Habari wahifadhi na marafiki zangu kwenye masuala haya ya wanyamapori, naamini mmekua na siku njema sana. Karibu kwenye makala zetu za kila siku ambazo kwa siku nyingi zilizopita tumekuwa tukichambua sheria ya uhifadhi wa wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009. Bado tunaendelea na uchambuzi wa sheria hii mama ya wanyamapori Tanzania. Kuna mambo mengi sana kwenye sheria hii ya wanyamapori ambayo nimejifunza na nikaamua kuwashirikisha marafiki na wasomaji wa mtandao huu wa wildlife Tanzania, nimeamua kuwashirikisha mambo haya ambayo mengi yameandikwa kwa lugha ya kingereza, hivyo nimeyafanya kuwa kwa lugha inayoeleweka haraka na watanzania wengi ili watanzania waelewe masuala haya ya wanyamapori na maliasili hizi, pamoja na sheria zinazosimamia maliasili hizi.
Bila kuwa na maneno mengi moja kwa moja tuendelee na uchambuzi wa sehemu ya kumi ya sheria hii.Sehemu hii ya kumi ya sheria ya uhifadhi wa wanyamapori ni muhimu sana kutupa mwanga kwenye masuala yanayohusu nyara na biashara ya nyara. Kwenye makala ya jana tulielezea maana ya nyara, aina za nyara na usajili wa nyara, leo tunaendelea na biashara ya nyara au kwa kingereza tunaweza kusema Dealing in Trophies. Karibu sana twende pamoja ndani ya sheria tukianzia kifungu cha 80.
80.-(1) Mtu hataruhusiwa kuendesha biashara ya nyara au utengengenezaji wa vitu kutokana na nyara kwa ajili ya kuuza, au kufanya biashara ya nyara isipokuwa kwa mujibu wa sheria na masharti ya lesseni ya uendeshaji wa biashara ya nyara. Ufafanuzi wa hapa ni kwamba mambo yote yanayohusiana na nyara au biashara ya nyara yanatakiwa kufanyika kwa kibali au lesseni iliyotolewa kihalali na mamlaka husika kwa mujibu wa sheria.
(2) Mkurugenzi anaweza, kulingana na mapendekezo na kanuni zozote zilizotungwa chini ya sheria hii, kutoa kwa raia yoyote lesseni ya uendeshaji wa biashara ya nyara kwenye kwenye fomu maalumu baada ya kufanya maombi ya kujaza fomu ya maelekezo inayoendena na masharti ya malipo ya ada kama ilivyoelekezwa. Ufafanuzi kidogo hapa ni kwamba atakayekuwa anapewa lesseni na Mkurugenzi atatoa lesseni hiyo kwa kujaza fomu ya kutoa na kukabidhi lesseni hiyo kwa muhusika na pia mwombaji wa lesseni atajaza fomu ya maombi ya lesseni na pia atalipa ada zote zilizoelekezwa kwenye fomu husika.
(3) Mtu myenye lesseni ya uendeshaji wa biashara ya nyara atapewa na kibali cha kukamata kutengeneza vitu kutokana na nyara, kuuza na kununua nyara lakini hatapewa kibali cha kuwinda, kuua au kupiga picha mnyama yoyote.
(4) Anyehusika na biashara ya nyara hatatakiwa kukubali, kununua, kutengeneza vitu kutokana na nyara, kuuza au kumpa mtu mwingine nyara zozote kabla ya nyara hizo kusajiliwa chini ya masharti ya Sehemu ya Kumi ya Sheria hii.
81.-(1) Mtu hataruhusiwa kutoa kwa njia ya zawadi, kuua, kubadilishana au kwa njia ya kununua au kukubali nyara yoyote isipokuwa kwa mujibu na masharti yaliyotajwa kwenye kibali kilichotolewa chini ya kifungu hiki.
(2) Mkurugenzi anaweza, kwa masharti na kanuni na masharti ya kumpa mtu mwingine nyara iliyotanjwa chini ya kifungu kidogo cha (1).
(3) Msharti ya kifungu hiki hayatatumika kwa nyara yoyote iliyouzwa kwa mwendeshaji wa biashara ya nyara au serikali au nyara zilizotengenezwa ambayo cheti cha usajili kilitolewa chini ya Sehemu ya kumi ya sheria hii.
- –(1)Mtu hataruhusiwa kusafirisha nje ya nchi nyara yoyote isipokuwa ana cheti cha usafirishaji wa nyara nje ya nchi au kwa kesi inayohusu spishi walioorotheshwa na CITES, awe na kibali kilichotolewa na mamlaka husika ya nchi wanachama wa CITES. Kwa ufupi ni kwamba CITES ni makubaliano ya kimataifa walioingia nchi wanachama ambao wamekubaliana kudhibiti biashara ya viumbe hai au wanyamapori (mimea na wanyama). Hivyo endapo kuna biashara za wanyamapori na mimea inatakiwa inatakiwa iendane na sheria za CITES, tutaelezea kwenye sehemu husika vizuri masuala yote ya CITES.
(2) Mkurugenzi anaweza, kwa mujibu wa kanuni zozote zilizotungwa chini ya sheria hii na baada ya malipo ya ada yoyote iliyoelekezwa, kutoa kwa mtu yeyote anayehusika na kusafirishaji wa nyara nje ya nchi, cheti cha usafirishaji wa nyara nje ya nchi au kibali cha CITES kwenye fomu ya maelekezo.
(3) Usafirishaji nje ya nchi au usafirishaji wa sampuli (specimens) unatakiwa uendane na masharti ya Sheria hii na inatakiwa kufanyika kwa kuzingatia sehemu ambayo imeelezewa na Waziri kwenye Gazeti la Serikali.
(4) Sampuli yoyote iliyo hai inatakiwa kubebwa kwa kipindi chochote cha usafirishaji kwa mujibu wa kanuni na masharti yaliyotolewa na Waziri. Ufafanuzi hapa ni kwamba endapo usafirishaji nje ya nchi utahusisha sampuli au viumbe hai, kwa kipindi chote cha usafirishaji sampuli hiyo itakuwa imebebwa au kushikiliwa kwenye vifaa au sehemu inayotakiwa kwa mujibu wa sheria.
(5) Vibebeo au mabox ambayo hutumika kwa usafirishaji wa sampuli hai (live specimens) yanatakiwa kuendana na masharti ya kimataifa ya usafirishaji wa anga ya wanyama walio hai yani kwa kingereza (International Air Transport Association, IATA).
83.-(1) Mtu hataruhusiwa kuleta kutoka nje ya nchi nyara yoyote isipokuwa kulingana na masharti ya kimaandishi kwa mamlaka ya Mkurugenzi ambayo ameiridhia na kutoa ruhusa hiyo na pia iendane na masharti ya CITES. Ufafanuzi hapa ni kwamba kwa wanaotaka kuagiza nyara za aina yoyote kuja nchi husika anatakiwa kwanza kabisa apate ridhaa ya kimaandishi ya kufanya hivyo kutoka kwa Mkurugenzi na pia anatakiwa kwenda sawa na masharti ya CITES.
(2) Licha ya masharti ya kifungu kidogo cha (1), nyara yoyote isiyokuwa ya CITES itatakiwa kuagizwa kutoka nje ya nchi kama ilivyoelekezwa kwenye kanuni zilizotungwa chini ya Sheria hii.
84.- (1) Mtu atakaye uza, nunua, kumpa mtu mwingine, kusafirisha, kukubali, kusafirisha nje ya nchi, au kuagiza nyara kutoka nchi nyingine na kuja ndani ya nchi husika kinyume au kwa kukiuka masharti yoyote ya Sehemu hii au matakwa ya CITES, anafanya kosa na atawajibika kwa kosa lake kulipa faini isiyopungua mara mbili ya thamani ya nyara au kufungwa jela kwa kipindi kisichopungua miaka miwili na kisichozidi miaka mitano au vyote kwa pamoja.
(2) Usafirishaji au usafirijaji nje ya nchi au uagizaji ambao ni kinyume na sehemu hii au kinyume na masharti ya CITES utafilisiwa. Ufafanuzi kwenye kifungu hiki ni kwamba endapo mtu atajihusisha na biashara ya nyara bila kufuata sheria za nyara za nchi husika na sheria nyingine za kimataifa zinazosimamia biashara ya nyara atachukuliwa hatua kali sana kisheria na pia atafilisiwa bishara hiyo ya nyara. Yani nyara zote anazoziuza au kununua zitachukuliwa na serikali na kuwa mali ya serikali kwa mujibu wa sheria hii ya wanyamapori hasa kifungu hiki cha 84.
Naamini kabisa kufikia hapa umeelewa mambo yote ya kisheria kuhusu biashara ya nyara kwa mujibu wa sheria hii ya wanyamapori ya mwaka 2009. Pia kuna kanuni na sheria nyingine muhimu zinazosimamia nyara na biashara ya wanyamapori, moja wapo ni sheria za kimataifa za CITES ambazo tutazichambua na kujifunza hapa kwenye makala zijazo. Hivyo Rafiki yangu nakuhimiza kuendelea kufuatilia makaza za mtandao huu wa wildlife Tanzania kwa maarifa zaidi. Pia ungewashirikisha wengine maarifa haya muhimu ili kwa pamoja tuendelee kufahama mambo haya ya wanyamapori na kwa pamoja tushiriki kwenye uhifadhi wa maliasili zetu. Ahsante sana!
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 248 681/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania