Habari mwifadhi mwenzangu?

Katika kuhakikisha kila kitengo na idara zilizowekwa kwa mujibu wa sheria ili kusimamia na kulinda maliasili za wanyamapori kwa ufanishi sheria inaruhusu kwa idara hii ya ulinzi wa wanyamapori kumiliki na kutumia silaha za moto kama vile bunduki, risasi na nyinginezo kwa ajili ya usalama wao na wanyamapori. Kama kipengele hiki kinavyoelezea Right to possess and use firearms and ammunition, ikiwa na maana ya haki ya kumiliki na kutumia bunduki. Kwenye kipengele hiki kinachoanza kwenye kifungu cha 13 ambapo tutaendelea.

13- (1) kwasababu ya kutekeleza majukumu na shughuli zao wana idara wote wa ulinzi, pia kwa mujibu wa sheria ya silaha kama bunduki na risasi wana haki ya kumiliki na kutumia silaha kwa mujibu wa sheria hii

(2) kila mwana idara ya ulinzi ana nguvu na haki kama ilivyo kwa vikosi vingine kwa mujibu wa sheria zao ambazo zinahusiana na matumizi ya bunduki na risasi au silaha za moto.

(3) Afisa yoyote mwenye mamlaka katika sekta ya wanyamapori anaruhusiwa kuitekeleza sheria hii, pia anaweza kutumia bunduki kwa mtu yeyote atakayekuwa amefanya kosa-

(a) anayetaka kukimbia au anayetaka kukimbia baadya ya kukamatwa

(b) ambaye anapinga kukamatwa;

pale ambapo afisa amejiridhisha na kuwa na sababu za kutosha kwamba hawezi kwa namna nyingine kumzuia mhalifu kutoroka na ameshampa onyo mtu huyo kwamba anakwenda kutumia bunduki yake dhidi yake na hilo onyo alilotoa kutokusikilizwa.

4) Afisa yoyote mwenye mamlaka kwenye sekta ya wanyamapori katika kuitumia sheria hii, anaweza kutumia bunduki yake dhidi ya mtu yeyote ambaye;

(a) kwa nguvu anazuia kukamatwa au anajaribu kuzuia kukamatwa kwa mtu mwingine kisheria au

(b) kwa kutumia nguvu, anatorosha au kumwokoa au anajaribu kumwokoa mtu yeyote ambaye yupo chini ya ulinzi wa sheria

(5) Afisa yeyote mwenye mamlaka kwenye sekta ya wanyamapori katika kutumia sheria hii, anaweza kutumia silaha yake pale ambapo afisa huyo ana sababu za kutosha za kufanya hivyo na endapo afisa huyo au mtu mwingine atakuwa kwenye hatari. Hii ikiwa na maana kwamba afisa yeyote kwenye sekta hii ya wanyamapori atatumia silaha yake au bunduki yake pale ambapo yupo kwenye hatari au afisa mwingine yupo kwenye hatari.

(6) Mamalaka aliyopewa afisa katika sekta ya wanyamapori katika sehemu hii ya tatu ya sheria itakuwa ni nyongeza na sio kwa kukiuka mamlaka nyingine ambayo amepewa ofisa huyo na kwa kukiuka sheria nyingine yoyote.

(7) Bila kuathiri mapendekezo ya sheria hii kwenye kifungu kidogo (1), afisa wanyamapori atakuwa na haki ya kumiliki na kutumia silaha za moto kwa mujibu wa sheria ya matumizi ya silaha za moto au sheria nyingine zilizoandikwa.

(8) kwa kusudi la sehemu hii ya sheria, “ofisa mwenye mamlaka” maana yake ni afisa wanyamapori anayetimiza majukumu yake kwenye idara ya wanyamapori(Wildlife Division), Hifadhi za Taifa, Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Afisa wanyamapori Wilaya, na hapa itajumuisha Afisa wanyamapori, wasimamizi wa wanyamapori, Askari wanyamapori wanaotimiza majukumu yao chini ya Afisa wanyamapori Wilaya (District Game Oficer).

Naamini kufikia hapa umepata kitu cha kukusaidia na kujua, katika kuhakikisha maliasili zetu zinaendelea kuwepo kwa vizazi vingi, njia nyingi inabidi zitumike kuhakikisha usalama na ulinzi wa maliasili hizi. Kwani bila kufanya hivyo tungekewa tumeshapoteza maliasili nyingi sana za wanyama na mimea. Hii yote ni juhudi ya serikali na makubaliano ya kimataifa kutumia silaha na zana nyingine kulinda maliasili zetu.

Hivyo sisi kama jamii na wadau wa maliasili hizi ambazo zipo kwenye maeneo yetu tunatakiwa kutoa mchango wetu kwenye ulinzi wa maliasili hizi, kama mnavyojua kazi zozote za kutumia silaha za moto ni kazi za hatari na zinazohatarisha maisha ya askari wetu na wote wanaofanya kazi kwenye sekta hii. Sisi nasi tunatakiwa kushiriki vita hivi kwa kuhakikisha tunatoa msaada wa mawazo, taarifa, vifaa na hata fedha kwa ajili ya ulinzi na usimamizi wa rasilimali hizi.

Mwisho, leo ndio tunahitimisha sehemu hii ya tatu ya uchambuzi wa sheria ya wanyamapori. Tuendelee kufuatilia na kujifunza sehemu ya nne ili tupate maarifa na kusaidia katika uhifadhi wa wanyamapori na maliasili nyingine.

Ahsante sana!

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 248 681/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania