Kati ya vitu ambavyo vimekuwa changamoto ambazo zinasumbua na kuumiza vichwa vya watu wengi ni eneo hili la migogoro isiyoisha baina ya watu na wanyamapori. Kuna tafiti nyingi sana zimefanywa kwenye eneo hili, kuna makala nyingi sana za kitaalamu zimeandikwa kwenye sehemu hii. Lakini yote katika yote Sheria ya uhifadhi wa Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009, inaeleza namna ya kushuhulika na migogoro au changamoto zinazoletwa na wanyama na binadamu. Kuna mambo mengi sana ya kujifunza kupitia sehemu hii, hivyo karibu tujifunze kwa pamoja.
69.-(1) Mkurugenzi atamteua ofisa mwenye mamlaka kwa kusudi la kuzuia au kudhibiti wanyama wasumbufu au ambao wamesababisha hasara kwa mali au kujeruhi au kupoteza maisha ya watu. Ufafanuzi hapa ni kwamba, Mkurugenzi anateua au kumpa kazi ofisa yoyote wa wanyamapori jukumu la kudhibiti wanyama wasumbufu wanaosababisha hasara kwa mali za watu na maisha ya watu.
(2) Msimamizi yoyote wa hifadhi, askari wa hifadhi, au askari wanyamapori anaweza, kwa faida ya umma kuua mnyama yoyote msumbufu kwenye sehemu ambazo sio hifdhi za taifa au Eneo la hifadhi ya Ngorongoro. Wanyama wote ambao watakuwa wasumbufu kwa watu na mali zao nje ya eneo la hifadhi za taifa na eneo la Ngorongoro atauwawa.
(3) Wanyama wasumbufu kama inavyotumika kwenye kifungu kidogo cha (1) itajumuisha makundi ya ndege waharibifu.
- Wanyama waliotajwa kwenye Jedwali la Nne la sheria hii ndio waliotangazwa kuwa ndio wanyama hatari. Ufafanuzi hapa, sheria hii inataja na kuwaainisha wanyama wote ambao ni hatari, kama tutakavyoona wanyama hao hatari ni kiboko, faru, nyati, mamba, fisi, na tembo hao ndio wanyama hari kwa mujibu wa sehemu hii ya sheria.
71.-(1) Waziri anaweza, kwa manufaa ya umma na baada ya kushauriana na Waziri anayehusika na masuala ya fedha, kuunda kanuni ambazo zitaeleza kiasi cha fedha kitakacholipwa kama kifuta machozi (consolation) kwa mtu au kundi la watu ambao wamepoteza Maisha, mifugo, mazao au kujeruhiwa kulikosababishwa na wanyama hatari. Hapa ni Waziri mwenye dhamana ndiye anahusika na kutoa kifuta machozi kwa wahanga wa wanyama hatari. Sehemu hii ndiyo yenye changamoto kubwa sana kwa wafugaji, wakulima na watu au jamii zinazoishi kando au karibu ya maeneo ya hifadhi ya wanyamapori.
(2) Bila kuathiri masharti ya kifungu kidogo cha (1), Waziri ataunda kanuni zitakazoeleza malipo ya fedha za kifuta machozi kwa mtu yeyote aliyepatwa na jeraha au kujeruhiwa, kifo, au uharibifu kwenye mazao yake kulikosababishwa na wanyama hatari, ikizingatiwa kuwa uharibifu unaohusiana na mazao, malipo hayatafanyika kwa zaidi ya heka tano. Ufafanuzi wa hapa ni kwamba endapo mtu ameshambuliwa shamba lake na wanyama hatari na mazao yake yameliwa na kuharibiwa, na shamba hilo ni zaidi ya hekari tano, malipo hayatafanyika kwa mashamba yaliyo zaidi ya hekari tano. Hili ni angalizo kwa wale ambao hawafahamu na wanalima au wanafanya shughuli za kilimo kwenye maeneo haya, sheria ya kifuta machozi haitawasaidia sana kwa wenye mashamba makubwa zaidi ya hekari tano.
(3) Mtu hatafikiriwa kuwa ana haki ya kupata kifuta machozi chini ya sheria hii ikiwa kuna ushahidi unaoonekana kwamba mtu huyo amesababisha vitendo vya uvunjaji wa sheria chini ya sheria hiia kwa mujibu wa sheria hii kwa kupoteza maisha au amejeruhiwa na mnyama mkali. Ufafanuzi hapa ni kwa wale wanaongia kwenye maeneo ya hifadhi ya wanyama bila kufuata utaratibu wa sheria, wengi wao huwa ni majangili wanaotaka kuwaua wanayama, endapo ikitokea mtu huyo akavamiwa na kuumiza au kuuwawa na wanyama hatari hatapewa kabisa kifuta machozi.
- –(1) Pale ambapo mnyama hatari, aliyeainishwa kwenye Jedwali la Nne, ambaye amejeruhiwa akaingia, pori tengefu, pori la akiba, hifadhi ya bahari, msitu wa akiba, hifadhi ya taifa, eneo la hifadhi ya jamii au Eneo la hifadhi ya Ngorongoro, mtu huyo ambaye amemjeruhi mnyama anatakiwa mara moja kutoa taarifa hiyo kwa ofisa wanyamapori aliyekaribu, afisa misitu, msimamizi wa hifadhi, askari wa wanyamapori vijijini au muhifadhi kama tukio hilo litakavyokuwa afisa atachukua tahadhari na jitihada zote kusaidiana na muhusika ili kumuua mnyama huyo. Kuna maswali mengi yamejibiwa na kifungu hiki cha sheria. Kwa wale wanaojihusiha na shughuli za uwindaji wanajua adha wanazopata endapo wamemjeruhi mnyama na kusababisha mnyama huyo kukimbia na kwenda maeneo mengine.
(2) Mtu yeyote atakayejeruhi mnyama yoyote hatari na kushindwa kumuua atatakiwa mara moja kutoa taarifa ofisa aliyekaribu sawa na yaliyoelezwa kwenye kifungu kidogo cha (1). Ufafanuzi hapa ni kwamba mtu yoyote ambaye atasababisha majera kwa mnyama hatari anatakiwa kutoa taarifa mapema sana kwa mamlaka husika.
(3) Kila taarifa iliyotolewa chini ya kifungu kidogo cha (1) inatakiwa kuonyesha spishi, tarehe, muda na sehemu iliyojeruhiwa, aina ya jeraha, na juhudi zilizofanywa kuua mnyama na taarifa nyingine ambazo zitasaidia kuonyesha mnyama alipo
(4) Pale ambapo mnyama yoyote atapatikana amekufa na Mkurugenzi amejiridhisha kwamba ndiye mnyama ambaye amejeruhiwa na kukimbia au kutoroka kutoka kwa mtu ambaye ana lesseni, kibali au mamlaka ya kimaandishi ya kuwinda au kukamata mnyama ambaye ni spishi moja na aliyepatikana amekufa, na kwa hivyo huyo mtu-
(a) baada ya kumjeruhi mnyama atatumia kila awezalo kumuua mnyama huyo; na
(b) kwa kupoteza mnyama aliyejeruhiwa, atatoa taarifa kama inavyotakiwa na kifungu kidogo cha (2), anaweza kuagiza nyara zozote za mnyama huyo zitatolewa kwa mtu huyo.
(5) Mtu yeyote atakayeshindwa kutekeleza au kuendana na masharti yoyote ya kifungu kidogo cha (1), (2) au (3), anafanya kosa na atakuwa na hatia, atahukumiwa kulipa faini isiyopungua laki mbili (200,000) lakini isizidi milioni tano (5,000,000), au kwenda jela kwa kifungo cha muda usiopungua miezi sita lakini isizidi miaka mitatu au vyote kwa pamoja.
73.-(1) Hakuna kitu kwenye Sheria hii ambacho kitakuwa ni kosa kuua mnyama yeyote katika harakati na juhudi za kujilinda na uhai wa binadamu au mifugo. Ufafanuzi hapa ni kwamba sheria hii inaruhusu kuua mnyama yeyote ambaye anataka kuhatarisha maisha ya binadamu na mifugo, na endapo utaua mnyama kwa sababu hizo kwamba mnyama anakuwa ni tishio au anahatarisha maisha yake na ya mifugo yake, ukiua mnyama kwa sababu hizi sio kosa.
(2) kifungu cha (2) hakitahusisha kuua mnayama kuwa kujihami au kwa ulinzi ikiwa-
(a) ni tabia ya mnyama huyo kwamba anahitaji kuuwawa kwa sababu ya madhara au kwa ufahamu wa mtu aliyemuua mnyama huyo.
(b) mtu aliyeua mnyama huyo, mtu huyo ambaye maisha yamelindwa wakati ambapo ulinzi utakapokuwa unahitajika, akafanya jambo ambalo linahusisha kosa kwa mujibu wa sheria hii au chini ya sheria hii.
(c ) Hakuna kifungu chochote kwenye sheria hii kitachukuliwa kuruhusu-
- Kutumia kwenye mashimo, mitego au njia yoyote ambayo itahusisha matokeo
- Mmiliki au mwenye umiliki wa mali yoyote ambaye yupo karibu na eneo lolote la hifadhi na kuamua kwenda kuwinda kwenye eneo hilo bila kibali chochote cha maandishi kutoka kwa ofisa wa hifadhi ya eneo hilo;
- Kuua mnyama yoyote wa Taifa bila kibali cha maandishi kutoka kwa Mkurugenzi kinachoonyesaha alikubaliwa kufanya shughuli hiyo.
(3)Mtu yeyote atakaye muua mnyama yeyote katika harakati za kuokoa au kulinda maisha yake atafanya mambo haya haraka iwezekanavyo-
(a) kuondoa kutoka kwa mnyama huyo Ngozi, meno, pembe na nyara nyingine;
(b) kutoa taarifa kuhusiana na tukio hilo la kuuwawa kwa mnyama kwa afisa wanyamapori aliyekaribu sawa sawa na kifungu cha 71 (1);
(c ) kukabidhi kwa ofisa nyara zote zilizotolewa kutoka kwa mnyama huyo, ambazo nyara zote zitakuwa ni mali ya Serikali;
(d) itakapohitajika na ofisa unatakiwa kuonyesha majeraha ya mnyama huyo na mahali ambapo mnyama huyo amefia au alipo uliwa.
(4) Nyama ya mnyama aliyeuwawa kutokana na harakati za kulinda na kuokoa Maisha ya watu chini ya sheria hii, kwa kibali cha maandishi kutoka kwaofisa ambaye taarifa ya mauaji ilitolewa, mnayama huyo atatupwa na mambo mengine yataendela na ukusanyaji na taarifa na ofisa wenye mamlaka kutoka Idara ya wanyamapori, Baraza la Kijiji, Hifadhi za Taifa, Hifadhi ya eneo la Mamlaka ya nGorongoro, kama kesi itakavyokuwa.
(5) Mtu yeyote atakayekiuka masharti na mapendekezo ya sheria hii anafanya kosa na kwa mujibu wa kifungu hiki cha sheria atalipa faini isiyopungua shilingi laki tano (500,000) lakini isizidi shilingi milioni tano (5,000,000), au kwenda jela kwa kifungo kisichopungua miaka miwili lakini kisichozidi miaka mitano au vyote kwa pamoja.
- Shughuli zozote za kibinadamu, makazi au ujenzi wowote utakaokuwa na athari za maisha ya wanyama na makazi yao hautaruhusiwa ndani ya mita mia tano kutoka katika mpaka wa eneo la hifadhi ya wanyamapori bila kibali kutoka kwa Mkurugenzi.
- Pale ambapo makosa yoyote yatakayochukuliwa kwa mujibu wa sheria hii mahakama ikajiridhisha kwamba mnyama ameuliwa au kujeruhiwa na mtuhumiwa, mahakama itadhania mnyama huyo ameuliwa au kujeruhiwa makusudi wakati wa kuwinda na mshakiwa au mtuhumiwa, isipokuwa mshakiwa akiri mwenyewe kwa ushahidi ambao utairidhisha mahakama kwamba kuuwawa au kujeruhiwa kwa mnyama huyo kulikuwa ni kwa ajali ambayo ilikuwa nje ya uwezo wake kuzuia kuuwawa kwa mnyama huyo na amechukua kila njia iliyo ilikuwepo kuepuka ajali kwa mnyama huyo au kuuwawa au kujeruhiwa kwa mnyama huyo ni kama ambavyo imeelezwa kwenye kifungu cha sheria hii 62.
- Licha ya mambo mengine ambayo yapo kinyume na sheria hii, Mkurugenzi anaweza kwa faida ya umma kuua, au kuruhusu kuua mnyama yoyote sehemu yoyote tofauti na Hifadhi za Taifa na Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro. Ufafanuzi hapa ni kwamba mnayama anaweza kuuliwa au kuruhusiwa kuuliwa sehemu yoyote isipokuwa ndani ya hifadhi za taifa na Eneo la hifadhi ya Ngorongoro.
Naamini kabisa kufikia hapa umepata mwanga mpana kuhusu sehemu hii ya sheria. Ni moja ya sehemu ya sheria yenye changamoto kubwa sana kwani ni sehemu ambayo wanyama na binadamu wanagombania ardhi moja na rasilimali moja. Sehemu hii ya sheria ndio inajibu maswali ya kifuta machozi na fidia ambayo hutolewa tu kwa mtu ambaye amesababishiwa hasara na uharibifu kwa mazao na mifugo n ahata Maisha ya binadamu.
Naamini tutaendele kuwa pamoja kwenye mwendelezo wa uchambuzi wa sheria hii muhimu ya wanyamapori. Hadi kufukia sehemu hii ya tisa, tumejifunza kwa pamoja mambo mengi ambayo yamekuwa msaada kwa wafanyakazi na watu wengine waliopo kwenye sekta hii muhimu.
Ahsante sana!
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 248 681/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania