Nishike hiki au kile, nifanye hiki au kile nisahihi kufanya jambo hili au ni kosa kufanya jambo hili, ni kosa kutofanya au kufanya jambo fulani, mashaka na wasiwasi, kutojiamini na kukosa weledi kwenye ufanyaji wa mambo ni dalili ya hali ya juu ya kukosa taarifa na maarifa sahihi kuhusu kitu fulani. Kutokuelewa cha kufanya kwenye kazi yako na kutokuwa na majibu ya moja kwa moja kwenye kazi na nafasi yako ni kukosa elimu ya msingi na uelewa wa baadhi ya mambo muhimu kama sheria. Kuelewa mipaka ya ufanyaji wa mambo na shughuli ulizopewa ni moja ya nyenzo nzuri sana ya kufanya kazi kwa ufanisi na kujiamini. Kujua ujibu nini, wakati gani na wapi ni baadhi ya mambo muhimu unayoweza kujifunza kutoka kwenye sheria, na hii ni kila sekta sio sekta ya wanyamapori pekee.

Karibu Rafiki yangu tuendelee na uchambuzi wa sheria ya wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009. Leo tunaendelea na uchambuzi wa Sehemu ya Kumi na moja (XI). Kati ya sehemu ambazo hujibu maswali mengi ambayo jamii inayo kuhusu nyara na nyara zipi ni mali ya serikali na zipi sio, makosa na adhabu za kukiuka au kuvunja masharti yanayohusiana na umiliki wa nyara.

85.-(1) Kulingana na mapendekezo ya kifungu kidogo cha (2) na kanuni zozote zilizotungwa chini ya sheria hii, zifuatazo zitakuwa ni nyaara za serikali na zitaendelea kuwa mali ya serikali-

(a) mnyama yoyote ambaye atakuwa amekamatwa au kuuliwa bila lesseni, kibali, kibali cha maandishi au mamlaka ya kimaandishi yaliyotolewa chini ya sheria hii, na sehemu yoyote ya mnyama huyo;

(b)mnyama yoyote atakayepatikana amekufa, na sehemu yoyote ya mnyama huyo;

(c) mnyama yoyote atakaye kuwa ameuliwa kwa sababu ya kujihami ili kutokupoteza maisha au mali na sehemu yoyote ya mnyama huyo; ufafanuzi hapa ni kwamba mnyama yoyote atakaye uwawa kwasababu za kujihami na kutaka kuhatarisha maisha ya mtu au mali za watu, nyara za mnyama huyo ni mali ya serikali.

(d) nyara yoyote ambayo itakuwa kwa mtu yeyote ambaye ameshindwa kumridhisha Mkurugenzi kwamba ameipata aliipata nyara hiyo kwa mujibu wa sheria au bila kuvunja sheria hii;

(e ) nyara yoyote ambayo uvunjaji wa masharti ya sheria hii ulifanyika; ufafanuzi, mnyama yoyote atakayeuwawa au kukamatwa bila kufuata mapendekezo na kanuni za sheria hii mnyama huyo akikamatwa atakuwa ni mali ya serikali.

(f)  nyara yoyote ambayo Waziri anaweza kuitangaza, baada ya kutoa taarifa kwenye Gazeti la serikali kuwa ni nyara ya Serikali;

(g) sampuli zilizotokea Tanzania na kusafirishwa nje ya nchi kinyume na  masharti ya sheria hii na utekelezaji wa kanuni za CITES;

(h) sampuli ambazo zimeagizwa kutoka nje ya nchi kinyume na masharti ya CITES ambazo haziwezi kurudishwa kwenye nchi zilikotoka.

(2) Nyara zozote zilizopatikana au zilizoonekana kwenye hifadhi ya Taifa au hifadhi ya Eneo la Ngorongoro au kutegemea ya kwamba kosa limeshafanyika kwa mujibu wa Sheria Hifadhi za Taifa, Sheria ya hifaadhi ya Eneo la Ngorongoro itakuwa ni mali ya Serikali.

86.-(1) Kulingana na masharti ya kifungu hiki cha Sheria, mtu hataruhusiwa kumiliki, kuuza, kununua au hata kujuhusisha na biashara ya Nyara za Serikali.

(2) Mtu atakayekiuka au kuvunja masharti yoyote ya sheria kifungu hiki cha sheria anafanya kosa na atawajibika kwa kuwa na hatia-

(a) palea ambapo mtu ameshitakiwa kuhusu nyara au sehemu yoyote ambayo ni nyara ya mnyama aliyetajwa kwenye Sehemu ya I ya  Jedwali la Kwanza la Sheria hii, na thamani ya nyara ikiwa haizidi shilingi laki moja,  atahukumiwa kwenda jela kwa kifungo kisichopungua miaka mitano lakini kisizidi miaka kumi na tano au kulipa faini isiyopungua mara mbili ya thamani ya mnyama huyo au vyote kwa pamoja; au. Kwa ufahamu kidogo baadhi ya wanyama waliotajwa kwenye Sehemu ya I (Part I) ya Jedwali la Kwanza (First Schedule) ni Babakoto sanje, Choroa, Chui, Duma, Faru, Kipunji, Mbuzi mawe, Mbwa mwitu, Mindi, Nyati, Simba nk. Kwenye makala ijayo nitawataja wote na kuwaelezea.

(b) pale ambapo mtu anashitakiwa kuhusu nyara au sehemu yoyote ya nyara ambayo ni ya mnyama aliyetajwa kwenye Sehemu ya I ya Jedwali la Kwanza la Sheria hii, na thamani ya nyara hiyo inazidi shilingi laki moja, atapata adhabu ya kulipa faini isiyopungua mara kumi ya thamani ya nyara hiyo au kuhukumiwa kwenda jela kwa muda usiopungua miaka ishirini lakini isizidi miaka thelathini au vyote kwa pamoja;

(c) kwa kesi yoyote ile ambapo-

(i) thamani ya nyara itakapokuwa ndio inahusishwa kwnye mashitaka kwamba haijafikia shilingi laki moja, faini isiopungua mara mbili ya thamani ya nyara italipwa au atakwenda jela kwa kifungo kisichopungua miaka mitatu lakini kisichozidi miaka kumi; ufafanuzi hapa ni kwamba endapo kutakuwa na mashtaka kuhusiana na thamani ya nyara kwamba haijafika shilingi laki moja, basi sheria imeweka wazi kuwa atakayelipa faini anatakiwa kulipa kiasi kisichopungua sawa na mara mbili ya thamani ya nyara hiyo au kwenda jela kwa kifungo kisichopungua miaka mitatu na kisichozidi miaka kumi.

(ii) pale ambapo mashtaka ya thamani ya nyara yanazidi shilingi milioni moja, kifungo cha jela kitakuwa miaka isiyopungua ishirini lakini isiyozidi thelathini na mahakama inaweza kuongeza adhabu nyingine ya kulipa faini isiyozidi shilingi milioni tano au mara kumi ya thamani ya nyara hiyo kwa vyovyote itakuvyokuwa kiasi kikubwa;

(3) Kwa kusudi la kifungu kidogo cha (2)-

(a) wakati wa kukadiria au kuangalia adhabu itakayotolewa, mahakama itahakikisha pale ambapo mshitakiwa anashitakiwa kuhusiana na nyara mbili au zaidi, zitachukuliwa jumla ya thamani ya nyara zote ambazo ameshitakiwa nazo, na kwa kesi yoyote masharti ya aya ya (a) au (b) ya kifungu kidogo cha (2) kitahusika kuhusiana na nyara zote ikiwa kati ya nyara hizo ni sehemu ya mnyama aliyetajwa kwenye Sehemu ya I ya Jedwali la kwanza la sheria hii.

(b) wakati wa kukadiria adhabu itakayotolewa chini ya kifungu hiki, mahakama itakokotoa au itapima thamani ya nyara yoyote au mnyama kulingana na cheti cha thamani ya nyara kama ilivyoelekezwa na Waziri kwenye kanuni au mapendekezo; na

(c) katika kukadiria adhabu itakayotolewa chini ya kifungu hiki, mahakama itakokotoa au kupima thamani ya mfugo yoyote kwa misingi ya bei ya kawaida ya mfugo kwenye soko la wazi linalouza kati ya mununuzi na muuzaji bila kutengemeana kila mmoja.

(4) Mashtaka yoyote ya ukosaji chini ya Sheria hii, hati iliyosiniwa na Mkurugenzi au afisa wanyamapori, inayoelezea thamani ya nyara zinazohusika kwenye mashtaka itafikiriwa na kukubaliwa na mahakama kuwa ni ushahidi wa kweli na uliojitosheleza kuhusiana na mada iliyotajwa au kuelezwa humo, ikijumlisha na ukweli kwamba saini iliyopo ndani ya maelezo hayo ni ya muhusika mwenye kushikilia  ofisi hiyo.

  1. (1) Mtu yeyote atakayeona nyara yoyote ya serikali ikiwa inamilikiwa na mtu ambaye hajapewa mamlaka ya kumiliki nyara za serikali, atatakiwa mara moja kutoa taarifa ya umiliki huo kwa afisa wanyamapori aliyekaribu, msimamizi wanyamapori, askari wanyamapori, msimamizi wa hifadhi, askari wa hifadhi au afisa wa polisi na kama itakavyohitajika kutoa au kuwasilisha nyara hizo kwa afisa huyo, msimamizi au askari na kutoa au kuonyesha muhusika anayemiliki nyara hizo.

(2) Mtu yeyote atakayekiuka kifungu kidogo cha (1), anafanya kosa na atahukumiwa kulipa faini isiyopungua au isiyochini ya laki moja lakini isiyozidi shilingi laki tano au kifungo jela kisichopungua miezi kumi na mbil na kisichozidi miezi kumi nane au vyote kwa pamoja.

89.Mkurugenzi atawajibika kutunza au kudhibi nyara zote za serikali kulingana na maelekezo ambayo anaweza kupewa na Waziri baada ya kushauriana na Waziri wa wakati huo anayewajibika na masuala ya fedha.

Msomaji wangu, naamini kabisa kufikia hapa makala hii itakuwa imejibu baadhi ya maswali yako kuhusiana na nyara na nyara za serikali. Sasa unaweza kuelewa nyara za serikali ni zipi, unaweza kuwa msaada kwenye maliasili zetu kwa kushirikiana na wahifahi na watu wanaofanya kazi kwenye sekta hii kwenye kuhifadhi maliasili zetu na wanyamapori tulio nao. Nyara za serikali ni jambo linalochukuliwa kwa uzito sana sehemu yoyote. Hivyo jiepushe na saidia mamlaka husika endapo umeona nyara au kama una taarifa zozote za kusaidia katika eneo hii.

Nakushukuru sana Rafiki yangu kwa muda wako, umesoma makala hii naamini imekusaidia na pia utawasaidia na wengine waelewe haya ulijifunza hapa kwa kuwashirikisha. Endapo una maswali, maoni, mapendekezo, au ushauri usisite kuwasiliana nami kwa mawasiliano haya hapa chini.

Ahasante sana!

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 248 681/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania