Habari msomaji wa makala za wildlife Tanzania, karibu kwenye msisitizo kidogo wa uchambuji na ufahamu wa sheria hii ya wanyamapori. Naamini kati ya vitu vinavyoturudisha nyuma kwenye maendeleo yetu binafsi na maendeleo ya jamii nzima ni ukosefu wa maarifa sahihi. Kujua jambo jinsi linavyotakiwa na kufanya jambo jinsi inavyotakiwa bado imekuwa na changamoto kwenye sehemu nyingi kutokana na kutofahamu baadhi ya mambo muhimu ambayo kila mtu anapaswa kuyafahamu ili aweze kuishi kwa uhuru na kufanya shughuli zake bila woga. Sheria ni kati ya mambo muhimu sana ambayo tunapaswa kujifunza mara kwa mara na kufahamu, zipo sheria za aina nyingi kwenye maisha ya binadamu.
Kulingana na kitengo ulichopo au sehemu unayoifanyia kazi kuna maelekezo ambayo yameandikwa, kuna sheria kwenye kila kitu unachotaka kufanya kwenye maisha, kuna sheria za biashara, kuna sheria za kazi, kuna sheria za nchi, kuna sheria za kilimo, kuna sheria za makampuni na uwekezaji, kuna sheria za wanyamapori kuna sheria za misitu, kuna sheria kwenye kila sekta, uwepo wa sheria hizi ni kusaidia kurahisisha utendaji wa kazi na kuondoa migongano na kutokuelewana katika kufanya kazi au shughuli nyingine za msingi.
Kwa wiki kadhaa sasa nimekuwa nachambua kwa lugha rahisi sheria ya uhifadhi wa wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009. Katika uchambuzi na kushirikisha wenzangu baadhi ya mambo yaliyopo kwenye sheria hii, nimeona uhitaji mkubwa sana na watu, wengi wana uhitaji sana kwenye mambo ya kisheria na kufahamu yaliyopo kwenye sheria hii ya wanyamapori. Kwa kweli nimegundua mambo mengi ambayo nitakushirikisha hapa tunapoendelea na uchambuzi wa makala hizi za kila siku.
Aidha watu wanapenda sana kufahamu, kuna watu wengi ambao sio wafanyakazi au wanaofanya kazi kwenye sekta hii ya wanyamapori wamejifunza mambo haya yaliyopo kwenye sheria hii vizuri na kuniuliza maswali mazuri na mambo mengi yaliyokuwa yanawasumbua baadhi yamepata majibu kutokana na kusoma makala hizi za uchambuzi wa sheria hii ya wanyamapori. Hivyo maarifa haya ni kwa kila mtu bila kubagua yupo wapi, kila mtu anayahitaji maarifa haya muhimu.
Ufahamu wa sheria hii ni muhimu sana kwa kila mtu, kila mtanzania na ambaye sio mtanzania, uelewa wa sheria hii itakusaidia kwenye mambo mengi sana, kwa mfano unataka kutembelea kwenye hifadhi au mbuga za wanyama, unataka kufanya uwekezaji kwenye sekta hii ya wanyamapori au unataka au unafanya biashara ya kitalii kwenye hifadhi za wanyama, ni muhimu sana kusoma na kuielewa sheria hii vizuri ili ufanye kazi zako kwa uhuru na kwa kujiamini. pia uelewa wa sheria hizi utasaidia sana kwenye masuala ya uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yetu kwa ujumla.
Hii ndio sababu kubwa ya wazungu kuwekeza kwenye hifadhi zetu za wanyama kwa mafanikio makubwa, kwani wanasoma na kuielewa sana sheria hii na sheria nyingine za uhifadhi wa wanyamapori, kanuni na mapendekezo yanayotolewa. Hivyo ndivyo wenzetu wanavyonufaika na kuchukua hatua. Kama unataka kuwekeza kwenye biashara ya utalii wowote ule hapa Tanzania nakupa shauri kwanza kaa chini soma sheria hii vizuri na pia soma kile kinachotakiwa kufanywa na kufuatwa hapo uelewa wa sheria na kanuni utakupa uhuru wa kufanya shughuli zako vizuri. Pia hata wale ambao wana miradi ya uhifadhi wa mazingira, au wanataka kuwa na miradi ya kuhifahi wanyamapori sehemu nzuri ya kuanzia ni kupata maarifa sahihi ya sheria hii na sehemu unakotaka kuanzisha mradi wako.
Nimeandika haya yote kukutia moyo wa kujifunza na kuendelea kufuatilia mambo yote muhimu yaliyopo kwenye sheri hii ya wanyamapori. Hivyo endelea kujifunza kila siku na tutajitahidi kila siku kuweka makala mpya inayohusu uhifadhi wa wanyamapori, pia itasaidia sana endapo utawashirikisha wengine maarifa haya ili watanzania wengi wapate ufahamu na maarifa haya muhimu. Kwa kuwa sijamaliza uchambuzi wa sheria ya wanyamapori tutaendelea Kesho kwa uchambuzi hadi tuimalize yote, kila sehemu na kipengele cha sheria tutakielezea hapa, hivyo karibu sana rafiki yangu, na mhifadhi mwenzangu tufanye kazi ya kuelimisha jamii yetu kwenye uhifadhi wa wanyamapori na pia faida za wanyamapori.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 248 681/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania