Ilikuwa ni tarehe 29/05/2017 nikiwa nimeshika gazeti la Mwananchi mkononi mwangu, na kama kawaida yangu naangalia taarifa ninazozipenda, nikakutana na tarifa kutoka ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira inayowaruhusu watu kuingia hifadhini bure kabisa. Hii ilikuwa ndio habari njema sana iliyonisukuma kuandika na kukushirikisha baadhi ya mambo muhimu kwenye jambo hili la Watanzania kuruhusiwa kuingia Hifadhi za Taifa bure kabisa. Napenda kupongeza jambo hili kwa dhati kabisa.
Moja ya vitu ninavyotamani kila mtazania ajue ni rasilimali zinazimzunguka, tumezungukwa na rasilimali nyingi sana, ambazo ni kivutio kwa asilimia kubwa ya watu. Najua kuna watanzania tangu wazaliwe hawajawahi kwenda hata mara moja kutembelea hifadhi za taifa. Na hii inasababishwa na sababu mbali mbali zikiwepo ukosefu wa kipato, kukosa hamasa, kutojali, na mengine mengi.
Nchi zenye mafanikio na maendeleo duniani kote hutokana na kujali vya kwao, kujali na kuthamini kile ulichonacho na kukilinda ndio msingi wa mafanikio kwenye Nyanja za uchumi, hata kama ni kidogo kiasi gani hicho hicho kidogo ulichonacho kuna mwengine hana hata hicho, pia ikumbukwe kuwa ingawa ni kidogo lakini kina upekee wake ambao haupatikani sehemu nyingine yoyote. Kile kinachozalishwa ndani ya nchi yako kikakubaliwa na wazawa na kununuliwa na wenyeji basi hapo umefanikiwa na inaonyesha moyo wa uzalendo wa kweli kwenye rasilimali na bidhaa za nchi yako.
Katika nchi kama yetu ya Tanzania, tusisubiri watu kutoka nchi nyingine ndio watutangazie utalii wetu na maliasili tulizo nazo. Tunahitaji kujikubali na kukubali kile tulicho nacho, sisi hatuna viwanda kama nchi nyingine, sisi hatua majumba mazuri ya kuliko nchi nyingine, sisi hatuna barabara nzuri na za kutosha kama nchi nyingine, sisi hatuna viwanda vya magari. Lakini asante Mungu aliyetupa vitu halisi kabisa ambavyo thamani yake haipungui mchana wala usiku, sisi tuna hifadhi nyingi za wanyamapori, sisi tuna hifadhi nzuri za baharini, sisi tuna mandhari halisi na nzuri ya pwani za bahari na maziwa, sisi tuna milima mikubwa inayomezewa mate na watu wa mataifa mengine, sisi tuna maelfu ya hekta za misitu ya asili, sisi tuna eneo kubwa la ardhi yenye rutuba na yakufaa kwa matumizi mbali mbali kama vile kilimo cha kisasa na kilimo cha asili, sisi tuna idadi kubwa ya maelfu na mamilioni ya gesi asilia,iliyoizunguka Tanzania katiaka pwani ya bahari, mito na maziwa, sisi tuna mito na mabonde makubwa yenye uasili wake kwa kiasi kikubwa, sisi tuna mabwawa na chemichemi asilia kwenye miamba, yenye maji moto na maji baridi.
Historia inaielezea Tanzania kuwa ni sehemu pekee duniani inayodhaniwa kuwa ni chimbuko la binadamu wa kwanza, kuna mbuga kubwa za wanyamapori, kuna idadi kubwa sana ya Wanyama wanaokula nyama ambao wamo hatarini kupotea duniani, lakini tafiti zinaonyesha kwa kiasi kikubwa idadi ya Wanyama hawa waliomo hatarini kupotea wanapatikana kwa wingi kwenye maeneo ya mapori na hifadhi za Taifa za Tanzania. Hii inamanisha Tanzania sio tu sehemu yenye watu wakarimu na wenye kukaribishana, bali ni sehemu pia salama kwa maisha ya Wanyama hawa adimu duniani, hivyo kwa kiasi kikubwa wanaipamba Tanzania duniani kote.
Pamoja na kwamba tuana utajiri na maliasili nyingi kiasi hicho bado kuna hali ya kutokujikubali kwa watanzania wengi, bado tunaona hatuna kitu, bado tunaona sisi ni wanyonge, bado tunaona sisi ni dhaifu kwa nchi nyingine. Mataifa mengine makubwa yanapotutisha na maviwanda yao makubwa au kuwa na miundombinu bora kuliko sisi, hatupaswi kuwaogopa maana walivyonavyo wao ni vya muda tu, lakini vya kwetu ni vya kudumu, endapo tutavitunza na kuvifanya viendelee kuwepo. Na sisi ifike wakati tuwaringishie vya kwetu, tutembee kifua mbele maana sisi ni wabarikiwa, Hivyo basi hatupaswi kutembea kihwa chini kama wau wasiona na matumaini, tunatakiwa kuelewa tulivyo navyo na kuvitumia kuwa na vile ambavyo hatuna.
Katika kuadhimisha siku ya mazingira duniani, serikali kupitia ofisi ya Makamu wa Rais mazingira ilitoa ruhusa kwa watanzania kuingia na kutembelea hifadhi za taifa buree kabisa, hili ni jambo jema sana, ambalo kwa mimi ninavyoona kwa jicho la mbali inatakiwa iwe ni njia ya kutujengea moyo wa uzalendo kwa kujua tulicho nacho na pia kupata ufahamu na elimu ya hifadhi ya mazingira hasa mazingira ya wanayama hawa muhimu. Utaratibu huu unatakiwa kuwa endelevu na wa kudumu, isiwe ni siku ya leo tu, bali kuwepo na mkakati wa makusudi wa kuwasaidia watanzania hata kwa njia hii ili na wao waweze kupata uelewa wa maliasili zao na pia waweze kushiriki kwenye suala zima la uhifadhi wa mazingira kwa ufanisi zaidi.
Katiaka kufuatilia nchi mbali mbali nimegundua kuwa nchi ya Brazili ambayo inavivutio vingi na vizuri, imekuwa na sera nzuri sana za utalii, ambapo asilimia kubwa ya wataii wa nchi hiyo ni wtalii kutoka ndani ya nchi hiyo, yani utalii wa ndani umeimarika zaidi kuliko utalii wa nje, kwa jinsi hiyo unakuta nchi inapata mapato mengi ya ndani na kusaidia kukuza uchumi wa nchi. Hili ni jambo ambalo tunapaswa kijifunza kutoka ka wenzetu wanavyojali vya kwao, na kuvipa thamani. Tunatakiwa tujali maliasili zetu na kuzienzi kwa kuwa watangazaji na watunzaji wa rasilimali hizi muhimu kwa nchi yetu.
Dhana hii ya kupeleka watanzania hifadhini itasaidia kuinua misingi ya uzalendo wa rasilimali za nchi na kuanza kujenga tabia za kutembelea hifadhi na sehemu nyingine za vivutio mabavyo vilivyoko kataka kila kona ya nchi ya Tanzania. Pamoja na hayo nawatakia kila la kheri watanzania wenzangu na  kutumia fursa hii vizuri kwa ajili ya kwenda kujifunza, kufurahia na kujua majukumu na kazi za hifadhi za taifa.
Asante sana, nakutakia utalii mwema;
Hillary Mrosso
0742092569










