Siku ya wanyamapori duniani inatukumbusha kutafakari namna tunavyoishi na mazingira yanayotuzunguka. Mazingira kama misitu, miti, maji, hali ya hewa, wanyama na wadudu.
Hivyo siku ya wanyamapori duniani inatupa nafasi kutafakari njia na juhudi tunazofanya kwenye uhifadhi wa Maliasili zetu za wanyama na mimea kama zinatosha. Ni muhimu sana kujifanyia tafakari za kina kwasababu matokeo na takwimu zinaongea mengi kuhusu juhudi zetu kwenye uhifadhi wa Maliasili hizi muhimu.
Katika maadhimisho haya ya siku ya wanyamapori duniani, ambayo hufanyika kila mwaka tarehe 3 Machi, yana kuli mbiu mbali mbali. Kauli mbiu ya mwaka 2026, ni Mimea dawa na Manukato; Kuhifadhi Afya, Urithi na Maisha (Medicinal and Aromatic Plants: Conserving Health, Heritage and Livelihoods).
Mimea ni sehemu muhimu sana ya uhifadhi wa mazingira asilia ya wanyama na viumbe hai wengine. Mimea inahifadhi mamilioni ya viumbe hai wanaaonekana kwa macho na wasioonekana kwa macho. Mimea ndio huunda misitu, misitu ni mchanganyiko wa mimea ya aina nyingi inayoota sehemu fulani.

Mimea ina faida nyingi sana kama chanzo cha kuzalisha hewa ya oksijeni, makazi ya viumbe hai, kuhifadhi vyanzo vya maji, kuzuia mmomonyoko wa udongo, kudhibiti mabadiliko ya tabia nchi, vyanzo vya dawa za asili za binadamu na wanyama, malighafi za ujenzi na utalii.
Kwa kuzingatia kauli mbiu ya mwaka huu, mimea dawa na manukato; kuhifadhi afya, urithi na maisha. Mimea imekuwa sehemu muhimu sana kama chanzo cha dawa nyingi asilia, mimea imetumika sehemu nyingi kama manukato, mimea ni urithi wetu na maisha yetu.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa, asilimia zaidi ya 80 ya watu duniani hutegema memea kama dawa. Lakini asilimia 25 ya dawa za kisasa zimetengenezwa kwa kutumia mimea. Hii inaonyesha jinsi mimea ilivyo sehemu muhimu ya afya ya mwanadamu.
Mimea mingi ambayo hutumika kama dawa na manukato hutokana na miti asilia. Kama iliyoripotiwa na Shirika la Chakula Duniani FAO kuwa, asilimia 60 hadi 80 ya mimea dawa yote hutoka katika miti au misitu asilia. Hii inatupa kufahamu kuwa misitu asilia ndio chanzo kikuu cha mimea na miti yote ambayo hutumiwa sehemu mbali mbali duniani kama dawa na manukato.
Kupitia taarifa hizo tunajifunza kuwa uhifadhi na utunzaji wa misitu yetu sio tu kama sehemu ya uhifadhi wa makazi ya wanyamapori, au hifadhi ya vyanzo vya maji, bali ni muhimu kwa uhifadhi wa vyanzo muhimu vya dawa kwa ajili ya afya na maisha ya binadamu.
Utafiti kutoka Chuo Kikuu cha Nelson Mandela nchini Tanzania umebaini kuwa, asilimia 80- 90 ya dawa zinazotengenezwa na kutumiwa na waganga wa jadi kwa ajili ya kutibu maradhi mbali mbali ya watu hupatikana kutoka katika miti asilia au misitu asilia.
Taarifa hii inaongeza uzito kwenye matumizi makubwa ya mimea asilia kama dawa, lakini pia inaonyesha picha nyingine kubwa kuwa mimea asilia inaweza kuvunwa au kukatwa bila kibali, hivyo kupelekea kuendelea kupotea na kutoweka bila taarifa za kutosha.
Hata hivyo, hapa tunaona upande mmoja wa uvunaji na matumizi makubwa ya mimea asili kama dawa. Bado kuna matumizi mengine mengi ya mimea asili kama mapambo, manukato, mbao, kuni, mkaa nk. Ambayo ni matumizi makubwa, hali hii inachangia sana mimea mingi kupotea bila kuwa na taarifa za kina.
Kuna ushahidi mwingine kutoka Shirika la TRAFFIC kuwa, asilimia 60 mpaka 90 ya mimea dawa na ya manukato iliyopo katika masoko na biashara imetoka katika misitu asilia. Utafiti huu uliofanywa na TRAFFIC unatuonyesha picha kubwa zaidi, huenda kuna biashara haramu nyingi za mimea asili kwa matumizi mbali mbali sehemu nyingi duniani.

Idadi kubwa ya mimea asili kuendelea kutumiwa kwa kiasi kikubwa kama dawa na mapambo sehemu mbali mbali duniani, imesababisha baadhi ya spishi au aina za mimea hii kuwa hatarini kutoweka kabisa mwituni.
Mimea mingi ya dawa iko hatarini kutoweka nchini Tanzania na kote ulimwenguni kutokana na uvunaji usio endelevu, hasa wa mizizi na magome. Hapa kuna mifano ya mimea ya dawa inayokabiliwa na hatari hiyo:
- Mkunungu (Zanthoxylum chalybeum): Unajulikana pia kama Oloisuki kwa Kimasai. Mmea huu unavunwa kwa kiasi kikubwa kwa ajili ya kutibu matatizo ya mfumo wa upumuaji, malaria, na maumivu ya tumbo.
- Mvumo wa Milimani (Warburgia salutaris): Mti huu unathaminiwa sana kwa kutibu maambukizi ya fangasi na bakteria, lakini idadi yake imepungua sana kutokana na uvunaji wa magome.
- Mpingo (Dalbergia melanoxylon): Ingawa unajulikana zaidi kwa mbao, pia una matumizi ya kidawa na unakabiliwa na hatari kubwa ya kutoweka kutokana na ukataji holela.
- Mninga (Pterocarpus angolensis): Hutumika kutibu magonjwa kama kuhara na matatizo ya ngozi, lakini unakatwa kwa wingi kwa ajili ya mbao na dawa.
- Mvule (Milicia excelsa): Mti huu mkubwa unatajwa kuwa miongoni mwa spishi zinazohitaji uhifadhi wa haraka nchini Tanzania kutokana na matumizi yaliyopitiliza.
- Mlonge (Moringa oleifera): Pamoja na kuwa unalimwa maeneo mengi, spishi za porini za jamii hii zinapotea kutokana na uharibifu wa makazi na uvunaji wa mizizi.
- Mti-sumu (Securidaca longipedunculata): Unatumika kutibu magonjwa mengi ya mfumo wa neva na ngozi, lakini ni miongoni mwa miti inayotoweka kwa kasi katika maeneo kama Shinyanga.
- Mvumbasi (Ocimum suave): Mmea huu unaonukia vizuri unavunwa sana kwa ajili ya kutibu mafua na matatizo ya tumbo, na hivyo kupungua katika maeneo ya Milima ya Tao la Mashariki.

Hiyo ni picha ya mimea ambayo kwasababu ya matumizi yake kuwa makubwa inaelekea kutoweka duniani. Pamoja na hayo, dunia inaendelea kupoteza maelfu na mamilioni ya hekari za misitu muhimu kutokana na sababu nyingine kama vile kilimo, kuchoma moto hovyo na kuongezeka kwa idadi ya watu.
Takwimu za dunia mwaka 2024, zinaonyesha dunia inakadiriwa kupoteza zaidi ya hekari milioni 8 za misitu asili. Na misitu hii ndio hubeba uhai wa viumbe wote duniani, inapotea kwa kasi kubwa sana.
Kuendelea kupotea kwa idadi kubwa ya misitu hii kunaendana sambamba na kuendelea kupotea kwa viumbe hai wengine ambao hutegemea misitu hii kama sehemu ya makazi, chakula na mazalia.
Asilimia 80 ya misitu hupotea kwasababu za maendeleo ya kilimo ambacho kinahitaji maeneo mapya na upanuzi wa mashamba, hata hivyo kuchoma moto misitu imekuwa ni moja ya changamoto kubwa iliyoongoza kwa mwaka 2024 kama kichocheo kikuu cha kupotea kwa misitu sehemu nyingi duniani.
Barani Afrika, misitu inapotea kwa kasi kubwa, inaripotiwa kuwa nusu ya upotevu wa misitu yote duniani hutokea barani Afrika. Mwaka 2015 hadi 2025, Afrika imepoteza zaidi ya hekari milioni 29.9 za misitu asilia. Kiasi hiki ni kikubwa sana ukilinganisha na upotevu uliotokea miongo kadhaa iliyopita.
Hata hivyo, inakadiriwa kuwa kiasi cha misitu inayopotea barani Afrika kila mwaka ni hekari milioni 3.45. Hii ni ishara mbaya kwa uhifadhi wa misitu asilia, idadi hii ni kubwa na inaendelea kuongezeka kila siku. Tunatakiwa kujiuliza, kasi hii ya upoteaji wa misitu inaendana na kasi ya uwekezaji katika uhifadhi wa misitu hii?
Kwa upande mwingine, Tanzania inashika nafasi ya 2 Kusini mwa Jangwa la Sahara na nafasi ya 3 duniani, kama nchi ambayo inaongoza kwa uharibifu na upotevu wa misitu yake asilia. Takwimu za mwaka 2024 pekee zinaonyesha Tanzania imepoteza zaidi ya hekari 469,000 za misitu yake asili.
Sababu za Tanzania kupoteza kiasi kikubwa hivi cha misitu yake ni pamoja na kilimo biashara, ambacho kimechangia asilimia 89 kwa ukataji miti, kilimo cha kuhama hama, mahitaji makubwa ya kuni, mkaa, kulisha mifugo eneo la hifadhi, majanga ya moto, ukataji mbao na miti kwa ajili ya ujenzi.

Nchi nyingine zinazoongoza kupoteza misitu yake ni Brazili, ambayo inashika nafasi ya kwanza duniani kwa kupoteza hekari 2,942,000 za misitu kwa mwaka, ikifuatiwa na Angola ambayo inakadiriwa kupoteza hakari 510,000 za misitu yake asilia, nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inafuata kwa kupoteza hekari 283,000 na Zimbabwe inashika nafasi ya nne kwa kupoteza hekari 267,000 ya misitu yake asilia kwa mwaka kama ilivyoonyeshwa hapa.
Ushahidi mwingine kutoka katika shirika la chakula duniani FAO unaonyesha nchi za ukanda wa Mashariki na Kusuni mwa Jangwa la Sahara zinakadiriwa kupoteza zaidi ya asilimia 53 ya maeneo ya misitu asilia katika bara la Afrika.
Kuendelea kupotea kwa misitu asilia kwa kasi kubwa hivi kunachochea majanga mengi kama vile mvua nyingi kupita kiasi, mafuriko, umasikini, ukame, njaa na magonjwa. Utunzaji wa misitu ni utunzaji wa afya na maisha yetu. Tutunze misitu hii kwa nguvu zetu zote.
Nchini Tanzania, asilimia zaidi ya 60 ya watu wanaishi vijijini, ambako ndio kwenye hifadhi ya misitu. Watu hawa wanahitaji matibabu, maji, kuni, mkaa, na huduma nyingine kutoka kwenye misitu ya karibu. Hivyo hutegemea misitu hiyo kwa mahitaji hayo na mengine.
Kuendelea kupotea kwa misitu hii kunapelekea kupotea kwa fursa za utalii na fura nyingine za uwekezaji kwenye misitu, kama vile miradi ya hewa ukaa. Miradi ya hewa ukaa hufanyika sehemu ambazo zina misitu iliyohifadhiwa vizuri kwa muda mrefu. Miradi hii imeleta na inaendelea kuleta fedha nyingi kwa serikali na jamii zenye misitu hii.
Wito wangu kwa jamii, tunatakiwa kutunza misitu, tusichome moto misitu yetu, ni muhimu sana kuliko tunavyofikiri. Fikiria ni miaka mingapi imepita hadi miti hiyo na misitu hiyo kufikia hapo ilipofikia. Utagundua ni miaka mingi sana, ukuaji wa misitu ni taratibu sana, lakini upotevu wake ni wa haraka sana.
Kitendo cha kukata miti na misitu iliyotumia zaidi ya mika 10-100 kufikia ilipo ni gharama kubwa sana. Huwezi kulinganisha na uhitaji na matumizi tunayotaka kufanya.
Tujihusishe kwenye kupanda miti mbadala, badala ya kuingia msituni kukata miti kwa ajili ya dawa, ni vizuri kutafuta namna ya kupanda miti hiyo kwenye maeneo yetu ili ikikua itumike kwa matumizi ya dawa, kuni, mapambo, ujenzi nk.
Tujitokeze kwenye program za kupanda miti, kusaidi kurudisha miti iliyopotea.
Kwa afya bora na maisha mazuri kwa viumbe wote, tutunze mimea na misitu yetu!
Imeandikwa na Hillary Mrossso
+255 683 864 2481Email: hmconserve@gmail.com

