Habari Rafiki, karibu kwenye makala yetu ya leo tunaendelea na uchambuzi wa sheria ya wanyamapori ya mwaka 2009. Tunaelekea mwishoni kabisa wa sheria hii muhiu ya wanyamapori ambayo ni sehemu ya kumi na saba ambayo inaelezea mambo mengi yanayohusiana na masharti ya sheria hii, adhabu kwa wanaokiuka, mashauri ya mahakama, masuala ya ushahidi na faini mbali mbali zilizopo kwenye sheria hii. Hivyo kama utakuwa umesoma makala zote za nyuma nilizoandika na kuchambua kuhusu sheria hii basi utaelewa sana sehemu hii muhimu ya kumi na saba.
Ningependa wasomaji wangu wote wa mtandao wa wildlife Tanzania waisome sehemu hii ya kumi na saba, kwani sitaichambua kwa kina kama sehemu nyingine. Hivyo kwa kuwa sehemu hii ni msisitizo na inahusu mambo ya kimahakama na ushahidi, ni vizuri sana ikasomwa ili watu waelewe lugha za kimahakama kwenye upande wa sheria ya wanyamapori Tanzania. Kama nilivyokwisha kuwaandikia kwenye makala iliyopita kwamba kesi na mashtaka mengi yanayohusu wanyamapori na maliasili ni kesi ngumu sana na zinatesa watu wengi waliohusika, kwa kuwa ni baadhi ya kesi ambazo huwa haziishi na huchukua miaka mingi mahakamani. Hivyo njia ya uhakika ya kuondokana na hayo yote ni kuacha kabisa kujihusisha na vitendo visivyo faa kwenye sekta hii ya wanyamapori.
Kwa wale wanaofanya kazi kwenye sekta hii ni muhimu sana wakaisoma sehemu hii ya sheria kwani ina mambo mengi ya kiutaratibu na ya kimahakama pale unapomkamata mtuhumiwa au mtu aliyevunja sheria hii. Kuna watu wanafanya kazi kwenye masuala ya wanyamapori, kama maaskari wanyamapori, maofisa wanyamapori, wasimamizi wa hifadhi za taifa, wawindaji na watu wanaofanya uwindaji wa kitalii, au biashara ya nyara, mahoteli ya kitalii, na wengine wote wanaofanya kazi kwenye sekta hii muhimu.
Pia hata wafugaji na wakulima wanapaswa kuisoma sheria hii ili waelewe mipaka na haki zao. Hii itasaidia uelewa na kupunguza migogoro kwenye sekta hii muhimu na mwingiliano wa sekta nyingine. Maana kumekua na malumbano na migogoro isiyoisha na ya muda mrefu kwenye masuala ya msingi kama vile ardhi na wanyamapori.
Napenda kuwaambia wasomaji wote wa mtandao huu, tutakuwa na makala nyingi zenye msaada kwa jamii na watu wote, najua kuna changamoto ya lugha kwenye uandishi , kwani baadhi ya vitu vingi vya msingi kama sheria zimeandikwa kwa lugha ya kingereza, hivyo nimelitambua hilo na kuamua kuanzisha mtandao huu kwa ajili ya kuelimisha na kujifunza mambo hayo kwa lugha rahisi na inayoeleweka kwa watanzania wengi. Karibu tuendelee kuwa pamoja. Ahsante sana!
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 248 681/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania