CITES ni kirefu cha Convention on International Trade in Endangered Species of Wild Fauna and Flora. Ikiwa na maana makubaliano ya kimataifa kuhusiana na biashara za spishi za wanyama na mimea iliyopo hatarini kutoweka. Haya ni makubaliano ya nchi zaidi ya 100 duniani ambazo zimekubaliana kudhibiti na kusimamia biashara za spishi za wanyamapori na mimea iliyopo hatarini kutoweka.Zipo spishi nyingi sana wanyama na mimea ambazo zimeingia kwenye orotdha ya kuwa hatarini kutoweka, lakini juhudi za makusudi za nchi wanachama kusaini makubaliano ya kusimamia na kudhibiti biashara haramu imesaidia sana kupunguza vitendo vya kijangili na biashara haramu.

Karibu twende kwenye sheria tuone inavyoeleza kuhusu sehemu hii ya kumi na tano, ambayo ni mahususi kwa biashara za kimataifa za spishi wanyamapori na sampuli. Karibu twende pamoja.

  1. – (1) biashara yoyote ambayo inaenda kinyume na masharti ya CITES haitaruhusiwa chini ya sheria hii na sampuli zote ambazo zitauzwa kinyume na utaratibu wa sheria zitabinafsishwa.

(2) Mtu hataruhusiwa, isipokuwa kwa makubaliano, vigezo na masharti ya kibali kilichotolewa na Mkurugenzi kinachokubaliana na masharti ya CITES, kusafirisha nje ya nchi au kuagiza kutoka nchi nyingie au kusafirisha kupitia au kusafirisha tena nje kutoka Tanzania, spishi yoyote ya wanyamapori, au sampuli au mazao yake.Ufafanuzi hapa ni kwamba mtu yeyote hataruhusiwa kufaanya biashara za kimataifa za spishi za wanyamapori na sampuli bila kibali kilichotolewa na uongozi na usimamizi wa CITES, hivyo usafirishaji, uagizaji wa spishi za wanyamapori unatakiwa uendane na masharti ya kifungu hiki cha sheria na sheria nyingine zilizoandikwa zinazosimamia biashara hii ya wanyamapori.

(3) Kusafirisha nje ya nchi, kuagiza kutoka nchi nyingine, kusafirisha na kusafirisha tena nje spishi za wanyamapori walioorotheshwa kwenye majedwali ya CITES na spishi yoyote ya wanyamapori na sampuli au mazao yataruhusiwa tu kwa makubaliano na masharti ya CITES, na kabla ya utoaji wa kibali, Mkurugenzi atajiridhisha mwenyewe kwamba-

(a)sampuli zimepatikana kwa njia sahihi na za kisheria;

(b)utolewaji wa kibali hautakuwa kwa njia yoyote wenye kusababisha madhara au hasara kwa viumbe hai waliobaki kinyume na sampuli moja iliyotolewa; na

(c) masharti yote kulingana na CITES na kila makubaliano ya kimataifa na kimkoa au vifaa vinavyo husiana na usafirishaji na uagizaji wa spishi na sampuli za wanyamapori au mazao ya nyara zilizotengenezwa ambazo Serikali ni mwanachama na imekubaliana nayo.

(4) Mkurugenzi atakuwa ni msimamizi wa mamlaka ya CITES lakini kwenye mambo yanayohusiana na spishi tofauti na zinazoangukia moja kwa moja chini ya CITES nje ya Tanzania Bara, Mkurugenzi atawakilisha usimamizi mamlaka inayohusika ya CITES.

(5) Waziri anaweza kuteua au kutaja wanasayansi mmoja au zaidi kwa ajili ya sehemu hii ili mambo yote yanayohusiana na spishi tofauti na wale wanaoangukia moja kwa moja chini ya kila mamlaka ya sayansi, kwamba mamlaka ya kisayansi atawakilisha mamlaka nyingine za kisayansi. Ufafanuzi kwenye kipengele hiki ni kwamba Waziri anaweza kuwateua wanasayansi kwa ajili ya mambo yanayohusiana na spishi za wanyamapori ambazo hazijafanyiwa uchunguzi wa kisayansi au ambazo hazija angukia kwenye mamlaka ya utafiti wa kisayansi.

(6)Kutegemeana na masharti ya sheria hii, seheria yoyote iliyoandikwa inyohusiana na usafirishaji nje ya nchi na uagizaji wa vitu kutoka nchi nyingine, na kanuni zote zilizotungwa na Waziri kulingana na wanyama waliotajwa na CITES, kwa maombi yatakayofanywa kwenye fomu ya maelekezo, na kwa kulipa ada iliyokuwa inatakiwa mkurugenzi anaweza kutoa kibali au ruhusa kwa usafirishaji kwnda nje ya nchi au kuagiza vitu kutoka nje ya nchi kuja nchini au kusafirisha tena vile mlivyoagiza kutoka Tanzania Bara nyara yoyote. Ufafanuzi kidogo hapa ni kuhusu kibali cha usafirishaji na uendeshaji wa biashara za spishi za wanyamapori, kama unavyoona mwenyewe sio jambo jepesi linatakwa kupitia sehemu nyingi kwa ukaguzi, uangalifu, na inakuwa na masharti na kanuni nyingi za kufuata ili kufanikisha usafirishaji huu.

(7) Mtu yeyote atakayevunja au kukiuka masharti ya sehemu hii anafanya kosa na atawajibika kwa kosa lake kulipa faini isiyopungua mara tatu ya thamani ya sampuli iliyokuwa inahusika na utendaji wa makosa au kifungo kisichopungua miaka mitano au vyote kwa pamoja. Ufafanuzi kidogo ni kwamba endapo mtu atavunja mojawapo ya masharti na kanuni za CITES au masharti mengine yaliyo chini ya sheria hii kuhusu usafirishaji wa kimataifa wa spishi na sampuli za wanyamapori atapata adhabu kali sana ya kulipa mara tatu ya thamani ya nyara iliyokuwa inatakiwa au kusafirishwa kwa biashara au mambo mengine.

Kufikia hapa ndio mwisho wa sehemu hii ya kumi na tano ya sheria hii ya wanyamapori, naamini umepata uelewa kuhusu mambo mengi yanayohusiana na uchambuzi wa sheria hii hasa kwenye  biashara za kimataifa za usafirishaji wa spishi za wanyamapori na sampuli. Nafikiri kutokana na sheria kuwa kali na kutotoa mwanya kwa wanaofanya biashara hii kiholela kumesababisha sehemu kubwa ya biashara hii kufanyika bila kufuata sheria hizi. Kuongezeka kwa biashara haramu na kutumia njia za mkato ndio changamoto kwenye sekta nzima ya uhifadhi wa maliasili zetu.

Hivyo basi naamini umeelewa utaraibu wa kisheria wa usafirishaji au uagizaji wa spishi za wanyamapori na sampuli. Endapo una maswali, maoni au ushauri karibu sana.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 248 681/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania