Habari Rafiki, naamini unaendelea vizuri kabisa, karibu kwenye sehemu hii ya sheria ambayo tunachambua mambo mbali mbali ambayo yapo kwa mujibu wa sheria na nimeona ni muhimu tuyajue kwa lugha rahisi. Leo bado tunaendelea na uchambuzi sehemu ya saba tupo kwenye kifungu cha 64, ambacho kinaanza na kipengele cha Mkurugenzi anaweza kurekebisha au kuboresha aina ya silaha zinazotumiwa katika kwenye masuala ya uwindaji. Hivyo fuatana nami ili twende pamoja kwenye mfululizo huu wa makala, karibu sana.

64.-(1) Mkurugenzi anaweza, baada ya kutoa taarifa kwenye Gazeti la Serikali, kuelezea aina au kiwango cha silaha ambazo zinatakiwa kutumiwa kwenye uwindaji kwenye spishi wa aina yoyote ya mnyama. Ufafanuzi hapa ni kwamba kuna aina nyingi za silaha au bunduki ambazo hutumiwa kwenye shughuli za uwindaji wa wanyamapori, aina ya silaha hutegemea na aina ya mnyama anayewindwa, kwa mfano silaha inayotumika kuwindia tembo sio sawa na inayotumika kuwindia swala. Hivyo ndivyo sheria hii inavyomaanisha kuhusu uwindaji na matumizi mengine ya maliasili.

(2) Pale ambapo masharti ya kifungu kidogo (1) yatakapotumika, mtu yeyote anayewinda mnyama yoyote au wanyama wa ngazi fulani kwa kutumia silaha ambazo zimekatazwa kwa uwindaji wa wanyama hao au spishi za wanyama hao, au endapo ametumia silaha ambayo hajaruhusiwa kuitumia kwenye masuala ya uwindaji wa wanyama wa aina fulani anafanya kosa na atawajibika kulipa faini ya kiasi kisichopungua mara mbili ya thamani ya mnyama aliyewindwa au kuhukumiwa kwenda jela kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja lakini kisizidi miaka miwili au vyote kwa pamoja. Ufafanuzi kidogo hapa, kwenye masuala yote ya uwindaji kuna sheria na kanuni zake ambazo zinasimamia masharti ya uwindaji na silaha ambazo hutumiwa kwenye uwindaji, kwa siku zijazo nitaandika makala kuelezea vizuri aina za silaha ambazo hutumika sana kwenye uwindaji wa wanyamapori.

Njia zisizo sahihi kisheria katika Uwindaji

  1. –(1) Mtu yeyote hataruhusiwa, isipokuwa kulingana na kibali cha maandishi cha Mkurugenzi ambacho alikitafuta na kukipata kwanza au kwa kulingana na kanuni na masharti yaliyo chini ya Sheria hii.-

(a) kutumia kwa kusudi la kuwinda mnayama yoyote;

(i) mashine yoyote ya gari inayozunguka (any mechanically propelled vehicle)

(ii) sumu, chambo (bait), chambo chenye sumu, silaha zenye sumu, nyavu za kuvulia, mtego wa mnyama (mtego wa kufyatuka), mtego, bunduki ya kutegeshea (set gun),  kombora, milipuko, mashimo ya mitego, risasi za duara au baruti, kitanzi au mtego, kujificha, mkuki, sengenge au kutumia kiwanja kilichozungushiwa boma;

(iii) mbwa au mnyama yoyote wa kufugwa;

(iv) silaha yoyote ya moto inayojiendesha yenyewe na zile silaha za moto zinazojiendesha nusu zenyewe na nusu zinasaidiwa na waendeshaji (operator) ambazo zina uwezo wa kurusha au kutoa risasi zaidi ya moja bila muhusika kuiruhusu kufyatua risasi hizo, au ambayo inajikoki yenyewe zaidi ya mara moja bila muhusika kuruhusu;

(v) kifaa chochote ambacho kina uwezo wa kupunguza au  kimetengenezwa kwa ajili ya kupunguza sauti ambayo hutolewa wakati wa kuiwasha silaha ya moto;

(vi) mwanga wowote wa kutengenezwa kama vile tochi, taa za magari  au mwanga wa gafla, vifaa vinavyotoa mwanga usiku ; na

(vii)  aina yoyote ya dawa ambazo zina uwezo  kuwatia ganzi au nusukaputi ili mnyama asiweze kutembea au kusimama.

(b) katika uwindaji wa mnyama yeyote na kusababisha moto wa aina yoyote; na

(c ) kuwinda mnyama yoyote-

  • Kutoka kwenye gari inayoenda au ndani ya umbali wa mita mia mbili kutoka mahali lilipo gari, isipokuwa wakati wa uwindaji wa ndege ndani ya maji;
  • Ukiachilia mbali kiboko, fisi maji, sheshe, nzohe, mamba, kuro, au ndege ambaye yupo ndani ya mita mia tano ya maji yaliyosimama kwa muda mrefu, bwawa, shimo la maji, sehemu ambayo wanyama wanakula au kulamba chumvi, mabaki ya chumvi;
  • Ndani ya kilomita moja ya hifadhi ya taifa, bustani ya wanyama, sehemu za mapumziko ya wanyama (game sanctuary), Eneo la hifadhi ya Ngorongoro au kiwanja cha ndege kidogo; na
  • Kipindi cha masaa ya giza.

(2) Mtu yeyote hataruhusiwa-

(a) kwa kusudi la kuwinda au wakati akiwa kwenye safari za uwindaji, kambi ndani ya kilomita ya kiwanja chochote cha ndege;

(b) kuvuta, kukata au kutoa nje sehemu yoyote ya mnyama aliyekufa karibu na hoteli, nyumba, bustani za wanyama au kambi inayotembelewa mara kwa mara na wageni;

(c ) kutupa mabaki ya mnyama yoyote kwenye maji, mabwawa, mashimo ya maji, maeneo yenye chumvi au sehemu zozote ambazo mara kwa mara hutumiwa na wanyama kama sehemu zao za kupumzikia;

(d) kuacha mabaki ya mizoga ya mnyama ndani ya kilomita mbili kwenye uwanja wa ndege au kilomita za kila barabara kuu inayotumiwa na watu wengi au umma, hoteli au nyumba za wageni, sehemu za hifadhi ya wanyama wenye matatizo, mashamba ya wanyamapori au bustani za wanyamapori ;na

(e) kuacha mabaki yoyote ya uchafu ya wanyama waliowindwa, kukataa, kutokuchoma nyara au kuwasha moto, au kuacha sehemu hiyo katika hali ambayo itahatarisha afya ya jamii au afya ya wanyama.

(3) Licha ya mapendekezo ya kifungu kidogo cha (1) mazuio (restrictions) yaliyowekwa na kifungu, ukiachilia mbali mazuio yaliyotamkwa kwenye aya (ii) ya sehemu (a) na kwa aya (b) ya kifungu kidogo (2), hayatatumika pale ambapo mnyama atawindwa chini ya na kulingana na mapendekezo ya kifungu cha 72.

(4) Waziri anaweza, kwa kanuni zilizotungwa chini ya sheria hii, kuweka masharti zaidi kwa njia ambazo zinatumika katika uwindaji wa wanyama kama atakavyoona inafaa.

(5) Mtu yeyote atakayekiuka au kuvunja masharti au mapendekezo ya kifungu kidogo cha (1) au (2) anafanya kosa na atawajibika kutoa faini ya kiasi kisichopungua milioni moja (1,000,000) lakini kisizidi milioni mbili (2,000,000) au kuhukumiwa kwenda jela kwa kifungo cha muda usiopungua mwaka mmoja lakini isizidi miaka mitatu, au vyote kwa pamoja;

Ikizingatiwa kwamba kosa linalohusiana na uwindaji au uuaji wa mnyama, mahakama itamwekea faini ya kiasi kisichopungua mara mbili ya thamani ya mnyama aliyewindwa au kuuwawa.

Naamini hadi kufikia hapa umepata mambo mazuri ya kukusaidia kwenye masula mbali mbali, kama unafanya kazi katika sekta hii utakuwa umefaidika kujua baadhi ya masharti ya sheria hii ya wanyamapori hivyo itakusaidia kufanya kazi yako kwa ubora na bila woga.

Karibu kwa maoni ushauri na maswali.

 

Ahsante sana!

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 248 681/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania