Habari msomaji wa makala za wildlife Tanzania karibu sana kwenye makala ya leo ambayo tutaenda kuichambua sheria yetu ya wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009. Hivyo fuatana nami ili tuweze kwenda pamoja, kwa makala ya jana ambayo nilielezea mfuomo wa usimamizi wa wanyamapori na majukumu ya mkurugenzi wa wanyamapori, tulifika mpaka kifungu cha 8, sasa leo nataka tuendelee na kifungu cha 9.
Katika kifungu hiki cha sheria ya wanyamapori ambacho kinaelezea UTOAJI WA CHETI CHA HESHIMA.
(9) Waziri anaweza kutoa cheti cha heshima kwa mtu yeyote ambaye-
(a) ameatoa huduma au ametumikia kwa muda usiopungua miaka ishirini katika sekta ya uhifadhi wa Wanyama Pori na kwa kutambua mchango wa huduma aliyotoa au
(b) ambaye amefanya au ametoa mchango mkubwa kwenye uhifadhi wa wanyamapori na kuwa mfano wa kuigwa.
Kama tulivyoona kwenye vifungu hivi vya sheria, waziri mwenye dhamana ana uwezo wa kutoa cheti cha heshima kwa mtu yeyote ambaye amefanya kazi katika sekta hii ya wanyamapori kwa muda usiopungua miaka 20, cheti hiki hutolewa kwa kutambua juhudi na mchano mkubwa ambao umechangia kwa kiasi kikubwa usalama kwenye uhifadhi na usimamizi wa wanyamapori.
Hivyo kwa mujibu wa sheria hii watu wote au wafanyakazi wote wanaofanya kazi kubwa kwenye sekta ya wanyamapori wana haki ya kutunukiwa vyeti vya heshima endapo watafanya kazi zao au majukumu yao ya uhifadhi wa wanyamapori kwa mujibu wa sheria hii. Hili ni jambo zuri sana na linalotia hamasa sana kwa watu waliojitoa kufanya kazi na kuhakikisha maisha na makazi ya wanyamapori na mimea vinaendelea kuwepo. Na kama sheria inavyosema hapo juu watu wenye kufanya kazi nzuri ambao hawana takwimu mbaya za kuhujumu rasiliamali au maliasili katika eneo hili watapewa cheti cha heshima.
Naamini wapo watu wanaopenda sekta hii na wamejitoa kupambana na kila hali ili kuendeleza uhifadhi wa wanyamapori, nimeona watu wenye juhudi hiyo, nimeona miradi ya uhifadhi wa wanyamapori ikifanya hivyo. Ni jambo zuri sana kwa serikali na mamlaka husika kutambua juhudi hizi. Kitu kizuri ni kwamba jambo hili limetamkwa na sheria yenyewe. Hivyo ndugu zangu wahifadhi na wote mnaojitoa kwa juhudi na maarifa kuboresha hifadhi zetu na wanyamapori wetu nataka niwaambie hakuna kazi inayoenda bure. Hata kama hautapewa cheti chochote fanya tu kwa ubora wako wote na kwa uwezo wako wote, wototo wako na wajukuu, au vitukuu wako watakuja kutambua kazi kubwa uliyoifanya kwenye eneo hili.
Asante sana kwa kusoma makala hii, endelea kufuatilia makala ijayo kwa kupata maarifa na taarifa muhimu, pia mshirikishe na mwenzako maarifa haya.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 248 681/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania