Japo kuna adui mwingine ambae ni ndege ajulikanae kama tai lakini ni mara chache sana hutokea mpaka tai kumuuwa mbega.

Tishio kubwa sana kwa mbega wekundu wa udzungwa ni uharibifi wa mazingira hasa unaotokana na ukataji miti, upanuzi wa maeneo kwa ajili ya kilimo, uchomaji mkaa, utengenezaji wa miundombinu ya usafiri mfano reli ya tazara umepelekea kuharibu sana makazi ya mbega wekundu wa udzungwa.

Binaadamu nae hajabaki nyuma kwani imeripotiwa kuwa watu huwawinda sana mbega hawa kama kitoweo na kupelekea kupungua sana kwa idadi ya wanyama hawa.

NINI KIFANYIKE KUWANUSURU MBEGA WEKUNDU WA UDZUNGWA

Kwakuwa tumeshaona tatizo kubwa linalopelekea kupungua mbega hawa basi kuna ulazima wakufanya haya yafuatayo

( a ) Kuongeza mipaka na ukubwa wa misitu hasa ile inayo pakana na Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa ili kurudisha hadhi ya misitu hii. Misitu hii ni kama ile ipatikanayo magharibi mwa Kilombero ambayo ni Ndundulu, Nyumbanitu, Ukami na Iyondo pia Udzungwa, Matundu na Nyanganje.

( b ) Upanuzi wa maeneo ya Hifadhi za Misitu ambayo inapaka pia na Pori la Akiba la Seluu kwani maeneo haya yana ulinzi wa kutosha hasa kwa kunusuru mbega hawa. Baadhi ya misitu ambayo inahitaji kuongezwa maeneo ni pamoja na Magombera, Ibiki pamoja na misitu mingine yote ambayo inapatikana karibu na Mto Msolwa.

( c )Kupambana na kutokomeza uchomaji wa misitu hasa usababishwao na upanuzi wa maeneo ya kilimo kwani imepelekea sana kuharibu mazingira ya mbega wekundu wa Udzungwa. Watu wamekuwa wakichoma misitu hovyo ili kuongeza maeneo ya kilimo ufikapo msimu wa kulima bila kujali nini athari ya upanuzi wa mashamba kwa viumbe wengine wanao patikana katika maeneo hayo.

( d ) Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali chini ya wizara hiyo mfano TANAPA kwa upande wa Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa, TAWA kwa upande wa Pori la Akiba la Seluu, TFS kwa upande wa Hifadhi za Misitu zianzishe mapitio ya wanyamapori yanayo unganisha

Msitu mmoja na mwingine ili kuruhusu mbega hawa kuweza kuenea maeneo mengi zaidi. Hii itapelekea hata kasi ya kuzaliana kuongezeka kwani watakuwa na eneo kubwa la kutawanyika.

( 7 )Usimamizi mahiri wa sheria za wanyamapori pia sheria za misitu hasa kwa upande wa ujangili ili kupunguza athari za ujangili kwa mbega hawa. Ujangili ni tatizo ambalo limekuwa likirudisha nyuma sana shughuli za uhifadhi.

HITIMISHO

Mbega wekundu wa Udzungwa ni jamii ya mbega wanao patikana katika maeneo ya safu za milima ya Udzungwa tu na huwezi kuwakuta maeneo mengine duniani kote. Hii ni fahari ya kujivunia kwasababu watu hutoka nchi mbalimbali na kuja hapa nchini ili kumjua mbega mwekundu wa Udzungwa yupoje.

Changamoto za uharibifu wa mazingira na ujangili hali kadhalika uchomaji wa misitu na utengenezaji wa miundombinu, vyote hivi kwa pamoja visipo tafutiwa ufumbuzi mapema basi mbega hawa watabaki kuwa historia tu kuwa walikuwepo hapa nchini kwetu Tanzania.

Napenda sana kuwapongeza TANAPA kwa kazi kubwa wanayo ifanya pale Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa kwani ni dhahiri wanahitaji pongezi hizi. Ukiangalia maeneo yote wanayo patikana mbega wekundu wa udzungwa utaona kuwa idadi kubwa ya mbega hawa wanapatikana katika Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa. Hii ni kutokana na usimamizi mzuri na utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi wa wanyama na mazingira kwa ujumla.

Mamlaka nyingine zikiwemo TAWA na TFS basi ziige mfano mzuri kwa TANAPA ili kupunguza adha wapatazo mbega hawa kwani ni faida kwa taifa na hasa kutokana na mchango wa maliasili kwenye pato la taifa kwa ujumla.

Basi nikusihi ndugu msomaja wa makala hizi kuendelea kufuatilia makala nyingine zijazo za wanyamapori ili kujifunza mengi zaidi juu ya wanyama hawa pamoja na mazingira wanayoishi.

Tukutane tena kwenye makala ijayo.

AHSANTENI SANA!

Kwa mengi kuhusu makala za wanyamapori,uhifadhi unaweza kuwasiliana na mwandishi wa makala hii kupitia;

Sadick Omary

Simu= 0714 116963 / 0765 057969 / 0785 813286

Email= swideeq.so@gmail.com

Au tembelea= www.mtaalamu.net/wildlifetanzania

” I’M THE METALLIC LEGEND”